Uchambuzi
wa Kitabu cha Homo Deus – A Brief History of Tomorrow: Utabiri wa Historia ya
Kesho kutokana na maendeleo ya mwanadamu
Habari rafiki yangu mpendwa
ambaye umeendelea kujifunza maarifa mbalimbali kupitia kupitia Makala zangu za
uchambuzi wa vitabu. Katika kipindi cha mwaka 2021 nimepanga kusoma vitabu 12
na vitabu vyote nitahakikisha nakushirikisha sehemu ya uchambuzi au uchambuzi
wote ili kwa pamoja tupate kujifunza maarifa yanakayosaidia kuboresha maisha
yetu. Karibu katika uchambuzi wa kitabu cha kwanza katika kipindi cha mwaka
2021. Husisite kuchangia kazi hii kwa kununua nakala za uchambuzi wa vitabu
mbalimbali.
Kama bado hujajiunga na kundi
letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la tafakari kila
siku, tafadhali JIUNGE
SASA.
Kitabu ninachokushirikisha
kupitia makala hii ni “Homo Deus: A Brief History of Tomorrow”
kutoka kwa mwandishi Yuval Noah Harari. Kwa kifupi mwandishi wa kitabu
hiki ni mwandishi maarufu ambaye ameandika vitabu vingi ambavyo vimefanya vyema
kwenye soko. Moja kitabu chake ambacho nimesoma na kupenda kazi zake ni Homo
Sapiens: A Brief History of Humankind. Kupitia kitabu hiki mwandishi
anatushirikisha historia ya mwanadamu toka kuumbwa kwa ulimwengu mpaka nyakati
ambazo aliandika kitabu (ikiwa unahitaji kunufaika na mabadiliko yanayotokea
kwenye historia ya maendeleao ya mwanadamu, nakushauri usome kitabu hiki).
Soma: Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha A Brief History of Humankind (Historia Fupi ya Mwanadamu)
Kupitia kitabu ambacho
nakushirikisha kupitia Makala hii, Mwandishi anatumia maneno ya Kilatini “Homo”
kumaanisha Mwanadamu na “Deus” kumaanisha Mungu kwa maana
yeye anahusika moja kwa moja na uwezo wa mwanadamu katika historia ya maendeleo
yake kwenye uso wa Dunia. Hivyo, kupitia kitabu hiki Mwandishi anaelezea uwezo
wa mwanadamu wa sasa kupitia mafanikio yaliyopo na kujaribu kujenga picha ya
mafanikio ya siku zijazo. Amejadili masuala mengi ya falsafa kama vile
ubinadamu, ubinafsi na vifo.
Karibu ushirikiane nami kujifunza machache kati ya mengi
ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:
1. Katika historia ya maendeleo
ya mwanadamu, mwanadamu amepitia kipindi ambacho ajenda kuu ya siku ilikuwa ni
namna ya kukabiliana na matatizo makuu matatu ambayo ni: Njaa, Milipuko ya
Magonjwa au majanga ya asili na Vita. Vizazi na vizazi, mwanadamu pamoja na
kutumia kila mbinu ikiwemo ya maombi kwa Mungu na miungu ya kila aina, mamilioni
ya watu waliendelea kufa kutokana na matatizo hayo matatu. Matatizo haya katika
kipindi cha mwanzo wa millenia ya kwanza baadhi ya Wanafalsafa walifikia hatua
ya kusema kuwa yawezekana ni sehemu ya mpango wa Mungu katika kudhibiti idadi
ya watu, hivyo hakuna njia yoyote ambayo inaweza kumuepusha mwanadamu na matatizo
hayo.
2. Hata hivyo, katika kipindi
cha miaka ya hivi karibuni mwanadamu ameweza kukabiliana na matatizo hayo
matatu kiasi ambacho siyo tatizo la kidunia tena. Kwa sasa mwanadamu anafahamu
nini anatakiwa kufanya kwa ajili ya kuepuka changamoto ya njaa, magonjwa au
majanga ya asili na athari za kivita. Kutokana na mafanikio hayo, nyakati hizi
tunashuhudia wanadamu wengi wanaokufa kutokana na magonjwa ya shibe
iliyopitiliza ikilinganishwa na wale wanaokufa kwa njaa; tunashuhudia wengi
wanakufa kwa uzee/makosa ya jinai ikilinganishwa na Watoto wanaokufa kwa
magonjwa kama ilivyokuwa zamani; na tunashuhudia idadi ya wanaojinyonga
inaongezeka ikilinganishwa na wale wanaokufa kutokana na athari za kivita.
