NENO LA LEO (FEBRUARI 21, 2021): KWA NINI WATU MSIBANI WANALIA?
Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku nyingine ambapo
tumepewa tena kibali cha kuwa hai. Chemi chemi ya uhai ambayo inaendelea kutiririka
ndani ya mioyo yetu ni fursa ya kuendelea kuishi kwa faida ya kizazi hiki na
vizazi vijavyo. Ikiwa siku za uhai wetu hapa Duniani zinahesabika, tuna wajibu wa
kuhakikisha kila siku tunayokuwa hai tuitumie kusogea kwenye kilele cha mafanikio
ya maisha. Katika kila tunalofanya tunakumbushwa kutambua kuwa ipo siku tutakiwa
kuachana na maisha ya Dunia hii.
Ni wazi kuwa kifo kinaogepesha kwa kila kiumbe chenye uhai, iwe kwa kiumbe ambacho kinapatwa na umauti au kwa jamii inayobakia, hakuna shujaa wa kifo. Kutokana na hali hiyo tunaona misiba ikitawaliwa na vilio na majonzi ya kila aina ambayo chimbuko lake ni kukosa uvumilivu wa kuondokewa na wapendwa wao. Hapa ndipo nikaona tutafakari swali la msingi la neno la tafakari ya leo ambalo linalenga kutupa majibu juu ya kwa nini watu wanalia kwenye misiba.
Soma: MUUJIZA WA KIFO: KWA KILA KIUMBE CHENYE UHAI MWISHO WAKE NI KIFO?
Toka enzi za zamani kupitia maandiko matakatifu tunaona kuwa misiba ilitawaliwa na vilio, huzuni na wasiwasi mkubwa (Mathayo 2:18; Mathayo 9:23; Ufunuo 21:4). Hivyo, katika nyakati za misiba, watu wanakosa tumaini kuhusu maisha ya baadae kwa kuwa wanajiona wapweke huku wakijiuliza maswali mengi yasiyo kuwa na majibu. Kila anayelia kwenye msiba anakuwa na maswali mengi yanayohusiana na marehemu sambamba na wale wanaobakia.
Ukweli unabakia kuwa msibani watu wanalia kutokana na jinsi wanavyofikria kuhusu maisha ya marehemu katika kipindi cha uhai wake na hata katika kipindi ambacho hatokuwepo. Mfano, wapo wanaolia kwa kuona kuwa mhusika ameondoka mapema huku akiacha pengo kubwa kwa wanafamilia au wategemezi. Wapo wanaolia kwa furaha inayotokana na jinsi mhusika alivyoweza kuishi maisha yenye kugusa watu wote (maisha ya mafanikio) katika kipindi kifupi cha uhai wake. Wapo wanaolia kwa kusikitika kumkosa marehemu katika kipindi ambacho walikuwa bado wanamhitaji. Pia, wapo ambao wanasikitika jinsi marehemu ambavyo amekutwa na umauti kabla ya kutimiza majukumu ya msingi katika kipindi cha uhai wake.
Kutokana na sababu hizo, sisi ambao bado tuna uhai
tunapata nafasi kutafakari kuhusu siku ya msiba wetu. Utake husitake, upende
husipende, ipo siku watu watakusanyika pamoja kwa ajili ya kuhitimisha safari
ya maisha yako hapa Duniani. Hivyo, kwa kuwa hakuna anayeweza kukwepa kifo,
katika siku hizi ambazo tuna uhai ipo haja ya kutafakari jinsi gani tunataka
watu wazungumzie jinsi tulivyoishi katika siku chache za uhai wetu. Mwandishi
Robin Sharma katika kitabu chake cha “The Greatness Guide” anatushirikisha kuwa
kila siku unatakiwa kuwa na tafakari ya kujiuliza: “ikiwa leo ingekuwa ni siku
yangu ya mwisho je ningefanya nini? Ningependa kuongea nani na ningemwambia
nini? Swali hili linakupata tafakari ya kila siku kuhusu siku za mwisho wa
maisha yako. Kwa kufanya hivyo, unafanikiwa kila siku kuishi kwa ukamilifu wa
majukumu ya msingi.
Mwisho, katika neno la tafakari ya leo tumejifunza kuhusu kwa nini watu wanalia msibani. Pia, tumeona kuwa kila siku tunayobahatika kuwa hai tunatakiwa kuitumia katika kujiandaa kwa safari ya siku ya mwisho wa uhai wetu. Tunaandaa safari ya kifo chema kwa kuhakikisha tunatimiza majukumu ya msingi katika maisha yetu ya kila siku, kama ni baba au mama wa familia hakikisha unatimiza majukumu yako, kama umepewa madaraka katika ngazi yoyote hakikisha unatimiza majukumu yako. Kumbuka, mbegu ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
ππΎππΎππΎππΎππΎ
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu
Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com