Karibu nikushirikishe mambo 25 niliyojifunza kwenye kitabu hiki ambacho kimeandikwa na Michael Neill. Mwandishi wa kitabu hiki ni mwanafamanikio na kocha bora kwenye masuala ya kuhamasisha watu kuishi ndoto zao kwa kipindi cha miaka 20 sasa. Katika kipindi hiki mwandishi amefanikiwa kuwa kocha, mshauri na mhamasishaji wa kimataifa kwa watu wenye nia ya kuishi ndoto zao katika maisha yao ya kila siku (biashara, kazi na kiroho).
Kwa ujumla kupitia kitabu hiki mwandishi anatushirikisha siri kumi ambazo zinaweza kutumiwa na kila mtu na hatimaye kumbadilisha mtu yeyote yule anayefanyia kazi mafundisho haya. Mwandishi kupitia kitabu hiki anatuhamasisha mafanikio yanayoanzia ndani mwa mtu (fikra) na hatimaye kujidhihilisha katika maisha ya kila siku. Pia anatushirikisha kuwa kila mmoja wetu alizaliwa akiwa na furaha na hivyo ni ndivyo makusudi ya maisha. Karibu tujifunze wote mambo muhimu 25 niliyojifunza kwenye kitabu hiki;
1. Mwandishi
anatufundisha kuwa kuna hatua tatu za mabadiliko ambazo mtu anapitia ili
kufikia viwango vya mafanikio. Na hatua hizi zote zinahusisha mabadiliko ya
ndani ambayo upelekea mabadiliko ya mfumo mzima wa maisha ya mhusika. Hatua hizo
ni:-
2. Hatua
ya kwanza ni mabadiliko kwenye tabia au changamoto husika – hapa ni pale mtu
yupo tayari kumtafuta mshauri ambaye atamsaidia kumpa maelekezo yatakayosaidia
kubadilisha tabia/changamoto ambayo imekuwa ikimkwamisha kufikia malengo yake.
Mfano, mtu anaweza kutafuta ushauri wa jinsi gani anaweza kukabiliana na
changamoto za kikazi, msongo wa mawazo, uvivu au uzembe. Mwandishi anatufundisha
kuwa hatua hii inatumika kubadilisha mtazamo wa mtu, fikra au matendo na katika
hatua hii watu wanabadilika kutoka kwenye kuwa na hofu na kujiamini, kwenye
maudhi na kuridhika au kutoka kwenye kutokuchukua hatua na kuanza kuchukua
hatua.
3. Hatua
ya pili inahusisha mabadiliko katika sehemu maaluma ya maisha – hapa ni pale ambapo mtu anahitaji
kukabiliana na tatizo linalomsumbua katika maisha yake ya kila siku au jamii
inayomzunguka. Mfano, mtu anaweza kuwa anahitaji kuboresha
maisha yake kwenye sekta ya mahusiano, mauzo, malezi, kujiamini n.k. katika
hatua hii muhusika anakuwa na programu ya kubadilisha sehemu ya maisha yake
ambapo anaweza kusoma vitabu au makala yanayohusiana na changamoto aliyonayo.
4. Hatua
ya mwisho inahusisha mabadiliko ya jumla
– hatua hii inahitimisha mabadiliko ya jumla katika mfumo mzima wa maisha
ya mhusika. Katika hatua hii muhusika anabadilika moja kwa moja kutoka kwenye
hali yake ya awali na kuingia kwenye ulimwengu mpya wa kusudi la maisha yake.
Hivyo katika hatua hii mtu anabadilisha mazoea yake yote katika kila nyanja ya
maisha. Mfano, mabadiliko ya jinsi mtu anavyojitazama mwenyewe, kujiamini na
mtazamo wake kwa watu wanaomzunguka. Hata hivyo, hatua hizi zinategemeana na
katika kila hatua lazima mhusika awe tayari kubadilika ndani mwake ili hatimaye
mabadiliko hayo yajitokeze katika mfumo wa maisha ya nje.
