Uchambuzi wa Kitabu cha Homo Deus – A Brief History of Tomorrow: Utabiri wa Historia ya Kesho kutokana na maendeleo ya mwanadamu

Uchambuzi wa Kitabu cha Homo Deus – A Brief History of Tomorrow: Utabiri wa Historia ya Kesho kutokana na maendeleo ya mwanadamu

Habari rafiki yangu mpendwa ambaye umeendelea kujifunza maarifa mbalimbali kupitia kupitia Makala zangu za uchambuzi wa vitabu. Katika kipindi cha mwaka 2021 nimepanga kusoma vitabu 12 na vitabu vyote nitahakikisha nakushirikisha sehemu ya uchambuzi au uchambuzi wote ili kwa pamoja tupate kujifunza maarifa yanakayosaidia kuboresha maisha yetu. Karibu katika uchambuzi wa kitabu cha kwanza katika kipindi cha mwaka 2021. Husisite kuchangia kazi hii kwa kununua nakala za uchambuzi wa vitabu mbalimbali.

Kama bado hujajiunga na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la tafakari kila siku, tafadhali JIUNGE SASA.

Kitabu ninachokushirikisha kupitia makala hii ni Homo Deus: A Brief History of Tomorrow” kutoka kwa mwandishi Yuval Noah Harari. Kwa kifupi mwandishi wa kitabu hiki ni mwandishi maarufu ambaye ameandika vitabu vingi ambavyo vimefanya vyema kwenye soko. Moja kitabu chake ambacho nimesoma na kupenda kazi zake ni Homo Sapiens: A Brief History of Humankind. Kupitia kitabu hiki mwandishi anatushirikisha historia ya mwanadamu toka kuumbwa kwa ulimwengu mpaka nyakati ambazo aliandika kitabu (ikiwa unahitaji kunufaika na mabadiliko yanayotokea kwenye historia ya maendeleao ya mwanadamu, nakushauri usome kitabu hiki).

Soma: Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha A Brief History of Humankind (Historia Fupi ya Mwanadamu)

Kupitia kitabu ambacho nakushirikisha kupitia Makala hii, Mwandishi anatumia maneno ya Kilatini “Homo” kumaanisha Mwanadamu na “Deus” kumaanisha Mungu kwa maana yeye anahusika moja kwa moja na uwezo wa mwanadamu katika historia ya maendeleo yake kwenye uso wa Dunia. Hivyo, kupitia kitabu hiki Mwandishi anaelezea uwezo wa mwanadamu wa sasa kupitia mafanikio yaliyopo na kujaribu kujenga picha ya mafanikio ya siku zijazo. Amejadili masuala mengi ya falsafa kama vile ubinadamu, ubinafsi na vifo.

Karibu ushirikiane nami kujifunza machache kati ya mengi ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:

1. Katika historia ya maendeleo ya mwanadamu, mwanadamu amepitia kipindi ambacho ajenda kuu ya siku ilikuwa ni namna ya kukabiliana na matatizo makuu matatu ambayo ni: Njaa, Milipuko ya Magonjwa au majanga ya asili na Vita. Vizazi na vizazi, mwanadamu pamoja na kutumia kila mbinu ikiwemo ya maombi kwa Mungu na miungu ya kila aina, mamilioni ya watu waliendelea kufa kutokana na matatizo hayo matatu. Matatizo haya katika kipindi cha mwanzo wa millenia ya kwanza baadhi ya Wanafalsafa walifikia hatua ya kusema kuwa yawezekana ni sehemu ya mpango wa Mungu katika kudhibiti idadi ya watu, hivyo hakuna njia yoyote ambayo inaweza kumuepusha mwanadamu na matatizo hayo.

2. Hata hivyo, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni mwanadamu ameweza kukabiliana na matatizo hayo matatu kiasi ambacho siyo tatizo la kidunia tena. Kwa sasa mwanadamu anafahamu nini anatakiwa kufanya kwa ajili ya kuepuka changamoto ya njaa, magonjwa au majanga ya asili na athari za kivita. Kutokana na mafanikio hayo, nyakati hizi tunashuhudia wanadamu wengi wanaokufa kutokana na magonjwa ya shibe iliyopitiliza ikilinganishwa na wale wanaokufa kwa njaa; tunashuhudia wengi wanakufa kwa uzee/makosa ya jinai ikilinganishwa na Watoto wanaokufa kwa magonjwa kama ilivyokuwa zamani; na tunashuhudia idadi ya wanaojinyonga inaongezeka ikilinganishwa na wale wanaokufa kutokana na athari za kivita.

