Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku nyingine
tumebahatika kuamka salama. Ni matumaini yangu kuwa upo salama na umeanza majukumu
ya siku kwa ajili ya kuendeleza pale ulipoishia jana. Kila mara naendelea
kukumbusha kuwa njia pekee ambayo itakufikisha kwenye mafanikio makubwa ni
kufanya vitu vyenye mwendelezo au muunganiko. Ikiwa unagusa gusa mambo mengi
kwa wakati mmoja ni dalili kuwa hautoweza kupata mafanikio makubwa zaidi.
Jiunge na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uhakika wa kupata neno la tafakari kila siku, tafadhali JIUNGE SASA.
Karibu katika neno la tafakari ya leo ambapo tutafakari umuhimu wa kutafuta pesa katika mazingira ambayo hatukubali kuendekeza pesa itawale kila sekta ya maisha yetu. Ni dhairi kuwa pesa ndo kila kitu kama ambavyo waenga wetu walisema: “pesa ni sabuni yar oho.” Lakini pamoja na ukweli huo tuna kila sababu ya kujiuliza na kuukubali kuwa: Je! Unatafuta pesa, au unatamani kuwa na furaha maishani? Tambua kuwa “Pesa hainunui furaha”. Ikiwa unaipima furaha yako kwa kiwango cha pesa unachomiliki ambacho unataka kumiliki utagundua kuwa kamwe hautakuja kuwa na furaha katika maisha yako yote.
Watu
wengi wanajitahidi kukusanya pesa kwenye akaunti za benki, uwekezaji, na soko
la hisa. Pamoja na kufanya hivyo, kwa nini kupenda pesa kunatajwa kuwa chanzo
cha maovu yote? Je! Kuna ukweli kuwa kupenda pesa ni kujitumbukiza kwenye uovu
wa maisha? Majibu ya maswali haya yanaweza kuwa katikati ya NDIYO na HAPANA. Pesa
inaweza kuwa chanzo cha maisha ya uovu au pesa inaweza kuwa chanzo cha kuishi
maisha ya kumtukuza na kumpeza Mungu kwa kuwa Mungu hapendi umasikini kwa watu
wake. Ili uishi hakuna ubishi kuwa unahitaji pesa. Ni ukweli kuwa ikiwa hauna pesa
hauwezi kumiliki nyumba, gari au kumdu gharama za chakula na mahitaji muhimu katika
maisha.
Soma: JINSI YA KUBADILI FIKRA KATIKA NYAKATI HIZI 4 ZA MAISHA YAKO.
Pamoja na yote hayo kuhusu umuhimu wa pesa katika maisha yetu ya kila siku, ni lazima uwe tayari kuchora mstari unaotenganisha shughuli za kutafuta pesa dhidi ya mahitaji yako muhimu katika maisha. Ni nadra sana kutegemea mtu asimamie majukumu yako kwa ufanisi katika masuala yanayohusu familia yako au ndani ya jamii. Tambua kuwa pesa pesa haitoshika mkono wako wakati unaumwa na kukupa faraja kama ambavyo utafarijiwa na wapendwa wako. Wala pesa hautazikwa nayo siku ya mazishi yako sana sana itabaki na kuendelea kugombanisha Watoto wako. Hebu kwa pamoja tutafakari tabia zifuatazo kama ni sehemu ya maisha yako:-
Tabia #1: Unatumia muda mwingi kufanya kazi kuliko kujali afya yako. Ikiwa unathamini kazi kuliko kutunza mazingira ya afya yako ni dalili moja wapo kuwa unaendekeza kutafuta pesa kuliko kujali afya yako. Unaendekeza kutafuta pesa kiasi ambacho hauna hata muda wa kutosha kwa ajili ya kulala. Unaendekeza kufanya kazi wakati ambao kuna dalili za ugonjwa ambao haujui tatizo ni lipi, hila kwa kuwa haujafikia kiwango cha kukuzuia kufanya kazi unaendelea na shughuli zako. Unaweza kushangaa mtu huyo huyo ana hela nyingi lakini hana hata bima ya afya ambayo ingemsaidia kupata matibabu wakati anapoumwa.
Tabia #2: Umejikita kwenye umiliki wa vitu. Nitakuwa na furaha siku nikimiliki gari, nitakuwa na furaha siku nikiwa baba au mama mwenye nyumba, au nitakuwa na furaha siku nikiweza kula nyama kila siku. Yamkini siku ukiwa na uwezo wa kumiliki au kupata vitu hivyo unajikuta kuwa ni vitu vya kawaida na havija kufikisha kwenye tumaini la maisha ya furaha ulilokuwa nalo awali. Hivyo, badala ya kuweka lengo kuu la maisha yako kwenye kukuza utajiri wako hakikisha una lengo ambalo litakuwezesha kutumia hazina kuu iliyopo ndani mwako kwa manufaa ya nafsi yako na jamii inayokuzunguka na pesa zitakufuata.
