UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya tano.

NENO LA SIKU_MACHI 23/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya tano.

Rafiki na mfuatiliaji wa masomo ya mtandao wa Fikra za Kitajiri, hongera kwa kuwa na siku bora katika maisha yako. Siku ya leo naamini imekuwa siku muhimu ya kukusogeza kwenye kilele cha mafanikio unayotamani katika kipindi cha uhai wako.

Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA

Karibu katika mwendelezo wa makala zinazokufunulia mbinu za jinsi gani unaweza kuwa tajiri kuanzia ngazi ya chini kabisa. Makala ya leo ni mwendelezo wa makundi ya biashara ambayo unaweza kuchagua kundi moja wapo na kuanzisha biashara ambayo itakuwezesha kukuza pato lako.

Ikiwa ni mara yako ya kwanza kufuatilia masomo haya nashauri usome makala zilizotangulia kupitia wavuti yetu ya FIKRA ZA KITAJIRI.  

SOMA: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya Nne

Tuhitimishe kujifunza makundi ya biashara kwa kuangazia kundi la mwisho la Biashara mtandaoni (online or electronic business).

Hili ni kundi la mwisho kuelezewa siyo kwa umuhimu wake bali kutokana na makundi yote tuliyojifunza yanaweza kuhusisha biashara mtandao kama njia ya kufungua masoko mapya au kuongeza mauzo.

Biashara ya “Kielektroniki” au “Mtandaoni" ni aina yoyote ya shughuli za kibiashara inayohusisha ubadilishaji wa taarifa za biashara kwa njia ya mtandao.

Hivyo, shughuli yoyote inayohusisha ubadilishaji wa bidhaa au huduma kwa malipo kati ya mtu binafsi, kundi la watu au taasisi kupitia mtandao inafaa kutafsiliwa kama biashara mtandao.

Biashara ya kielektroniki inazingatia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano ili kuwezesha shughuli za biashara nje ya uhusiano wa ana kwa ana kutokana na kuunganishwa na mtandao.

Biashara ya kielektroniki inatofautiana na makundi mengine ya biashara kutokana na shughuli za kuuza na kununua kukamilishwa kupitia mtandao.

Pia, e-business huwezesha kufanywa michakato yote ya biashara (usafirishaji wa ndani/nje, utengenezaji na uendeshaji, uuzaji na kununua, huduma kwa wateja) ndani ya mnyororo wa thamani kupitia mitandao ya ndani au nje. 

Biashara mtandao ni fursa hai kwa kila mtu katika karne hii ya mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano. Kundi hili la biashara limezalisha na litaendelea kuzalisha mabilionea wengi kutokana na kukua kwa kasi ya watumiaji wa mtandao.

Mfano, mtandao wa First Site Guide unatoa takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka 2021 takribani “watu bilioni 1.79 walinunua vitu kupitia mtandao.” Katika kipindi hicho 70% ya biashara ndogo hadi za kati ziliwekeza zaidi katika matumizi ya mfumo wa biashara za kidijitali. 

Mifano ya baadhi ya mabilionea ambao wamekuza utajiri wao kupitia matumizi ya biashara mtandao ni: Jeff Bezos, mmiliki wa Kampuni ya Amazon ambayo inajihusisha na kuuza na kununu bidhaa kwa njia ya mtandao; Jack Ma, mmiliki wa Kampuni ya Alibaba inayowezesha kuuuza na kununua kupitia mtandao; Bill Gates, mmiliki wa Kampuni ya Microsoft ambayo inajihusisha na uuzaji wa mifumo ya kompyuta; Mark Zuckerberg, mmiliki wa mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na WhatsApp;  Larry Page, mmiliki wa mtandao wa Google; Pierre Omidyar, mmiliki wa eBay; Garrett Camp, mmiliki wa mtandao wa Uber unaowezesha kuunganisha wateja na vyombo vya usafiri mjini.

