Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku nyingine
tumebarikiwa kuwa hai huku tukiwa na deni la kuboresha maisha yetu kupitia siku
hii. Ni jumapili ambayo waumini wa dini ya Kikristo wanaungana kusherekea sikukuu
ya Pasaka ikiwa ni maadhimisho ya kukufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Pia, ni
jumapili ambayo kama taifa tunaingia siku ya 18 kati ya siku 21 za maombolezo ya
kifo cha mpendwa wetu, shujaa wa Afrika, Hayati Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli.
Katika
mfululizo wa mafundhisho yetu kuhusu majuto kwa wanaokaribia kukata roho
tuliona kuwa watu wengi katika dakika za mwisho wa uhai wao huwa wanajutia
kupoteza muda na rasilimali kutokana na kuishi maisha ya watu wengine. Tumeumbwa
kwa ajili ya kila mmoja kuishi kuonesha uwezo wake ambaye alilirithishwa toka
enzi alipoumbwa. Miongoni mwa urithi ambao kila mmoja alipewa ni uwezo wa
kujithamini (Self-esteem).
Uwezo wa kujithamini unajiumuisha tathmini ya nafsi ya mtu mwenyewe. Uwezo huu unajumuisha imani ulizonazo juu yako mwenyewe (kwa mfano, "sipendwi", "nastahili") pamoja na hali za kihemko, kama ushindi, kukata tamaa, kiburi, na aibu. Kwa ujumla kujithamini kunahusisha tathimini ya nafsi yako (kufikiria kuhusu uwezo wa nafsi yako) ambapo unaweza kujitathimini katika hali chanya au hasi. Hata hivyo, uwezo wa kujitathimini katika hali chanya unabadilika kulingana na mhusika anavyoruhusu athari za maneno ya watu wanaomzunguka. Hivyo ikiwa unaruhusu watu sumu katika maisha yako athari yake yake ni kupunguza uwezo wako wa kujithamini. Karibu tuangalie baadhi ya kauli ambazo zimekuwa zikiathiri uwezo wako wa kujiamini:-
Kauli #1: Umekuwa kituko. Mfano, fikiria umeamka asubuhi na kujiandaa vyema kuelekea kwenye majukumu yako ya siku husika, umejipamba kwa mavazi ambayo unaamini yamekutoa, ghafla unakutana na mtu au kundi la watu wanakuambia kauli kama vile “unaonekana kituko”. Hakika siku nzima ukiwa kazini utaendelea kuwa na wasiwasi juu ya mwonekano wako kwa kila unayekutana nae. Kinyume chake ni sahihi ikiwa utakutana na mtu ambaye atakuambia hakika umependeza, siku nzima utaendelea kujiamini na kuonesha uwezo wako pasipo kuhofia mwonekano wako. Kauli hii inaweza kutumiwa na watu sumu kwa ajili ya kudhoofisha uwezo wako wa kujiamini ili wao wapate kutekeleza ajenda yao katika siku husika ambayo pengine wewe ndiyo huwa unakuwa kikwazo.
Kauli #2: “Inaonekana hujui unachozungumza”. Hakuna mtu anayependa kuambiwa kuwa anachozungumza ni nje ya mazungumzo yanayoendelea. Kauli kama hii inapelekea mhusika kuondoa ubora wa kujiamini kwenye mazungumzo yalipo mezani. Maana maneno hayo yanaweza kujidhoofisha ndani kwa ndani kutokana na kuogopa aibu za kuzungumza kitu ambacho hauna uelewa wa kutosha hivyo, ili kuepuka aibu mhusika anakaa kimya. Kwa kufanya hivyo, watu sumu wanapata nafasi ya kutawala jukwaa. Mfano, kama ilikuwa ni kwenye kikao, ujasiri wa kupingana na hoja zao unapungua kwa kuwa utaanza kuwaza juu ya ufahamu wako kwenye mada inayozungumzwa.