5. Mabadiliko
yoyote kwenye maisha ya mtu ili yadumu ni lazima yajengwe kwenye mfumo wa
maisha unaolenga kuwa na mafanikio ya muda wote (life time success). Ili
kufanikiwa katika mabadiliko ya namna hii ni lazima mfumo mpya wa maisha uambatane
na vitendo. Pia, kufanikisha mfumo wa namna hii ni lazima mhusika aishi maisha
ya furaha yanayoleta hamasa kwani hamasa huleta shauku na kwa pamoja hamasa na
shauku huleta maisha yenye kila aina ya mafanikio.
6. Ukiamini
juu ya jambo flani kwa kipindi kirefu na ukaweza kuliona jambo husika katika
picha kuna uwezekano mkubwa wa kuona uhalisia wa jambo hili katika maisha yako.
Kwa maana hii yale tunayoyawaza kwa muda mrefu na kuyajengea imani ndo yanaamua
mwonekano wa maisha yetu katika ulimwengu huu. Imani zetu juu ya maisha, fedha,
furaha na mazingira yanayotuzunguka zina nafasi kubwa ya kuamua jinsi maisha
yetu yalivyo. Hivyo yale tunayoyaona, yale tunayoyasikia, yale tunayoyafanya na
yale tunayoyahisi ni matokeo ya fikra na mtazamo wetu juu ya mambo hayo.
Jifunze kuona ukweli/uchanya katika kila hali au tukio unalokutana nalo.
Soma: Hii Hapa Kauli Mbiu Ambayo Nakusihi iwe Mwongozo wako kipindi chote cha mwaka 2017
Soma: Hii Hapa Kauli Mbiu Ambayo Nakusihi iwe Mwongozo wako kipindi chote cha mwaka 2017
7. Kitu
chochote kinachotokea katika maisha yetu ni lazima kianzie kwenye mfumo wa
mawazo na baadaye ndo kinajidhihirisha kwenye mfumo wa hisia. Ubongo kupitia
kwenye milango mitano ya fahamu unapokea taarifa na kuzihifadhi ndani ya mfumo
wa fikra/mawazo. Kinachowatofautisha watu ni namna gani tunavyotafsiri taarifa
hizi na jinsi zinavyofanyiwa kazi kwa kila mmoja wetu. Kwa maana nyingine chochote
katika dunia hii kipo jinsi kilivyo kutokana na fikra/mtazamo wetu juu ya kitu
hicho. Hakuna jambo baya au zuri bali mtazamo wetu juu ya ubaya au uzuri wa
jambo husika ndo unalifanya jambo hilo lionekane baya au zuri.
8. Matarajio
yako hujenga uzoefu wako. Kwa maana hiyo wewe ni muumbaji mkuu wa yale
yanayotokea kwenye maisha yako ya kila siku. Kama ambavyo tunameona kuwa kile
unachokiwaza ndicho unachoishi, vivyo hivyo matarajio yetu kwa maisha ya baadae
ndo yanatujengea uzoefu kwa maisha ya sasa. Lakini habari njema ni kwamba kila
mmoja wetu anaweza kubadili matukio ya maisha yake kwa kubadili fikra/mtazamo
wake.
9. Mara
nyingi tumekuwa tukiangalia michezo ya filamu na hatimaye kuona ile michezo
katika uhalisi wa maisha yetu. Vilevile mwandishi wa kitabu hiki anatufundisha kuwa
maisha yetu tunaweza kuyaona katika mfumo wa mchezo wa filamu huku sisi tukiwa
ni wahusika wakuu (stering) wa hiyo filamu. Jipe muda wa kutafakari juu ya
umahili wa mhusika mkuu wa filamu ambayo ulitokea kuikubali sana kati filamu zote
ambazo umeangalia na tafakari jinsi gani mhusika mkuu alivyokuwa imara katika
kukwepa vikwazo mbalimbali hadi akakufanya uwe na hisia kana kwamba maisha yake
ya kila siku yapo jinsi alivyocheza katika filamu hiyo. Baada ya kupata picha
hiyo jitafakari wewe kama mhusika mkuu wa filamu ya maisha yako, ona jinsi
unavyokwepa vikwazo na jinsi unavyosherekea ushindi katika kila sekta ya maisha
yako na hatimaye tafakari jinsi unavyomaliza filamu hii kwa ushujaa wa hali ya
juu. Mwisho kama mhusika mkuu ione filamu ya maisha yako kwa jinsi
unavyofanikiwa au kushindwa kwenye sekta ya mahusiano, uhuru wa kifedha, kuwa
baba au mama bora, jinsi gani watu wanakuwa wema au wabaya kwako, jinsi gani
unafanikiwa kwenye ulimwengu wa kiroho na kijamii, jinsi unavyofanya kazi au
biashara zako, jinsi unavyomiliki majumba na magari ya kifahari pia ione picha
inayokujia ukikabiliana na changamoto za kiafya na mengine mengi.
