Rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri ni matumaini yangu kuwa upo vizuri na unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuyaboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
fikra za kitajiri kwa ajili ya kupata chakula cha akili yako kutoka kwenye
uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Kama
kawaida mtandao wa fikra za kitajiri unaendelea kutimiza ahadi yake ya
kukuletea uchambuzi wa kitabu kimoja kila mwisho wa wiki (ijumaa) ili kupitia
uchambuzi wa vitabu hivi tuendelee kuyaboresha maisha yetu.
Lengo kubwa la mtandao wa
fikra za kitajiri ni kuona wewe unaanza kuishi kusudi la maisha yako ambapo kazi
kubwa iliyopo mbele yako ni kubadilisha fikra zako. Mtandao huu
umedhamiria kufanya kila liwezekanalo ili kukupatia maarifa yatakayo kusaidia
ubadili fikra zako ili ziwe za kitajiri katika kila sehemu ya maisha yako.
Kujiunga na mtandao wa fikra za kitajiri BONYEZA HAPA na
kujaza fomu ili upate makala moja kwa moja
kwenye barua pepe yako.
Katika wiki hii ya sita ninakuletea
uchambuzi wa kitabu cha Noble Purpose ambacho kimeandikwa na mwandishi William
Damon. Mwandishi kupitia kitabu hiki anahamasisha kila mtu kuishi kusudi la
maisha yake ili kuwa na maisha yenye furaha. Kwa ujumla mwandishi anatufundisha
kuwa maisha ni zaidi ya kuziridhisha tamaa za mwili na badala yake chimbuko la maisha yenye
furaha ya kweli ni kuishi kalama za wito wetu kwa ajili ya kuishi maisha yenye faida kwenye jamii. Muhimu tunafundishwa kuwa ili kufanikiwa
katika maisha haya ni lazima tuongozwe na roho mtakatifu au waweza sema nguvu
iliyo nje ya upeo wa fahamu zetu kulingana na imani yako.
Karibu tufaidike wote
maarifa niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki:-
1. Ili
kuishi maisha yenye furaha ni lazima uongozwe na vitu vitatu (a) kitu
unachokiishi (something to live on) (b) kitu kinachokufanya uishi (something to
live for) na (c) kitu ambacho upo tayari kufa kwa ajili yake (something to die
for). Hapa mwandishi anatufundisha kuwa maisha ambayo hayana misingi angalau
miwili kati ya hii mitatu ni maisha ambayo ni mfu. Ili uishi maisha yenye
madhumuni katika ulimwengu huu ni muhimu kuhakikisha unatumia misingi hiyo
mitatu katika yale unayoyafanya.
2. Kadri
tunavyofahamu sisi ni nani na ulimwenguni humu tumo kwa makusudi gani inasaidia
kukuza safari yetu ya kuishi maisha ya mafanikio. Haijalishi kusudi la maisha
yako ni lipi cha msingi ni wewe kutambua kwa nini uliumbwa katika ulimwengu na
baada ya hapo wajibu wako ni kuishi kwa kadri ya wito wako. Wapo wenye wito wa
kumtumikia Mungu, wapo wenye wito wa kuwa baba/mama wa familia bora, kuwa
mwanamuziki, mwanasiasa au mfanyabiashara hivyo kuanzia sasa hakikisha
unatambua kusudi la maisha yako na anza kuliishi mara moja.
3. Kadri
unavyotambua kusudi la maisha yako ndivyo unapata msukumo wa nguvu kubwa kutoka
ndani mwako kwa ajili ya kufanikiwa zaidi. Hapo ndipo utatambua kuwa kuna nguvu
na vipawa zaidi ambavyo vilikuwa havijatumiwa kutokana na wewe kutokujitambua
wewe ni nani na umeumbwa kutimiza madhumuni yapi katika ulimwengu huu.
4. Hakikisha
kila siku unafanya jambo ambalo linachangia kufikia kusudi la maisha yako. Hapa
ni muhimu kufahamu kuwa ili kufanikiwa kuishi kusudi la maisha yako ni lazima
uwe tayari kuipangilia siku yako ili kila siku ikupe ushindi mdogo na ushindi
huu utumike kama msingi wa kufikia kusudi kubwa la maisha yako.
5. Ili
tuishi kusudi la maisha yetu ni lazima kwanza tutambue vipaumbele vya maisha
yetu kwa kuhakikisha tunatanguliza kutumia kalama na ujuzi wetu kufanya yale
ambayo yanaridhisha roho zetu. Hapa tunakiwa kufahamu kuwa katika maisha furaha
ya kweli inatokana na kufanya yale ambayo nafsi zetu zinaridhishwa na matokeo
ya matendo yetu. Kama una matendo ambayo yanasababisha huzuni ya roho huna budi
kuachana nayo mara moja ili utoe nafasi kwa matendo yanayoifurahisha roho yako.