3. Kuhusu tatizo la njaa,
historia inaonesha kuwa Mwanadamu amepitia kipindi ambacho kutokana na umasiki
idadi kubwa ya watu walikufa kutokana na ukosefu wa chakula. Katika nyakati
hizo kosa dogo au mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yangeathiri mazao ilitosha
kuteketeza familia nzima kwa ukosefu wa chakula. Historia inaonesha kuwa
takribani asilimia 5 hadi 10 ya Wamisri au India iliteketea kutokana na ukame. Katika
kipindi hicho miundombinu na vyombo vya usafiri ilikuwa changamoto hivyo
ilikuwa ni ngumu kuokoa jamii ambayo ilikabiliwa na changamoto ya njaa. Katika
kipindi hicho njaa ilikuwa ni ajenda ya kidunia kwenye kila bara, na silaha kuu
ya mwanadamu ilikuwa maombi, Ee Mwenyezi Mungu tuepushe na njaa au tuwezeshe
kupata chakula cha siku. Hata hivyo, njaa kwa sasa siyo changamoto ya kidunia
tena kutokana kukua kwa miundombinu ya uzalishaji pamoja na usafirishaji. Hali
hii imepelekea jamii ya sasa kuangamia kutokana na shibe iliyopitiliza
ikilinganishwa na wanaoangamia kwa njaa.
4. Baada ya njaa adui mkubwa wa
mwanadamu katika historia ya maendeleo ya mwanadamu alikuwa ni majanga ya asili
kama vile milipuko ya magonjwa na magonjwa ya kuambukiza. Mwanadamu wa
wakati huo usamalama wa afya kwa siku ya leo haukutosha kumpa uhakika wa kuwa
salama kesho yake. Mwanadamu alijua wazi kuwa kesho naweza kuumwa na kufa
kutokana na magonjwa. Historia inaonesha kuwa katika miaka ya 1330 katika
maeneo ya bara la Asia, Ulaya na Kasikazini mwa Afrika takribani watu milioni
75 hadi 200 walikufa kutokana na janga kubwa la tauni. Katika bara la Ulaya
takribani watu wanne kati ya kumi walikufa kutokana na tauni. Zipo sehemu
ambazo takribani ya nusu ya idadi ya watu katika sehemu hizo iliangamizwa na
tauni. Jamii ya kipindi hicho haikuwa na mbinu mbadala za kupambana na mlipuko
huo zaidi ya kutegemea sara na makusanyiko ya pamoja achilia mbali uwezo wa
kuponya. Ukiachilia mbali athari za mlipuko wa tauni, historia ya mwanadamu
inaonekana kupitia kwenye majanga ya milipuko ya magonjwa na magonjwa ya
kuambukiza. Fikiria kuhusu magonjwa kama vile Polio, UKIMWI, Malaria, Ebola,
Mafua ya ndege, Mafua ya nguruwe, na mengineyo ambayo yaliua maelfu ya watu
katika kila kona ya Dunia. Hata hivyo, Mwanadamu wa karne ya sasa ameonesha
uwezo wa kupambana na magonjwa hayo kwa kuwezesha ugunduzi wa chanjo au tiba
dhidi ya magonjwa husika.
5. Kuhusu vita, historia
ya maendeleo ya mwanadamu imepitia nyakati ambazo vita ilikuwa ni sehemu ya
ajenda ya kila siku kutokana na uhasama kati ya mataifa. Kila taifa liliwekeza
nguvu na rasilimali ya kwa ajili ya kulinda himaya yake. Katika nyakati hizo
vita ilitokana na tamaa ya kupata mali kwa njia ya mabavu. Njia ya haraka ya
kumiliki ardhi, madini, mafuta au nguvu kazi ilikuwa ni lazima upigane vita na
mtu mwenye umiliki wa vitu hivyo. Hata hivyo, katika Ulimwengu wa sasa vita
katika kila kona ya Dunia inaendelea kupungua kutokana kubadilika kwa mifumo ya
upatikanaji mali. Umiliki wa mali katika karne ya sasa umebadilika kutoka
kwenye umiliki wa rasilimali kama vile ardhi, madini, mafuta au watu (nguvu
kazi) na kuhamia kwenye umiliki wa maarifa. Kwa sasa muhimu siyo ardhi, madini
au mafuta bali unaelewa nini kuhusu rasilimali hizo ndicho kitakufanya uwe
tajiri. Hivyo, msingi wa uchumi wa jamii ya sasa ni maarifa ikilinganishwa na
jamii zilizotangulia ambazo msingi mkuu wa uchumi ulikuwa ni umiliki wa
rasilimali kama mafuta, madini au ardhi.
