Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa
ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI
kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 22 katika
kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu nikiwa na
lengo kubwa la kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe
kila sekta ya maisha yako.
Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo
mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujajifunza kitu chochote katika
makala hizi nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye
mambo ambayo umeyazoea.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na
mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao wa fikra za kitajiri moja
kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kabla
ya kuendelea kushirikisha uchambuzi wa kitabu cha leo nitumie muda huu kuomba
radhi kwa kuchelewa kukutelea uchambuzi huu ndani ya wiki iliyoisha jana. Hii imetokana
na sababu zilizo nje ya uwezo wangu kwa kuwa mazingira niliyopo kwa sasa hayana
nishati ya umeme ya uhakika.
Kitabu
cha wiki hii ni “A Brief History of
Humankind” kutoka
kwa mwandishi Yuval Noah Harari.
Mwandishi
ametumia anatumia kitabu kwa ajili ya kutushirikisha matukio muhimu katika
historia ya mwanadamu. Kupitia kitabu hiki utagundua kuwa kadri nyakati
zinavyobadilika ndivyo mwanadamu amekuwa akipitia kwenye mabadiliko mengi ya kimwili,
kiakili na kimaendeleo. Mabadiliko haya yamepelekea binadamu kukabilia na
mazingira kwa mbinu tofauti kulingana na changamoto anazokabiliana nazo kwa
wakati husika.
Kwa ujumla, tunafahamu
kuwa hapo zamani yapata miaka bilioni 13.5 iliyopita muunganiko wa maada
(matter) na nishati kwa uwepo wa muda (time) flani na nafasi (space) kwa pamoja
viliunda umbo ambalo lijulikanalo ‘big bang’.
Historia ya tukio hili ndiyo inatupa sayansi ya fizikia (Physics).
Miaka 300,000 tangu kuumbwa
kwa umbo hilo; maada na nishati vilianza kuunda maumbo yaliyojulikana kama
atomi (atoms) ambazo kwa pamoja ziliunda molekuli (molecules). Historia ya
tukio hili ndiyo inatupa sayansi ya kemia (Chemistry).
Miaka bilioni 3.8
iliyopita katika sayari ya ijulikanayo kama Dunia, molekuli ziliungana kuunda
maumbo yajulikanayo kama viumbe. Historia ya tukio hili ndio inatupa sayansi ya
biolojia (biology).
Yapata miaka 70,000
iliyopita, viumbe katika kundi/aina (species) ya Homo sapiens (hili ndilo jina la kisayansi la binadamu) walianza
kuunda miundo ya kipekee ijulikanayo kama tamaduni. Hatimaye maboresho ya
matukio ya tamaduni katika nyakati tofauti ndiyo yakatupa msamiati wa neno “Historia”.
Hapa ndipo tunaanzia kwa ajili ya kuona historia ya mwanadamu.
Kwa ujumla historia
ya mwanadamu inagawanyika katika makundi matatu ambayo ni (a) mapinduzi ya
utambuzi (Cognitive revolution) ambayo yalianza yapata miaka 70,000 iliyopita,
(b) mapinduzi ya kilimo (agricultural revolution) ambayo ni yapata miaka 12
elfu iliyopita na (c) mapinduzi ya kisayansi (scientific revolution) ambayo
yalitokea yapata miaka 500 iliyopita. Kwa kifupi kitabu hiki kinaelezea namna
ambayo mapinduzi haya kwa pamoja yalivyoathiri maisha ya mwanadamu na mazingira
yanayomzunguka kwa ujumla.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka katika kitabu hiki:
1. Historia
ya mwanadamu inaanzia katika kipindi ambacho mwanadamu alikuwa ni mnyama hasiye
na manufaa. Historia ya mwanadamu inaanzia katika kipindi ambacho mwanadamu
aliishi katika koo ambazo alikaa katika familia za msituni sawa na wanyama
wengine kama sokwe mtu, nyani, tembo na wengineo. Katika kipindi hiki mchango
wa mwanadamu katika kuboresha mazingira yanayomzunguka haupo kabisa. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba katika kipindi hiki mwanadamu aliyategemea mazingira
yamtunze kwa asilimia mia moja pasipo yeye kujishughulisha. Hii inajumuisha
yeye kuishi kwenye mapango pamoja na kutegemea mizizi na matunda kama chakula
chake. Jambo muhimu la kukumbuka ni kwamba kinachomtofautisha mwanadamu na
wanyama wengine ni uwezo wake mkubwa wa kufikiri. Na hii ni sifa ya kipekee
ambayo inawaunganisha wanadamu wote pasipo kujali rangi au matabaka yao. Sifa hii
ndio ilimwezesha mwanadamu kuanza maisha ya kuboresha mazingira kutoka kwenye
kula vyakula vibichi mpaka kwenye ugunduzi wa moto.