Tabia #3: Kazi kwanza familia na marafiki baadae. Ikiwa kipaumbele chako namba moja ni kazi mbele ya familia na marafiki ni dalili nyingine kuwa unaifukuzia pesa zaidi katika maisha yako. Pamoja na kazi unahitaji kuwa na muda kwa ajili ya kukaa pamoja na familia au kufarahi pamoja na marafiki. Watoto wanahitaji kucheza na wewe kwa maana katika michezo hiyo utagundua kalama nyingi zilizopo ndani mwao. Pia, kupata muda wa kuwa na familia yako kila mmoja ndani ya familia kuna kitu tajifunza kutoka kwa mweza wake, Watoto wanahitaji kujifunza kutoka kwa wazazi wao.
Tabia #4: Hauna hobi nje ya kazi. Nje ya kazi kuna vitu vingi ambavyo vinasaidia kuamsha hisia za furaha katika maisha ya kila siku. Unahitaji kugundua hobi zako ili ziwe sehemu ya kukuburudisha nyakati ambazo umetoka kwenye majukumu yako ya kazi au nyakati ambazo umepumzika na familia. Fikiria kuhusu kutembelea mbuga za Wanyama ikiwa una hobi ya kutembea. Au fikiria kuhusu michezo mbalimbali.
Tabia #5: Unafanya kazi kiasi cha kusahau kupata chai au chakula. Wakati mwingine watu wanashindwa kupata chai, chakula au maji ya kunywa kwa imani kuwa wanabana matumizi. Hiyo hela unaitafuta kwa ajili ya nini ikiwa hata hauwezi kuitumia kwa ajili ya kuboresha afya yako? Ni kweli kila mara nakuhamasisha umuhimu wa kuiheshimu pesa ili na yenyewe ipate kukuheshimu, lakini katika kupanga bajeti hakikisha unaweka vipaumbele muhimu kukuhusu wewe na familia yako.
Tabia #6: Unaendelea kuitumikia kazi unayoichukia. Asilimia kubwa ya watu katika jamii wanafanya kazi au biashara ambazo hawazipendi hila wanaendelea kuzitumikia kwa kuwa wanahitaji pesa. Hii pia ni dalili kuwa wewe ni mtumwa wa pesa japo hujitambui kuwa ni mtumwa kama watumwa wengine.
Tabia #7: Muda wote mazungumzo yako ni kuhusu pesa. Mara nyingi watu hupata shida kuzungumza na wewe kwa sababu mazungumzo yako yote yanahusu pesa. Ikiwa hauwezi kutofautisha aina ya kundi unalongea nalo ili kuchuja mazungumzo yako. Zipo nyakati ukiwa na marafiki zako muda wote unajikita kwenye kuzungumzia mambo ya kazini kwako wakati hakuna ambaye anahitaji kusikiliza hadithi zako. Mazungumzo ya aina hii yanachosha kwa wale ambao wana ajenda ya kuwa na furaha katika maisha badala ya kuendekeza pesa kama chanzo cha furaha.
Tabia #8: Unadharau watu ambao hawana pesa au kazi. Fanya tathimini inayolenga kugundua namna unavyohusiana na watu wanaokuzunguka. Je! Una muda wa kuongea na majirani zako bila kuangalia viwango vya maisha yao? Je! Muda mwingi unautumia kushirikiana na watu wenye hali kama yako na kudharau makundi mengine? Je! Unawapa nafasi sana matajiri na watu wenye umaarufu ikilinganishwa na watu wa kawaida?
Tabia #9: Thamani yako inapimwa na pesa. Ikiwa kila mara unafikiria kuwa uthamani wa maisha yako upo katika pesa ni dalili kuwa unakimbiza na pesa na kusahau vitu vingine. Mfano, ikiwa hauna pesa ya kutosha kutoa kwa familia, basi unajiona hauna thamani. Au, kila mchango unaotoa kwa watu wengine unaupima kwenye thamani ya pesa.
Tabia #10: Hautosheki na hali uliyonayo au vitu
unavyomiliki. Ikwa
hauwezi
kukumbuka ni lini katika maisha
yako umewahi kuridhika na kile ulichonacho hasa kwenye umiliki wa fedha na mali. Ikiwa hauna kikomo ulichojiwekea juu ya kiwango chako cha kuridhika, kwani kila wakati unataka zaidi. Zote hizo ni dalili kuwa umetawaliwa na pesa. Kwa asili
tumeumbwa kutaka zaidi ya kile tulichonacho lakini ili udhibiti hali hiyo ni
lazima utambue ni wapi unataka kufika.
Mwisho, kupitia neno la tafakari ya leo tumejifunza tabia 10 ambazo zinaelezea ikiwa tumeyatoa maisha yetu kwa ajili ya kufukuzia pesa muda wote. Maisha ni zaidi ya kutafuta pesa, yapo mengi mazuri ya kufurahi na kujivunia kuhusu uumbaji wa Mungu nje ya kujikita kwenye kufikiria pesa muda wote. Kumbuka, mbegu ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganishi hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema OFA hii.
👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu
Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com