NENO LA LEO (APRILI 11, 2021): JINSI YA KUBADILI FIKRA KATIKA NYAKATI HIZI 4 ZA MAISHA YAKO.
Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku siku ya
jumapili ambapo naamini tunaendelea shughuli zinazojitika kwenye kuboresha maisha
yetu. Ni katika siku hii nakukumbusha kuwa mtihani mkuu tulionao katika maisha
ya kila siku ni kuhusianisha kila tunachofanya kwenye maisha bora tunayotamani.
Wakati mwingine ninaposema maisha bora wengi wetu huwa tunakimbilia kutafsiri aina ya maisha flani ambayo yamejitika kwenye umiliki wa vitu (materialism view of life). Lakini natamani kila mmoja afikirie maisha yake bora katika uwanda mpana ambao unahusisha kuishi maisha yanayomwezesha kuonesha uwezo wake halisi katika kila sekta ya maisha yake.
Katika
neno la tafakari ya leo tutapitia sehemu nne ambazo pengine kupitia mtazamo
wetu imepelekea tushindwe kuonesha uwezo halisi katika maisha ya kila siku. Lengo
ni kwamba kupitia neno hili tupate kubadilisha mtazamo wetu kuhusu sehemu hizo
na hatimaye tufanikiwe kupata zaidi katika maisha yetu. Mtazamo na imani zetu
kuhusu watu na vitu vinavyotuzunguka una mchango mkubwa katika yale
tunayofanikisha kwenye maisha yetu ya kila siku. Katika hilo, Mwandishi na
mhamasishaji Wayn Dyer aliwahi kusema kuwa: “Unapobadilisha
jinsi unavyoangalia vitu, vitu unavyoangalia hubadilika.” Tafsiri yake
ikiwa ni kwamba tunajizuia wenyewe kupitia mtazamo wetu kuhusu vitu/watu
wanaotunzunguka.
Katika kubadilisha mtazamo wetu kuhusu vitu na watu wanaotuzunguka ni lazima tutambue utatu wa utambuzi (cognitive triad) ambao unahusisha fikra, hisia na tabia. Siku hizi ukilinganisha na nyakati zilizopita, akili ya mwanadamu imetawaliwa na urahibu wa uhasi na machafuko kwa kiasi kikubwa kwa sababu hayo ndiyo anasikia kila wakati. Kila siku tunaendelea kutenganishwa kati yetu na mbaya zaidi tunatenganishwa na nafsi zetu. Habari njema ni kwamba pamoja na kwamba hatuwezi kudhibiti matukio yanayotokea kwenye maisha yetu ya kila siku; tunao uwezo wa kuitawala akili yetu. Kupitia uwezo huo tunaweza kudhibiti maisha yetu katika sehemu zifuatazo:-
NYAKATI AMBAZO UNAKABILIWA NA VIKWAZO/CHANGAMOTO. Ni jambo la heri kuona kuwa tunao uwezo wa kubadili vikwazo au changamoto kuwa fursa. Je unajihisi kuwa msongo unaotokana na mahitaji ya kifedha? Hiyo ni fursa kwako kuanza kutafuta mbinu mpya za kuongeza mfereji mpya wa kipato. Je! Kazini unakabiliwa na changamoto ya kutokubalika kiutendaji? Hiyo ni fursa kwako kuongeza ujuzi na maarifa mapya kuhusiana na fani yako. Ni sahihi kuwa kuna wakati mwingine inaweza isiwe rahisi kubadilisha kila changamoto kuwa fursa lakini tunayo nafasi ya kuondoa hisia hasi kwenye vikwazo/changamoto zilizopo mbele yetu. Katika kila kikwazo/changoto tunao wajibu wa kufikiria ni fursa ipi iliyojificha katika kikwazo/changamoto husika.
