NENO LA LEO (FEBRUARI 9, 2021): ULISHAWAHI KUJIULIZA KWA NINI VITA SIKU HIZI IMEPUNGUA?
Habari
ya asubuhi rafiki yangu mpendwa na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku
nyingine ambayo tumepewa kibali cha kuendelea kuwa hai. Kupitia kibali hiki
wote tunakaribishwa kuendelea kutoa thamani dhidi ya watu wanaotuzunguka.
Katika kila tunalofanya tunakiwa kujiuliza kwa nini tunatekeleza jukumu hilo na
kwa faida ya nani? Swali hili ndilo linatupa changamoto ya kuhakikisha maisha
yetu yanakuwa ya thamani kwa jamii inayotuzunguka.
Katika
neno la tafakari ya leo ambapo nitakushirikisha sababu kuu kwa nini vita
imepungua katika karne ya sasa ikilinganishwa na karne zilizopita. Historia ya
maendeleo ya mwanadamu inaonesha kuwa kuna nyakati ambazo vita ilikuwa ajenda
kuu ya mwanadamu. Hali hii ilitokana na ukweli kwamba uadui kati ya jamii moja
au taifa moja na jingine ulikuwa juu. Uadui ulikuwa juu kutokana na mtawanyiko husiyo sawa wa rasilimali.
Katika nyakati hizo vita ilikuwa haikwepeki kutokana na ukweli kwamba ilitumika kama nyenzo kuu ya kujimilikisha mali (wealth acquisition) kutoka kwa mtu mwingine au taifa jingine. Vita ilitumika kwa ajili ya kumiliki rasilimali kama vile ardhi, madini, mafuta au nguvu kazi. Hii ndo ilikuwa njia ya kujiongezea utajiri huku ukimpunguza nguvu mpinzani wako. Kupitia njia hii mataifa makubwa yaliweza kukandamiza mataifa madogo. Vivyo hivyo, katika jamii matajiri waliweza kuongeza utajiri wao kwa kuwadhurumu wanyonge.
Katika
karne ya sasa vita imepungua kutokana na kubadilika kwa mbinu za kumiliki mali.
Katika karne hii umiliki wa mali umehama kutoka kwenye umiliki wa vitu na
kuhamia kwenye umiliki wa maarifa. Si ardhi, madini, mafuta wala nguvu kazi
vitakavyokufaidisha katika hii ya sasa bali maarifa uliyonayo kwenye jinsi
kutumia vitu hivyo ndicho kitakufaidisha. Ndiyo maana katika ulimwengu
utashangaa mataifa yenye hazina kubwa ya madini ni yale ambayo madini
yamehifadhiwa kwenye stoo. Hali iko hivyo pia kwenye umiliki wa hazina ya
mafuta.
Pia, katika hali kama hiyo utagundua kuwa matajiri wakubwa wanaongoza kipindi hiki ni wale ambao wanatokana na matumizi ya akili ikilinganishwa na wale ambao wanatokana na umiliki wa rasilimali. Fikiria kuhusu matajiri kama Jack Ma, Mark Zuckerberg, Elon Mask, Jeff Bezos, Bill Gates na wengineo. Wote hawa wametokana na matumizi makubwa ya teknolojia ambayo ni kipimo sahihi cha kiwango kikubwa cha matumizi ya akili. Hivyo, katika Ulimwengu wa sasa vita katika kila kona ya Dunia inaendelea kupungua kutokana kubadilika kwa mifumo ya upatikanaji mali. Umiliki wa mali katika karne ya sasa umebadilika kutoka kwenye umiliki wa rasilimali kama vile ardhi, madini, mafuta au watu (nguvu kazi) na kuhamia kwenye umiliki wa maarifa.
Mwisho, katika neno la tafakari ya leo nimekushirikisha sababu ambayo imepelekea ajenda ya vita kupungua kwenye ajenda kuu za mwanadamu wa sasa. Tumeona kuwa katika nyakati hizi muhimu siyo ardhi, madini au mafuta bali unaelewa nini kuhusu rasilimali hizo ndicho kitakufanya uwe tajiri. Hivyo, msingi wa uchumi wa jamii ya sasa ni maarifa ikilinganishwa na jamii zilizotangulia ambazo msingi mkuu wa uchumi ulikuwa ni umiliki wa rasilimali kama mafuta, madini au ardhi. Swali la kujiuliza ni Je unatumia mbinu zipi kujiongezea utajiri katika karne ya sasa? Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya
pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka
kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu
inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN
TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com