NENO LA LEO (FEBRUARI 4, 2021): ZINDUKA! JE HAUWEZI KUFANYA KAZI NJE YA FANI ULIYOSOMEA?
Habari
ya leo rafiki yangu mpendwa na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku mpya
katika siku za uhai wetu hapa Duniani. Ni siku ambayo tunaalikwa kuendeleza thamani
kwa ajili ya jamii inayotunzunguka na viumbe wote kwa ujumla. Maisha ya mwanadamu
hapa Duniani ni sawa na maua ambayo yanachanua na kupendesha kisa kunyauka. Katika
kipindi ambacho maua yamechanua na kupendeza huwa kipindi ambacho Wanyama na
wadudu wa kila aina wanakimbilia maua hayo kwa sababu mbalimbali.
Hivyo, tunaweza kusema kuwa mafanikio ya Ua katika kipindi ambacho limechanua yanapimwa na idadi ya wadudu au wanyama ambao liliweza kuvutia katika kipindi ambacho lilikuwa limechanua na kupendeza. Huo ndio ukweli hata kwenye maisha ya mwanadamu. Tunapima mafanikio ya mwanadamu kwa kuangalia ni jinsi gani aliweza kuwa wa thamani kwa jamii inayomzunguka na viumbe wengine katika kipindi cha uhai wake hapa Duniani.
Katika neno la tafakari ya leo nitakushirikisha kuhusu umuhimu wa kufanya kazi zaidi ya fani uliyosomea. Wote tunakubaliana kuwa kizazi cha sasa kina idadi kubwa ya Vijana ambao wamefikia walau kadato cha nne hadi elimu ya juu ikilinganishwa na vizazi vilivyopita. Kwa kipimo hicho tunakubaliana kuwa kizazi cha sasa kimepiga hatua kwenye ustaarabu (civilization) na kufukuza ujinga (enlightenment) ikilinganishwa na vizazi vilivyopita.
Hata hivyo, tunakubaliana kuwa katika kipindi hiki tunashuhudia idadi kubwa Vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa wanakimbia maeneo ya Vijiji na kuhamia Mjini. Ni wazi kuwa wengi wanakimbia shughuli za Vijijini ambazo zinaonekana kuwa ngumu ikilinganishwa na ngazi ya elimu waliyopata. Ni wasomi hawa ambao hawataki kujishughulisha na shughuli za kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa taifa na chanzo kikuu cha chakula.
Katika hali kama hiyo tunatakiwa kutafakari mustabali wa maendeleo ya mwanadamu hasa katika ngazi ya mtu mmoja mmoja. Ni rahisi kutabiri kuwa ajira itaendelea kuwa changamoto kadri siku zinavyosogea. Hali hii inatokana na ukweli kwamba idadi ya wasomi inaongezeka kila siku huku teknolojia ikiendelea kukua. Ukuaji wa teknolojia unaendelea kupunguza nafasi za ajira kutokana na kupungua kwa kazi za kutumia nguvu (manual work) ikilinganishwa na kasi ukuaji wa kazi za kidigitali. Tafsiri yake ni kwamba tutaendelea kushuhudia idadi kubwa ya wasomi wakizunguka na bahasha kwa ajili ya kutafuta kazi ikilinganishwa na idadi ya wasomi wanaopata ajira.
Katika
hali kama hiyo, tunakumbushwa kuwa kusoma siyo kigezo cha kuchagua kazi za
kufanya. Kuna hatua ambayo unatakiwa kuweka pembeni usomi wako na kufanya kazi
yoyote ili mradi upate kuingiza kipato. Hii ni pamoja na wale ambao tayari
wameajiriwa kulingana na fani walizosomea. Ikiwa unahitaji kuongeza kipato
zaidi hakuna namna nyingine zaidi ya kuwa tayari kufanya kazi za ziada tena kwa
malengo makubwa nje ya fani uliyosomea. Kama unaweza kufuga kibiashara
hakikisha unachangamkia fursa hiyo, ikiwa unaweza kufanya biashara fanya hivyo,
ikiwa unaweza kufanya kazi za ziada nje ya masaa ya mwajiri wako fanya hivyo,
na ukiwa unaweza kuwekeza fanya hivyo. Kubwa, ni kwamba husiogope macho ya watu
wanaokuzunguka kutekeleza kazi ambayo unaona ina tija kwako.
Mwisho, katika neno la tafakari ya leo nimekushirikisha umuhimu wa kufanya kazi nje ya fani uliyosomea. Dunia inabadilika na sisi tunatakiwa kubadilika ili kuendena na kasi ya mabadiliko hayo. Husikubali kubakia kuwa mtazamaji kwa kung’ang’ania usomi wako. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya
pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka
kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu
inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com