NENO LA LEO (APRILI 9, 2021): TUNAISHI KATIKA KIPINDI CHA URAHIBU WA TAARIFA ZENYE MWELEKEO HASI
Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni wakati
mwingine tumeamka tukiwa salama na tunaendelea na majukumu ya siku. Naendelea kukumbusha
kuhakikisha haupotezi mwelekeo katika malengo muhimu ambayo umejiwekea katika kipindi
cha mwaka huu. Ni rahisi kupoteza dira hasa katika kipindi hiki ambacho mambo
yanaonekana kuwa mengi wakati mud ani kidogo.
Kila kukicha linaibuka jipya na hayo yanayotokea yanaweza kukuvunja moyo wa kuendelea na majukumu ya msingi uliyojipangia katika siku husika. Na huo ndiyo ukweli maana tunaishi katika Ulimwengu ambao taarifa nyingi zenye mwelekeo hasi zinapewa nafasi kubwa kuliko taarifa zenye mwelekeo chanya. Wafuatiliaji wa taarifa au wasomaji wa taarifa wengi wameshakuwa na urahibu (addiction) wa kufuatilia taarifa hasi kuliko taarifa chanya.
Ushawahi kujiuliza kwa nini magazeti mengi utakuta taarifa hasi inapewa nafasi kubwa tena kwenye ukurasa wa mbele ikilinganishwa na taarifa chanya? Wamiliki wa vyombo vya habari wanafanya hivyo kwa kuwa wanahitaji kukidhi kiu ya wasomaji huku wakikuza biashara zao. Ukweli ni kwamba, habari hasi hupata umakini wa watu wengi zaidi, kama ni kwenye mitandao watu wengi watabofya taarifa husika zaidi hali ambayo itasababisha mapato zaidi kwa wamiliki wa jukwaa la taarifa husika.
Uandishi
wa taarifa ni biashara sawa na zilivyo biashara nyingine, hivyo, kukuza
biashara hizo wamiliki wanatafuta taarifa ambazo zitafuatiliwa na watu wengi. Na
taarifa hasi zitaendelea kupendwa zaidi hasa katika kipindi hiki cha mapinduzi
ya teknolojia ya mawasiliano. Hali iko hivyo kwa kuwa ubongo wa mwanadamu umesukwa
katika hali ya kuombeana mabaya zaidi kuliko mema.
SOMA: SHERIA 12 ZA MAFUNDISHO YA KARMA KATIKA KULIISHI KUSUDI LA MAISHA YAKO
Je kuna athari gani kufuatilia taarifa hasi katika maisha yako ya kila siku? Utafiti uliofanywa na Watafiti Shawn Achor na wenzake uligundua kuwa: “dakika 3 tu za kusikiliza au kusoma habari hasi asubuhi zinaweza kuharibu hamasa yako kwa siku nzima.” Tafsiri yake ni kwamba kwa kuwa tunaishi katika Ulimwengu wenye urahibu wa Habari hasi, mara nyingi tumekuwa tukiharibu hamasa ya kufanya kazi katika siku husika kwa kuendekeza kufuatilia taarifa za Habari kila mara. Pia, kuendekeza kufuatilia taarifa za Habari tunajikuta tunapoteza furaha ya siku bila ufahamu wetu kwa kuwa kupitia taarifa hasi tunajikuta huzuni inatawala.
Ikiwa umetambua kuwa Magezeti na Vyombo vya Habari vinapendelea kuandika taarifa hasi na chonganishi ikilinganishwa na taarifa chanya kwa nini uendelee kupoteza hamasa na furaha yako kwa kufuatilia taarifa za aina hiyo? Kila kinachoandikwa kinaandikwa kwa makusudi maalumu, mwandishi anaweza kuandika taarifa husika kwa lengo la kupata wafuatiliaji wengi lakini hasijue taarifa husika ina athari gani kwenye akili za watu. Je! kuna haja gani ya kuendelea kufuatilia taarifa hasi na chonganishi?
Mwisho, kupitia neno la tafakari ya leo tumejifunza kuwa tunaishi katika Ulimwengu wenye urahibu wa taarifa hasi na chonganishi. Taarifa hizi zimeharibu maisha yetu pasipo ufahamu wetu. Ni wazi kuwa kupitia taarifa tunazofuatilia kila mara hisia za chuki, huzuni, hasira na wivu vinatawala akili yetu na kupelekea mafarakano katika jamii. Maamuzi yapo mikononi mwako kuamua unafuatilia taarifa za aina gani na unatumia mbinu zipi kuchuja taarifa zinazokufikia. Kumbuka, mbegu ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Ongeza maarifa yako kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
ππΎππΎππΎππΎππΎ
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN
TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com