3. Kuhusu tatizo la njaa, historia inaonesha kuwa Mwanadamu amepitia kipindi ambacho kutokana na umasiki idadi kubwa ya watu walikufa kutokana na ukosefu wa chakula. Katika nyakati hizo kosa dogo au mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yangeathiri mazao ilitosha kuteketeza familia nzima kwa ukosefu wa chakula. Historia inaonesha kuwa takribani asilimia 5 hadi 10 ya Wamisri au India iliteketea kutokana na ukame. Katika kipindi hicho miundombinu na vyombo vya usafiri ilikuwa changamoto hivyo ilikuwa ni ngumu kuokoa jamii ambayo ilikabiliwa na changamoto ya njaa. Katika kipindi hicho njaa ilikuwa ni ajenda ya kidunia kwenye kila bara, na silaha kuu ya mwanadamu ilikuwa maombi, Ee Mwenyezi Mungu tuepushe na njaa au tuwezeshe kupata chakula cha siku. Hata hivyo, njaa kwa sasa siyo changamoto ya kidunia tena kutokana kukua kwa miundombinu ya uzalishaji pamoja na usafirishaji. Hali hii imepelekea jamii ya sasa kuangamia kutokana na shibe iliyopitiliza ikilinganishwa na wanaoangamia kwa njaa.

4. Baada ya njaa adui mkubwa wa mwanadamu katika historia ya maendeleo ya mwanadamu alikuwa ni majanga ya asili kama vile milipuko ya magonjwa na magonjwa ya kuambukiza. Mwanadamu wa wakati huo usamalama wa afya kwa siku ya leo haukutosha kumpa uhakika wa kuwa salama kesho yake. Mwanadamu alijua wazi kuwa kesho naweza kuumwa na kufa kutokana na magonjwa. Historia inaonesha kuwa katika miaka ya 1330 katika maeneo ya bara la Asia, Ulaya na Kasikazini mwa Afrika takribani watu milioni 75 hadi 200 walikufa kutokana na janga kubwa la tauni. Katika bara la Ulaya takribani watu wanne kati ya kumi walikufa kutokana na tauni. Zipo sehemu ambazo takribani ya nusu ya idadi ya watu katika sehemu hizo iliangamizwa na tauni. Jamii ya kipindi hicho haikuwa na mbinu mbadala za kupambana na mlipuko huo zaidi ya kutegemea sara na makusanyiko ya pamoja achilia mbali uwezo wa kuponya. Ukiachilia mbali athari za mlipuko wa tauni, historia ya mwanadamu inaonekana kupitia kwenye majanga ya milipuko ya magonjwa na magonjwa ya kuambukiza. Fikiria kuhusu magonjwa kama vile Polio, UKIMWI, Malaria, Ebola, Mafua ya ndege, Mafua ya nguruwe, na mengineyo ambayo yaliua maelfu ya watu katika kila kona ya Dunia. Hata hivyo, Mwanadamu wa karne ya sasa ameonesha uwezo wa kupambana na magonjwa hayo kwa kuwezesha ugunduzi wa chanjo au tiba dhidi ya magonjwa husika.

5. Kuhusu vita, historia ya maendeleo ya mwanadamu imepitia nyakati ambazo vita ilikuwa ni sehemu ya ajenda ya kila siku kutokana na uhasama kati ya mataifa. Kila taifa liliwekeza nguvu na rasilimali ya kwa ajili ya kulinda himaya yake. Katika nyakati hizo vita ilitokana na tamaa ya kupata mali kwa njia ya mabavu. Njia ya haraka ya kumiliki ardhi, madini, mafuta au nguvu kazi ilikuwa ni lazima upigane vita na mtu mwenye umiliki wa vitu hivyo. Hata hivyo, katika Ulimwengu wa sasa vita katika kila kona ya Dunia inaendelea kupungua kutokana kubadilika kwa mifumo ya upatikanaji mali. Umiliki wa mali katika karne ya sasa umebadilika kutoka kwenye umiliki wa rasilimali kama vile ardhi, madini, mafuta au watu (nguvu kazi) na kuhamia kwenye umiliki wa maarifa. Kwa sasa muhimu siyo ardhi, madini au mafuta bali unaelewa nini kuhusu rasilimali hizo ndicho kitakufanya uwe tajiri. Hivyo, msingi wa uchumi wa jamii ya sasa ni maarifa ikilinganishwa na jamii zilizotangulia ambazo msingi mkuu wa uchumi ulikuwa ni umiliki wa rasilimali kama mafuta, madini au ardhi.