6. Maisha
ya kusudi la maisha yako yapo hapo ulipo na wala husitegemee kuwa ni yapo
sehemu nyingine. Maisha haya yanahusisha matendo yetu ya kila siku japo ni
wachache wanajua hilo. Kama wewe ni mwalimu fikiria kufundisha wanafunzi wako
kuliko mwalimu yeyote yule ambaye amewahi kuwepo, kama ni daktari lenga
kuwahudumia wagonjwa kwa roho moja, kama ni mfanyabiashara fikiria kutoa huduma
bora kwa wateja wako kwa kadri uwezavyo na kama wewe ni kiongozi au mwajiri
fikiria kuwatendea watu wako unaowaongoza kwa kadri unavyoweza kuwaridhisha.
Haya ndiyo maisha bora ambayo kila mtu ameumbwa kuyaishi.
7. Maana
halisi ya kusudi la maisha yako ni lile lengo kubwa la maisha yako ambalo ni
imara na linajumuisha kila sekta ya maisha yako na unapaswa kulikamilisha
katika maisha yako si tu kwa ajili ya faida yako bali kwa ajili ya jamii nzima.
Somo la kujifunza hapa ni kuwa kusudi la maisha ni (a) lengo kubwa ambalo ni
msingi wa maisha yako yote (b) imara na halitakiwi kubadilika mara kwa mara (c)
ni ufunguo wa sisi kuujua ukweli wa tuliumbwa kukamilisha nini hapa duniani (d)
linajikita kwenye kukamilisha kitu katika maisha yetu si tu kwa faida yetu tu
bali kwa ajili ya wengine. Kutokana na ukweli huu utagundua kuwa unapoishi
kusudi la maisha yako utajikuta katika ulimwengu wa matendo mema ambayo hayana
athari mbaya kwa maisha ya wengine wanaokuzunguka.
8. Wito
wako upo kwenye kazi yako ya kila siku. Watu wengi wameshindwa kuishi wito wa
maisha yao kwa vile wamekuwa wanatofautisha kazi wanazofanya na wito wao. Hapa
tunafundishwa kuwa wito wetu upo kwenye kazi zetu za kila siku na hivyo ili
kuishi wito huu ni lazima kwanza uipende kazi yako na hatimaye kupitia kazi hiyo
watu wengi wanufaike na matunda yako. Kwa ukweli huu pale unapoiona kazi yako
kama wito wako au kusudi halisi la maisha yako moja kwa moja kazi itabadilisha
mtazamo wako wote juu ya kazi yako na hivyo kufanikiwa kupata mafanikio makubwa
kwako wewe na wale unaowahudumia.
9. Unapoikubali
kazi yako kama wito wako inakuwa mwanzo wa safari ya kuishi kusudi la maisha
yako. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kazi unayofanya inachukua sehemu kubwa
ya muda wako na hivyo husipokuwa na furaha katika muda huu ni vigumu kupata
furaha kwa muda uliobakia. Kanuni hii inatakiwa kufanya kazi kwa wafanyakazi
wote pasipokujali cheo, muda walionao kazini au kazi wanazofanya. Kama unafanya
kazi ya kufagia barabara fagia kana kwamba hakuna mtu mwingine ambaye atafagia
vizuri kuliko wewe vivyo hivyo kwa kazi nyinginezo unazofanya fanya kama vile
wewe ndo mtaalamu namba moja kwa ubora katika kazi hiyo.
10. Unapoiona kazi yako kama wito huna budi
kusukumwa na wito huo kufanya kazi badala ya kusukumwa na malipo ya fedha ya kazi
husika. Hapa tunafundishwa kuwa katika kila kazi tunayofanya hatupaswi
kutanguliza fedha mbele badala tunatakiwa kutoa huduma yenye thamani kubwa kwa
wale tunaowahudumia na hatimaye fedha zitafuatia baadae. Pia tunasisitizwa
kuweka lengo la kutoa huduma bora kwa wateja badala ya kuweka lengo la kuongeza
faida tu. Nilichojifunza hapa ni kwamba unapojikita kwenye kuongeza faida tu ni
rahisi kutumia mbinu ambazo sio halali kama vile kushindwa kujali afya za
wateja unaowahudumia na hivyo kwenda kinyume na kusudi la maisha yetu.