6. Je baada ya kukabiliana na matatizo hayo makuu kwa
ufanisi mkubwa kiasi ambacho siyo ajenda ya Dunia, ajenda kuu ya mwanadamu
inatakiwa kuwa ipi? Katika ulimwengu wenye shibe, afya, na amani ni kipi
kinahitaji kutawala maisha ya mwanadamu? Katika ulimwengu ambao teknolojia hai
(biotechnology) na teknolojia ya kila aina inakua kwa kasi ni ipi ajenda ya
mwanadamu katika maisha ya kila siku? Pamoja na mafanikio yote ya mwanadamu
katika kudhibiti matatizo makuu matatu, bado mwanadamu wa Ulimwengu wa sasa kuna
sehemu hajafanikiwa kukabiliana na njaa, vita na magonjwa katika baadhi ya
sehemu. Hivyo, matatizo hayo siyo kwamba yameisha kabisa bali yamepungua
kutokana na ukweli kwamba mwanadamu wa karne hii anaweza kukabiliana na
matatizo haya ikilinganishwa na vizazi vilivyotangulia. Hii haimaanishi kupuuza
maelfu ya watu ambao wanakufa kutokana na majanga hayo bali mantiki ya msingi
ni kwamba uwezo wa kukabiliana na majanga hayo umeongezeka kwa mwanadamu wa
sasa. Fikiria idadi ya watu ambao wanaishi chini ya dola moja katika kila kona
ya Dunia, fikiria watu ambao wanakufa kwa UKIMWI, Malaria na magonjwa mengineyo
hasa katika bara la Afrika na mataifa yanayoendelea; na fikiria idadi ya watu
ambao wanakufa kwa vita kutokana na ongezeko la ugaidi katika maeneo mengi ya
Dunia ya sasa.
7. Ushindi wa mwanadamu wa karne
hii katika kukabiliana na majanga hayo matatu kunatoa tumaini la mafanikio kwa
maisha yajayo. Katika karne hii hatuwezi kumlaumu Mungu wala asili ikiwa
tutashindwa kukabiliana na magonjwa, vita au njaa. Hivyo, kwa ushindi huo
mwanadamu wa sasa ana kila nyenzo ambayo anaweza kuitumia kutatua athari za
majanga hayo katika jamii. Hali hii inatokana na ukuaji wa teknolojia ya
mawasiliano ikiwamo ukuaji wa miundombinu ya usafiri, teknolojia ya habari,
teknolojia ya vifaa vya mionzi au afya kwa ujumla sambamba na ukuaji wa ukuaji
wa teknolojia ya mifumo ya ulinzi.
Je ni ipi inatakiwa kuwa ajenda ya mwanadamu wa karne hii?
Ajenda ya mwanadamuwa karne hii inajikita
kwenye mambo yafuatayo:-
8. Siku za mwisho wa maisha. Mwandishi
anatushirikisha kuwa katika karne hii mwanadamu ataanza kupambana na namna
anavyoweza kuepuka kifo. Kila mtu kwa sasa atakuwa anapambana kuhakikisha kuwa
thamani ya mwanadamu ipo kwenye jinsi anavyopambana kurefusha siku uhai wake na
watu wanaomtegemea. Ajenda hii hadi sasa inabebwa na watu wote bila kujali
itikadi zao – sekta ya afya, sekta ya kilimo, sekta ya uhifadhi wa mazingira, wanasheria,
wanasiasa na wasanii wa fani zote wote wamebeba ajenda hii kupitia kazi zao. Haki
ya kuishi ni ya msingi na ya thamani kwa kila mtu mwenye uhai. Katika historia,
kifo kiliendelea kuchukuliwa hakiepukiki na njia ya utakaso wa maisha mapya na
ya milele. Hivyo, kifo kulichukuliwa kama chanzo cha kuingia kwenye maisha mapya
baada ya maisha ya Duniani. Hali hii ilichochewa na maandiko matakatifu kwa madhehebu
yote iwe Ukristo, Uislamu au Hindu. Tafsiri yake ni kwamba kifo kinamuondolea
mwanadamu haki yake ya kuishi.