6. Je baada ya kukabiliana na matatizo hayo makuu kwa ufanisi mkubwa kiasi ambacho siyo ajenda ya Dunia, ajenda kuu ya mwanadamu inatakiwa kuwa ipi? Katika ulimwengu wenye shibe, afya, na amani ni kipi kinahitaji kutawala maisha ya mwanadamu? Katika ulimwengu ambao teknolojia hai (biotechnology) na teknolojia ya kila aina inakua kwa kasi ni ipi ajenda ya mwanadamu katika maisha ya kila siku? Pamoja na mafanikio yote ya mwanadamu katika kudhibiti matatizo makuu matatu, bado mwanadamu wa Ulimwengu wa sasa kuna sehemu hajafanikiwa kukabiliana na njaa, vita na magonjwa katika baadhi ya sehemu. Hivyo, matatizo hayo siyo kwamba yameisha kabisa bali yamepungua kutokana na ukweli kwamba mwanadamu wa karne hii anaweza kukabiliana na matatizo haya ikilinganishwa na vizazi vilivyotangulia. Hii haimaanishi kupuuza maelfu ya watu ambao wanakufa kutokana na majanga hayo bali mantiki ya msingi ni kwamba uwezo wa kukabiliana na majanga hayo umeongezeka kwa mwanadamu wa sasa. Fikiria idadi ya watu ambao wanaishi chini ya dola moja katika kila kona ya Dunia, fikiria watu ambao wanakufa kwa UKIMWI, Malaria na magonjwa mengineyo hasa katika bara la Afrika na mataifa yanayoendelea; na fikiria idadi ya watu ambao wanakufa kwa vita kutokana na ongezeko la ugaidi katika maeneo mengi ya Dunia ya sasa.

7. Ushindi wa mwanadamu wa karne hii katika kukabiliana na majanga hayo matatu kunatoa tumaini la mafanikio kwa maisha yajayo. Katika karne hii hatuwezi kumlaumu Mungu wala asili ikiwa tutashindwa kukabiliana na magonjwa, vita au njaa. Hivyo, kwa ushindi huo mwanadamu wa sasa ana kila nyenzo ambayo anaweza kuitumia kutatua athari za majanga hayo katika jamii. Hali hii inatokana na ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano ikiwamo ukuaji wa miundombinu ya usafiri, teknolojia ya habari, teknolojia ya vifaa vya mionzi au afya kwa ujumla sambamba na ukuaji wa ukuaji wa teknolojia ya mifumo ya ulinzi.

Je ni ipi inatakiwa kuwa ajenda ya mwanadamu wa karne hii? Ajenda ya mwanadamuwa karne hii inajikita kwenye mambo yafuatayo:-

8. Siku za mwisho wa maisha. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika karne hii mwanadamu ataanza kupambana na namna anavyoweza kuepuka kifo. Kila mtu kwa sasa atakuwa anapambana kuhakikisha kuwa thamani ya mwanadamu ipo kwenye jinsi anavyopambana kurefusha siku uhai wake na watu wanaomtegemea. Ajenda hii hadi sasa inabebwa na watu wote bila kujali itikadi zao – sekta ya afya, sekta ya kilimo, sekta ya uhifadhi wa mazingira, wanasheria, wanasiasa na wasanii wa fani zote wote wamebeba ajenda hii kupitia kazi zao. Haki ya kuishi ni ya msingi na ya thamani kwa kila mtu mwenye uhai. Katika historia, kifo kiliendelea kuchukuliwa hakiepukiki na njia ya utakaso wa maisha mapya na ya milele. Hivyo, kifo kulichukuliwa kama chanzo cha kuingia kwenye maisha mapya baada ya maisha ya Duniani. Hali hii ilichochewa na maandiko matakatifu kwa madhehebu yote iwe Ukristo, Uislamu au Hindu. Tafsiri yake ni kwamba kifo kinamuondolea mwanadamu haki yake ya kuishi.

