Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku mpya
ambayo naamini tumeamka salama na tupo tayari kuendeleza jitihada za kuboresha
maisha yetu. Leo hii tunaingia siku ya 19 kati ya siku 21 za maombolezo ya kifo
cha mpendwa wetu, shujaa wa Afrika, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Katika
neno la tafakari ya jana tujifunza kuhusu kauli ambazo watu sumu wanatumia
kupunguza uwezo wa kujithamini kwa watu wengine. Pia, katika mafundisho
yaliyopita tuliona kuwa watu wengi katika kipindi cha kukata roho wanajutia
kuishi maisha ambayo hawakuweza kudhihirisha uwezo wao halisi katika kipindi ambacho
walikuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Katika neno la tafakari ya leo tutajifunza
tabia 5 ambazo zitakuongezea uwezo wa kujithamini ili kwa kufanya hivyo upate
uwezo wa kujiamini zaidi (self confidence) katika kila unachofanya.
SOMA: KAULI 6 AMBAZO WATU SUMU WANATUMIA KUKANDAMIZA UWEZO WAKO WA KUJITHAMINI
Kwa ujumla uwezo wa kujiamini unajumuisha mtazamo wako kuhusu ujuzi na uwezo wako. Inamaanisha unajikubali na unajiamini na unaweza kudhibiti hisia zako katika maisha ya kila siku. Unajua uwezo na madhaifu yako vizuri, na una mtazamo chanya juu ya nafsi yako. Kutaokana na tafsiri hii, kupitia ikiwa una kiwango cha juu cha kujiamini tunategemea unaweza kuwasiliana na wengine kwa ujasiri, unaishi matarajio na malengo yako halisi, kukosoa wengine na kuwa tayari kukosolewa au kujifunza na unachukulia madhaifu yako kama changamoto ya muda ambayo umedhamiria kuitatua. Karibu tujifunze kwa pamoja tabia ambazo zitaongeza uwezo wetu wa kujiamini:-
Tabia #1: Jifunze kutunza mwili wako. Ikiwa hauna tabia ya kutunza mwili wako ni vigumu kujiamini maana mwonekano wa mwili wako una nafsi kubwa katika kujiamini mbele za watu. Unapokuwa unautunza vyema mwili wako kwa kuzingatia kanuni za kulinda mwili wenye afya bora moja kwa moja akili, mwili na roho kwa pamoja vinajenga hali ya kujiamini zaidi. Unaweza kutunza mwili wako kwa kuzingatia ushauri huu:-
Zingatia mlo sahihi. Mlo sahihi una faida nyingi kwenye mwili sambamba na kuongeza viwango vya juu vya kujiamini na kujithamini. Unapoulisha mwili wako chakula kizuri unajihisi kuwa na mwili wenye afya, nguvu, na mwonekano mzuri hivyo kupelekea kila mara kujivunia mwili wako. Hali hiyo inakuongezea uwezo wa kujiamini.
Kufanya mazoezi ya viungo. Tafiti zinaonesha kuwa watu wanaofanya mazoezi ya viungo wanakuwa na ujasiri zaidi ikilinganishwa na watu ambao hawana mazoezi. Mazoezi ya viungo yanasaidi mwili wa mhusika kujengeka na kuimarisha vyema misuri hali inayopelekea wahusika wajiamini zaidi. Pia, mwili wenye mazoezi ya viungo ni nadra kushambuliwa na magonjwa ya mara kwa mara.
Kufanya tajuhudi (Meditation). Kama ambavyo tumeona kwenye umuhimu wa mazoezi ya viungo ndivyo ilivyo kwenye mazoezi yanayohusisha akili. Tajuhudi ni zoezi au tabia inayohusisha kiwango cha juu cha kutafakari kuhusu maisha yako kwa ujumla. Kupitia tabia hii unaweza kujitambua wewe ni nani, unatakiwa kuishi maisha yapi na kwa nini maisha hayo. Hali hii itakuongezea uwezo wa kujikubali na kujithamini zaidi. Pia, kupitia tajuhudi utafanikiwa kuachana na mitazamo hasi kuhusu wewe mwenyewe na mazingira yanayokuzunguka.
Kuwa na muda wa kutosha kwa ajili ya usingizi. Muda wa kutosha kwa ajili ya kupumzika ni tiba tosha kwa ajili ya mwili wenye afya. Usingizi unaweza kupelekea ushindwe kutimiza majuku yako kwa ufanisi, kutokana na kuwa na mwili uliosinyaa kila mara.
Tabia #2: Jifunze kujiongezea maarifa kupitia usomaji. Kujisomea maarifa mbalimbali ni tabia ambayo itakuwezesha akili yako isizeeke haraka. Kupitia tabia hiyo unaongeza uwezo wa kujiamini zaidi kwenye kila sekta ya maisha yako kwa kuwa unakuwa na taarifa, ujuzi na maarifa sahihi yanayoendana na wakati uliopo. Chochote unachosoma iwe hadithi za ukweli na uongo, historia, vitabu kuhusu viumbe, tamthilia, vitabu vya maarifa mbalimbali au mafundisho ya vitabu vya dini, una nafasi ya kujiimarisha zaidi kimwili, kiakili na kiroho. Kupitia usomaji unapata nafasi ya kutafakari, kupitia usomaji unatapa nafasi ya kuachana na mawazo hasi, na kupitia usomaji unajifunza kuhusu wewe mwenyewe, watu wanaokuzunguka na mazingira yanayokuzunguka kwa ujumla wake.