9. Tofauti na Imani ya kidini, sayansi
na utamaduni wa kisasa kuna mtazamo tofauti kuhusu kifo na maisha. Kifo hakichukuliwi
tena kama fumbo kwa mwanadamu na hakika hakuna mtazamo wa kuwa kifo ni maandalizi
ya maisha ya baadae. Badala yake kifo kinaonekana kuwa ni tatizo la kiufundi
ambalo linatakiwa kutatuliwa ili mwanadamu aendelee kupata haki yake ya msingi –
“haki ya kuishi”. Je wanadamu wanakufaje? Hadithi za zamani na enzi za
kati zilionesha Kifo katika picha ambayo kuna Mtoa roho ambaye alipotaka kuvuna
roho ya mtu atakutana na mtu huyo katika maangaiko ya siku na ghafla anamgusa
begani na kumwambia Njoo! Katika hali ya kushangaa mtu huyo anaomba: “Hapana
siyo sasa, tafadhali! Subiri mwaka mmoja, mwezi, siku au saa! Lakini mtoa roho
anapiga kelele akisisitiza Hapana! Lazima uje sasa. Na hivi ndivyo kifo
kilivyodhaniwa kutokea.
10. Je ukweli kuhusu kifo ni
upi? Katika hali halisi, wanadamu hawafi kutokana na kazi ya Mtoa roho kama
ilivyofhaniwa au kwa sababu ya Mungu aliamuru kifo kiwe mpango wa kuachana na
maisha ya Ulimwengu na kuingia kwenya maisha mapya, badala yake watu wanakufa
kutokana na tatizo flani la kiufundi katika mfumo mzima wa mwili wa mwanadamu. Mfano,
tatizo hilo linaweza kuwa moyo kushindwa kufanya kazi ya kusukuma damu kutokana
na mafuta yaliyoganda kwenye Mshipa Mkuu wa damu (Ateri) au seli za saratani
kuenea kwenye ini. Au bacteria au virusi kuingilia mfumo wa mapafu na hivyo
kupelekea kukosa hewa ya kutosha katika mwili. Hivyo, kifo kinatokana na tatizo
la kiufundi na kila tatizo la kiufundi lina suluhisho la kiufundi. Suluhisho
hilo ndilo ambalo linampa mwanadamu wa karne hii ajenda ya kutafuta namna
ambavyo anaweza kuepuka kifo. Kwa sasa suluhisho hilo bado halijapatikana lakini
mwanadamu wa sasa anawekeza nguvu na rasilimali nyingi kwa ajili ya kupata
suluhisho la kuondoa tatizo la kiufundi linalopekea kifo kitokee. Mfano, tafiti
zinaendelea namna ya kuondoa seli za kansa kwenye mfumo wa ini, mapafu au namna
ya kuweka moyo mpya mara baada ya moyo kushindwa kufanya kazi.
11. Je ukweli uko wapi kuhusu kukwepa kifo? Pamoja
na kwamba wanaoamini katika kutafuta suluhisho la kifo wanamaani kuwa ifikapo
mwana 2100 au 2200 kizazi kitakachokuwepo kinaweza kuishi maisha ya milele au
angalau kuongeza umri wa kuishi hadi miaka 500 ikilinganishwa na umri wa sasa,
bado ni ngumu kuamini kuwa unaweza kuishi bila kufa. Mwandishi anatushirikisha
kuwa tafiti za kuepuka kifo zitaendelea kufanyika lakini itabakia kuwa kila
tafiti itasogeza kizazi kilichopo kwenye tumaini jipya katika kukabiliana na
kifo. Siku za kuishi zinaweza kuongezeka kwa kizazi cha karne ya 21 lakini ni ngumu
kusema kuwa suluhisho la tatizo la kiufundi linalopekea kifo linaweza kupatikana
kwa karne hii. Hivyo, tafiti za kisayansi zitaendelea kusaidia katika kupunguza
vifo katika umri mdogo. Wanasayansi wanaweza kuendelea kuamini katika kutafuta
suluhisho la kifo kwa kuwa tumaini hilo ndilo njia ya pekee ya kuwezesha tafiti
ziendelee kufanyika kwa lengo ya kuboresha zaidi maisha ya mwanadamu.
