FAHAMU SABABU 6 ZINAZOATHIRI UWEZO WA KUJITHAMINI (SELF-ESTEEM)

NENO LA LEO (APRILI 6, 2021): [BURIANI JPM] FAHAMU SABABU 6 ZINAZOATHIRI UWEZO WA KUJITHAMINI (SELF-ESTEEM)

Habari ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku nyingine tumepata kibali cha kuendelea kuwa hai. Ni siku ambayo tunaalikwa kuendelea kuendelea jitihada za kuboresha maisha yetu. Kila siku tuna jukumu kubwa la kujijua sisi ni nani dhidi ya mazingira yanayotuzunguka. Bila kusahau leo ni siku 20 kati ya siku 21 za maombolezo ya kifo cha mpendwa wetu, shujaa wa Afrika, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kupitia kifo hiki tumepata nafasi ya kujifunza mambo mengi kuhusu kifo na jinsi gani tunatakiwa kuishi maisha yenye thamani ili kuepuka majuto katika siku za mwisho wa uhai wetu.

 Kama bado hujajiunga na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la tafakari kila siku, tafadhali JIUNGE SASA. 

Katika neno la tafakari ya jana tulijifunza tabia tano ambazo zitakuwezesha kuishi maisha ya kujithamini na hivyo kuongeza uwezo wa kujiamini katika kila unalofanya. Kupitia neno la tafakari ya leo nimeona nikushirikishe sababu zinazoathiri uwezo wako wa kujithamini ili kupitia sababu hizo utambue ni zipi ambazo zimekuwa tatizo katika maisha yako ya kila siku. Ikumbukwe mafundisho haya ninakushirikisha baada ya mfululizo wa mafundisho yaliyopita kuhusu majuto kwa watu wanaokaribia kukata roho. Moja ya majuto tuliona kuwa wengi wanajutia kuishi maisha ambayo hawakuweza kudhihirisha uwezo wao halisi katika kipindi ambacho walikuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Karibu tujifunze kwa pamoja:-

SOMA: TABIA 5 AMBAZO ZITAKUFANYA UJIAMINI ZAIDI

Sababu #1: Umri. Umri una mchango mkubwa kwenye kiwango cha uwezo wa kujithamini kwa mhusika. Katika hatua ya ukuaji wa binadamu kuna kipindi ambacho maisha ya mhusika yanakuwa mikononi mwa watu wengine (wazazi au walezi). Tafiti zinaonesha kuwa uwezo wa kujithamini tunaongezeka kulingana na umri hadi kufikia kipindi ambacho uwezo huo unaanza kupungua kutokana na uzee. Tafiti hizo zinaonesha kuwa watu waliopo kwenye umri wa zaidi ya miaka sitini na tano wapo kwenye kilele cha viwango vya kujithamini, hasa juu ya ufanisi wa binafsi, ikilinganishwa na waliopo kwenye umri mdogo.

Sababu #2: Marafiki na Familia. Watu ambao unatumia muda mwingi kuwa nao karibu wana nafasi kubwa katika kuchangia kiwango chako cha kujithamini. Kupitia marafiki unaweza kuongeza uwezo wa: kujiamini, kujiheshimu, mtazamo wa mwonekano wako, au wanaweza kukubomoa kabisa kwa kushusha kiwango cha kujithamini. Bila kusahau kuwa wapo watu wengine kwa makusudi au bila ufahamu wao kila mara wanatoa kauli ambazo zinashusha kiwango chako cha kujithamini. Pia, familia yako ina mchango chanya au hasi kwenye kiwango chako cha uwezo wa kujithamini.

Sababu #3: Eneo la kazi. Mazingira ya kazi. Ni wazi kuwa muda mwingi wa maisha yako unautumia ukiwa shuleni kipindi cha masomo na kazini. Sehemu hizi mbili zina nafasi kubwa ya kuathiri kiwango cha uwezo wa kujithamini kwa njia chanya au hasi. Zipo shule au Vyuo kulingana na jina lake Mwanafunzi anajiona yupo kwenye kiwango cha juu cha kuheshimika. Vivyo hivyo, zipo taasisi au kampuni ambazo kila mtu anatamani siku moja kuwa sehemu ya wafanyakazi wa taasisi hizo. Hata hivyo, mtazamo huo unaishia kujenga picha ya mhusika kwenye jamii inayomzunguka hila ndani taasisi au shule/chou mhusika anaweza kukuza au kushusha uwezo wa kujithamini kulingna na na mazingira ya watu wanaomzunguka. Mfano, Walimu au walezi wako kazini wanaweza kujenga au kubomoa uwezo wako wa kujithamini bila kujali shule/chuo au taasisi unayofanyia kazi au kusoma.

Sababu #4. Ulemavu. Hii ni sababu nyingine ambayo inaathiri uwezo wa kujithamini kwa mhusika katika upande hasi. Watu wengi wenye ulemavu wa viungo vya mwili mara nyingi huwa wanaishi kwa kutokujikubali hasa ikiwa hawajajengwa vizuri kisaikolojia katika kipindi cha ukuaji wao. Hata hivyo, kila mwanadamu ameumbwa kwa jinsi alivyo kwa makusudi maalumu. Wapo watu ambao wametumia ulemavu wao kuwa kusudi kuu la maisha yao. Wakati unasikitika kwa kukosa kiungo kimoja cha mwili yupo mwingine ambaye hana mikono wala miguu lakini anaishi maisha ya kujivunia jinsi alivyo.

Sababu #5: Nafasi ya kiuchumi na kijamii. Hili liko wazi kuwa mwenye uchumi mzuri au nafasi ya uongozi kwenye jamii kiwango cha uwezo wake wa kujithamini kipo juu ikilinganishwa na mtu mwenye uchumi mdogo au mtu ambaye hana cheo katika jamii. Hata hivyo, wapo watu ambao kwa asili wana kiwango kikubwa cha kujithamini (kujiheshimu, kujiamini/ujasiri) bila kujali nafasi ya uchumi au cheo walichonacho.

Sababu #6: Ushawishi wa vyombo vya Habari au mitandao ya kijamii. Kila picha tunayoiona kwenye mitandao ya kijamii au kwenye vyombo vya Habari ina nafasi katika kuathiri uwezo wetu wa kujithamini. Vivyo hivyo, kwa kila filamu tunayoangalia au vitabu, makala au matangazo ya biashara tunayosoma. Mfano, matangazo mengi ya biashara yanakuwa na sifa ya kukushawishi kuchukua hatua husika hasa kununua bidhaa au kutumia huduma husika. Ushawishi huo una nafasi ya kukuathiri kwa njia chanya au hasi kiwango chako cha kujithamini.

KUJIUNGA NA PROGRAMU MAALUM YA "JILIPE KWANZA": SOMA MAKALA HII KWA KUBONYEZA MAANDISHI HAYA YENYE RANGI 

Mwisho, kupitia neno la tafakari ya leo nimekushirikisha sababu 6 ambazo zinaathiri kwa njia chanya au hasi uwezo wako wa kujithamini na hivyo uwezo wa kujiamini. Tumia sababu hizo kujifanyia tathimini binafsi ili kujua ni sababu zipi ambazo zinapelekea hali uliyonayo katika maisha yako ya kila siku. Kumbuka, mbegu ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.

 

PS:  Ongeza maarifa yako kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.

👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾

BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU

 

BORN TO WIN ~ DREAM BIG

Mwalimu Augustine Mathias

Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410

Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com

onclick='window.open(