NENO LA LEO (FEBRUARI 6, 2021): JE WAJUA UMEENDELEA KUTAJIRISHA WENGINE HUKU UKISAHAU UTAJIRI WAKO?
Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku nyingine
ambayo tumepewa kibali cha kuamka tukiwa wenye afya. Kila siku inatupa nafasi
ya kutenda yaliyo mema ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kwenye ukamilisho wa
matendo yetu hapa Duniani. Ili tupate kutenda matendo mema hatuna budi kuhakikisha
kila siku inakuwa msingi wa maisha ya siku inayofuata. Huo ndiyo ukweli pekee ikiwa
tunahitaji kuishi maisha yenye mafanikio hapa Duniani.
Katika
neno la tafakari ya leo nitakushirikisha sehemu kuu ambazo umeendelea kutajirisha
watu huku ukisahau kuweka hazina yako. Binadamu ni viumbe ambavyo vinaishi kwa
kutegemeana katika maisha ya kila siku. Kupitia kutegemeana huko watu wachache
ambao ni wabunifu wanaanzisha huduma ambazo zinawafanya watu wengine walazimike
kutegemea huduma hizo katika maisha ya kila siku. Zipo huduma ambazo ni za
lazima katika maisha ya kila siku lakini zipo huduma ambazo mtu hawezi kufa kutokana
na kukosa huduma hizo.
Hata hivyo, Wamiliki wengi wa biashara au huduma wana sifa ya kulazimisha bidhaa/huduma zao kwa watumiaji. Wengi wanafanya hivyo kwa kuhakikisha huduma/bidhaa wanayozalisha inakuwa na sifa ya kumlazimisha mtumiaji kuwa na ushirika na bidhaa/huduma husika. Bidhaa/huduma husika inamfanya mtumiaji ajenge tabia mpya katika mfumo wake wa maisha ya kila siku. Kupitia tabia mpya, mhusika anajikuta kila siku kwenye uhitaji wa huduma/bidhaa husika pasipo hiyari yake. Kadri tabia inavyozoeleka zaidi, mhusika anajikuta amekuwa teja (addicted) wa huduma/bidhaa husika pasipo ufahamu wake. Kwa kufanya hivyo anajikuta kwenye mazingira ya kutumia pesa zaidi huku akiendelea kutajirisha wamiliki wa bidhaa/huduma. Hebu tafakari athari ya matumizi yako ya pesa kwenye huduma/bidhaa zifuatazo:-
Matumizi ya simu janja (smart phones) kwenye mitandao ya kijamii. Ni kweli kuwa Dunia imebadilika na tunatakiwa kuendana na mabadiliko hayo. Matumizi ya mitandao ya kijamii yanaendelea kushika kiasi ambacho watu wamekuwa na urahibu kwenye mitando hiyo. Kwa sasa watu wengi ambao wanamiliki simu janja wanajikuta kila baada ya dakika kadhaa analazimika kufungua kwenye mitandao ya kijamii ili kujua yanayoendelea. Hata hivyo, ili mhusika anafanikiwe kutimiza kiu hiyo analazimika kuhakikisha simu yake ina kifurushi na kifurushi tafsiri yake ni pesa. Kumbe, unaendelea kupoteza pesa nyingi huku ukimtajirisha mmiliki wa mitandao ya simu. Jiulize ingekuwa kila unapojiunga na kifurushi cha simu ungekuwa unatenga pesa sawa na hiyo uliyoiweka kwenye simu na kuiwekeza sehemu salama, toka ulipoanza kutumia simu hadi sasa ungekuwa tajiri kiasi gani?
Matumizi ya ving’amuzi (TV subscription charges). Watoa huduma wa Ving’amuzi wao wanachofanya ni kucheza na akili yako kwa kuhakikisha wanakuweka ‘package’ ya chaneli ambazo unalazimika kulipia ili upate kuziona katika runinga yako. Wanafanya hivyo kupitia michezo ambayo inapendwa na watu wengi, au wanafanya hivyo kwa kubuni tamthilia mbalimbali ambazo zinafuatiliwa na watazamaji wengi. Yote hayo ni kwa ajili ya kuteka akili ya mteja ili kila mwisho wa kifurushi atamani kujiunga kifurushi kipya.
Matumizi kwenye vinywaji au uvutaji sigara. Ni sehemu nyingine ambayo watu wanakuwa na urahibu pasipo ufahamu
wao. Mtumiaji wa sigara kila mara anakuwa na kiu ya kuvuta sigara kiasi ambacho
yuko radhi akose pesa ya mambo mengine ya msingi ili mradi tu amalize kiu yake.
Vivyo hivyo, kwenye matumizi ya vinjwaji iwe kwa vinjwaji vikali au laini. Kuna
mtu kila anapoona chupa ya pepsi au coca mate yanajaa mdomoni. Hali hiyo inapekelea
alazimike kumaliza haja yake kwa kununua kinjwaji ambacho alishajenga uteja
kutokana na matumizi ya mara kwa mara.
Mwisho,
katika neno la tafakari ya leo nimekushirikisha umuhimu wa kutafakari athari ya
matumizi ambayo kwenye maisha ya kila siku tunafanya kwenye kuimarisha uchumi wetu.
Zipo sehemu nyingi ambazo tunaingia matumizi ya pesa iwe kidogo au kubwa lakini
kutokana na kwamba tumeshajenga uteja kwenye sehemu hizo, athari yake ni kwamba
katika kipindi cha muda mrefu. Tunaweza kutumia mbinu hizo hizo kwenye kukuza
utajiri wetu kwa kuhakikisha tunakuwa na utamaduni wa kujilipa kwanza kabla ya
kufanya matumizi yoyote kwenye kila shilingi inayoingia mikononi mwetu.
Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea
mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda
mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com