9. Tofauti na Imani ya kidini, sayansi na utamaduni wa kisasa kuna mtazamo tofauti kuhusu kifo na maisha. Kifo hakichukuliwi tena kama fumbo kwa mwanadamu na hakika hakuna mtazamo wa kuwa kifo ni maandalizi ya maisha ya baadae. Badala yake kifo kinaonekana kuwa ni tatizo la kiufundi ambalo linatakiwa kutatuliwa ili mwanadamu aendelee kupata haki yake ya msingi – “haki ya kuishi”. Je wanadamu wanakufaje? Hadithi za zamani na enzi za kati zilionesha Kifo katika picha ambayo kuna Mtoa roho ambaye alipotaka kuvuna roho ya mtu atakutana na mtu huyo katika maangaiko ya siku na ghafla anamgusa begani na kumwambia Njoo! Katika hali ya kushangaa mtu huyo anaomba: “Hapana siyo sasa, tafadhali! Subiri mwaka mmoja, mwezi, siku au saa! Lakini mtoa roho anapiga kelele akisisitiza Hapana! Lazima uje sasa. Na hivi ndivyo kifo kilivyodhaniwa kutokea.

10. Je ukweli kuhusu kifo ni upi? Katika hali halisi, wanadamu hawafi kutokana na kazi ya Mtoa roho kama ilivyofhaniwa au kwa sababu ya Mungu aliamuru kifo kiwe mpango wa kuachana na maisha ya Ulimwengu na kuingia kwenya maisha mapya, badala yake watu wanakufa kutokana na tatizo flani la kiufundi katika mfumo mzima wa mwili wa mwanadamu. Mfano, tatizo hilo linaweza kuwa moyo kushindwa kufanya kazi ya kusukuma damu kutokana na mafuta yaliyoganda kwenye Mshipa Mkuu wa damu (Ateri) au seli za saratani kuenea kwenye ini. Au bacteria au virusi kuingilia mfumo wa mapafu na hivyo kupelekea kukosa hewa ya kutosha katika mwili. Hivyo, kifo kinatokana na tatizo la kiufundi na kila tatizo la kiufundi lina suluhisho la kiufundi. Suluhisho hilo ndilo ambalo linampa mwanadamu wa karne hii ajenda ya kutafuta namna ambavyo anaweza kuepuka kifo. Kwa sasa suluhisho hilo bado halijapatikana lakini mwanadamu wa sasa anawekeza nguvu na rasilimali nyingi kwa ajili ya kupata suluhisho la kuondoa tatizo la kiufundi linalopekea kifo kitokee. Mfano, tafiti zinaendelea namna ya kuondoa seli za kansa kwenye mfumo wa ini, mapafu au namna ya kuweka moyo mpya mara baada ya moyo kushindwa kufanya kazi.

11. Je ukweli uko wapi kuhusu kukwepa kifo? Pamoja na kwamba wanaoamini katika kutafuta suluhisho la kifo wanamaani kuwa ifikapo mwana 2100 au 2200 kizazi kitakachokuwepo kinaweza kuishi maisha ya milele au angalau kuongeza umri wa kuishi hadi miaka 500 ikilinganishwa na umri wa sasa, bado ni ngumu kuamini kuwa unaweza kuishi bila kufa. Mwandishi anatushirikisha kuwa tafiti za kuepuka kifo zitaendelea kufanyika lakini itabakia kuwa kila tafiti itasogeza kizazi kilichopo kwenye tumaini jipya katika kukabiliana na kifo. Siku za kuishi zinaweza kuongezeka kwa kizazi cha karne ya 21 lakini ni ngumu kusema kuwa suluhisho la tatizo la kiufundi linalopekea kifo linaweza kupatikana kwa karne hii. Hivyo, tafiti za kisayansi zitaendelea kusaidia katika kupunguza vifo katika umri mdogo. Wanasayansi wanaweza kuendelea kuamini katika kutafuta suluhisho la kifo kwa kuwa tumaini hilo ndilo njia ya pekee ya kuwezesha tafiti ziendelee kufanyika kwa lengo ya kuboresha zaidi maisha ya mwanadamu.

