Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni asubuhi
nyingine ambayo tumepewa nafasi tena ya kuboresha maisha yetu. Kila siku
tunaalikwa kuendelea kujitambua na kuishi kusudi na shauku halisi la maisha
yetu. Kuhusiana na jukumu hilo, Mwanamziki Don Williams katika moja ya nyimbo
zake aliimba kuwa “we are always searching who we really are” ikitafsiriwa
kuwa “mara zote tunafuta uhalisia wa nafsi zetu.”
Leo
ni siku ya mwisho ambapo bendera ya Tanzania itapepea nusu mlingoti kama ishara
ya taifa letu kuendelea na maombolezo ya kifo cha mpendwa wetu, shujaa wa
Afrika, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Ni kipindi ambacho Watanzania
wengi wamelia machozi na kujikuta kila wanapotazama maisha ya Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli machozi wanayolia yanafutwa na zawadi za matendo aliyofanya katika
kipindi cha uhai wake. Kama ambavyo maandiko matafakatifu yanasema: “ni afadhali
kwenda kwenye matanga kuliko kwenda kwenye karamu, kwa sababu walio hai yawapasa
kuwa kifo chatungojea sisi wote (Mhubiri 7:2)”, hakika tumetumia kifo hiki
kujifunza mengi kuhusu kifo na jinsi gani tunatakiwa kuishi maisha yenye
thamani ili kuepuka majuto katika siku za mwisho wa uhai wetu.
SOMA: MAJUTO KWA WANAOKARIBIA KUKATA ROHO – SEHEMU YA MWISHO
Katika neno la tafakari ya leo tutajifunza mbinu ambazo zitakuwezesha kuishi shauku (passion) na kusudi halisi la maisha yako. Neno la leo ni miongoni mwa mfululizo wa mafundisho ambayo yanalenga kukuwezesha kuepuka majuto katika kipindi cha mwisho wa uhai wako hapa Duniani. Lengo kuu ni kukuwezesha katika kipindi cha mwisho wa uhai wako kila utakapotazama nyuma matendo yako yakupe faraja na tumaini kwa maisha yanayofuata.
Neno shauku (passion) linaweza kutafsiriwa kama “hali ya kupenda sana au kutamani au kujitoa kwa ajili ya shughuli/kazi, kitu, au dhana flani kwa msukumo halisi kutoka ndani mwako.” Kusudi la maisha ni “injini ya kukuongoza kuishi maisha yenye thamani – ule msukumo halisi unaokuongoza kutekeleza yale unayofanya.” Inahusisha malengo makuu ya maisha yako, kuongoza maamuzi ya maisha, kushawishi tabia, na mtazamo wako kuhusu maisha kwa ujumla wake. Kipi kinakusukuma kuamka kila siku asubuhi kufanya majukumu yako ya msingi tena yale ambayo siyo kwa ajili ya malipo. Je wito wako ni nini katika maisha ya hapa Duniani? Karibu tujifunze kwa pamoja hatua za kutambua shauku na kusudi halisi la maisha:-
Hatua #1: Ugunduzi wa nafsi yako (Jifahamu mwenyewe). Ugunduzi wa nafsi unakuwezesha kujijua wewe ni nani na umeumbwa kwa ajili ya kukamilisha nini hapa duniani. Jiulize maswali haya: Je wito wako ni upi? Je vipaji vyako ni vipi? Je una kalama zipi? Je! Unapenda nini? Ni nini kinachochochea moto wako wa ndani katika kuendelea kufanya yale unayofanya? Je! Maisha yako yote umeyatoa kwa ajili ya nini? Kipi kinakusukuma kutoka kitandani kila siku asubuhi? Maswali yote haya yanalenga uzame ndani ya nafsi na kujifanyia tathimini halisi ili upate kujua uwezo halisi uliopo ndani mwako badala ya kungojea uwezo kutoka nje.
Hatua #2: Tambua hisia zako kuhusu maisha. "Kuishi kwa kusudi" inajumuisha kufanya yale ambayo ni muhimu kwako kulingana na hisia, maadili na imani yako kukuhusu wewe na mazingira yanayokuzunguka kwa ujumla wake. Unaamini nini kuhusu maisha? Unaamini nini kuhusu nafsi yako? Je maisha yako ni kwa ajili ya nini? Unaamini nini kuhusu watu wanaokuzunguka? Haya ni maswali ambayo yatakupa muunganiko halisi wa nafsi yako dhidi mazingira yanayokuzungukwa kwa ujumla (watu, vitu na hali ya hewa). Maswali haya yatakuwezesha kuwa na maisha yenye mpangilio na kujisikia hai katika kila unachofanya huku ukiwa na shauku kutoka ndani.