2. Kadri
nyakati zilivyopita ndivyo ubongo wa mwanadamu uliboreshwa kupitia vinasaba na
hivyo kupitishwa kizazi kimoja hadi kingine. Katika sayansi kupitia jeni
(genes) vizazi vipya vinarithishwa ubongo ulioboreshwa na hatimaye kufanikisha
maisha ya mwanadamu kuboreshwa kizazi kimoja hadi kingine. Ni kupitia sayansi
hii tunaona mwanadamu alivyoanza ugunduzi katika mazingira yake ikiwa ni pamoja
na kuboresha miundombinu ya kujisitiri (nguo), usafiri (uvumbuzi wa magari na
boti) na mawasiliano. Uvumbuzi huu kuna ukweli kuwa umewezeshwa na uwepo wa
lugha ya mawasiliano kwani tofauti na mawasiliano/sauti za wanyama wengine lugha
ya wanadamu inaweza kuundwa katika maneno ambayo kwa pamoja yanaunda sentensi
na sentensi hizo zinawezesha mazungumzo kati ya mtu mmoja na mwingine na
hatimaye kwa pamoja wanaafikiana juu ya mada husika. Pia, lugha ya mwanadamu
ina upekee wa kuweza kuongelea juu ya vitu ambavyo mwanadamu hajawahi kuona,
kugusa au kunusa.
3. Hatuwezi
kufahamu asili, historia na saikolojia
yetu pasipo kufahamu kwa undani maisha ya chimbuko letu ambalo kwa imani ni
Adam na Hawa. Katika historia hii tunafahamu kuwa mwanadamu alipitia katika
kipindi cha kutangatanga kwa kutegemea nyama, matunda na mizizi. Baadae mwanadamu
akaingia katika kipindi cha kutegemea kilimo na ufugaji na kipindi hiki wanasaikolojia
wanasema kuwa ni kilikuwa na mchango mkubwa kwenye masuala ya kijamii na
saikolojia ya mwanadamu wa sasa. Mpaka sasa tunazungumzia mapinduzi ya viwanda,
teknolojia ya habari na mawasiliano kama sehemu ya mafanikio ya mwanadamu
ambayo amepitia tokea kuumbwa kwake. Hata hivyo pamoja na maendeleo haya
mwandishi anatushirikisha kuwa bado binadamu wa sasa pamoja na kuwa umiliki wa
rasilimali fedha, vitendea kazi na kila kitu lakini bado binadamu huyu hana
furaha na mazingira yake ikilinganishwa na binadamu wa enzi za kutegemea mazingira
kwa asilimia mia.
4. Mtawanyiko
wa watu katika maeneo mengi hasa ambayo yamezungukwa na maji hapo awali ilikuwa
vigumu kwa mwanadamu kufikia maeneo hayo. Ili kufikia maeneo hayo na kuweza
kuyageuza mwanadamu alijifunza ujuzi wa kutengeneza boti ambazo zilimwezesha
kufika kwenye maeneo ya visiwa vingi kama Madagascar na bara la Australia. Kadri
mwanadamu alivyozidi kufungua makazi mapya katika katika maeneo yaliyofichika
ndivyo pia alianza uharibifu wa mazingira ikiwemo kusababisha kutoweka baadhi
ya viumbe kama wanyama wakali na mimea. Kutoweka kwa viumbe hawa pia
kulichangiwa na mabadiliko ya asili ya tabianchi katika maeneo mengi ikiwa ni
pamoja na tabia za viumbe husika hasa kwenye uwezo wao wa kuzaliana na muda wa
kubeba mimba.
