Uchambuzi wa Kitabu cha Conquering Fear: Jinsi ya kuishinda hofu katika Ulimwengu huu wenye matukio yasiyotabirika.

Uchambuzi wa Kitabu cha Conquering Fear: Jinsi ya kuishinda hofu katika Ulimwengu huu wenye matukio yasiyotabirika.

Habari rafiki yangu mpendwa, hongera kwa kuendelea kuwa sehemu ya wanaojifunza kupitia Makala zangu za uchambuzi wa vitabu. Makala hizi nimekuwa nashirikisha jamii kupitia mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI pamoja na kundi la WhatsApp. Karibu katika uchambuzi wa kitabu cha leo ambacho ni cha 9 kati ya vitabu 30 ambavyo niliweka lengo la kuvisoma katika kipindi cha mwaka huu 2020.

Kama bado hujajiunga na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la tafakari kila siku pamoja na kujumuika na watu wenye mtazamo sawa, tafadhali JIUNGE SASA.

Kitabu ninachokushirikisha kupitia makala hii ni Conquering Fear” kutoka kwa mwandishi Harold S. Kushner. Katika kitabu hiki mwandishi anatushirikisha namna ambavyo tunaweza kuisha maisha yasiyo na hofu hata kama tunaishi kwenye Ulimwengu ambao umejaa matukio yasiyotabirika.

Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi wanaishi kwa kuhofia mambo mengi kama vile kuhofia wapendwa wao kupatwa na changamoto kama vile magonjwa; ajali; athari zitokanazo na vita/ugaidi; Wanyama wakali; ukosefu wa fedha kwa ajili ya mahitaji muhimu ya maisha; vifo vya wapendwa wetu (watoto, wenza, wazazi au ndugu wengine); uoga wa kukataliwa au kusalitiwa; na majanga ya kidunia (mafuriko, ukame, tetemeko la ardhi au wadudu waharibifu).

Pia, jambo jingine ambalo linalopelekea hofu kwa watu ni kuhusiana na usalama wa kazi au biashara zao. Mara nyingi watu wanatimiza wajibu wao kwa ajili ya kuridhisha waajiri wao lakini hiyo haizuii kuondolewa kazi pale mabadiliko ya lazima kwenye taasisi yanapotokea. Hata hivyo, hofu hii inatufanya tushindwe kufurahia maisha kwa kiwango chake.

Athari zinazotokana na hofu ni nyingi kwenye maisha ya mwanadamu. Athari hizi zinajumuisha magonjwa yanayotokana na msongo wa mawazo; uhasama katika jamii; ulevi; urahibu (addiction) wa madawa ya kulevya; na kuongezeka kwa watu wenye matatizo yatokanayo na ulaji wa hovyo (eating disorders). Wajibu wetu namba moja ni kuhakikisha tunajifunza mbinu za kukabiliana na hofu ili tupate furaha halisi ya maisha. Ukweli ni kwamba bila kuishinda hofu hakuna chochote ambacho tutafanikisha katika kipindi cha uhai wetu.

Karibu ushirikiane nami kujifunza machache kati ya mengi ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:

1. Ukweli ni kwamba mambo mengi ambayo huwa tunahofia ni ya kufikrika. Uhalisia ni kwamba si vyote tunavyohofia huwa vinajidhihirisha katika maisha yetu. Yapo mengi ambayo katika maisha tunayaohofia lakini huwa hayatokei na pengine tunajikuta kwenye kuhatarisha afya yetu kwa kuendekeza tabia ambazo tunasema zinatuliza hofu. Mfano, mtu kwa kuogopa mshutuko wa kishindo na mwanga wa radi anawasha sigara na kusahau kuwa sigara ina athari kuliko hicho kilichomshtua. Vivyo hivyo, watu wengi wanazama kwenye ulevi wa pombe kali wakihisi wanapoteza mawazo kwenye yale wanahofia maishani mwao.