Hatua #3: Ainisha vipaumbelea vyako halisi. Katika hatua ya kwanza umefanikiwa kujijua wewe ni nani na umeumbwa kwa ajili ya kukamilisha nini. Utagundua kuwa katika kupata majibu ya maswali hayo katika hatua ya kwanza na ya pili kuna vitu vingi ambavyo unatakiwa kuvikamilisha ili maisha yako yawe na thamani. Katika hatua ya tatu unatakiwa kuorodhesha vipaumbele vyote na kuchambua vya muhimu ili maisha yako utayatoe kwa ajili ya vipaumbele hivyo. Kila siku uhakikishe yale unayofanya yanachangia kwenye ukamilifu wa vipaumbele vyako. Ili ufanikiwe ni lazima upunguze mizaha katika maisha kwa maana nguvu, rasilimali, akili na muda wako unatakiwa kuelekezwa katika kutekeleza mambo ya msingi katika maisha kulingana na vipaumbele vyako. Pia, unatakiwa kujifanyia tathimini kuhusu imani ambazo umekuwa unaendekeza kuhusu maisha ya kila siku kama ni sahihi. Ondoa uongo wote ambao umekalilishwa katika kipindi cha ukuaji wako.
Hatua #4: Jiamini na kusahau mtazamo wa wengine juu yako. Wewe ni mtu pekee na wa kipekee katika dunia hii – hakikisha unakuwa wewe mwenye upekee. Kwa asili kila mmoja ni mdadisi hata kabla ya kujifunza sheria au maadili kulingana na makuzi au malezi ya sehemu uliyokulia. Yawezekana umeshindwa kuishi maisha yako halisi kutokana na kujibana kwenye maadili au sheria za shehemu husika. Tambua kuwa hakuna njia sahihi au mbaya ya kuishi bali jambo la msingi ni kuisikiliza dhamira yako inataka nini kulingana na imani yako kuhusu maisha. Ikiwa hauifuati dhamira yako, unaishi kwa kuendeshwa naa masharti ya wengine - na kamwe hakuna mtu anayeweza kukuambia wewe ni nani. Fanya kile kinachofaa kwa mtazamo wako na kwa unagalifu ikiwa unajua kipi ni bora katika maisha yako. Weka mkono wako moyoni mwako na jiambie, "Ninaamini uwezo wangu wa kufanya maamuzi yaliyo bora kwangu kwa ajili ya wengine."
Hatua #5: Ishinde hofu na kuchukua hatua ya kwanza. Kwa asili mwanadamu anakuwa na hofu hasa katika kuanzisha jambo ambalo liko nje ya mazoea yake. Hakuna njia nyingine ya kuliishi kusudi la maisha yako zaidi ya kuishi mabadiliko unayohitaji kwa kuanza kuchukua hatua. Kadri unavyojizoesha kufanya mara kwa mara kile ambacho umegundua kuwa kusudi la maisha yako ndivyo unazoea.
Hatua #6: Zingatia msingi
wa imani yako. Hii ni hatua muhimu hasa ikiwa wewe ni mfuasi wa dini.
Hatua hii itakuwezesha kuwa na muunganiko wa kusudi la maisha yako kwa mtazamo
wa mafundisho ya dini au imani yako. Pitia maandiko ya dini au imani yako ili
kujua yanasema nini kuhusu wewe na maisha yako hapa duniani. Fahamu kwa mapana
mazingira yanayokuzunguka katika mtazamo wa imani yako. Fahamu kwa mapana ufupi
wa maisha yako hapa duniani kwa mtazamo wa maandiko ya dini au imani yako.
Mwisho, kupitia neno la tafakari ya leo nimekushirikisha hatua 6 ambazo zitakuwezesha kutambua na kuishi shauku na kusudi la maisha yako. Kila mmoja ameumbwa kwa ajili ya kusudi maalumu hapa duniani. Je kusudi lako ni lipi? Kumbuka, mbegu ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Ongeza maarifa yako kupitia usomaji wa
vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha
hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs.
3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN
TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com