Uchambuzi wa Kitabu cha Conquering Fear: Jinsi ya kuishinda hofu katika Ulimwengu huu wenye matukio yasiyotabirika.
Habari rafiki yangu mpendwa,
hongera kwa kuendelea kuwa sehemu ya wanaojifunza kupitia Makala zangu za
uchambuzi wa vitabu. Makala hizi nimekuwa nashirikisha jamii kupitia mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI pamoja na kundi la WhatsApp. Karibu katika uchambuzi wa
kitabu cha leo ambacho ni cha 9 kati ya vitabu 30 ambavyo niliweka lengo la kuvisoma
katika kipindi cha mwaka huu 2020.
Kama bado hujajiunga na kundi
letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la tafakari kila
siku pamoja na kujumuika na watu wenye mtazamo sawa, tafadhali JIUNGE
SASA.
Kitabu ninachokushirikisha
kupitia makala hii ni “Conquering Fear” kutoka kwa
mwandishi Harold S. Kushner. Katika kitabu hiki mwandishi
anatushirikisha namna ambavyo tunaweza kuisha maisha yasiyo na hofu hata kama
tunaishi kwenye Ulimwengu ambao umejaa matukio yasiyotabirika.
Mwandishi anatushirikisha
kuwa watu wengi wanaishi kwa kuhofia mambo mengi kama vile kuhofia wapendwa wao
kupatwa na changamoto kama vile magonjwa; ajali; athari zitokanazo na vita/ugaidi;
Wanyama wakali; ukosefu wa fedha kwa ajili ya mahitaji muhimu ya maisha; vifo
vya wapendwa wetu (watoto, wenza, wazazi au ndugu wengine); uoga wa kukataliwa
au kusalitiwa; na majanga ya kidunia (mafuriko, ukame, tetemeko la ardhi au
wadudu waharibifu).
Pia, jambo jingine ambalo
linalopelekea hofu kwa watu ni kuhusiana na usalama wa kazi au biashara zao.
Mara nyingi watu wanatimiza wajibu wao kwa ajili ya kuridhisha waajiri wao
lakini hiyo haizuii kuondolewa kazi pale mabadiliko ya lazima kwenye taasisi
yanapotokea. Hata hivyo, hofu hii inatufanya tushindwe kufurahia maisha kwa
kiwango chake.
Athari zinazotokana na hofu
ni nyingi kwenye maisha ya mwanadamu. Athari hizi zinajumuisha magonjwa
yanayotokana na msongo wa mawazo; uhasama katika jamii; ulevi; urahibu
(addiction) wa madawa ya kulevya; na kuongezeka kwa watu wenye matatizo
yatokanayo na ulaji wa hovyo (eating disorders). Wajibu wetu namba moja ni
kuhakikisha tunajifunza mbinu za kukabiliana na hofu ili tupate furaha halisi
ya maisha. Ukweli ni kwamba bila kuishinda hofu hakuna chochote ambacho
tutafanikisha katika kipindi cha uhai wetu.
Karibu ushirikiane nami kujifunza machache kati ya mengi
ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:
1. Ukweli ni kwamba mambo mengi ambayo huwa tunahofia
ni ya kufikrika. Uhalisia ni kwamba si vyote
tunavyohofia huwa vinajidhihirisha katika maisha yetu. Yapo mengi ambayo katika
maisha tunayaohofia lakini huwa hayatokei na pengine tunajikuta kwenye
kuhatarisha afya yetu kwa kuendekeza tabia ambazo tunasema zinatuliza hofu.
Mfano, mtu kwa kuogopa mshutuko wa kishindo na mwanga wa radi anawasha sigara
na kusahau kuwa sigara ina athari kuliko hicho kilichomshtua. Vivyo hivyo, watu
wengi wanazama kwenye ulevi wa pombe kali wakihisi wanapoteza mawazo kwenye
yale wanahofia maishani mwao.
