NENO LA LEO (FEBRUARI 18, 2021): MUUJIZA WA KIFO: KWA KILA KIUMBE CHENYE UHAI MWISHO WAKE NI KIFO?
Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni asubuhi
nyingine tunapewa kibali cha kuwa hai kwa ajili kuendelea kuwa bora katika
katika kuliishi lengo la maisha yetu. Katika kipindi hiki, kama taifa na Dunia
kwa ujumla tunaendelea kushuhudia idadi kubwa ya watu ambao wanapoteza maisha.
Huzuni inaendelea kutawala kutokana na vifo ambavyo vinatokea ghafla kwenye
kila kona ya Dunia. Hali hii inatukumbusha kuwa hakuna anayejua siku yake ya
mwisho ni lini. Mwanadamu sawa na viumbe hai wengine kila siku inayopita
anasogea kwenye hitimisho ya siku za maisha yake hapa Duniani.
Katika neno la tafakari ya leo nitakushirikisha kuhusu muujiza wa kifo ambacho kimeendelea kuwa kitendawili kisicho na majibu katika historia ya maendeleo ya Mwanadamu. Kifo, kifo, kifo, kweli unaogopeka na kila aliyejaribu kupingana na ukweli wako mwisho wake ulipofika nae ulimuondoa. Watu wanajaribu kupambana na kifo lakini siku ya mwisho ikifika hakuna anaweza kupinga. Mwandishi wa vitabu Oscar Wilde, aliwahi kunukuliwa kuwa “kifo ndio kitu pekee kinachoniogopesha. Sikipendi. Mtu anaweza kushinda kila kitu siku hizi isipokuwa kifo”.
Katika historia ya mwanadamu, kifo kiliendelea kuchukuliwa hakiepukiki na kilionekana kuwa njia ya utakaso wa maisha mapya na ya milele. Hivyo, kifo kilichukuliwa kama chanzo cha kuingia kwenye maisha mapya baada ya maisha ya Duniani. Katika mtazamo huu, kifo kiliendelea kuchukuliwa kama adhabu ikiwa utaona kufa umeondolewa mema ya Dunia hii au zawadi endapo utachukulia kifo kama njia ya kuingia kwenye maisha mapya.
Hata hivyo, kifo kimeendelea kuwa ni siri kwani hakuna majibu ya wazi jinsi kinavyotokea. Mfano, hakuna majibu juu ya ni wakati gani au katika umri upi kifo kitatokea. Iwe Watoto hata kabla ya kuzaliwa, wakati wa kuzaliwa, katika umri mdogo, katika umri wa ujana na katika umri wa uzee wote wanapatwa na kifo. Iwe masikini, tajiri, mtu anayetegemewa na kundi la watu wote hakuna ambaye anakwepa kifo. Je katika hali kama hiyo tuendelee kuogopa kufa? Mwandishi wa kutoka Urusi Anton Chekhov (1860 – 1904) alinukuliwa kuwa “kifo ni kinatisha, lakini mbaya zaidi ni hisia kwamba unaweza kuishi milele na usife kamwe”. Tafsiri yake ni kwamba pamoja na kwamba kifo kinaogopesha lakini hatuna budi ya kuwa tayari kukipokea.
Kwa
ujumla tunaweza kusema kuwa “hakuna kifo cha mtu kinachotokea bila kutoa fundisho
kwa wale wanaobakia, na wale walio wategemezi wa marehemu hurithi sehemu ya fundisho
hilo kwa ajili ya ukombozi wa maisha katika utu wa Dunia hii”. Katika hilo,
mwanafalsafa Lao Tzu kutoka China aliwahi kunukuliwa “Maisha na Kifo ni uzi
mmoja, inategemea uzi huo huo unatazamwa kutoka upande upi”. Hivyo, katika maisha ya kila siku tunatakiwa kutambua kuwa kifo ni sehemu ya maisha.
Mwisho, katika neno la tafakari ya leo tumejifunza kuhusu kifo na kuona kuwa pamoja na kwamba kifo kinaogopesha lakini hatuna budi kuwa tayari kukabiliana na ukweli kwamba ipo siku tutakufa. Kifo uambatana na huzuni na vilio kwa wale wanaobakia, lakini mwisho wake hakuna namna zaidi ya kukubaliana na ukweli kuwa kifo cha mmoja kati yetu katika jamii ni ukumbusho kwa wanaobakia kuwa wote tupo njia moja. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
ππΎππΎππΎππΎππΎ
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN
TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com