2. Ukweli ni kwamba katika Ulimwengu huu kuna nafasi ya matukio mabaya kutokea na kuathiri maisha yetu. Na ukweli ni kwamba kwa uwezo wetu yapo mengi ambayo yakitokea hatuna uwezo wa kuyazuia lakini hii haimanishi kuwa muda wote tunatakiwa kuwa watumwa kutokana na hofu ya mambo hayo. Takwimu zinaonesha kuwa matukio tunayohofia huwa yanatokea mara chache sana katika kipindi cha uhai wetu. Fikiria yote uliyokuwa unahofia toka enzi za ukuaji wako na jiulize ni matukio mangapi yalijidhihirisha katika uhalisia wake. Mfano, jiulize ni mara ngapi ulisafiri kwenye chombo chochote cha usafiri huku ukiwa na hofu kwa kukumbuka ajali iliyowahi kutokea ikiuhusisha aina ya chombo ambacho unasafiria kwa wakati huo. Pamoja na hofu hiyo ulisafiri na kufika salama mwisho wa safari yako.

3. Katika kipindi ambacho tunajikuta kwenye hali ambayo moja kwa moja tunaona kuwa tukio lililopo mbele yetu lipo nje ya uwezo wetu wa kulitatua ndipo wengi hujawa na hofu zaidi. Mfano, kama unakabiliwa na ugonjwa ambao matibabu unayopewa hayaoneshi kusaidia au katika kipindi cha matukio ambayo yanapelekea vifo vya watu wengi katika taifa. Ni kipindi kama hichi ambapo nyumba za ibada huwa zinapokea waumini wengi kwa ajili ya kujikabidhi kwa Muumba wao. Kumbe, Sara/Dua ni moja ya moja ya mbinu ambayo inasaidia kukabiliana na hofu iliyopo mbele yetu. Kupitia Sara/Dua watu wanawasilisha hofu, matatizo na hisia walizonazo kwa Mungu kwa ajili ya kupata nguvu, hamasa na tumaini jipya dhidi ya changamoto zilizopo mbele yao.

4. Pamoja na kwamba Sara/Dua ni kwa ajili ya kuomba Muumba arejeshe tumaini jipya katika kipindi cha hofu na upweke, Mwandishi anatushirikisha kuwa njia bora ya kuongea na Muumba ni nyakati zote. Sara/Dua haitakiwi kuonekana na kumuita Mungu kwa ajili ya kutatua matatizo tu bali sara inatakiwa kuleta muunganiko wa mwanadamu na Muumba wake. Kupitia sara mwanadamu anamkaribisha Muumba ili awe ndani mwake na kila tendo analofanya liwe limepewa baraka na Muumba.

5. Kuna njia tatu ambazo watu hutumia kuufanya wenye matukio katili yaonekane ya kawaida katika maisha ya mwanadamu. Njia ya kwanza ni kukataa kuwa hakuna matukio (denial strategy) yanayotekea bila kustahili yatokee – Wanaokubaliana na njia hii, wana Imani kuwa Ulimwengu ni wa haki na chini ya mapenzi ya Muumba hakuna tukio ambalo linatokea kwa watu bila kustahili tukio husika. Watu wa mlengo huu wanaamini hakuna jambo linalowapata watu pasipo watu hao kulisababisha. Mfano, kama kuna janga la mafuriko limetokea sehemu flani – watu wa mlengo huu watajifariji kwa kusema mafuriko yametokea kwa kuwa sehemu hiyo imezidisha maovu kama ilivyokuwa wakati wa Nuhu akitengeneza Safina. Tatizo lililopo katika njia hii ni kwamba inatoa maamuzi (judgement) kwa wengine kuhusika katika tukio husika wakati mwanadamu hajaumbwa kumuona mwenzake kama adui/mkosaji. Mwanadamu ameumbwa kwa ajili ya kuaminiana na kutengeneza marafiki wao kwa wao.

6. Njia ya pili ni wale wanaopingana na nadharia ya Darwin maarufu kama Surivor of the fittest. Kulingana na Darwin Asili (Nature) iliruhusu viumbe wenye uwezo wa kupambana (fittest) kupitisha jeni (genes) zao kutoka kizazi kimoja hadi kingine na kadri viumbe hivi vilivyopambana na asili ndivyo viliimarika zaidi kimaumbile kwa ajili ya kuendeleza jeni vizazi na vizazi. Wanaoamini katika njia hii nadharia yao ni kwamba: “mafanikio ya mwanadamu yanapatikana kupitia ushirikiano na wanadamu wengine na siyo kwa mapambano kati yao”. Hivyo, Sheria ya asili ni kwamba “Mwenyezi Mungu ameumba mwanadamu na mafanikio ya mwanadamu dhidi ya Asili ni kuhakikisha anashirikisha wengine vipaji au rasilimali alizonazo kwa ajili ya mafanikio ya wote wanaomtegemea”. Hivyo, badala ya kupambana mwanadamu dhidi wanadamu wenzake katika kukabiliana na majananga ya asili, wanadamu wanatakiwa kushirikiana dhidi ya majango hayo.