Kwa hapa Tanzania, mitandao maarufu inayowezesha biashara mtandao ni pamoja na: KiKuu (uagizaji wa bidhaa kutoka China); Kupatana (mauzo mtandao ya bidhaa mbalimbali); Zoom Tanzania (mauzo ya bidhaa mtandaoni); na Bolt (kuunganisha wateja na usafiri mjini). 

FAIDA ZA BIASHARA MTANDAONI. Kama ambavyo tuliona faida na changamoto za kila kundi la biashara, biashara mtandaoni ina faida zifuatazo:-

Huondoa vikwazo vya eneo na mipaka: Unapofanya biashara kwa njia ya mtandao ni rahisi kuuza kwa wateja nje ya eneo lako maana mtandao unakuunganisha watu kote ulimwenguni.

Pia, mtandao unakuwezesha kueneza taarifa za biashara yako kwa kasi na hupatikanaji wa taarifa hizo muda wote (masaa 24).

Hii ni tofauti na kuuza bidhaa au huduma kwa kuweka biashara yako kwenye pango la biashara.

Kwa mfumo wa kufanya biashara nje ya mtandao, unategemea kupata wateja wanaoweza kulifikia duka au huduma yako katika muda wako wa kazi. 

Hupunguza muda na pesa zinazotumika: Kufanya biashara mtandao kunaondolea kodi za pango la eneo la biashara, umeme, maji na gharama gharama nyingi za uendeshaji.

Mfano, kwa teknolojia ya mtandao mtu mmoja aweza kuhudumia wateja zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja kwa kuunganishwa na teknolojia.

Pia, gharama za mawasiliano na matangazo zinapungua kutokana na teknolojia kuwezesha ujumbe maalumu wa biashara yako kusambazwa kwa watu wengi. 

Huharakisha huduma kwa wateja: Huduma kwa Wateja kupitia mtandao ni rahisi ikilinganishwa na makundi mengine ya biashara.

Zaidi ya hayo, aina hizi za huduma kwa wateja zinazonyumbulika kwa kuwa zinaweza kufanyika zaidi ya saa za kazi za ikilinganishwa na makundi mengine ya biashara.

Pia, ni rahisi kutunza kumbukumbu za malalamiko au maoni ya wateja kuhusu bidhaa au huduma unazouza.

Urahisi wa kuanzisha: Biashara ya mtandao ni rahisi kuanzishwa maana haitaji uwe na mtaji mkubwa. Unaweza kuanzisha biashara hii hata ukiwa nyumbani kwako maana hitaji la msingi ni kifaa kilichounganishwa na mtandao na chenye programu maalumu za kuunganisha na wateja wako.

Ni rahisi kufanya tathimini: Kupitia ‘software’ maalumu za kuwezesha biashara mtandao ni rahisi kuwa na kumbukumbu muhimu za uendeshaji wa biashara yako. Hii nyenzo muhimu ya kufanya tathimini ya mwenendo wa biashara yako.

Mfano, ni rahisi kujua jinsi bidhaa au huduma yako imekuwa na manufaa katika nyakati tofauti kulingana na matukio muhimu katika kipindi cha mwaka mmoja. Kupitia taarifa hizo ni rahisi kujua matakwa ya wateja wa muda mrefu au kugundua ikiwa kuna wateja wapya.

Njia ya kuepuka usumbufu wa gharama za kodi na tozo: Unapofanya biashara yenye pango au eneo maalumu la biashara kuna kodi na tozo nyingi kulingana na kanuni za nchi husika.

Unapofanya biashara mtandao kuna baadhi ya kodi au tozo ambazo utafanikiwa kuzipunguza. Mfano, kupitia biashara mtandao hautoulizwa leseni ya Halmashauri au tozo za usafi n.k.