5. Mapinduzi
ya kilimo na ufugaji yalilenga kuongeza shibe ya chakula hasa mizizi, nafaka,
matunda na wanyama wa kufugwa kwa ajili ya uhakika wa nyama. Mazao mengi
yaliyolimwa enzi hizo hadi sasa yanalisha idadi kubwa ya watu ni pamoja na
mazao ya nafaka kama ulezi, mtama, mahindi na viazi mviringo. Wanazuoni kwa
pamoja wanakubaliana kuwa mapinduzi ya kilimo yalikuwa ni hatua moja mbele
katika historia ya mafanikio ya mwanadamu. Hii inadhihirisha namna ambavyo
mwanadamu ameweza kuendelea kwa kutumia uwezo wa ubongo wake kutokana sheria ya
asili ya kupitisha jeni (genes) nzuri pekee kutoka kizazi kimoja cha mwanadamu
hadi kingine. Kadri uzalishaji ulivyoongezeka ndivyo na idadi ya watu
iliongezeka kutokana na ukweli kwamba wakati wa shibe watoto wa kike wana
nafasi kubwa ya kupevuka mapema na hivyo kuzaa mapema ikilinganishwa na wakati
wa chakula kisichotosheleza.
6. Mapinduzi
ya kilimo na ufugaji yalimwezesha mwanadamu kuanzisha makazi ya kudumu na hivyo
kuepuka kuhama hama kwa ajili ya kutafuta chakula. Matokeo yake ilikuwa ni
kuanzisha kazi za usanifu wa majengo kwa kutumia mawe na matope kwa ajili ya
kujisitiri. Hii ilianzisha jamii nyingi kuanza kuishi katika familia zaidi na
kuepuka maisha ya kuishi kama kundi moja. Hatua hii ilimwezesha mwanadamu
aendeleze ugunduzi hasa uliojikita katika kuboresha mazingira yake pamoja na
kuboresha mfumo wa kilimo na ufugaji. Mfano, mwanadamu alianza kujenga nyumba
kwa ajili ya kuishi pamoja na kuanza kutumia wanyamakazi kwa ajili ya kuongeza
ukubwa wa eneo linalolimwa pamoja na kuongeza uzalishaji wa mazao. Ni katika kipindi
hiki pia mwanadamu alianza kujiwekea akiba kutokana na kutokuwa na uhakika wa
misimu inayofuatia katika uzalishaji wa mazao. Uzalishaji wa mazao na mifugo
kadri ulivyoongezeka ndivyo mwanadamu alianza kuwekeza kwenye ugunduzi wa
vyombo vya usafirishaji na hatimaye kukua maeneo ya biashara ambayo yalikuwa
katika miji na hatimaye kuwa majiji.
7. Kadri
uzalishaji ulivyoongezeka ndivyo tabaka ya watawala (machifu) pamoja na dini
zilivyoongezeka. Hii ilipelekea kuanzishwa kwa watawala katika sehemu
mbalimbali na hivyo suala la kujilinda dhidi ya watawala wengine likaanza
kupewa nafasi. Hii ilipelekea uhitaji wa kutunga sheria na kuhakikisha kila
mwanajamii ndani ya utawala wake analinda na kutii sheria husika. Sheria hizi
zilianzisha matabaka ya watala na wataliwa na hivyo uwepo wa watendewa kazi na
watumishi. Mara nyingi sheria hizi zilizirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi
kingine na hivyo kulazimisha umuhimu wa kutunza kumbukumbu muhimu kwa mwanadamu.
Hii ilipelekea mwanadamu kuanza kuwekeza kwenye mifumo yauwekaji wa kumbukumbu
kwa kutumia mfumo wa maandishi na hivyo kuwalazimisha wanadamu kuanza kujifunza
kusoma na kuandika. Hatimaye hii ilipelekea mwanadamu kuanzisha mawasiliano kwa
njia ya namba hivyo kupelekea kuanzishwa kwa mahesabu kwa ajili ya sayansi.