10. Mwandishi
wa kitabu hiki anatufundisha kuwa kila mmoja wetu ni muumbaji na uumbaji huu
umejengwa kwenye misingi na kanuni. Hivyo ili kila mmoja wetu afanikiwe kuwa
muumbaji bora ni lazima kwanza ajifunze misingi na kanuni hizo. Na uumbaji wa
aina yoyote ile ni lazima pawepo vitu vitatu;
Moja: uwepo wa nishati (Energy); Na hii ni
sheria ya asili ambayo tayari wanafizikia walishaiweka wazi kuwa kila kitu
tunachoweza kusikia, kuona, kuhisi, kuonja, kuongea au kugusa ni lazima pawepo
nishati au chanzo kama kisababishi kikuu. Na nishati hii ndio imewezesha uumbaji
wa vitu vyote hapa duniani.
Mbili: Ufahamu (Consciousness); Kupitia
ufahamu tunaweza kujitofautisha sisi wenyewe kutoka kwa wengine, tunaweza
kutofautisha kitu kimoja na kingine, vilevile tunaweza kutofautisha sauti,
milio, rangi n.k. Hivyo uwezo wetu katika kuumba vitu unategemea mazoea
tulionayo kwenye kutofautisha vitu vinavyotuzunguka.
Tatu: Mawazo/fikra (Thought); Mawazo
au fikra katika uumbaji yanachangia pale ambapo yanakaa katika akili ya mtu kwa
muda mrefu na hatimaye mhusika kuyatafsiri katika vitendo kwa kutumia nishati
na ufahamu wake. Kwa maana hii tunaweza kupata kanuni ya uumbaji ambayo ni;
Uumbaji = Nishati + Ufahamu + Mawazo.
Kwa
kifupi; katika uumbaji wa vitu tunapaswa kufahamu kuwa ni lazima pawepo sababu
au kisababishi cha kwanini tunataka kufanya hivyo – unaweza kuiita nishati au
chanzo, pili lazima pawepo nia au nguvu inayokusuma katika kubuni vitu – hii
ndo mawazo/fikra na mwisho ni lazima pawepo uzoefu na uelewa wa vitu au
mazingira yanayokuzunguka – hii ndo ufahamu.
11. Mwandishi
anatufundishi kuwa kama unataka kuwa muumbaji bora ni lazima uepuke malalamiko.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba malalamiko ni kinyume cha uumbaji na hivyo
kadri unavyolalamika ndivyo unavyodumaza karama zako za uumbaji wa vitu. Hivyo
kama tunavyofanya mfungo (fasting) kwa ajili ya kuyatafakari matendo yetu mbele
ya mwenyezi Mungu ndivyo tunatakiwa kujiweka kwenye mfungo wa malalamiko
(complaint fasting) kwa muda wote maisha yetu. Katika kila tukio ambalo
ulitakiwa kulalamika jiulize ni kipi unaweza kufanya au kujifunza kupitia tukio
husika. Mtu anaanza kuwa muumbaji bora pale anapotambua kuwa kila jambo
linaanzia ndani mwetu; uzuni, furaha, msongo wa mawazo, hamasa na shauku vyote
hivi vinaanzia ndani mwetu kama vile maandiko matakatifu yanavyosema kuwa sio
kimuingiacho mtu ni najisi bali kimtokacho mtu.