7. Njia ya tatu ni wale ambao wanaamini kuwa tunaishi katika Ulimwengu hatarishi wenye kila aina ya matukio hatarishi na Mungu amempa uwezo mwanadamu wa kukabiliana na matukio hayo. Maisha yetu yapo kwa ajili ya matukio hatarishi kwa kuwa hakuna anayejua tukio baya litakalompata masaa yajayo. Hakuna anayejua kifo chake kitakuwa cha aina gani wala mateso na maumivu kiasi gani yatampata. Wale wanaoamini njia hii wanaishi nadharia kuwa: “maisha ya Sara/Dua na matendo mema kwa wengine yanasaidia kupunguza matukio hatarishi katika maisha yao ya baadae”.

8. Tofauti iliyopo kati ya maumivu (pain) na matesho ni kwamba: maumivu ni mwitikio wa mwili dhidi ya tukio lisilo rafiki wakati matesho ni mwitikio wa kihisia dhidi ya maumivu. Mfano, mtu kujihisi hana tumaini tena katika maisha au kuwa na huzuni kutoakana na maumivu anayopitia. Maana yake ni kwamba hakuna namna ya kuepuka maumivu lakini kitendo cha kuishi kwa mateso ya maumivu hayo ni maamuzi ya mhusika. Chukulia mfano wa maumivu ambayo mama anapitia wakati wa uchungu wa kujifungua. Mateso ya maumivu haya yanapungua pale anapofikiria zawadi ya mtoto iliyopo ndani ya maumivu hayo. Ndivyo ilivyo maumivu ya Ulimwengu huu, hatupaswi kuogopa au kuwa na hofu dhidi ya matukio hatarishi ambayo hatujui yatatokea lini na badala yake tunatakiwa kuzama kwenye matukio mema yanayotusubiria maishani. Ndiyo maana neno “husiogope” limetajwa mara kadhaa kwenye maandiko matakatifu. Hii ndiyo amri ya 11 ambayo tunatakiwa kuiishi katika maisha yetu ya kila siku.

HOFU YA UGAIDI (THE FEAR OF TERRORISM)

9. Moja ya hofu ambayo inawakabiri watu wa karne ya sasa ni matukio ya kigaidi. Hofu hii inakuwa kubwa hasa kwa mataifa ambayo yamewahi kukumbwa na matukio ya kigaidi. Mfano, Mwandishi anatushirikisha kuwa Marekani ni moja ya mataifa ambayo raia wake wanaishi kwa hofu kubwa kutokana na tukio la kigaidi la 11 Septemba, 2001. Tukio hili lilihusisha kulipuliwa ndege nne pamoja na majengo pacha ya eneo maalumu la biashara (World Trade Centre) yaliyokuwa na ghorofa 110 jijini New York. Kabla ya tukio hili ambalo lilitekelezwa na kundi la Al-Qaeda, Wamarekeni waliishi maisha ambayo walijiona wako salama ndani ya nchi yao kuliko taifa lolote lile. Mwandishi anatushirikisha kuwa kanuni ya gaidi huwa ni rahisi “kuua watu wachache na kuogopesha maelfu ya watu”. Hivyo, eneo lengwa la magaidi siyo tu eneo la tukio kwa kuwa maeneo ambayo hayafikiwi na athari ya moja kwa moja yanabakia kuishi kwa hofu ya tukio husika na hatimaye kubadilisha mfumo au tabia ya eneo husika.