8. Historia
haineshi uwepo wa usawa katika makundi ya mwanadamu. Mwandishi anatushirikisha
kuwa historia ya mwanadamu inaonesha kuwa yalikuwepo makundi wa watu wa ngazi
ya juu, kati na chini. Watu wa ngazi ya juu walineemeka na matunda ya
uzalishaji kutoka kwa watu wa tabaka la chini na kati. Hii ilipelekea
kuanzishwa kwa tabaka la watumwa ambalo lilitumikishwa kufanya kazi zote kwa
ajili ya watu wa tabaka tawala. Hii iliendelea kuweka matabaka mengi katika
jamii, mfano matabaka kati ya, wanaume na wanawake, watu weupe na weusi au
matajiri na masikini. Kwa ujumla chanzo cha matabaka haya ilikuwa ni uongo
ambao uliwekwa na watu wachache kwa ajili ya kujinufaisha wao wenyewe huku
wakiendelea kuwakandamiza wengine.
9. Baada
uonevu wa muda mrefu kati nusu ya karne ya 20 wanazuoni walianzisha kampeni za
kuwa binadamu wote ni sawa. Kampeni hizi ziliambatana na uenezaji wa dini
katika maeneo mengi. Kampeni hizi zilionyesha kuwa kila tamaduni katika jamii
husika ilikuwa na thamani yake, miiko na tamaduni hizi zinabadilika kulingana
na nyakati. Pamoja na kwamba mwanadamu amekuwa na lengo la kutengeneza jamii
moja kubwa yenye tamaduni zinazofanana, jitihada hizo zimekuwa zikigonga mwamba
kwani kila anapokaribia kwenye lengo ndivyo tamaduni nyingine kubwa zinaibuka. Jitihada
hizi zinahusisha nguvu ya dini, lugha na siasa katika kuunganisha watu wa
matabaka mabalimbali.
10. Kuanzishwa kwa matumizi ya madini ya
dhahabu kama kitu chenye thamani kwa ajili ya kubadilisha na bidhaa/huduma
nyingine kulileta mabadiliko makubwa katika historia ya maendeleo ya mwanadamu.
Hapa ndipo sarafu ya dhahabu ilipoanza kuamua nguvu ya uchumi kwani ilikuwa ni
msingi wa kuuza na kununua. Matokeo yake ikawa ni kukinzana kwa wafuasi wa dini
kubwa mbili kati ya Wakatoliki na Waislamu hasa kutokana na utofauti wa sarafu
zilizotengenezwa na pande hizo mbili kwa wakati huo. Sarafu iliwezesha ukuaji
wa uchumi katika maeneo mengi kwani iliweza kuondoa mapungufu ya biashara ya
kubadilishana bidhaa kwa bidhaa au huduma na huduma.
11. Fedha ni zaidi ya sarafu au noti za
benki kwani kwa ujumla fedha inahusisha thamani ya kila ya kitu ambacho watu
wapo tayari kutumia kwa ajili ya kupata kitu kingine na hatimaye kufanikisha
kubadilishana vitu na huduma nyingine. Kwa maana hii fedha inawezesha watu
kulinganisha thamani ya bidhaa/huduma. Kwa maana hii fedha katika mfumo wa
sarafu au noti ni sehemu ndogo ya thamani ya fedha zilizopo kwani fedha nyingi
ipo katika mfumo wa namba na wala sio keshi (noti au sarafu). Fedha inafanya
kazi katika mfumo wa fikra ambao watu wamejiwekea juu ya fedha na mfumo huo
umejengwa juu ya msingi wa uhaminifu kati ya pande mbili husika. Kwa ujumla
katika historia ya maendeleo ya mwanadamu fedha ilikuwa na mchango mkubwa wa kuwaunganisha
watu kutoka pande mbalimbali pindi walipofanya biashara.
