NENO LA LEO (FEBRUARI 7, 2021): JE UMEKUWA IMARA NA HODARI KIASI GANI?
Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku mpya ambayo
ni matumaini yangu kuwa tumeamka salama na kila mmoja anaendelea na majukumu ya
leo. Kila siku tunapewa nafasi ya kuboresha maisha yetu kupitia majukumu yetu
ya kila siku. Mimi na wewe tuna kila sababu ya kuhakikisha tunatekeleza mambo
ya msingi kwa ajili ya ukamilisho wa kusudi kuu la maisha yetu hapa Duniani.
Katika neno la tafakari ya leo tutaona tutajifunza umuhimu wa kuwa Hodari na Imara dhidi ya changamoto zinazotukabili. Neno la tafakari ya leo nimeliandaa kutoka kwenye wosia wa Mfalme Daudi kwa Solomoni (1 Wafalme 2: 1 – 9). Katika maandiko hayo matakatifu tunaona jinsi Mfalme Daudi baada ya kuona siku za uhai wake zinafikia ukomo aliamua kumrithisha mwanae Solomoni. Kwa kunukuu sehemu ya wosia hii inaanza kwa maneno haya “kama ilivyo kwa viumbe vyote kufa, siku zangu zimekwisha. Uwe Imara na Hodari” (1 Wafalme 2: 1).
Mfalme Daudi anatumia maneno “uwe imara na hodari” kumpa ujasiri Solomoni katika majukumu yake mapya. Maneno hayo yanatakiwa kumuongoza Solomoni katika nyakati ambazo atatakiwa kusimamia maamuzi yake kama Mfalme. Tunaweza kusema kuwa maneno hayo yalitumika kwa mtu ambaye alikuwa anaandaliwa kuwa Mfalme mpya, lakini katika maisha yetu ya kila siku maneno hayo ni msingi wa kutuongoza kwa maana kila mtu ni Mfalme katika maisha yake. Kila siku tunaalikwa kuwa imara na hodari dhidi ya changamoto tunazokabiliana nazo; tunaalikwa kuwa imara na hodari dhidi ya hila na maneno ya watu; tunaalikwa kuwa imara na hodari kwenye shughuli zetu za uzalishaji mali; na tunaalikwa kuwa imara na hodari kwenye uongozi binafsi au uongozi wa wafuasi wetu.
Ukisoma maandiko matakatifu kuhusu maisha ya Mfalme Solomoni utajifunza kuwa pamoja na kwamba alipewa majukumu makubwa akiwa bado mtoto mdogo lakini alifanikiwa kutokana na wosia alioupata kutoka kwa baba yake. Kupitia Maandiko Matakatifu tunaona kuwa siku za mwanzo wa Ufalme wake, alimuomba Mwenyezi Mungu ampe moyo wa kusikia ili apate kutambua mema na mabaya (1 Wafalme 3: 5 – 10). Tafsiri yake ni kwamba kwa Solomoni hekima (kalama ya kutambua mema na mabaya) ilikuwa kila kitu katika majukumu yake mapya. Hakutaka kuomba maisha marefu wala kuomba mali nyingi katika kipindi cha Ufalme wake bali kwake yeye alitakuwa aishi kwa ajili ya kutumikia. Na kwa kufanya hivyo alifanikiwa kiutawala na kufanikiwa kupata mali kuliko mtu yeyote aliyepata kuishi Duniani humu.
Kupitia
ombi la Mfalme Solomoni tunajifunza kuwa katika maisha yetu ya kila siku tunajiangamiza
wenyewe kwa kushindwa kutambua mema na mabaya. Kwa kutokutambua mema na mabaya
tunashindwa kuwa imara na hodari kutokana na kuendekeza tamaa za mwili au hofu
katika maisha ya kila siku. Kwa kutokutambua mema na mabaya tunaendekeza
mahitaji binafsi na kusahau kuwa mafanikio yetu yanapatikana kupitia kuwatumika
watu wengine. Kumbe, ikiwa unahitaji kuokoa nafsi yako ni lazima ujifunze namna
ya kuokoa nafsi za watu wengine kwanza.
Mwisho, katika neno la tafakari ya leo tumekumbushwa umuhimu wa kuwa imara na hodari dhidi ya changamoto za maisha ya kila siku. Pia tumefundishwa kuwa uimara na uhodari unapatikana pale tunapokuwa na uwezo wa kutambua mema na mabaya katika maisha yetu ya kila siku. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
ππΎππΎππΎππΎππΎ
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com