12. Haki ya kuwa na furaha. Ajenda
kubwa ya pili ya mwanadamu wa karne hii itakuwa ni kutafuta ufunguo wa furaha. Katika
historia, wanafalsafa (great thinkers), manabii na watu wa kawaida walielezea
furaha kama kitu cha muhimu na bora kuliko hata maisha yenyewe. Katika Ugiriki
ya kale mwanafalsafa Epicurus alielezea kwamba kuabudu miungu ni kupoteza muda
kwa kuwa hakuna maisha baada ya kifo, hivyo, furaha ndiyo linatakiwa kuwa kusudi
pekee la maisha. Watu wengi enzi hizo walikataa nadharia ya Epicurus lakini katika
Ulimwengu wa sasa furaha inakuwa ndiyo chaguo la kwa kwa watu wengi. Kutilia shaka
juu ya maisha ya baadae hupelekea wanadamu siyo tu kutotaka kufa bali pia kutaka
furaha katika maisha haya ya kidunia. Kwa mtazamo wa Epicurus, furaha lilikuwa
hitaji na kiu ya mtu binafsi, katika Ulimwengu wa kisasa furaha na hitaji la
watu wote. Ndiyo, maana Serikali zinaweka mipango ya matumizi ya rasilimali
sambamba na kuimarisha ulinzi ili kuwalinda watu wake dhidi ya magonjwa, vita
na njaa. Hauwezi kuwa na furaha ikiwa unakabiliwa na matatizo hayo katika
maisha ya kila siku.
13. Katika karne ya 19 na 20, Watawala
walijikita kwenye kujiimarisha kiuchumi na kinguvu. Mipango mingi iliyofanyika
katika karne hizo ililenga hayo ili kuwa na taifa linalojitosheresha kimahitaji
na imara kwenye ulinzi wan chi. Hudma zote zilizotolewa kwa jamii hazikulenga
kufanikisha furaha ya watawaliwa bali kukidhi malengo makuu ya kiuchumi na
ulinzi. Elimu ilitolewa kwa vijana ili wapate uelewa wa masomo ya hesabu, sayansi
na mengineyo ili iwe rahisi kukabiliana na maadui. Vile vile, huduma za afya
zilitoelewa ili kuimarisha watu wawe na nguvu za kuzalisha sambamba na kuwa na
jeshi imara. Mataifa mengi yalipima ufanisi wake kwa kuangalia ukubwa wa eneo
la utawala, idadi ya watu na ukuaji wa pato la taifa na siyo furaha ya wananchi
wake. Hata hivyo, katika karne hii, Wanafalsafa, wanasiasa na hata wanauchumi
wanapiga kelele umuhimu wa kuhakikisha ukuaji wa pato la taifa uendene na ukuaji
wa furaha ya wananchi.
14. Je kuna uhusiano kati ya uzalishaji na furaha? Ni
wazi kuwa uzalishaji mali ni njia ya upatikanaji wa vitu muhimu kwa ajili ya maisha
yenye furaha japo siyo hakikisho la kuwa na furaha (production is only the means
for happiness, not the ends). Zipo jamii za watu ambazo uzalishaji upo chini
lakini jamii hizo zina furaha ikilinganishwa na jamii zenye uzalishaji mkubwa. Hivyo,
je kadri uzalishaji unavyoongezeka kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya chakula, kadri
uvumbuzi wa kukabiliana na magonjwa na kadri vita inavyozidi kupungua katika
kizazi cha karne hii tutegemee kuwa rufaha itazidi kutawala ikilinganishwa na
vizazi vilivyopita? Siyo kweli! Kuipata furaha siyo kazi rahisi – siyo umiliki
wa vitu, ujali, unywaji, tiba, mapenzi wala umaarufu ambavyo vitakufanya uwe na
furaha maana vyote hivyo vitakupa furaha ya muda tu – ndani mwako baada ya muda
utajikuta unarudia hali ya sononeko/huzuni ya rohoni. Urafiki wa kina na muda
mrefu ndiyo utatufanya tuwe na furaha ya kweli katika maisha. Mambo mengine yanatakiwa
kufanyika kwa kiasi.
Uchambuzi wa kitabu chote utapatikana kwa gharama ya Tshs.
5,000/=. Jiunge na mtandao wa Fikra za Kitajiri kwa KUBONYEZA HAPA.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Mwalimu Augustine Mathias
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com