12. Haki ya kuwa na furaha. Ajenda kubwa ya pili ya mwanadamu wa karne hii itakuwa ni kutafuta ufunguo wa furaha. Katika historia, wanafalsafa (great thinkers), manabii na watu wa kawaida walielezea furaha kama kitu cha muhimu na bora kuliko hata maisha yenyewe. Katika Ugiriki ya kale mwanafalsafa Epicurus alielezea kwamba kuabudu miungu ni kupoteza muda kwa kuwa hakuna maisha baada ya kifo, hivyo, furaha ndiyo linatakiwa kuwa kusudi pekee la maisha. Watu wengi enzi hizo walikataa nadharia ya Epicurus lakini katika Ulimwengu wa sasa furaha inakuwa ndiyo chaguo la kwa kwa watu wengi. Kutilia shaka juu ya maisha ya baadae hupelekea wanadamu siyo tu kutotaka kufa bali pia kutaka furaha katika maisha haya ya kidunia. Kwa mtazamo wa Epicurus, furaha lilikuwa hitaji na kiu ya mtu binafsi, katika Ulimwengu wa kisasa furaha na hitaji la watu wote. Ndiyo, maana Serikali zinaweka mipango ya matumizi ya rasilimali sambamba na kuimarisha ulinzi ili kuwalinda watu wake dhidi ya magonjwa, vita na njaa. Hauwezi kuwa na furaha ikiwa unakabiliwa na matatizo hayo katika maisha ya kila siku.

13. Katika karne ya 19 na 20, Watawala walijikita kwenye kujiimarisha kiuchumi na kinguvu. Mipango mingi iliyofanyika katika karne hizo ililenga hayo ili kuwa na taifa linalojitosheresha kimahitaji na imara kwenye ulinzi wan chi. Hudma zote zilizotolewa kwa jamii hazikulenga kufanikisha furaha ya watawaliwa bali kukidhi malengo makuu ya kiuchumi na ulinzi. Elimu ilitolewa kwa vijana ili wapate uelewa wa masomo ya hesabu, sayansi na mengineyo ili iwe rahisi kukabiliana na maadui. Vile vile, huduma za afya zilitoelewa ili kuimarisha watu wawe na nguvu za kuzalisha sambamba na kuwa na jeshi imara. Mataifa mengi yalipima ufanisi wake kwa kuangalia ukubwa wa eneo la utawala, idadi ya watu na ukuaji wa pato la taifa na siyo furaha ya wananchi wake. Hata hivyo, katika karne hii, Wanafalsafa, wanasiasa na hata wanauchumi wanapiga kelele umuhimu wa kuhakikisha ukuaji wa pato la taifa uendene na ukuaji wa furaha ya wananchi.

14. Je kuna uhusiano kati ya uzalishaji na furaha? Ni wazi kuwa uzalishaji mali ni njia ya upatikanaji wa vitu muhimu kwa ajili ya maisha yenye furaha japo siyo hakikisho la kuwa na furaha (production is only the means for happiness, not the ends). Zipo jamii za watu ambazo uzalishaji upo chini lakini jamii hizo zina furaha ikilinganishwa na jamii zenye uzalishaji mkubwa. Hivyo, je kadri uzalishaji unavyoongezeka kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya chakula, kadri uvumbuzi wa kukabiliana na magonjwa na kadri vita inavyozidi kupungua katika kizazi cha karne hii tutegemee kuwa rufaha itazidi kutawala ikilinganishwa na vizazi vilivyopita? Siyo kweli! Kuipata furaha siyo kazi rahisi – siyo umiliki wa vitu, ujali, unywaji, tiba, mapenzi wala umaarufu ambavyo vitakufanya uwe na furaha maana vyote hivyo vitakupa furaha ya muda tu – ndani mwako baada ya muda utajikuta unarudia hali ya sononeko/huzuni ya rohoni. Urafiki wa kina na muda mrefu ndiyo utatufanya tuwe na furaha ya kweli katika maisha. Mambo mengine yanatakiwa kufanyika kwa kiasi.

Uchambuzi wa kitabu chote utapatikana kwa gharama ya Tshs. 5,000/=. Jiunge na mtandao wa Fikra za Kitajiri kwa  KUBONYEZA HAPA.

 

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.


Born to Win ~ Dream Big 


Mwalimu Augustine Mathias

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com

Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com

onclick='window.open(