Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku mpya
ambapo tunaalika kuendelea kuboresha maisha yetu kupitia majukumu ya siku ya
leo. Matumaini yangu ni kwamba umeamka salama ukiwa tayari kuendeleza bidii inayolenga
kufanikisha malengo yako. Husikubali kupoteza mwelekeo kutokana na kelele
nyingi ambazo zinaibuka kila kukicha. Katika kipindi hiki ambacho taarifa ni
nyingi tena ambazo hazina tafiti za kutosha huna budi kutunza nguvu na muda wako
kwa ajili ya kutekeleza majukumu yako ya msingi.
Katika la tafakari ya jana tuliona kuwa tunaishi katika Ulimwengu wenye urahibu na taarifa hasi au chonganishi. Tuliona kuwa taarifa zina mwelekeo huo kwa kuwa kwa asili wanadamu wanapenda taarifa zinazoongelea ubaya dhidi ya wenzao ikilinganishwa na mema yao. Katika neno la tafakari ya leo tutaona namna unavyoweza kujilinda dhidi ya hisia za wasiwasi na hofu zinazotokana na taarifa za kila mara. Ikumbukwe kuwa tofauti na zamani ambapo taarifa ziliripotiwa kupitia redio, TV na magazeti, siku hizi taarifa unazo mkononi mwako kupitia simu janja yako. Hapa ndipo tunatakiwa kutumia mbinu zifuatazo ili kuepuka kupoteza utulivu wa akili kwenye majukumu ya msingi kwa kuendekeza taarifa hasi au chonganishi.
SOMA: TUNAISHI KATIKA KIPINDI CHA URAHIBU WA TAARIFA ZENYE MWELEKEO HASI
Karibu tujifunze wote:-
Tambua kuwa kila taarifa ina lengo lilojificha nyuma yake. Hakuna ubishi kwamba tunaishi kwenye Ulimwengu ambao taarifa hasi zinapewa kipaumbele. Pia tunatambua kuwa ni muhimu kila mtu ana haki kujua kila kinachotokea. Hata hivyo, ni ukweli kwamba vyombo vya habari vinajikita kwenye taarifa zenye ya asili ya kusisimu na mihemko kutokana na matukio hasi pekee. Taarifa yenye sifa hizo ndiyo inapewa kipaumbele ikilinganishwa na taarifa za kuelimisha au kusifia mazuri ya watu katika jamii.
Tambua kuwa Vyombo vya Habari vinagombania muda wako. Siku hizi Waandishi na Watangazaji wa habari hawaleti tu taarifa za moja kwa moja (breaking news), katika muda maalum kama ilivyokuwa zamani bali upokeaji wa Habari umekuwa ni masaa 24. Hii inamaanisha kuwa watu katika fani ya Habari wanashindania umakini wa wafuatiliaji kwa kugeuza habari ziwe na sifa kusisimua. Kwa maneno mengine taarifa zinaandaliwa kwa ajili ya kuteka akili za watu ili waendelee kufuatilia taarifa zaidi kila mara. Kwa kufanya hivyo, vyanzo vya taarifa husika vinaongeza idadi ya wafuatiliaji na hivyo kukuza mapato yao kupitia wafuatiliaji hao. Hivyo, kila taarifa unasoma au kusikia unatakiwa kutambua kuwa tukio husika limeongezwa hali ya kimhemko au kusisimu zaidi ili kuvutia wasomaji. Na huo ndiyo ukweli kuwa taarifa ambazo zimeongezwa chumvi ndo zinapendwa na watu katika jamii tunayoishi.
Chagua vyanzo vyako vya Habari kwa Uangalifu. Taarifa unazipata kutoka kwenye vyanzo vipi? Vipo vyanzo vya Habari ambavyo mara zote vinalenga kukuza ukubwa wa tukio kwa ajili ya kupandikiza uhasama, chuki na migogoro katika jamii. Katika kipindi hiki cha mapinduzi ya teknolojia ya Habari kila mmoja anaandika lake ili mradi tu afanikiwe kuteka hisia zako na huku akitekeleza ajenda yake. Hata hivyo, vipo baadhi ya Vyombo vya Habari (Magazeti, Redio na TV) ambavyo haviongezi chumvi sana kwenye matukio yanayoripotiwa. Katika kila taarifa unayosoma au kuangalia au kusikiliza unatakiwa kuruhusu mfumo wako wa fikra kuchambua taarifa husika na siyo kuipokea na kuiamini moja kwa moja. Jiulize, Je! Chapisho au taarifa hii inalenga kufikisha ujumbe gani?' Je! ni kwa nini taarifa hii katika wakati huu?
Tambua mipaka yako na fikiria taarifa zipi hupaswi kuzifuatilia. Lengo kubwa la kufuatilia taarifa za Habari ni kujua kinachoendelea katika jamii unayoishi na Duniani kwa ujumla. Ikiwa unaona taarifa unazofuatilia zinakutoka nje ya lengo hilo una kila sababu ya kuanza kujiwekea mipaka kwenye baadhi ya taarifa, mfumo wa kufuatilia na wakati wa kufuatilia taarifa kila siku. Mfano, kama unaona tatizo linalokusumbua kutokana na taarifa unazofuatilia linachochochewa na picha wanazoweka, unaweza kujaribu kusikiliza habari kwenye redio. Au, unaweza kuamua kubadilisha muda wa kufuatilia Habari kutoka asubuhi hadi jioni ili kuepusha kuharibu siku yako. Ili ufanikiwe kwenye adhima hii, kuna programu ambazo unaweza kujaribu kujidhibiti kuzitumia kwenye simu yako ya mkononi.
Nyamazisha akaunti zozote za kuchochea kufuatilia taarifa. Nimetangulia kusema kuwa tofauti na zamani siku hizi taarifa zipo mkononi mwako ikiwa una simu janja. Siku hizi pia kuna TV Mtandao (Online TV) na ipo mitandao ya kijamii, vyanzo vyote hivi vinaendelea kukuza urahibu (addiction) kati yetu wa kuendelea kufuatilia yanayojiri kwenye jamii. Mbaya zaidi ni kwamba taarifa nyingi zinazotolewa kupitia majukwaa mengi kwa sasa haririwi. Kila mtu anaandika na kurusha kwenye mtandao ambao ana wafuasi wake. Ili kuepuka usumbufu wa kutoka kwebye mitandao ya kijamii unaweza kuhakikisha mitandao yote ya kijamii unaiweka kwenye mfumo tulivu (silent mode). Au unaweza kupunguza mitandao ya kijamii ya kuifuatilia.
Ikiwa
unasumbuliwa na magonjwa ya afya ya akili, jiweke mbali na Habari. Ikiwa
haujisikii vizuri kiakili, iwe ni kwa sababu ya hali ya afya ya akili au unapitia
wakati mbaya kwa ujumla, basi fikiria kujiweka mbali na taarifa za Habari kama
sehemu ya tiba. Kuendelea kufuatilia taarifa za Habari katika kipindi ambacho
haujisikii vizuri kiafya inaweza kupelekea afya yako kuwa mbaya zaidi kutegemeana
na jinsi unavyopokea taarifa husika.
Mwisho, kupitia neno la tafakari ya leo tumejifunza hatua ambazo tunaweza kuchukua ili kujiepusha au kuishi katika Ulimwengu wenye urahibu na taarifa hasi na chonganishi. Tunao uwezo wa kuchambua taarifa za kulisha ubongo, hivyo hakikisha unatumia uwezo huo kudhibiti athari ya taarifa hasi katika maisha yako ya kila siku. Kumbuka, mbegu ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Ongeza maarifa yako kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu
Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com