Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni wakati
mwingine tumepata bahati ya kuwa hai katika siku ya leo. Naamini kuwa umeanza
majukumu yako ya siku kama sehemu ya kuendelea kuboresha maisha yako. Katika neno
la tafakari ya leo naendelea kukumbusha wajibu wako ambao ni deni katika kila
siku ambayo unabahatika kuwa hai. Wajibu huo si mwingine bali ni kutambua kuwa
kila siku tuna deni la kuishi kwa ajili ya ukamilisho wa kusudi kuu la maisha
yetu.
Katika kutimiza wajibu huo ni lazima tutambue kuwa: “Mwanadamu anaishi kwa ajili ya kujiendeleza katika vitu muhimu vitatu ambavyo ni: roho, mwili na akili.” Sehemu hizi tatu katika Maisha yeu ni muhimu na hakuna sehemu ambayo ni bora kuliko nyingine hivyo hakuna sehemu ambayo itaishi kwa ukamilifu pale ambapo sehemu nyingine zinaachwa.
Kumbe, kila siku tuna wajibu wa kutambua kuwa: “Siyo sahihi kuendeleza roho na kusahau mwili na akili au kuendeleza akili huku ukisahau mwili na roho.” Hapa ndipo tunaona umuhimu wa utajiri kutokana na ukweli kwamba mtu hawezi kujiendeleza kimwili bila mahitaji muhimu ya chakula; mavazi; kinga dhidi ya mvua, jua kali au Wanyama wakali; na vitu muhimu vinavyomuwezesha kufanya kazi.
Vivyo hivyo, mtu hawezi kujiendeleza kiakili kama hana uwezo wa kupata vitabu na muda wa kuvisoma; bila kuwa na uwezo wa kutembea nje ya mazingira aliyozoea na kujifunza kwa kuona; au uwezo wa kujifunza kutoka kwa marafiki wenye maarifa mbalimbali. Pia, ili kujiendeleza kiroho mhusika anatakiwa kuishi Maisha ya upendo na ni ukweli mtupu kuwa hakuna upendo katika Maisha ya dhiki kwa kuwa upendo msingi wake mkuu ni kuishi maisha ya kutoa kwa wengine. Ni wazi kuwa ikiwa mtu anapungukiwa maisha yake yanatawaliwa na dhiki inayopelekea mhusika kutanguliza nafsi yake.
Kwa utangulizi huo tuna kila sababu ya kukubaliana kuwa: “Utajiri ni haki yako ya kuzaliwa.” Tunaweza kuongea chochote kuhusiana na Maisha ya umasikini lakini ukweli unabakia kuwa ili mtu aishi maisha yenye mafanikio ni lazima awe tajiri. Ukweli ni kwamba mtu anaweza kuwa na kipaji lakini ili aweze kuendeleza kipaji hicho ni lazima awe na vitu vya msingi ambavyo vitamwezesha kukuza kipaji chake.
Maendeleo ya mtu kiroho, kimwili na kiakili yanahitaji mhusika amiliki vitu vya msingi ambavyo upatikanaji wake unahitaji mhusika awe na pesa. Kwa tafsiri hiyo uhai wa mtu unahusisha kila mtu kupata haki ya kutumia vitu vya msingi ambavyo vitamuwezesha kujiendeleza kimwili, kiroho na kiakili. Kwa maneno mengine ni “kila mtu ana haki ya kuwa tajiri.” Hivyo, utajiri ni haki ya kuzaliwa ambayo kila mtu anatakiwa kuidai asili haki hiyo katika kipindi cha uhai wake.
Ikiwa utajiri ni haki ya kuzaliwa ni lazima kwa pamoja tukubaliane kuwa: “Kuridhika na hali ya umasikini ni dhambi.” Huo ndiyo ukweli maana furaha ya kuishi ni kuendelea kupata zaidi kutoka kwenye mazingira yanayokuzunguka. Na kadri unavyopata zaidi ndivyo unatengeneza utajiri, mamlaka na nguvu ambazo zinakuwesha uishi maisha ya ukamilifu. Naam, maisha yenye kupata kila hitaji muhimu katika uhai wako.
Hivyo, hakuna maana ya kuridhika na uchache
(umasikini) wakati umeumbwa kwa ajili ya kupata zaidi (utajiri). Kwa asili kila
mwanadamu anatamani kufikia mafanikio makubwa sana katika maisha. Dhamira au
matamanio hayo amerithishwa toka enzi za kuumbwa kwake. Hata hivyo ili
mwanadamu ili afikie mafanikio ya matamanio yake ni lazima atumie vitu
vinavyomzunguka na kiwango cha upatikaji wa vitu hivyo kinategemeana na uwezo
wa kifedha ambao mhusika anao.
Mwisho, kupitia neno la tafakari ya leo tumejifunza kuwa utajiri ni haki ya kuzaliwa kwa kila mmoja wetu. Baada ya kuumbwa tumepewa akili na rasilimali katika mazingira tunayoishi. Kupitia matumizi ya akili tunatakiwa kutumia rasilimali zinazotuzunguka ili tupate utajiri ambao ni haki yetu ya kuzaliwa. Kumbuka, mbegu ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganishi hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema OFA hii.
👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu
Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com