2. Ukweli ni kwamba katika Ulimwengu huu kuna nafasi ya
matukio mabaya kutokea na kuathiri maisha yetu. Na ukweli ni kwamba kwa uwezo
wetu yapo mengi ambayo yakitokea hatuna uwezo wa kuyazuia lakini hii haimanishi
kuwa muda wote tunatakiwa kuwa watumwa kutokana na hofu ya mambo hayo. Takwimu
zinaonesha kuwa matukio tunayohofia huwa yanatokea mara chache sana katika
kipindi cha uhai wetu. Fikiria yote uliyokuwa unahofia toka enzi za ukuaji wako
na jiulize ni matukio mangapi yalijidhihirisha katika uhalisia wake. Mfano,
jiulize ni mara ngapi ulisafiri kwenye chombo chochote cha usafiri huku ukiwa
na hofu kwa kukumbuka ajali iliyowahi kutokea ikiuhusisha aina ya chombo
ambacho unasafiria kwa wakati huo. Pamoja na hofu hiyo ulisafiri na kufika salama
mwisho wa safari yako.
3. Katika kipindi ambacho tunajikuta kwenye hali
ambayo moja kwa moja tunaona kuwa tukio lililopo mbele yetu lipo nje ya uwezo
wetu wa kulitatua ndipo wengi hujawa na hofu zaidi. Mfano, kama unakabiliwa na
ugonjwa ambao matibabu unayopewa hayaoneshi kusaidia au katika kipindi cha
matukio ambayo yanapelekea vifo vya watu wengi katika taifa. Ni kipindi kama
hichi ambapo nyumba za ibada huwa zinapokea waumini wengi kwa ajili ya
kujikabidhi kwa Muumba wao. Kumbe, Sara/Dua ni moja ya moja ya mbinu ambayo
inasaidia kukabiliana na hofu iliyopo mbele yetu. Kupitia Sara/Dua watu
wanawasilisha hofu, matatizo na hisia walizonazo kwa Mungu kwa ajili ya kupata
nguvu, hamasa na tumaini jipya dhidi ya changamoto zilizopo mbele yao.
4. Pamoja na kwamba Sara/Dua ni kwa ajili ya kuomba
Muumba arejeshe tumaini jipya katika kipindi cha hofu na upweke, Mwandishi
anatushirikisha kuwa njia bora ya kuongea na Muumba ni nyakati zote. Sara/Dua
haitakiwi kuonekana na kumuita Mungu kwa ajili ya kutatua matatizo tu bali sara
inatakiwa kuleta muunganiko wa mwanadamu na Muumba wake. Kupitia sara mwanadamu
anamkaribisha Muumba ili awe ndani mwake na kila tendo analofanya liwe limepewa
baraka na Muumba.
5. Kuna njia tatu ambazo watu hutumia kuufanya wenye
matukio katili yaonekane ya kawaida katika maisha ya mwanadamu. Njia ya kwanza ni kukataa
kuwa hakuna matukio (denial strategy) yanayotekea bila kustahili yatokee – Wanaokubaliana na njia hii, wana Imani kuwa
Ulimwengu ni wa haki na chini ya mapenzi ya Muumba hakuna tukio ambalo
linatokea kwa watu bila kustahili tukio husika. Watu wa mlengo huu wanaamini
hakuna jambo linalowapata watu pasipo watu hao kulisababisha. Mfano, kama
kuna janga la mafuriko limetokea sehemu flani – watu wa mlengo huu watajifariji
kwa kusema mafuriko yametokea kwa kuwa sehemu hiyo imezidisha maovu kama
ilivyokuwa wakati wa Nuhu akitengeneza Safina. Tatizo lililopo katika njia
hii ni kwamba inatoa maamuzi (judgement) kwa wengine kuhusika katika tukio
husika wakati mwanadamu hajaumbwa kumuona mwenzake kama adui/mkosaji. Mwanadamu
ameumbwa kwa ajili ya kuaminiana na kutengeneza marafiki wao kwa wao.
6. Njia ya pili ni
wale wanaopingana na nadharia ya Darwin maarufu kama Surivor of the fittest. Kulingana na Darwin Asili (Nature) iliruhusu viumbe
wenye uwezo wa kupambana (fittest) kupitisha jeni (genes) zao kutoka kizazi
kimoja hadi kingine na kadri viumbe hivi vilivyopambana na asili ndivyo
viliimarika zaidi kimaumbile kwa ajili ya kuendeleza jeni vizazi na vizazi.