12. Fedha ilifanikisha uwepo wa Himaya
mbalimbali katika historia ya maendeleo ya mwanadamu. Kwa ufupi Himaya ni aina
ya Serikali yenye utawala, wataliwa, mipaka pamoja na tamaduni zake ambazo
utumika kama utambulisho wa Himaya husika. Watawala wa Himaya hizi wengi wao
walikuwa na mfumo wa uongozi wa kidektaita japo zipo nyingine ambazo ziliongozwa
kwa mfumo wa kidemokrasia. Mfano wa Himaya za kidemokrasia ni kama Himaya ya
Uingireza. Kwa ujumla Himaya hizi zilikuwa na mchango mkubwa katika historia ya
mwanadamu kwani zilisaidia kuwaleta pamoja watu tofauti na hatimaye watu hawa
wakafanya kazi chini sheria za Himaya yao.
13. Tukiacha mchango wa fedha pamoja na
Himaya katika kuunganisha watu, Dini pia ilikuwa na mchango mkubwa wa
kuunganisha watu matabaka, koo, sehemu na rangi tofauti. Tofauti na dini ya
siku hizi ambayo kwa kiasi imekuwa ni chanzo cha kuwatengenisha watu kulingana
na imani zao, katika historia ya mwanadamu dini ilikuwa na mchango mkubwa kwani
ilifundisha watu kuwa watiifu wa sheria zilizopo pamoja na watu wenye mamlaka. Mchango
mkubwa wa dini ulikuwa wa kufundisha watu kuwa kuna nguvu kubwa iliyoko juu
yenye mamlaka kuliko wanadamu wote. Pia, kupitia mafundisho hayo watu
walihamasishwa juu ya umuhimu wa kuishi maisha ya upendo, amani na usawa pasipo
kujali matabaka wala rangi zao kwani Mungu ni mmoja na Mungu ni Upendo. Kwa maana
hii hauwezi kutaja maendeleo ya mwanadamu pasipo kutaja mchango wa dini ya
Ukristu na Uislamu.
14. Biashara ya bidhaa na huduma, Himaya na
Dini kwa pamoja vilitoa mchango mchango mkubwa wa ukuaji wa uchumi wa
mwabanadamu. Mwandishi anatushirikisha kuwa Mtawala Costantine wa Himaya ya
Roma baada ya kugundua kuwa Himaya yake ilikuwa na watu wenye matabaka na imani
tofauti aliamua kuchagua Ukristu kuwa dini ya Himaya yake. Hapa ndipo tunaona
kuwa Himaya ya Roma ilifanikiwa kuwa Himaya yenye nguvu kubwa kiuchumi kwa muda
mrefu kwa vile watu wake walikuwa chini ya msingi wa Imani moja.
15. Hatuwezi kuzungumzia historia ya
maendeleo ya binadamu pasipo kuangalia mchango wa Mapinduzi ya Sayansi (The Scientific
Revolution). Mapiinduzi ya Sayansi kwa kiasi kikubwa yamebadilisha uso wa Dunia
hii pamoja na viumbe vyote vilivyomo kiasi ambacho mtu aliyekufa kabla ya
mapinduzi haya akifufuka kwa sasa anaweza kuuliza kuwa hapa peponi au kuzimu. Hii
ni kutokana na mabadiliko makubwa ambayo mwanadamu ameyafanya kupitia ugunduzi
wa kisayansi na hatimaye kufanikisha uwepo wa vitu vipya katika mazingira
yanayomzunguka ikiwa ni pamoja na maendeleo katika afya ya mwanadamu. Mapinduzi
haya yameambatana na ongezeko la binadamu katika Dunia. Siri kubwa ya mapinduzi
ya kisayansi imekuwa ni uwekezaji mkubwa wa rasilimali katika tafiti
mbalimbali. Kutokana na ukweli huu mataifa ambayo yamewekeza sana kwenye tafiti
yamefanikiwa kupiga hatua kubwa kiuchumi na hatimaye kufanikisha mabadiliko ya
maisha ya mwanadamu na mazingira yake.
