NENO LA LEO (MACHI 04, 2021): FAHAMU KANUNI 12 ZA KUISHI MAISHA YENYE MAONO.
Habari ya leo rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni wakati mwingine napata nafasi ya kuongea na wewe kupitia makala hii ya siku ya leo. Makala ya leo ni mwendelezo wa mafundisho kuhusu maono na namna ambavyo kila mmoja wetu anaweza kuishi maisha yanayoongozwa na maono. Kupitia mafundisho ya leo tutajifunza kanuni kumi na mbili ambazo tunatakiwa kuziishi katika maisha ya kila siku ikiwa tunahitaji kuongozwa na maono.
Kama bado hujajiunga na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la tafakari kila siku, tafadhali JIUNGE SASA.
Karibu tujifunze kwa pamoja:-
Kanuni #1: Mara zote ongozwa na maono yaliyo wazi. Kukamilisha maono yako unatakiwa kuongozwa na kusudi la maisha ambalo lipo wazi. Watu wote waliofanikiwa kimaisha; kwa kutaja tu baadhi Abrahamu, Musa, Daniel na wengine wote tunaowafahamu katika historia ya maisha mwanadamu kama vile J.K. Nyerere, Nelson Mandera, Kwame Nkrumah, Albert Einsten na wengineo kwa pamoja kila mmoja wao aliongozwa na kusudi maalumu ambalo lilimfanya atimize maono yake. Kusudi hilo linakuwa ni kiu yako ambayo kila siku unatamani kuona unafakisha hitaji husika.
Kanuni #2: Tambua uwezo ulionao katika kufanikisha kuishi maono yako. Unapogundua ndoto ya maisha yako pia utagundua uwezo uliyopo ndani mwako kwa ajili ya kutimiza ndoto hiyo. Kumbuka kuwa uwezo huo unategemea jukumu ambalo Muumba anakusudia ulitimize kupitia maisha yako. Na kulingana na jukumu hilo amekupa uwezo ambao unatakiwa kuutumia kukamilisha jukumu husika. Uwezo huu umejificha ndani mwako na haujatumika kutokana na kuishi maisha ya kujitathimini chini ya kiwango.
Kanuni #3: Tengeneza Mpango wa Kufanikisha Maono yako. Ili ufanikiwe unahitaji kuwa na mpango ambao unakuongoza katika safari ya kuishi maono uliyonayo. Mwenyezi Mungu amekupa maono hila wajibu wako ni kuhakikisha unaandaa mpango kwenye karatasi kwa ajili ya kuutumia mpango huo kutimiza maono uliyopewa. Katika kuandaa mpango wa kutimiza maono yako ni lazima uanze kwa kujiuliza maswali haya: a) Mimi ni nani? b) Je nataka kuelekea wapi? na c) Je kwa sasa nina uwezo gani au namiliki nini?
Kanuni #4: Kuwa na Hamasa juu ya Maono yako. Hamasa ndio itakuongoza kugundua thamani halisi ya maisha yako. Hamasa ndio inawaongoza watu kugundua kitu cha muhimu na thamani katika maisha kuliko maisha yao yenyewe. Kumbuka kuwa maandiko matakatifu yanasema wale wenye kutaka kuokoa maisha yao wenyewe watayapoteza (Mathew 16:25). Tafsiri yake ni kwamba uzima wa kweli upo kwenye maisha yako kwa ajili ya wengine. Unatakiwa kuikana nafsi yako kwa ajili ya kusudi maalumu la maisha yako. Je una njaa/kiu kiasi gani kwa ajili ya kutimiza maono yako? Kiwango cha kiu/njaa uliyonayo ndicho kinaonesha hamasa yako kuishi maisha ya maono.