11. Unaweza kupata kusudi la maisha yako
sehemu yoyote ile. Kusudi la maisha yako linaweza kuwa kwenye jamii yako ya
karibu, marafiki, ndugu, familia, imani (kanisani au msikitini), jamii na hata
kwa watu walio mbali na upeo wako. Mfano katika ngazi ya familia kusudi la maisha
yako linaweza kuwasaidia wafamilia wote kufikia ndoto zao au kuwasaidia wale
wasiojiweza. Vivyo hivyo kusudi la maisha yako linaweza kuwa baba/mama bora wa
familia. Hivyo hauna sababu ya kuumiza kichwa sana ukifikiria ni wapi utapata
kusudi la maisha yako badala yake anzia hapo ulipo. Kwa upande wa imani unapata
nafasi ya kutambua kwa undani upendo wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu.
12. Unaweza kuishi kusudi la maisha yako
kupitia matendo mema kwenye jamii. Matendo haya yanajumuisha upendo kwa watu wote
mfano, upendo kwa wazee, watoto, walemavu, yatima na wajane. Unaweza kuanzisha
mfuko au taasisi ya kusaidia watu wenye mahitaji na kupitia taasisi hiyo
ukafanikiwa kuwafiki watu wengi. Mfano, angalia maisha ya Mother Theresa,
unaweza ukafuatilia historia ya maisha yake kwenye mtandao kama haujui historia
yake.
13. Kusudi la maisha yako linaweza kuwa
kwenye utamaduni wako. Baadhi ya tamaduni zinawaongoza wanajamii kuishi maisha
yenye thamani kwa watu wengine. hivyo kupitia utamaduni wako unaweza kupata
kusudi la maisha yako. Mfano, baadhi ya tamaduni zetu zinatenga wajibu wa watu
kulingana na umri au jinsi zao, hivyo kupitia tamaduni hizi unaweza kupata
kusudi la maisha yako.
14. Kusudi halisi la maisha yako ni lazima
lijikite kwenye matendo ya halali kwenye jamii inayokuzunguka. Ni lazima yale
tunayoyafanya kupitia wito wetu yawe ni matendo yanayokubalika kisheria pasipo
kufanya hivyo tunakuwa bado hatujafahamu ukweli juu ya maisha yetu.
15. Ni lazima tuwe tayari kuomba msamaha au
kujisahihisha pale inapotokea matendo yetu yameenda kinyume na matarajio yetu hadi
kusababisha madhara kwa wengine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba sisi ni
binadamu na hivyo ni rahisi kufanya makosa. Hata hivyo kama bado huna nafasi ya
kufanya marekebisho ya makosa yako kabla hayajasababisha madhara makubwa fanya
hivyo mara moja pale unapopata angalizo. Hivyo ni muhimu maamuzi na matendo yetu
ambayo yanailenga jamii yakafanywa kwa tahadhari na unyenyekevu wa hali ya juu.
16. Kila mtu anaweza kuishi kusudi la
maisha lakini njia pekee ya kujua kama kusudi hilo ni halisi ni kuona kama
linaendana na misingi ya kijamii. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuna watu wanaishi
maisha yenye kiburi na kila aina ya ubinafsi labda kutokana na madaraka yao lakini
bado wakajiona kuwa wanaishi kusudi la maisha yao. Jambo la kujifunza hapa ni kwamba
matendo yetu ni lazima yakubalike kwenye jamii zetu kwa kuzingatia sheria na
tamaduni zetu.
17. Maisha yaliyojengwa kwenye misingi ya
kusudi la maisha ni maisha ambayo yametumiwa vizuri ulimwenguni hapa na kinyume
chake ni kwamba maisha ambayo hayajajengwa kwenye kusudi lake ni maisha
yaliyopotezwa. Hii haijalishi maisha hayo ni marefu au mafupi, masikini au
tajiri, afya njema au maradhi, yenye madaraka au yasiyokuwa na madaraka. Hivyo
ni muhimu kila mmoja wetu kutafuta kusudi halisi la maisha yake na kuanza
kuliishi mara moja.
18. Tafiti za kisaikolojia zinaonyesha kuwa
watu wenye furaha ya maisha ni wale ambao hawatumii nguvu nyingi kupata furaha
hiyo. Kwa maana nyingine ni kwamba watu wenye furaha ya maisha ni wale ambao
wamejitosa kufanya vitu ambavyo vinawapa furaha ya nafsi zao. Hivyo, kama
unataka kuishi maisha yenye furaha huna budi kufahamu ni yapi yanairidhisha
nafsi yako na kuanza kuyatekeleza mara moja. Mambo hayo si mengine bali ni yale
yanayounda msingi wa kusudi la maisha yako.
19. Kusudi la maisha yako linaweza kuwa
wokovu kwa maisha ya wengine. Hapa mtu yupo tayari kupoteza maisha yake ajili
ya kuokoa maisha ya wengine au nchi yake. Mfano, katika nyakati za vita kuna
baadhi ya watu ambao wapo tayari kufa kwa ajili ya kuilinda nchi yao. Hata hivyo,
humu duniani kuna kila aina ya vita ambayo kila mmoja wetu anapigana kuishinda.