CHANGAMOTO. Kila kundi la biashara lina changamoto zake, biashara mtandaoni inakabiliwa na changamoto zifuatazo:-

Ukosefu wa muunganiko wa ana kwa ana: Unapofanya biashara mtandao unamnyima mteja fursa ya kukutana na muuzaji, kuchunguza au kuhojiana ana kwa ana kuhusu bidhaa au huduma zako.

Hii ni tofauti na utaratibu wa biashara uliozoeleka ambao humwezesha mteja kuchunguza au kuhoji kuhusu bidhaa au huduma kabla kufanya malipo.

Muda wa kusubiria: Unaponunua bidhaa mtandaoni ni lazima uwe tayari kusubiria kipindi cha muda wa siku kadhaa kabla ya kupokea bidhaa husika.

Hii ni tofauti na makundi mengine ya biashara ambapo mteja hupokea bidhaa yake pale anapokamilisha malipo. 

Usalama na Uaminifu: Mtandaoni kuna wafanyabiashara waaminifu na baadhi wanafanya ulaghai unaopelekea watu kuogopa kufanya biashara kwa mtandao.

Pia, kukua kwa teknolojia kunaweza kupelekea udukuzi wa taarifa binafsi za mteja hali ambayo inatia doa uaminifu wa biashara za mtandaoni.

Baadhi ya wateja bado hawaamini biashara za mtandaoni kwa kutokana na uwepo wa ulaghai wa kila aina kwenye mitandao. 

HITIMISHO. Kwa karne hii ambayo tunashuhudia ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano, biashara mtandao ni fursa ambayo kila mfanyabiashara anatakiwa kuifahamu.

Dunia inahama kutoka kwenye mifumo ya kuuza na kununua kwa kutumia pesa taslimu na kuelekea kwenye malipo kwa njia mtandao.

Ni rahisi kufanya biashara mtandaoni maana wakati mwingine siyo lazima uwe na mtaji, siku hizi kuna watu wanaingiza pesa nyingi kwa kutangaza bidhaa za watu wengine (wamiliki wa maduka) na kisha kuuza mtandaoni na kurejesha halali ya mmiliki wa duka.

Pia, ni rahisi kuuza ujuzi au maarifa uliyonayo kupitia njia ya mtandao. Mfano, unaweza kuendesha semina au programu za mafunzo na kuziuza kwa njia ya makundi ya WhatsApp au majukwaa mengine. 

NB. Wasiliana nami kwa ajili ya kupata mwongozo kwenye masuala ya udhibiti, bajeti na uwekezaji wa pesa zako kupitia WhatsApp +255 786 881 155.


JIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI 

Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.


Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.




UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya Nne

NENO LA SIKU_MACHI 22/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya Nne.


Hongera mpendwa rafiki yangu kwa kuendelea kufuatilia masomo ya Mtandao wa Fikra za Kitajiri. Naamini umekuwa na siku bora kwa ajili ya kuendelea kuboresha maisha yako.

Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA

Karibu katika makala ya leo ambapo tutajifunza kundi la tatu la biashara ambayo unaweza kuanzisha kama njia mbadala ya kukuza pato lako.

Katika makala zilizopita tuliangalia makundi mawili yanayobeba biashara za aina mbalimbali ambazo unaweza kuchagua kundi mojawapo na kuanzisha biashara ya ndoto zako.

Kama hukufanikiwa kusoma makala hizo unaweza kufuatilia mfululizo wa makala zote kupitia wavuti yetu ya FIKRA ZA KITAJIRI.  


Karibu katika makala ya leo ambapo tutajifunza kundi la biashara zinazohusiana na uzalishaji/utengenezaji wa bidhaa (product manufacturing).

Hili ni kundi la biashara ambalo linahusisha kubadilisha malighafi kwenda kwenye bidhaa au vitu ambavyo vinahitajiwa na watumiaji wa mwisho.