NYAKATI AMBAZO UNAJIHISI VIBAYA KWENYE UMBO LA MWILI. Bahati nzuri siku hizi ni rahisi kujifunza namna ambavyo unaweza kuwa na umbo na la mwili unalopenda kupitia mitandao ya kijamii. Zipo mbinu mbalimbali ambazo unaweza kujifunza tena bila gharama kupitia mitandao ya kijamii kuhusiana na namna ya kuboresha mwili wako. Hata hivyo, fursa kubwa iliyojificha kwenye umbo la mwili husilolipenda ni kutambua kuwa mwili miili yetu ni chombo cha kufanyia kazi. Tunakuwa na maumbile ya miili ambayo yaliyoharibika tofauti na zamani kwa kuwa tumeendekeza uzembe. Tunayo fursa ya kurudi kwenye uhalisia wa kuwa miili yetu ni kwa ajili ya kutembea, kucheza, kukimbia na kufanya kazi za kila aina. Kumbe, badala ya kufadhaika na maumbile ya miili yetu tunatakiwa kushukuru jinsi tulivyo na kujiuliza na kutumia miili kufikia matamanio ya maisha yetu. Tunatakiwa kushukuru kwa kiungo cha mwili wetu jinsi kilivyo na kuhakikisha kila kiungo kinatumiwa katika kuliishi kusudi la maisha yetu.
NYAKATI AMBAZO UNAFIKIRIA SANA NA UNA MSONGO WA MAWAZO. Uhasi na machafuko mara nyingi unapewa nafasi zaidi katika akili zetu ikilinganishwa na hali au matukio chanya. Tunaweza kupunguza matumizi ya mitandao ya kijamii na ufuatiliaji wa taarifa lakini bahati mbaya ni vigumu akili yetu kuchuja uhasi na kujikita kwenye uchanya zaidi. Hata hivyo, katika utatu tambuzi (cognitive triad), tunajifunza kutambua uhusiano wa fikra, hisia na tabia. David Burns, mtaalamu wa magonjwa ya akili, katika kitabu chake Feeling Good: The New Mood Therapy anamwambia msomaji wake kuwa: "Hisia hufuata fikra yako kama vile watoto wa bata wanavyomfuata mama yao. Japo kinachoongonza bata Watoto ukweli ni uaminifu kwa mama yao ambao hauthibitishi kwamba mama anajua aendako!" Ili kukabiliana na fikra hasi, David Burns anasema, ni kuanza kutambua ni wakati gani unahama kutoka kwenye fikra chanya na kuingia kwenye fikra hasi. Baada ya kugundua wakati ambao umeanza kunasa kwenye mitego ya fikra hasi sasa unatakiwa kukanusha fikra hizo kwa mifano ya chanya. Kisha endelea kujikita kwenye fikra ambazo zitapelekea furaha, faraja, amani na upendo.
NYAKATI ZA KUKABILIANA NA HASARA, MABADILIKO AU KUPOTEZA. Kitamaduni, huwa tunakimbia masomo ambayo yamejificha katika huzuni. Mara nyingi, tunathamini ufanisi na tija katika kuimarisha uhusiano dhidi ya nafsi zetu na mahusiano ya watu wanaotuzunguka. Hata hivyo, katika nyakati za hasara, mabadiliko ya ghafla au kupoteza kitu au mtu wa thamani hisia ya huzuni na mafadhaiko huwa inatawala. Hali hii inatoka na uhalisia kuwa kwa asili ni ngumu kukubaliana na hasara, kuachilia sehemu uliyozoea kabla ya mabadiliko au kukubaliana na kupoteza kitu cha thamani au mtu wa thamani uliyempenda zaidi. Katika nyakati za huzuni tunaweza kuhisi "tumetengwa, kukosa tumaini la baadae au kujihisi hatuna faraja tena.” Katika nyakati kama hizo tunashauriwa kujifunza kukubaliana na hasara, mabadiliko au upotevu na kwa kufanya hivyo tunaweza kujifunza zaidi kuhusu jinsi tulivyo, kutukumbusha juu ya misingi ya kuishi, na wajibu wetu katika kuishi maisha yenye huruma za kibinadamu.
Mwisho, kupitia neno la tafakari ya leo tumejifunza jinsi ambavyo fikra, hisia na tabia zinavyoathiri maisha yetu ya kila siku. Kudhibiti fikra ni kazi ngumu kwa watu wengi lakini kadri unavyojifunza kufanya hivyo utafurahia matokeo yake. Unafanikiwa kudhibiti fikra hasi maisha yako yatazawadiwa na matokeo chanya. Kumbuka, mbegu ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Ongeza maarifa yako kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu
Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com