Kanuni #5: Jenga Imani dhidi ya maono yako. Kuona ni kazi ya macho wakati maono ni kazi ya roho. Unaweza kuwa na macho ya kuona lakini ukakosa maono kwa kuwa hiyo ndiyo zawadi kubwa ambayo Mungu amempa mwanadamu. Uwezo wa kuona vitu visivyoonekana au uwezo wa kuumba vitu ambavyo havijaumbika ndiyo zawadi ya kipekee ambayo inamfa Mwanadamu afanane na Muumba wake kwa sura na mfano wake (Mwanzo 1:26). Maono yanamwezesha mtu kuona vitu kwa jinsi vinavyotakiwa kuwa (ambavyo havijaumbika) wakati macho yasiyo na maono yanaona vitu jinsi vilivyo (vilivyoumbwa tayari). Tafsiri yake ni kwamba hatupaswi kuruhusu yale ambayo macho yetu yanaona kuamua kile ambacho roho yetu inaamini. Kwa maneno mengine ni kwamba tunatakiwa kutembea katika Imani kuliko kutembea kwa upeo wa macho yetu. Ukiwa na Imani ni rahisi kuona vitu unavyotarajiwa kuwa navyo na kuviishi katika maisha ya sasa. Imani inakuwezesha kuona vikwazo kama sehemu ya fursa za kukufikisha kwenye maisha ya maono yako. Na ni kupitia Imani unakuwa na tumaini la maisha na kuishi maisha yasiyo na chembe ya uoga wala hofu.
Kanuni #6: Fahamu mchakato wa Maono. Mwenyezi Mungu ana mpango na makusudi kwa kila maisha ya mwanadamu na mpango huo unajidhihirisha taratibu katika maisha ya mhusika. Hata hivyo, pamoja na kwamba Mungu ana makusudi na maisha ya kila mwanadamu ni mara chache sana kukufunulia kuhusu kusudi hilo bali anakuongoza hatua kwa hatua katika kulitambua na kuliishi katika maisha ya kila siku. Mungu amefanya hivyo ili kila mwanadamu ajifunze na kujenga tabia kadri anavyopiga hatua kuelekea kwenye kusudi la maisha yake. Kama kila mtu angepewa mafanikio anayotaka bila kutumia jitihada zozote maisha yasingekuwa na thamani. Wengi tunaona mafanikio tunayotamani katika maisha yetu katika picha kubwa hila tunatamani tupate mafanikio hayo kesho yake. Mpango wa Mungu haupo hivyo unahitaji kuona kilele cha mafanikio katika maisha yako na kuweka mikakati ya kuishi kila siku kwa ajili ya kufikia kilele hicho.
Kanuni #7: Jenga vipaumbele vya maono ya maisha yako. Maisha yako jinsi yalivyo ni majumuisho na matokeo ya maamuzi na machaguzi unayofanya kila siku ya maisha yako. Ili ufanikiwe kuishi maono ya maisha yako ni lazima uwe na vipaumbele ambavyo vinakusogeza kwenye kilele cha maono ya maisha yako. Vipaumbele hivyo ndivyo vinatakiwa kuwa msingi kwako katika kufanya maamuzi ya kuchagua yapi unaweza kufanya au kutofanya katika maisha yako ya kila siku. Maisha yamejaa mbadala unapochagua kuacha tukio moja unakuwa umeamua kuchagua mbadala wake. Hapa ndipo unatakiwa kujua thamani ya kutumia maneno NDIYO na HAPANA katika maisha yako ya kila siku. Kadri unavyosema NDIYO kwenye tukio moja unakuwa umesema HAPANA kwenye mbadala wake.
Kanuni #8: Tambua mchango wa watu wanaokuzunguka. Hakuna namna nyingine ya kufikia kusudi la maisha yako bila uwepo wa mchango wa jamii inayokuzunguka. Katika jamii unatakiwa kufahamu makundi ya aina mbili; kundi la kwanza ni la watu ambao wapo tayari kukusaidia au kukuwezesha kutimiza kusudi la maisha yako na kundi la pili ni watu ambao watakukwamisha kutimiza kusudi la maisha yako. Wapo watu ambao Mwenyezi Mungu amekuandalia tayari kwa ajili kukushika mkono katika safari yako ya kutimiza kusudi la maisha yako. Wajibu wako ni kuwatambua watu hao na kujua namna ya kuishi nao katika maisha yako ya kila siku.