Ni biashara ambazo huongeza thamani ya vitu kupitia mabadiliko ya kiufundi, kimwonekano au kemikali, umbo, na ubora na kuzalisha bidhaa mpya kulingana na mahitaji ya watumiaji wa mwisho.

Tofauti kubwa ya biashara katika kundi hili na biashara za kundi la kuuza bidhaa ni; biashara ya utengenezaji wa bidhaa inahusika na kuzalisha bidhaa ambazo wachuuzi (merchants) huziingiza sokoni kwa watumiaji wa mwisho.

Mfano wa biashara hizi ni kama vile: utengenezaji wa vito vya thamani kutoka kwenye madini ghafi; utengenezaji wa vifaa vya samani kutoka kwenye mazao ya misitu; utengenezaji wa vinjwaji kutoka kwenye matunda au malighafi yoyote; utengenezaji wa nyuzi za vitambaa au kuzalisha nguo; uzalishaji wa vifaa vya ujenzi.

Pia, ifahamike kuwa siyo kila biashara huzalisha au kutengeneza bidhaa ambazo zipo tayari kuingizwa sokoni, kuna biashara ambazo unaweza kuzalisha bidhaa zitakazotumiwa kama malighafi na kampuni nyingine za ulizashaji au utengenezaji wa bidhaa.

FAIDA ZA BIASHARA YA KUZALISHA AU KUTENGENEZA BIDHAA. Kama ambavyo tuliona katika makundi ya biashara yaliyotangulia, biashara ya kuzalisha au kutengeneza bidhaa zako mwenyewe ina faida na changamoto zake. Baadhi ya faida za biashara katika kundi hili ni pamoja na:-

Gharama ndogo za uagizaji wa bidhaa: Unapozalisha bidhaa zako mwenyewe unapunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa kwa kuwa wachuuzi hubeba gharama hizo kutoka eneo la uzalishaji hadi kwenye soko (kwa watumiaji wa mwisho).

Kupitia uzalishaji wa bidhaa unaokoa gharama za kusafirisha bidhaa ndani na nje ya nchi. Fikiria ni gharama kiasi gani ambazo wafanyabiashara (wachuuzi) wanaingia kwa kuagiza bidhaa nje nchi kama vile Uchina, Uturuki au Marekani. 

Gharama ndogo za kuajiri: Wafanyakazi wengi wa viwandani ni wale wenye elimu au ujuzi wa kawaida ikilinganishwa na waajiriwa wengine kwenye kampuni za usambazaji na mauzo ya bidhaa.

Pia, kwa kuzalisha au kutengeneza bidhaa zako mwenyewe unazalisha ajira kwa vijana katika eneo lako la kiwanda. Hali hii itakuwezesha kupunguza ukosefu wa ajira kwa jamii inayokuzunguka ikiwa ni pamoja na ndugu au jamaa zako wa karibu.

Kuepuka gharama zinazotokana na gharama za kubadilisha fedha: Unapoagiza bidhaa nje nchi kuna ongezeko la gharama zinazotokana na kupanda na kushuka kwa viwango vya fedha za kigeni ikilinganishwa fedha za nchi yako.

Kutengeneza bidhaa zako katika nchi unayoishi kutakuondolea gharama za kila mara gharama zisizotabirika  kutokana na viwango vya kubadilisha pesa.

Ni rahisi kuzalisha bidhaa zinazoendana na mahitaji ya wateja wako. Wafanya biashara wengi wanaingia hasara inayotokana na kuagiza mzingo wa bidhaa ambazo hazikidhi mahitaji ya watumiaji wa mwisho.

Kuna bidhaa ambazo unaweza kununua kwa matarajio ya kutengeneza faida lakini ukajikuta umelaza mtaji kutokana na bidhaa hizo kutokukidhi ubora wa viwango au mahitaji ya bei ya wateja wako.

Unapozalisha bidhaa zako mwenyewe ni rahisi kuhakikisha unalinda ubora sambamba na kuzalisha bidhaa kulingana na mahitaji ya watumiaji wa mwisho.