Wanaoamini katika njia hii nadharia yao ni kwamba: “mafanikio ya mwanadamu yanapatikana kupitia
ushirikiano na wanadamu wengine na siyo kwa mapambano kati yao”. Hivyo, Sheria ya asili ni kwamba “Mwenyezi
Mungu ameumba mwanadamu na mafanikio ya mwanadamu dhidi ya Asili ni kuhakikisha
anashirikisha wengine vipaji au rasilimali alizonazo kwa ajili ya mafanikio ya
wote wanaomtegemea”. Hivyo, badala ya kupambana mwanadamu dhidi wanadamu
wenzake katika kukabiliana na majananga ya asili, wanadamu wanatakiwa
kushirikiana dhidi ya majango hayo.
7. Njia ya tatu ni
wale ambao wanaamini kuwa tunaishi katika Ulimwengu hatarishi wenye kila aina
ya matukio hatarishi na Mungu amempa uwezo mwanadamu wa kukabiliana na matukio
hayo. Maisha yetu yapo kwa ajili ya matukio
hatarishi kwa kuwa hakuna anayejua tukio baya litakalompata masaa yajayo.
Hakuna anayejua kifo chake kitakuwa cha aina gani wala mateso na maumivu kiasi
gani yatampata. Wale wanaoamini njia hii wanaishi nadharia kuwa: “maisha ya
Sara/Dua na matendo mema kwa wengine yanasaidia kupunguza matukio hatarishi
katika maisha yao ya baadae”.
8. Tofauti iliyopo kati ya maumivu (pain) na matesho ni
kwamba: maumivu ni mwitikio wa mwili dhidi ya tukio lisilo rafiki wakati
matesho ni mwitikio wa kihisia dhidi ya maumivu. Mfano, mtu kujihisi hana
tumaini tena katika maisha au kuwa na huzuni kutoakana na maumivu anayopitia. Maana
yake ni kwamba hakuna namna ya kuepuka maumivu lakini kitendo cha kuishi kwa
mateso ya maumivu hayo ni maamuzi ya mhusika. Chukulia mfano wa maumivu ambayo
mama anapitia wakati wa uchungu wa kujifungua. Mateso ya maumivu haya
yanapungua pale anapofikiria zawadi ya mtoto iliyopo ndani ya maumivu hayo. Ndivyo
ilivyo maumivu ya Ulimwengu huu, hatupaswi kuogopa au kuwa na hofu dhidi ya
matukio hatarishi ambayo hatujui yatatokea lini na badala yake tunatakiwa
kuzama kwenye matukio mema yanayotusubiria maishani. Ndiyo maana neno
“husiogope” limetajwa mara kadhaa kwenye maandiko matakatifu. Hii ndiyo amri ya
11 ambayo tunatakiwa kuiishi katika maisha yetu ya kila siku.
HOFU
YA UGAIDI (THE FEAR OF TERRORISM)
9. Moja ya hofu ambayo inawakabiri
watu wa karne ya sasa ni matukio ya kigaidi. Hofu hii inakuwa kubwa hasa kwa
mataifa ambayo yamewahi kukumbwa na matukio ya kigaidi. Mfano, Mwandishi
anatushirikisha kuwa Marekani ni moja ya mataifa ambayo raia wake wanaishi kwa
hofu kubwa kutokana na tukio la kigaidi la 11 Septemba, 2001. Tukio hili
lilihusisha kulipuliwa ndege nne pamoja na majengo pacha ya eneo maalumu la
biashara (World Trade Centre) yaliyokuwa na ghorofa 110 jijini New York. Kabla
ya tukio hili ambalo lilitekelezwa na kundi la Al-Qaeda, Wamarekeni waliishi
maisha ambayo walijiona wako salama ndani ya nchi yao kuliko taifa lolote lile.
Mwandishi anatushirikisha kuwa kanuni ya gaidi huwa ni rahisi “kuua watu
wachache na kuogopesha maelfu ya watu”. Hivyo, eneo lengwa la magaidi siyo tu
eneo la tukio kwa kuwa maeneo ambayo hayafikiwi na athari ya moja kwa moja
yanabakia kuishi kwa hofu ya tukio husika na hatimaye kubadilisha mfumo au
tabia ya eneo husika.