Kanuni #9: Tambua uwezo ulionao katika kuishi maono yako. Mungu amekuumba na kukupa zawadi ya maono na zawadi hiyo inaambatana na uwezo wenye vipawa/vipaji ndani yake. Watu wengi wanakuwa waoga kufikia ndoto kubwa iliyopo ndani mwao kwa vile kila wanapoifikiria wanajitathimini kwa wakati husika na kujiona hawana uwezo wa kuiweka ndoto hiyo katika uhalisia wake. Wajibu wako ni kutambua nini unataka katika maisha yako na kuhakikisha unaandaa kwa maandishi mpango utakaokuwezesha kutimiza hitaji hilo la maisha yako. Pengine yawezekana ndoto yako ni kubwa kiasi ambacho unaogopa, pengine unajiona kwa sasa hauna rasilimali na uwezo wa kukuwezesha kuiweka ndoto yako katika uhalisia wake.
Kanuni #10: Kuwa Imara katika safari ya kufanikisha maono yako. Kila maono ni lazima yajaribiwe ili kupima ukweli na uimara wake. Unatakiwa kutambua kuwa safari ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio ya maono yako kutakuwepo na dhiki, msongo wa mawazo, kukatishwa tamaa, nyakati za machukizo, kupingwa au kukataliwa na mengine mengi. Uimara wako katika nyakati hizo ndio utakaokuwezesha kusonga mbele na hatimaye kusherekea mafanikio ya maono yako. Msimamo wako wa kuishi kulingana na kanuni au vipaumbele vya maisha yako ndio utakuwezesha kupita salama katika nyakati ngumu za maisha yako.
Kanuni #11: Kuwa mvumilivu kusubiria ukamilisho wa maono yako. Ukamilimisho wa maono yako unategemea na kiwango cha uvumilivu hadi pale ambapo utavuna matunda. Ni watu wachache sana ambao wanaweza kuvumilia hadi mwisho kwani walio wengi huwa wanahitaji mafanikio ya haraka haraka na matokeo yake wanakata tamaa. Wengi huwa wanaishia njiani kutokana na kushindwa kuvumilia hadi mwisho. Ni katika uvumilivu huu unatakiwa kutambua kuwa maisha unayopitia kwa sasa hata kama hayana uhalisia na matamanio ya maono yako ni kwa ajili ya kukuandaa kuelekea kwenye mafanikio ya maono yako.
Kanuni #12: Kaa katika Muunganiko na chanzo halisi cha maono yako. Kama ambavyo tumeona kuwa maono ni zawadi pekee ambayo Muumba amempa mwanadamu, kanuni hii inatukumbusha umuhimu wa kuwa na muunganiko na muumba wetu ambaye ni chanzo halisi cha maono yetu. Ni kupitia sara Mwanadamu anaunganika na Muumba wake. Kupitia sara Mwanadamu anaendelea anafunuliwa na Muumba wake kuhusu kusudi la maisha yake. Pia, kupitia muunganiko wa sara Mwenyezi Mungu anampa hamasa ya kuendelea kupiga hatua zaidi kutimiza kusudi la maisha yake.
Mwisho, kupitia makala hii tumehitimisha mafundisho kuhusu maisha yenye maono kwa kujifunza kanuni 12 ambazo zinatakiwa kutuongoza katika maisha ya kila siku. Maisha ni maono, na kupitia maono utakombolewa kutoka kwenye vikwazo ambavyo unaviona kwa macho nakuingia kwenye nafasi ya kile ambacho roho yako inakuambia kuwa hapa ndipo maisha yako yanatakiwa yafikie. Kumbuka, mbegu ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu
Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com