NENO LA LEO (FEBRUARI 3, 2021): TUNGUMZE KUHUSU PESA: KWA NINI UNAHITAJI KUTAFUTA PESA?
Habari
ya leo rafiki yangu mpendwa na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku nyingine
ambayo tumepewa kibali kwa ajili ya kuendelea kuwa bora. Kila siku inafungua
ukurasa mpya kwetu kufanya kitu cha thamani. Wote tunaalikwa kuhakikisha tunatumia
siku husika katika kutekeleza majukumu ya msingi ambayo kwa ujumla wake
yanakamilisha mafanikio ya maisha yetu hapa Duniani.
Katika neno la tafakari ya leo nataka tuzungumze kuhusu pesa na kwa nini una kila sababu ya kuisaka pesa. Neno “FEDHA” limekuwa ni kitendawili ambacho kila mtu anatoa majibu kulingana na mazoea yake kwenye ulimwengu wa fedha. Wapo wanaosema fedha kamwe haiwezi kutosha, fedha hazitunziki, fedha hazitakiwi kuongelewa au fedha zipo chache na kwa watu wachache ambao ni wateule. Ni kutokana na mtazamo huu watu wengi linapokuja suala la kuwa na uhuru wa kifedha maswali mengi yanakuwa; nitaweza vipi kutengeneza pesa? Naweza vipi kuitunza pesa isipotee? Nawezaje kuifurahia pesa yangu kwa sasa huku nikiendelea kutengeneza pesa kwa ajili ya siku zijazo?
Pesa ni nyenzo tu kwa ajili ya kufanikisha baadhi ya majukumu tulionao. Ubaya au uzuri wa pesa unategemea na namna tunavyoitumia katika kukamilisha hayo majukumu. Endapo imetumiwa vyema fedha itakusaidia kukamilisha majukumu yote muhimu katika maisha yako ya kila siku. Endapo fedha itatumiwa vibaya itamfanya mhusika kukosa uhuru wa kuwa karibu na watu wake wa karibu na hata kukosa mahitaji muhimu ya maisha. Pia, fedha inapotumiwa vibaya mhusika anaweza kuingia kwenye madeni makubwa ikiwa ni pamoja na kukosa uhuru wa maisha yake. Jambo muhimu la kujifunza ni kwamba unatakiwa kuidhibiti fedha na usipofanya hivyo itakudhibiti yenyewe. Njia bora ya kudhibiti pesa yako ni kuwa na vipaumbele vya namna ya kuitumia kutekeleza matakwa yako muhimu bila kupoteza utu wako.
Mifumo ya kuweka au kutoa pesa kwenye akaunti yako ya benki siku hizi imerahisishwa kwa kutumia mfumo wa mtandao. Siku hizi unaweza kufanya huduma zote za kibenki ukiwa umekaa Ofisini au nyumbani kwako kwa kutumia simu yako au kompyuta mpakato. Hata hivyo, unashauriwa kuhakikisha mifumo hii hisiwe sehemu ya kurahisisha matumizi ya hovyo ya fedha zako.
Kipindi cha muda unaotakiwa ili pesa inayowekezwa itumike kwa siku za baadae ndicho kinaamua njia ipi ya uwekezaji itumike kwa ajili ya kuwekeza peza zako. Hii ina maana kwamba kama unategemea pesa unayowekeza uitumie ndani ya wiki mbili zijazo au mwezi hauwezi kuiweka kwenye akaunti ya akiba ukitegemea kufaidika kupitia ongezeko la riba. Lakini kama pesa hiyo ipo kwenye mipango ya mwaka mmoja na kuendelea huna budi kuiwekeza kwenye sehemu ambayo fedha itaongezeka kupitia ongezeko la riba au kupitia gawio.
Watu wengi wanashindwa kutenga fedha kwa ajili ya uwekezaji ili kukidhi mahitaji ya fedha kwa siku za baadae lakini kamwe hawajahi kukosa fedha kwa ajili ya vitu visivyo vya lazima kama vile kununua kila toleo la nguo zinazoingia au fedha za vocha kwa ajili ya vifurushi. Ili uwe na uhuru wa kifedha ni lazima mhusika awe tayari kwa ajili ya kujibana kwenye matumizi yasiyo ya lazima na fedha hizo zitengwe kwa ajili ya uwekezaji.
Katika uwekezaji unahitaji kutenga fedha kwa ajili ya mahitaji muhimu kwenye uzee wako au fedha kwa ajili ya kustaafu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kama kiumbe hai kila siku unaongezeka umri na kadri unavyoongezeka umri ndivyo uwezo wa kufanya kazi unavyozidi kupungua. Matokeo yake kuna kipindi ambacho hautakuwa na uwezo wa kufanya kazi wakati mahitaji ya fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji muhimu ya maisha yatakuwa yameongezeka.
Mwisho, katika neno la tafakari ya leo nimekushirikisha kuhusu pesa na kwa nini unatakiwa kuisaka pesa ili uwe na uhuru wa kifedha. Ili uwe uhuru wa kifedha ni lazima utimize hatua mbili ambazo ni kudhibiti matumizi ya fedha na kuhakikisha unajilipa kwanza. Hatua hizi zinategemeana kutokana na ukweli kwamba unapodhibiti matumizi ya fedha unaokoa fedha ambazo unatakiwa kuziwekeza kwa ajili ya kukuza pato lako (kujilipa kwanza). Hii ndio siri ya kuwa tajiri na ili ufanikishe siri hii unatakiwa kuanza sasa kwa kuhakikisha kila mara unapopata fedha utenge fedha kwa ajili ya kuwekeza kabla kufanya matumizi mengine. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
ππΎππΎππΎππΎππΎ
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com
onclick='window.open(