10. Ni vigumu kama mtu mmoja mmoja kuzuia ugaidi lakini linalowezekana ni kuepuka hofu ya matukio ya kigaidi. Ili kuepukana na hofu ya magaidi, jambo moja muhimu ni kufahamu kuwa lengo la gaidi ni kusambaza hofu zaidi ya eneo analotekeleza tukio la kigaidi. Hivyo, shabaha ya gaidi siyo tu wale wanaokufa kwenye tukio analotekeleza bali idadi ya watakaoishi kwa hofu baada ya tukio husika. Hivyo, njia sahihi ya kukabiliana na ugaidi ni kuipinga hofu ya matukio ya kigaidi. Fanikio kubwa la magaidi ni pale ambapo watu wanabadilisha mfumo wa maisha mara baada ya tukio kutekelezwa. Tafsiri yake ni kwamba endapo jamii ikitambua kuwa baada ya matukio ya kigaidi ni lazima kuendeleza mfumo wa maisha wa awali moja kwa moja magaidi wanakosa nguvu. Hii imekuwa kinyume kwa Raia wa Marekani baada ya tukio la 11 Septemba, 2001 na ndiyo maana hadi sasa ugaidi ni tishio namba moja kwa taifa la Marekani.

11. Matukio ya kigaidi yanatakiwa kutazamwa sawa na matukio mengine ambayo huwa yanapelekea vifo na majonzi kwa baadhi ya familia na taifa kwa ujumla. Tatizo ni pale ambapo jamii inaogopa matukio ya kigaidi kuliko matukio hatarishi mengine kama vile ajali za vyombo vya usafiri, mlipuko wa njia au Vituo vya Mafuta, vimbunga na matukio mengine ya asili. Jamii imejifunza kukabiliana na matukio hatarishi kwa kuhuzuni kwa pindi yanapotekea na kusahau ili kuruhusu maisha yaendelee. Hatuwezi kukabiliana na ugaidi kwa kunyosheana vidole kutokana viashiria vya gaidi kati yetu sisi kwa sisi na badala yake ni kuruhusu maisha yaendelee kana kwamba hakuna tishio la ugaidi.

12. Ubaya huwa haudumu japo changamoto huwa ni pale ubaya unajificha ndani ya kivuli cha Imani ya dini. Changamoto ya ugaidi huwa ni pale magaidi wanajificha kwenye kivuli cha dini ya Kiislamu. Ugaidi ni moja ya udhahifu wa mwanadamu ambao unapelekea kutendeka mambo mengi mabaya dhidi ya mwanadamu. Hata hivyo kadri siku zinavyosogea ndivyo viongozi wa dini ya Kiislamu wanaelimisha makundi ya watu ili kuondoa dhana ya kuhusisha misimamo ya kigaidi na dini. Hali hii ni kutokana na ukweli kwamba hakuna dini inayohubiri utengano, dhuruma, uonevu au mauaji dhidi ya raia wasiyo na hatia.

HOFU YA MAJANGA YA ASILI (THE FEAR OF NATURAL DISASTER)

13. Katika historia ya maisha ya mwanadamu tumeshuhudia majanga ya asili ya kama vile tetemeko la ardhi, vimbunga, mioto, ukame au mafuriko katika kona mbalimbali za Ulimwengu. Majanga haya yamekuwa yakiambatana na vifo vya watu wengi kiasi cha kuacha kundi kubwa la watu kwenye huzuni na majonzi. Mara nyingi Wahubiri wa neno la Mungu wamekuwa wakihusisha majanga ya asili kuwa ni adhabu ya Mungu kutokana na kukithiri kwa maovu. Ukweli ni kwamba Mungu hatumii majanga ya asili kama adhabu ya kuongezeka kwa dhambi kwa kuwa majanga haya huwa yanaambatana yanadhuru watu masikini ikilinganishwa na wenye uwezo. 

Hii ni sehemu tu ya uchambuzi wa kitabu hiki. Uchambuzi wote una kurasa 15 na unapatikana kwa kuchangia Tshs. 3,999.00 kupitia namba ya Voda 0763745451 (Majina Augustine Mathias Mugenyi). Ukishalipia nitumie ujumbe wa sms ili nikutumie nakala tete ya uchambuzi wa kitabu hiki kwa mfumo wa Pdf. Unaweza kutumiwa kwa njia ya barua pepe (email) au WhatsApp.

BORN TO WIN ~ DREAM BIG

 

Mwalimu Augustine Mathias

Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410

Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com

Tovuti: fikrazakitajiri.blogspot.com 

onclick='window.open(