Tabia #3: Hama kutoka kwenye ukanda wa faraja (Comfort zone). Inaweza kushangaza au kuwa ngumu, lakini unapoondoka kwenye mazoea ya awali inakuwezesha kutafuta changamoto mpya. Katika mazingira mapya na changamoto mpya unajifunza mambo mengi ambayo yatakuwezesha kujiimarisha zaidi kimaisha ikilinganishwa kama ungeendelea kuishi kwa mazoea. Hivyo, kila mara unatakiwa kujipa changamoto mpya kwa ajili ya kuongeza uzoefu wako kwenye kila sekta ya maisha. Kwa kufanya hivyo utafanikiwa: kuongeza ujuzi na kujifunza maarifa mapya; kutambua uwezo wako halisi katika kutatua changamoto za kimaisha; kupanua mtazamo na uelewa wako kuhusu maisha; na kuongeza ujasiri wako.
Tabia #4: Tumia nguvu ya mazungumzo chanya ndani ya nafsi. Mazungumzo chanya kuhusu nafsi yako yanakuwezesha kukuza matumaini, kukuza kiwango cha huruma, kuondoa shaka, kuchukua changamoto mpya, na kuepuka makosa. Kwa upande mwingine, mazungumzo hasi kuhusu nafsi yako yanaweza kupunguza uwezo wako wa kufanya kazi, au kupunguza ujasiri wako. Hali hii inatokana na ukweli kwamba mazungumzo hasi yana asili ya kushawishi ujione kuwa "hauwezi kushughulikia" au “kuona ugumu” katika kila kitu na kufifisha "ubunifu na morali ya kujaribu." Ukiwa katika kundi la watu kabla ya kuanza kuchangia mada iliyopo mezani anza kwa kuchangia mada husika ndani ya nafsi yako kwa kutazama ufahamu wako kuhusu mada husika. Tafakari kuhusu mifano hii michache:
Badala ya kusema "Siwezi kushughulikia hili," au "Hii haiwezekani," jaribu kujikumbusha kwamba "Ninao uwezo wa kufanya…..," au "Ninachopaswa kufanya ni kujaribu kwanza kabla ya kuhitimisha kuwa siwezi.";
Badala ya kujisemea "siwezi kufanya chochote sahihi hasa baada ya kushindwa" kila mara unapokosea, jikumbushe kwa kujisemea "Kuanguka mara kwanza ni mwanzo wa kufungua nafasi za kufanya vizuri zaidi wakati ujao” au “pamoja na kutofanikiwa angalau sijapoteza muda, nguvu na rasilimali maana nimejifunza mengi”.
Tabia
#5: Kubali na sherekea tofauti zako. Wakati mwingine, tofauti zako ukijilinganisha
na wengine zinaweza kuwa ndio chanzo cha kutokujipenda, kujikubali au kujithamini
mwenyewe. Unaweza kuwa unajilinganisha na wengine, lakini unajiona haufikii
viwango vyao kutokana na nadharia ambazo umeweka kichwani mwako kuhusu watu hao.
Tatizo ni kwamba kadri unavyoangalia mazuri ya wengine unasaha kunagalia mazuri
uliyonayo badala yake unaishia kuangalia mabaya yako pekee. Wakati unafanya
hivyo na kuishi kujidharau wapo watu wengine ambao wanatamani wangefanikiwa kupata
mazuri yako. Fikra za namna hii ni sumu kwa maendeleo yako maana kila mara
utaendelea kufifisha uwezo wako halisi. Kumbe, unatakiwa kutambua kuwa tofauti
zetu ni jambo la kawaida maana wote hatuwezi kuwa sawa. Tofauti hizo ndizo
zinachochea mafanikio kati yetu katika makundi ya kijamii tunayoishi. Udhaifu
wako ni nguvu na tija kwa mtu mwingine, na mazuri yako pia ni tija kwako na
watu wengine. Sherekea tofauti zako na
tofauti za wengine ukitambua kuwa Wewe ni wa kipekee, na wa aina yake na
tofauti zako ni sehemu ya upekee wako katika kufanikisha kusudi kuu la Muumba
wako.
Mwisho, kupitia neno la
tafakari ya leo nimekushirikisha tabia 5 ambazo zitakuwezesha kuongeza uwezo
wako wa kujithamini na kujiamini. Tumia tabia hizo kila mara na hakika utaona
tofauti ndani ya muda mfupi. Kumbuka, mbegu ikidondoka ardhini ni
lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia
neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Ongeza maarifa yako kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu
Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com