CHANGAMOTO. Biashara katika kundi hili kama ilivyo kwa makundi mengine zinakabiliwa na changamoto kama vile:- 

Mtaji mkubwa. Ili uzalishe bidhaa zako mwenyewe unatakiwa uwe na mtaji wa kutosha kwa ajili ya kununua mashine za kutengeneza bidhaa sambamba na ujenzi wa kiwanda. 

Kulinda viwango vya ubora. Kila bidhaa zinazozalishwa zinatakiwa kukidhi matakwa ya viwango vya ubora kulingana na kanuni za uzalishaji wa bidhaa husika.

Kwa hapa, Tanzania kabla ya kuzalisha bidhaa unatakiwa kuzingatia matakwa ya TBS ili bidhaa yako iruhusiwe kuuzwa ndani na nje ya nchi.

Upinzani wa kibiashara. Unapozalisha bidhaa zako mwenyewe una hatari ya kuhakikisha unamaliza changamoto za wazalishaji wengine katika sekta yako.

Ikumbukwe kuwa unapozalisha bidhaa mpya unakabiliwa na changamoto ya kushawishi wateja waamini bidhaa zako ikilinganishwa na bidhaa nyingine za aina hiyo katika soko.

Ugumu wa kupanua biashara yako. Kadiri biashara inavyokua, ndivyo matatizo yanaanza kutokea hasa kutokana changamoto za mashine kadri zinavyotumika zaidi (tering and wear).

Kuna gharama ambazo unatumia kurekebisha mitambo ambazo zingetumia kukuza biashara. Kuhakikisha kuwa vifaa vyako vinafanya kazi na pasipo kuchelewesha uzalishaji wa bidhaa ni mojawapo ya changamoto muhimu za ambazo unatakiwa kuzishinda. 

Hitimisho. Ikiwa umeamua kufanya biashara fikiria kundi la biashara zinazohusiana na uzalishaji au utengenezaji wa bidhaa. Kila kundi la biashara ambalo tumejifunza hadi sasa lina changamoto na faida zake.

Hata hivyo, changamoto zipo kila sehemu na ndiyo maana hutakiwa kuogopa changamoto hizo ikiwa umejiridhisha kwenye uendelevu wa biashara ambayo umeichagua.

Hatua ya kwanza kabisa kama ambavyo tuliona katika makala zilizopita, ni kuhakikisha una tafiti za kutosha kuhusiana na biashara ambayo unataka kuingiza mtaji wako.

Kundi la biashara za kuzalisha au kutengeneza bidhaa zako mwenyewe ni kundi ambalo lipo hai kuwekeza bila kuogopa changamoto ambazo tumeainisha katika makala hii.

Pia, haupaswi kuogopeshwa na neno kiwanda maana unaweza kuanza na kiwanda kidogo na ukaendelea kukipanua taratibu hadi kufikia kiwanda kikubwa.

Mwisho, nakushauri kabla ya kuanzisha uzalishaji wa bidhaa huna budi kufanya tafiti za kutosha kabla ya kuzama kwenye biashara unayohisi ni fursa hai.

 

NB. Wasiliana nami kwa ajili ya kupata mwongozo kwenye masuala ya udhibiti, bajeti na uwekezaji wa pesa zako kupitia WhatsApp +255 786 881 155.


JIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI 

Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.


Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.




UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya Tatu

NENO LA SIKU_MACHI 21/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya Tatu.


Rafiki yangu na mfuatiliaji wa masomo ya Mtandao wa Fikra za Kitajiri hongera kwa kuwa na siku bora ambayo inakupa msingi wa kufikia mafanikio ya ndoto za maisha yako.

Naamini umeendelea kutumia siku za maisha yako kama msingi wa kutengeneza ushindi unaolenga kufikia kilele cha mafanikio ya maisha yako.

Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA

Karibu katika makala ya leo ambapo tutajifunza kuhusu kundi la pili la biashara ambalo unaweza kulitazama wakati unafikiria aina ya biashara ya kufanya.

Katika makala iliyopita tuliangalia kundi la kwanza la biashara linalojumuisha biashara zote ambazo zinajikita kwenye kuuza huduma.

Kama ni mara ya kwanza kusoma makala mfululizo wa makala hizi, nashauri utembelee wavuti yetu ya FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kufuatilia makala zilizopita.


Katika makala ya leo tutajifunza kundi la Biashara zinazohusisha uuzaji wa bidhaa (Business related to sales of products). 

Tofauti kubwa ya biashara za kundi hili na zile za kundi la kwanza ni: biashara ya uuzaji wa bidhaa inahusisha kuuza vitu ambavyo vinaonekana na kushikika (physical and tangible objects). 

Bidhaa za biashara ni vitu ambavyo makampuni huuza ili kupata pesa. 

Kwa maneno mengine, biashara za kuuza bidhaa ni zile ambazo wateja hununua bidhaa kutoka kwa wafanyabia shara ili kukidhi mahitaji yao. 

Inaweza kuwa bidhaa kwa ajili ya ujenzi, vyakula, nguo, vipuri, malighafi (nafaka, chuma, madini n.k) au bidhaa za dukani. 

Biashara katika kundi hili zinahusisha kuonesha (display) bidhaa zinazouzwa ili mteja ashawishike kununua kulingana na mahitaji yake. 

Utaratibu ambao umezoeleka wa kuonesha bidhaa kwa wateja ni kupitia mfumo wa kuweka bidhaa dukani au eneo maalumu la biashara. 

Pia, kutokana na ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano, wafanyabiashara wengi huonesha bidhaa wanazouza kupitia njia ya mtandao (wavuti au kwenye mitandao ya kijamii). 

Biashara za bidhaa zinaweza zinaweza kuangukia kwenye makundi haya:-

Biashara ya kuuza malighafi: Ni biashara ambazo zinahusisha uzalishaji na uuzaji wa malighafi kwa ajili ya kutengenezea bidhaa nyingine. 

Mfano, uuzaji wa madini ghafi kama vile chuma, almasi au dhahabu; uuzaji wa nishati kama vile mafuta ghafi (ambayo hayajasafishwa), makaa ya mawe au kuni; au uuzaji wa bidhaa za kilimo na mifugo. 

Biashara hii huwezesha upatikanaji wa bidhaa zinazolishwa viwandani kwa ajili ya matumizi nyumbani, ofisini, ujenzi wa miradi na sekta ya usafirishaji.

Bidhaa zilizochakatwa: Ni biashara ambayo imezoeleka katika maeneo mengi ya jamii. 

Biashara hizi hujumuisha kuuza bidhaa kwa ajili ya watumiaji wa mwisho au kwenye viwanda vinavyohusika na utengenezaji wa bidhaa nyingine kabla ya kuuzwa kwa watumiaji wa mwisho. 

Mfano, biashara za kuuza vipuri vinavyotumika kutengeneza nagari (viwanda hununua vipuri hivyo kuunda magari lakini na watumiaji wa mwisho hununua vipuri kwa ajili ya marekebisho ya magari).

Biashara ya kuuza bidhaa za ujenzi: Biashara hii inahusisha uuzaji wa vifaa muhimu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kwa matumizi mbalimbali au ujenzi wa miradi. 

Biashara ya kuuza bidhaa za mahitaji ya kila siku: Matokeo ya mwisho ya shughuli nyingi za utengenezaji wa bidhaa ni kuwapa watumiaji wa mwisho bidhaa zinazokidhi mahitaji ya kila siku. 

Biashara hizi hujumuisha uuzaji bidhaa za mahitaji ya mwanadamu kama vile nguo, chakula, vifaa vya nyumbani au vifaa vya mawasiliano. 

