Ardhi ni Mali. Fahamu Kwa Nini Unapaswa Kuwekeza Kwenye Ardhi - Sehemu ya Kwanza

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Nimatumaini yangu kuwa unaendelea vizurio kwa ajili ya kuyaboresha maisha yako. Karibu tena katika makala yangu ya leo ambapo nitakushirikisha mambo muhimu juu ya uwekezaji kwenye rasilimali ardhi. Ndiyo namaanisha ardhi hii ambayo pengine hukuwahi kujua kuwa ni rasilimali ambayo itakuwezesha kufikia ndoto zako. 

Leo hii katika sehemu ya kwanza nitakushirikisha umuhimu wa kumiliki ardhi na makala itakayofuatia itahusu aina ya uwekezaji ambao unaweza kufanya pindi unapokuwa tayari unamiliki ardhi. Karibu fahamu siri ambazo zitakufanya uwe kati ya wamiliki wa ardhi:

1. Kuongezeka kwa idadi ya watu. Takwimu za idadi ya watu kwa dunia zinaonyesha kuwa inakadiriwa ifikapo 2050 idadi ya watu itaongezeka hadi kufikia bilioni 9.9 ikilinganishwa na bilioni 7.4 kwa mwaka 2016. Kwa Tanzania idadi ya watu pindi tunapata uhuru (1960) ilikuwa milioni 10.1 ikilinganishwa na makadirio ya idadi ya watu milioni 48.8 kwa mwaka 2016. 

Rafiki yangu naamini mpaka sasa kutokana na takwimu za kuongezeka kwa idadi ya watu tayari umepata picha ya kwani nini nakuhamasisha umiliki ardhi. Kama bado haujapata picha kwa kifupi leo hii naomba nikudokeze kuwa kadri idadi ya watu inavyoongezeka ndivyo watu hawa wanahitaji chakula, wanahitaji sehemu za makazi na biashara au uwekezaji. Hivyo ni wajibu wako sasa kuhakikisha unatumia fursa hii ya kuongezeka kwa idadi ya watu kwa kuweka maandalizi mapema ya kumiliki ardhi ambayo unaweza kuitumia kwa ajili ya uzalishaji wa chakula, mazao ya biashara au uwekezaji wa majengo ya biashara na makazi.

2. Kukua kwa kasi kwa miji na majiji. Kadri miji au majiji yanavyokuwa ndivyo na mahitaji ya chakula, bidhaa za mifugo na mahitaji ya ardhi ya makazi na uwekezaji inavyozidi kuongezeka. Naamini mpaka sasa wewe umekuwa shuhuda wa namna ambavyo maeneo mengi yaliyokuwa ni senta za kawaida kwa sasa unakuta tayari senta hizo ni miji midogo. Kwa sasa miaka kumi ni mingi sana kwa ukuaji wa vijiji na mitaa. Kama nilivyotangulia kusema kuwa ukuaji wa miji na majiji unambatana fursa kibao hasa kwenye sekta ya ardhi wanaonufaika na fursa hizo ni wale ambao walijiandaa mapema kwa kumiliki maneo hayo au maeneo ya karibu na miji hiyo kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji. Amua sasa kumiliki ardhi kwa ajili ya kunufaika na fursa hizi.

3. Ardhi inapanda thamani kwa muda mfupi. Rafiki naamini kuwa umewahi kuwasikia watu wakisema maeneo haya miaka ya nyuma yalikuwa yanapatikana kwa bei sawa na bure. Lakini kwa bahati mbaya ukimuuliza ulifanikiwa kununua ekari ngapi au viwanja vingapi anaishia kukuambia kuwa kipindi hicho maeneo hayo yalikuwa ni maporini hivyo wala hakujali kukunua na pengine ataishia kusema ningejua kuwa yatakuwa ya thamani kiasi hiki ningenunua. 

Hivi ndivyo inavyokuwa watu wanakumbuka shuka kumekucha. Thamani ya ardhi ndani ya miaka mitano inaweza kuongezeka hata mara tano ya kiasi ulichonunulia lakini kwa bahati mbaya ni wachache sana ambao wamekuwa na mtazamo wa kuchangamkia fursa hizi. Binafsi huwa ninapenda sana Kanisa Katoliki kwa mtazamo wake kwenye ardhi, ukitembelea maeneo mengi utakuta wanamiliki maeneo makubwa sana tena katikati ya miji. Hivyo rafiki yangu ninakushauri uwe na uchu wa ardhi kama wa Kanisa Katoliki. Changamkia fursa ya ardhi maeneo ya vijijini na mijini pia kwa kadri uwezavyo baada ya miaka mitatu hadi mitano nakuhakikishi utakuja kunipa neno la shukrani.

4. Ardhi ni mali hisiyooza wala kuhamishika. Hii ni faida nyingine ya uwekezaji kwenye ardhi. Unaweza kununua ardhi kwa sasa na husiifanyie chochote mpaka pale ukishajiweka sawa ndo unaweza kuanza kutumia rasilimali hiyo kitu ambacho ni kinyume na uwekezaji wa aina nyingine. Na uzuri mwingine wa ardhi ni kwamba haihamishiki hivyo unaweza kukunua sehemu yoyote ile na kukamilisha taratibu za umiliki na hakikisha unapanda mazao ya kudumu kama vile miti, migomba, mibuni, michikichi au minazi kama alama yako ya kudumu kiasi kwamba hata kama ukihama siku ukirudi utakuta ardhi yako ikiwa bado inakusubiria. Muhimu hakikisha kabla ya kuondoka tafuta msimazi ili kuepuka kurudi ukakuta imevamiwa.

5. Ni uwekezaji ambao hautaji mtaji mkubwa. Hadi sasa kuna maeneo mengi nchi hii ambayo ukiuliza bei ya ekari moja utashangaa kiasi cha fedha utakachotajiwa. Maeneo mengi hasa vijijini ardhi bado inapatikana kwa bei ya chee kiasi kwamba ukiwa na milioni moja unaweza kununua ardhi si chini ya ekari tano kwenda juu.

Haya ni machache kati ya mengi ambayo nimekushirikisha juu ya umuhimu wa kumiliki ardhi. Karibu katika mtandao wa fikra za kitajiri kwa ajili kuendelea kupata hamasa na ushauri utakaokuwezesha kuishi ndoto za maisha yako. 


Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi. Nakutakia mapambano mema.

Ili kupata makala za namna hii moja kwa moja kwenye barua pepe BONYEZA HAPA. 

Karibuni kwenye fikra tajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win~Dream Big

Augustine M. Bilondwa
0786881155
fikrazatajiri@gmail.com



Karibu Ujiunge na Mtandao wa Fikra za Kitajiri 

* indicates required

onclick='window.open(