Kauli
#3: “Ni makosa yako ndiyo yametufikisha hapa." Kauli
hii inaweza kutumiwa pengine bila ya taarifa sahihi kuhusiana na kile
unachotuhumiwa. Tafsiri yake ni kwamba pengine kundi la watu sumu linaweza
kutumia kauli hiyo kwa ajili ya kufunika maovu yao kupitia wewe. Pia, unaweza
kufanya mambo mengi mazuri lakini kwa kosa moja dogo, kundi la watu sumu
wakatumia kosa hilo kukuangamiza au kufunika mazuri yako. Hii inamaanisha nini?
Watu sumu, risasi yao kubwa wanayoitumia ni "unyanyasaji" dhidi ya
watu ambao ni hatari kwao. Kupitia risasi hiyo watarudia kila mara kuhusu makosa
yako na kamwe hawawezi kutaja mema yako. Kama hujitambui utatolewa kwenye reli
na kuanza kuimba nyimbo zao.
SOMA: SIFA 7 ZA WATU SUMU KATIKA MAISHA YAKO
Kauli
#4: “Nahisi hauko salama." Kauli hii inaweza kutumika kukuondolea
hali ya kujiamini mbele ya bosi wako au mtu yeyote mwenye mamlaka zaidi yako. Kupitia
kauli kama hiyo unaanza kuwaza madhaifu yako ikilinganishwa na mema yako mbele
ya bosi au umati wa watu wanaokusikiliza kwa ajili ya kutoa maamuzi yenye maslahi
kwao. Na pengine watu sumu wanaweza kutumia kauli kama hizo bila ya kujua
athari ya kauli hizo kwenye uwezo wa mhusika katika kujithamini.
Kauli #5: "Sitaki Kuwa Kwenye Urafiki/Mahusiano na Mtu Ambaye ……." Kauli kama hii inatumika kwenye kudhoofisha uwezo wa mhusika katika kuanzia au kuendeleza urafiki/mahusiano. Kwa vyovyote vile, rafiki wa kweli au mwenza hapaswi kusema kauli kama hii ikiwa anathamini urafiki/mahusiano husika. Lakini ukweli ni kwamba watu sumu wanatumia kauli hizo kwenye makundi ya marafiki au kwa wenza wao bila kujali athari ya kauli hizo. Na pengine hali hii inatokana na tabia ya watu sumu kutanguliza mahitaji yao binafsi ikilinganishwa na maslahi mapana ya kundi au mahusiano. Tabia hii pia ni matokeo ya watu sumu kuamini wao ni wakamilifu ikilinganishwa na wenza wao au kundi la watu wengine katika jamii au kwenye urafiki husika.
Kauli #6: “Wewe ni …….” Mfano, mtu anaweza kukuambia
wewe ni mshamba katika hali ya utani. Ikiwa utajitathimini hata
kama kauli hiyo haina uhalisia tayari utakuwa ushaanza kujiuliza maswali mengi
yanayohusiana na kauli kama hiyo. Maneno haya haya yanaweza kupelekea ukate
tamaa dhidi ya kile ambacho unafanya au kuamini.
Mwisho, kupitia neno la
tafakari ya leo nimekushirikisha kauli 6 ambazo mara nyingi zinatumiwa na watu
kwa makusudi au bila ufahamu wao na athari yake ni kupunguza uwezo wako wa kujithamini.
Zipo kauli nyingi za aina hii ambazo mara kwa mara zimekuwa zikitutoa kwenye
mstari wa kujiamini katika maisha ya kila siku. Kauli hizi pia zinapelekea
kujijengea imani dhaifu kuhusu uwezo wetu halisi katika maisha ya kila siku. Nakushauri
upuuzie baadhi ya kauli zinazolenga kukudhoofisha ili upata kudhihirisha uwezo
wako halisi katika maisha ya kila siku. Kumbuka, mbegu
ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii
niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika
Maisha yako.
PS: Ongeza maarifa yako kupitia usomaji wa
vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha
hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs.
3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN
TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com