FAIDA ZA BIASHARA YA KUUZA BIDHAA. Biashara ya kuuza bidhaa inaweza kuwa bora ikilinganishwa na biashara ya kuuza huduma kutokana na faida zifuatazo:-

Inahusisha uuzaji wa bidhaa zinazoshikika na kuonekana. Mteja ni rahisi kushawishiwa kununua kwa kuangalia ubora wa muundo wa bidhaa. 

Katika baadhi ya matukio, wateja wanaweza kugusa au kuendesha bidhaa kabla ya kununua, au wanaweza kuwa na fursa ya kuiona ikitumika kupitia maonyesho au video za mtandaoni.

Bidhaa zimeundwa kukidhi mahitaji ya mteja. Ikiwa mteja haridhiki na bidhaa, anaweza kuirejesha kwa urahisi au kuibadilisha na bidhaa nyingine. 

Hii ni tofauti na biashara ya kuuza huduma ambayo mara nyingi siyo rahisi kutathimini ubora wa huduma kabla ya kuilipia. 

Ni rahisi kupima thamani ya bidhaa. Biashara ya bidhaa, ni njia rahisi kwa mteja kubainisha thamani tarajiwa (perceived value) ya bidhaa kabla ya kununua. 

Hali hii huchochea mzunguko wa mauzo ya bidhaa hasa zile ambazo hudhaniwa kuwa na thamani kubwa ikilinganishwa na bei ya mauzo ya bidhaa husika.

CHANGAMOTO. Baadhi ya changamoto za biashara ya kuuza bidhaa ni:- 

Uwepo wa bidhaa nyingi na za aina moja. Ni kawaida kuona bidhaa za aina moja katika soko zilizozalishwa na kampuni tofauti, hali hii hupelekea baadhi ya bidhaa kutouzika kwa wingi. 

Baadhi ya baadhi ambazo hazina jina kwenye soko zinaweza kupelekea kuchelewesha mauzo au kutumia nguvu kubwa ya kushawishi wateja.

Ugumu wa kubadilisha bidhaa ikishatengenezwa. Ikiwa muundo au viwango vya bidhaa iliyozalishwa haikidhi mahitaji ya wateja katika soko ni ngumu kubadilisha bidhaa hiyo kwa urahisi. 

Inapotokea bidhaa haifanyi vizuri kwenye soko ni lazima bidhaa zilizozalishwa ziishe kwenye soko kabla ya kubadilisha muundo au viwango vya bidhaa husika. 

Hali hii inaweza kusababisha hasara kwa wazalishaji au wachuuzi wa bidhaa husika.

Uhitaji wa lazima wa eneo maalumu la biashara au kutunzia bidhaa. Unapofanya biashara ya kuuza bidhaa ni lazima uwe na eneo la kuuzia au stoo ya bidhaa husika na wakati mwingine vyote kwa pamoja. 

Hii ni tofauti na baadhi ya biashara ya kuuza huduma maana wakati mwingine siyo lazima kuwa pango la biashara. 

Mfano, siyo lazima mshereheashaji awe na pango la biashara.

Hitimisho. 
Kupitia makala ya leo tumejifunza kundi la pili la biashara ambayo unaweza kuifanya. 

Kundi la biashara za kuuza huduma ni miongoni mwa biashara ambazo zimeenea katika maeneo tunayoishi. 

Unaweza kuanzisha biashara katika kundi hili kwa kuzingatia mahitaji ya bidhaa katika soko unalolilenga. 

Pia, unaweza kununua bidhaa na kuziongezea thamani kabla ya kuziuza kwa wateja wako.

NB. Wasiliana nami kwa ajili ya kupata mwongozo kwenye masuala ya udhibiti, bajeti na uwekezaji wa pesa zako kupitia WhatsApp +255 786 881 155.

WAHI SASA UJIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI 
Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.

Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.