16. Fedha imekuwa
na mchango mkubwa katika kujengeka kwa Himaya nyingi lakini pia fedha hizo
zimekuwa ni chanzo cha kuanguka kwa baadhi ya Himaya. Mwandishi anafafanua kwa
kueleza kuwa katika Himaya nyingi kadri uchumi ulivyoongezeka ndivyo na idadi
ya watu ilivyoongezeka mara dufu na matokeo yake uchumi wa Himaya husika
uliendelea kudumaa na pengine kushuka kabisa. Kinyume na siku za nyuma kwa sasa
fedha imetengenezwa kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa ni kipindi cha nyuma kwa
vile siku hizi kuna uwezekano wa kutumia kipato chako cha siku zijazo katika
matumizi au mipango yako ya sasa (mikopo ya muda mrefu). Msingi wa mafanikio
haya umetokana na uaminifu katika nyakati zijazo, kwa maana nyakati zijazo
zinaaminiwa kuwa zitakuwa na rasilimali za kutosha kwa ajili ya kuwezesha watu
wote kuishi maisha mazuri pasipo kuumizana mmoja baada ya mwingine.
17. Mapinduzi ya mtaji (capitalism) yamefanikisha
mapinduzi katika sekta ya viwanda na hivyo kubadilisha sura nzima ya maisha ya
mwanadamu na mazingira yake. Hata hivyo ni lazima tukumbuke kuwa ili viwanda
viendelee kuzalisha ni lazima pawepo malighafi na nishati. Hivyo endapo
malighafi na nishati vikiisha viwanda hivi havitakuwa na msaada katika
maendeleo ya mwandamu. Hata hivyo mwanadamu ameendelea kuwa mbunifu kwa wa ajili
ya kuepuka upungufu wa malighafi na nishati ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa
panakuwepo mbadala wa nishati au malighafi katika uzalishaji wa bidhaa za
viwandani.
18. Mapinduzi ya viwanda yameambatana na uharibifu
wa mazingira na hivyo kusabisha kutoweka kwa viumbe wa baharini na nchi kavu. Mwandishi
natushirikisha kuwa kadri maendeleo yalivyozidi kushika kasi ndivyo uso wa
dunia umeendelea kupoteza ukijani wake na kugeuzwa sehemu ya mavumbi na
majumba. Uharibifu huu umepelekea mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaendelea
kuhatarisha afya na uhai wa mwanadamu.
19. Pamoja na maendeleo ambayo
yameshuhudiwa katika miaka 500 iliyopita bado mwanadamu wa sasa ameendelea
kuishi maisha yasiyo na furaha ikilinganishwa na binadamu wa kale. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba furaha ya mwanadamu ina uhusiano mkubwa na hisia zake
juu ya yeye mwenyewe pamoja na mazingira yake. Mara nyingi katika jamii watu
wameshindwa kuwa na furaha kwa kuhusisha mahitaji yao na furaha. Kwa maana
nyingine watu wamekuwa wanaishi maisha ya sasa kwa huzuni wakitegemea kuwa
wakipata vitu flani katika maisha yao ndipo wataishi maisha ya furaha. Huu ni
ushahidi tosha kuwa kuna uwezekano mkubwa binadamu wa kale ambaye alitegemea
mazingira kwa kila kitu aliishi maisha ya furaha ikilinganishwa na binadamu wa
sasa.
20. Binadamu kama viumbe wengine
wanaoongozwa na sheria za asili. Pamoja na maendeleo ambayo mwanadamu
amefanikiwa kuyapata katika historia yake bado kuna mipaka ya asili ambayo
itaendelea kumuongoza yale anayofanya. Pamoja na uvumbuzi wa kompyuta na
mwendelezo wa mwanadamu kutaka kuumba vitu bado kuna akili ambayo ipo juu ya
uwezo wake. Ndio maana binadamu amefanikiwa kutengeneza roboti na anaendelea na
tafiti za kuunganisha kompyuta na mfumo wa fikra za binadamu lakini bado hakuna
dalili kuwa binadamu atafanikiwa kugundua chanzo halisi cha uhai.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Hakika
nilichokushirikisha hapa ni sawa na robo ya kile ambacho mwandishi
anatushirikisha kwa ajili ya ukuaji wa kiroho. Kwa maana hii nakushauri usome
nakala ya kitabu hiki kwa ajili ya kujifunza mengi zaidi. Kupata nakala ya
kitabu hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com