SIFA 7 ZA WATU SUMU KATIKA MAISHA YAKO

NENO LA LEO (APRILI 3, 2021): [BURIANI JPM] SIFA 7 ZA WATU SUMU KATIKA MAISHA YAKO

Habari ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku mpya katika siku za uhai wetu hapa Duniani. Ni siku ambayo kama taifa tunaingia kwenye siku ya 17 kati ya siku 21 za maombolezo ya kifo cha mpendwa wetu, shujaa wa Afrika, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kupitia msiba huu naendelea kukushirikisha masomo ambayo yanalenga kukuimarisha kimwili na kiroho katika siku chache ambazo kila mmoja wetu ameandikiwa kuishi kwenye ulimwengu huu.

 Kama bado hujajiunga na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la tafakari kila siku, tafadhali JIUNGE SASA. 

Katika neno la tafakari ya leo nitakushirikisha sifa za watu sumu kwa ajili ya hustawi wa maisha yako. Katika mafundisho ya majuto kwa watu wanaokaribia kukata roho tuliona kuwa wengi huwa wanajutia kupoteza muda na rasilimali kutokana na kuendekeza au kusikiliza makundi ya watu. Watu sumu ni wengi na wengine tunajumuika nao kila mara japo hatutambui jinsi wanavyoathari maisha yetu katika kufikia mafanikio tunayotamani.

 SOMA: MAJUTO KWA WANAOKARIBIA KUKATA ROHO – SEHEMU YA MWISHO 

Mwandishi wa kitabu cha “Emotional Intelligence” Travis Bradberry (Ph.D) ananukuliwa katika kitabu hicho kuwa: "Iwe ni uzembe, ukatili, ugonjwa wa mwathiriwa, au ujinga tu, kundi la watu sumu wana uwezo wa kuendesha ubongo wako katika hali ya msongo ambayo inapaswa kuepukwa kwa gharama yoyote." Kulingana na saikalojia ya sasa, watu sumu wana baadhi au zaidi ya sifa zifuatazo:-

Sifa #1: Wana uwezo mkubwa wa kudanganya. Mara nyingi watu sumu huwa wanajifanya kujua kila kitu kuhusu maisha. Katika hali hiyo wako radhi kukudanganya na hatimaye kukutoa kwenye kile unachoamini ili mradi waendeshe akili yako. Athari yake ni kwamba ikiwa utakubali kudanganyika utajikuta umeacha mawazo au vitendo ambavyo ulidhamiria vikufikishe kwenye hitaji lako kwa wakati husika.

SOMA: TABIA 10 AMBAZO HUTOJUTIA KUZIISHI MAISHANI MWAKO

Sifa #2: Wanahukumu. Watu sumu mara nyingi huwa ni wepesi wa kutoa hukumu hata kabla ya kujua undani wa tukio husika. Mara nyingi huku zao huwa zinatolewa kulingana na mtazamo na uelewa wao. Kutokana na hukumu hizo unaweza kujiona mwenye makosa hali ambayo itapelekea kupoteza mwelekeo kimaisha. Hali hii ya kuhukumiwa na kudharauriwa inaweza kukufanya uamini katika kile unachohukumiwa na matokeo yake ni kupoteza uwezo wa kujiamini na kufifisha tumaini la baadae katika maisha.

Sifa #3: Wanatanguliza matakwa na mahitaji yao binafsi. Mara zote watu sumu wanatanguliza matakwa yao kuliko maslahi mapana ya kundi au wahusika kwenye mahusiano husika. Watu wa aina hii watakuwa karibu yako wakati wana uhitaji kutoka kwako lakini katika kipindi ambacho unahitaji msaada kutoka kwao watajiweka mbali na wewe. Mara nyingi watu wa aina hii watakupigia au kukutembelea nyakati ambazo wanahitaji msaafa wako. Katika hilo, watu hawa wapo tayari kufanya lolote ili mradi tu watimize mahitaji yao.

Sifa #4: Watajaribu kukubadilisha ili uendane na tabia zao. Mtu yeyote ambaye anahitaji kukubadilisha kitabia ili uwe sawa na tabia zake kabla ya kumfuata unatakiwa uchunguze nia yake kwanza. Rafiki wa kweli ni yule ambaye anatambua na kukubali kuwa watu wana haiba, fikra, mtazamo au tabia tofauti.

Sifa #5: Watakushusha au kukufanya uchekwe mbele za watu. Kutokana na tabia ya watu sumu kujipandisha katika kila hali, wanalazimika kushusha kila mtu ambaye anaonekana kuwa hatari kwao. Ikiwa unaonekana hatari kwao watakutafutia kila aina ya kashfa ili mradi tu kushusa umaarufu wako. Wanafanya hivyo kama mbinu ya kuficha maovu yao.

Sifa #6: Wanachukia mafanikio yako. Watu wa aina hii kadri unavyofanikiwa ndivyo wanakutafutia vikwazo vya kukuharibia. Kwa ujumla mafanikio yako yanakuwa ni sehemu ya machukizo kwao. Na katika hilo wana welevu mkubwa wa kutambua njia unazopitia na namna ya kukukwamisha kufikia mafanikio zaidi.

Sifa #7: Ni wasumbufu. Mara zote wanataka kila jambo lifanyike kwa utaratibu wanaotaka wao. Ni ukubaliane na njia yao au hakuna njia. Hawana suluhu na hawako tayari kurekebisha njia au mbinu zao ili kuendana na mipango yako. Akili yao ni ngumu kubadilika ili kuendena na matakwa ya watu wengine.

KUJIUNGA NA PROGRAMU MAALUM YA "JILIPE KWANZA": SOMA MAKALA HII KWA KUBONYEZA MAANDISHI HAYA YENYE RANGI   

Mwisho, katika neno la tafakari ya leo nimekushirikisha sifa 7 za watu sumu katika maisha yako. Tumia sifa hizo kutambua watu sumu katika maisha yako ya kila siku kuepuka majuto katika maisha yako. Kumbuka, mbegu ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.

PS:  Ongeza maarifa yako kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.

👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾

BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU

 

BORN TO WIN ~ DREAM BIG

Mwalimu Augustine Mathias

Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410

Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com
onclick='window.open(