Hivyo unaweza kuangalia ni vita ipi inawatesa watu wengi na wewe ukajitosa
kuwasaidia ili wapambane dhidi ya vita hiyo.
20. Ulimwengu unakusubiria utumie kalama/vipawa
ulivyopewa kwa ajili kuboresha dunia hii kuwa mahali pazuri kwa viumbe wote. Hivyo,
kadri unavyozidi kuchelewa kutumia vipawa hivyo ndivyo unavyozidi kupoteza
jambo ambalo ni kinyume na malengo ya uwepo wako hapa duniani. Pia, tunatakiwa
kukumbuka kuwa suala la kuishi kusudi la maisha yako sit u faida kwa ulimwengu
bali ni fadia na kwako pia kwa vile unaboresha afya yako ya kiroho, kiakili na
kimwili.
Mambo
Muhimu ya Kuzingatia katika Kutafuta Ukweli wa Kusudi/Dhamira ya Maisha Yako.
Mwandishi anatushirikisha kanuni tisa kwa ajili ya
kufikia kusudi la maisha yetu. Karibu tujifunze wote kanuni hizi:-
21. Kamwe hatupaswi kusema ni mapema mno au
tumechelewa kuishi kusudi la maisha yetu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba
kusudi la maisha yako unaweza kuliishi katika sehemu yoyote na muda wowote wa
maisha yako.
22. Pamoja na kwamba kusudi la maisha yako
lipo sehemu yeyote ile, ukweli ni kwamba ni rahisi kulipata kusudi la maisha
katika sehemu ambazo una uzoefu nazo. Sehemu hizi zinaweza kuwa familia yako,
marafiki, kanisani, kipaji chako, ajira au biashara yako na mazingira
yanayokuzunguka kwa ujumla.
23. Tafuta watu ambao ni “role model” wako.
Hawa ni watu ambao kupitia maisha yao unapata hamasa ya kufikia maisha ya ndoto
zako. Ni watu ambao wameishi maisha ya mafanikio kwenye jamii zao hivyo na wewe
kupitia wao unaweza kujifunza mengi. Hapa unaweza kuanza kuwa karibu na wale
ambao unatamani maisha yao kwa ajili ya kujifunza kutoka kwao.
24. Kama inawezekana pata sapoti kutoka kutoka
kwa watu wenye mtazamo kama wako. Lakini kuwa tayari kusimama kwenye kusudi la
maisha yako hata kama hakuna mwenye mawazo au maisha ya namna hiyo. Hii ni
kutoka na ukweli kwamba kusudi la maisha yako linaweza kuwa sio maarufu kwa
wakati huu na hivyo ukajikuta hauna sapoti kutoka kwa watu wengine.
25. Kuwa tayari kusimama imara kwa vikwazo
na changamoto za hapa na pale. Katika safari yako utapata mafanikio pamoja na
kushindwa kufikia baadhi ya malengo lakini katika yote haya haupaswi kuicha
njia yako.
26. Endelea kuwa mnyenyekevu na mwenye
hekima katika matendo yako. Haupaswi kudanganywa au kuridhika na mafanikio
unayoyapata kutoka kwenye kusudi la maisha yako na badala yake unatakiwa
kuendelea kuishi maisha yenye faida kwa watu wote.
27. Kuwa na uhakika kuwa kusudi la maisha
yako linaendelea kuwa halisi lakini pia na njia unazotumia kulifikia kusudi
hilo hazina athari kwa wengine. katika kila hatua jiulize maswali haya: Je nini
nahitaji kupata katika maisha haya? Kwa nini nahitaji kupata kitu/vitu hivi? na
Je njia ninazotumia kupata vitu hivyo ni halali? Ni rahisi sana kupata kusudi
la maisha yako lakini vigumu kuliishi kwa kuzingatia njia na sababu
zinazokusukuma kuishi kusudi hilo.
28. Sherekea kusudi la maisha yako na ona
fahari ya kuliishi kwa watu wanaokuzunguka. Hii ni kutokana na ukweli kwamba
kusudi la maisha yako ni zawadi tena zawadi ambayo unapaswa kuitumia kwa faida
ya wengi.
29. Hakikisha zawadi ya kusudi la maisha
yako inarithiwa na vizazi na vizazi. Wafanye watoto wako na jamii nzima
ijufunze kutoka kwako na hata pale ambapo ukomo wa maisha yako utaisha utakuwa
umeacha alama kwa wengine.
Mpendwa
rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri, haya ni machache kati ya
mengi ambayo nimejifunza kwenye Noble Purpose, naamini kama
utayafanyia kazi yataboresha maisha yako. Niendelee kukuomba usambaze jumbe
hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye
tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza
makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki
za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win~Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: 0786881155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com