10. Ni vigumu kama mtu mmoja mmoja kuzuia ugaidi lakini
linalowezekana ni kuepuka hofu ya matukio ya kigaidi. Ili kuepukana na hofu ya
magaidi, jambo moja muhimu ni kufahamu kuwa lengo la gaidi ni kusambaza hofu
zaidi ya eneo analotekeleza tukio la kigaidi. Hivyo, shabaha ya gaidi siyo tu
wale wanaokufa kwenye tukio analotekeleza bali idadi ya watakaoishi kwa hofu
baada ya tukio husika. Hivyo, njia sahihi ya kukabiliana na ugaidi ni kuipinga
hofu ya matukio ya kigaidi. Fanikio kubwa la magaidi ni pale ambapo watu
wanabadilisha mfumo wa maisha mara baada ya tukio kutekelezwa. Tafsiri yake ni
kwamba endapo jamii ikitambua kuwa baada ya matukio ya kigaidi ni lazima kuendeleza
mfumo wa maisha wa awali moja kwa moja magaidi wanakosa nguvu. Hii imekuwa
kinyume kwa Raia wa Marekani baada ya tukio la 11 Septemba, 2001 na ndiyo maana
hadi sasa ugaidi ni tishio namba moja kwa taifa la Marekani.
11. Matukio ya kigaidi yanatakiwa kutazamwa sawa na
matukio mengine ambayo huwa yanapelekea vifo na majonzi kwa baadhi ya familia
na taifa kwa ujumla. Tatizo ni pale ambapo jamii inaogopa
matukio ya kigaidi kuliko matukio hatarishi mengine kama vile ajali za vyombo
vya usafiri, mlipuko wa njia au Vituo vya Mafuta, vimbunga na matukio mengine
ya asili. Jamii imejifunza kukabiliana na matukio hatarishi kwa kuhuzuni kwa
pindi yanapotekea na kusahau ili kuruhusu maisha yaendelee. Hatuwezi
kukabiliana na ugaidi kwa kunyosheana vidole kutokana viashiria vya gaidi kati
yetu sisi kwa sisi na badala yake ni kuruhusu maisha yaendelee kana kwamba
hakuna tishio la ugaidi.
12. Ubaya huwa haudumu japo changamoto huwa ni pale
ubaya unajificha ndani ya kivuli cha Imani ya dini. Changamoto ya ugaidi huwa
ni pale magaidi wanajificha kwenye kivuli cha dini ya Kiislamu. Ugaidi ni moja
ya udhahifu wa mwanadamu ambao unapelekea kutendeka mambo mengi mabaya dhidi ya
mwanadamu. Hata hivyo kadri siku zinavyosogea ndivyo viongozi wa dini ya
Kiislamu wanaelimisha makundi ya watu ili kuondoa dhana ya kuhusisha misimamo
ya kigaidi na dini. Hali hii ni kutokana na ukweli kwamba hakuna dini
inayohubiri utengano, dhuruma, uonevu au mauaji dhidi ya raia wasiyo na hatia.
HOFU YA MAJANGA YA ASILI (THE FEAR OF NATURAL DISASTER)
13. Katika historia ya maisha ya mwanadamu tumeshuhudia
majanga ya asili ya kama vile tetemeko la ardhi, vimbunga, mioto, ukame au mafuriko
katika kona mbalimbali za Ulimwengu. Majanga haya yamekuwa yakiambatana na vifo
vya watu wengi kiasi cha kuacha kundi kubwa la watu kwenye huzuni na majonzi. Mara
nyingi Wahubiri wa neno la Mungu wamekuwa wakihusisha majanga ya asili kuwa ni
adhabu ya Mungu kutokana na kukithiri kwa maovu.
Ukweli ni kwamba Mungu hatumii majanga ya asili kama adhabu ya kuongezeka kwa
dhambi kwa kuwa majanga haya huwa yanaambatana yanadhuru watu masikini
ikilinganishwa na wenye uwezo.
Hii ni sehemu tu ya uchambuzi wa kitabu hiki. Uchambuzi wote una kurasa 15 na unapatikana kwa kuchangia Tshs. 3,999.00 kupitia namba ya Voda 0763745451 (Majina Augustine Mathias Mugenyi). Ukishalipia nitumie ujumbe wa sms ili nikutumie nakala tete ya uchambuzi wa kitabu hiki kwa mfumo wa Pdf. Unaweza kutumiwa kwa njia ya barua pepe (email) au WhatsApp.
BORN
TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 0763 745 451/0786
881 155/0629 078 410
Barua pepe:
fikrazakitajiri@gmail.com
Tovuti: fikrazakitajiri.blogspot.com