Pata
mapumziko na stori hii
“Hapo zamani Muumbaji alitaka kuficha ujumbe kwa wanadamu na hivyo akavikusanya viumbe vyote hisipokuwa mwanadamu na kuviuliza ni wapi ambapo anaweza kuficha ujumbe huo. Ndege aina ya Tai alikuwa wa kwanza kumshauri kwa kusema nipe ujumbe huo nitaruka juu ya milima na kuuficha huko na binadamu hawataweza kufika huko. Muumbaji akasema hapana, binadamu ni wabunifu siku moja watatawala milima na mwishowe wataweza kuuona huu ujumbe. Samaki aina ya papa akasema nipatie ujumbe huu nami nitauficha kwenye kina kirefu cha bahari nao hawataweza kuuona, Muumba akasema hapana binadamu wataweza kufika huko na hatimaye watafanikiwa kupata huo ujumbe. Faru akasema nipe huo ujumbe nami nitaufukia ardhini katika maeneo ya nyika ambapo mwanadamu hawezi kuuona, Muumba akasema hapana nyikani ni rahisi sana kwa mwanadamu kupafikia na siku moja wakati akichimba uso wa dunia ataweza kupata huu ujumbe. Ndipo muumba akawa amekata tamaa kwa ushauri anaopewa. Hatimaye fuko aliye kipofu na mzee akasema kwa nini ujumbe huo husiuweke ndani mwao kwani sehemu hii ndo sehemu ya mwisho kwao kuangalia! Muumba akakubali na kusema huo ni ukweli. Je kwa mtazamo wako hii ni kweli? Majibu unayo.
12. Kuna
hatua mbili zinazotutofautisha nazo ni hatua ya “kiini” (essence) na hatua ya “binafsi” (persona).
Katika hatua ya kiini wote tunakuwa sawa, mfano, wote tunahitaji kupenda au
kupendwa, sote tunataka kuwa na faraja, wote tunaka kuwa na maisha yenye kila
aina ya furaha na amani. Lakini tunakuja kuachana kwenye hatua “binafsi”,
katika hatua hii tofauti yake na hatua ya “kiini” ambayo kila mmoja wetu
amezaliwa nayo ni kwamba hatua hii ya pili inahitaji kutengenezwa na kuboreshwa
kupitia mazoea yetu ya kila siku. Hivyo hapa ndipo tunaona makundi ya watu
tofauti katika jamii yetu kutokana na jinsi wanavyojiendeleza ili kuboresha
hatua hiyo ya pili.
13. Kwa uzoefu maisha ya
mwanadamu yanazungukia kati ya maisha ya furaha na maisha ya huzuni. Ili kuyafurahia maisha ni lazima ujifunze kutumia muda mwingi
kwenye sehemu ya furaha kuliko sehemu ya huzuni. Kuwa na maisha ya furaha sio
lazima uwe na utajiri wa majumba, magari, fedha au mashamba kwani wapo watu
wengi wenye vitu hivyo lakini rohoni mwao wana huzuni. Hivyo maisha ya furaha
yanaanzia rohoni mwako na wewe ni mwamuzi mkuu wa aina ya maisha unayoyataka.
Na siri kubwa ya kuishi maisha ya furaha ni kutenda matendo mema katika jamii
inayokuzunguka.
14. Ili
uishi maisha ya furaha ni lazima ujifunze kuwaza katika hali chanya ili
kuhakikisha kuwa unadhibiti mawazo hasi ambayo yanasababisha maisha ya uzuni.
Watu wengi wameshindwa kuishi maisha ya furaha kwa kudhani kuwa furaha ni kitu
kinachotoka nje ya uwezo wao. Huu ni mtazamo potofu kutokana na ukweli kuwa
furaha/uzuni ni ile hali ya maisha ambayo mtu ameamua kuishi.
15. Kwa kutumia sheria ya asili ya mvutano (the law of attraction) ambayo inasema fafana uvuta fanana (like attracts like) vivyo hivyo fikra/mawazo uleta vitu na sisi ni matokeo yale tunayoyawaza kwa muda mrefu. Katika maisha ya mafanikio tunatakiwa kutumia sheria hii kuishi maisha ya furaha kwani kwa kufanya hivyo tutavuta vitu vingi na watu wengi kwa yale tunayoyafanya. Kufanikiwa katika sheria hii ya asili tunatakiwa kuhakikisha kuwa mawazo, hisia, nia na matamanio yetu tunayaweka kwenye yale tunayoyataka yatokee katika maisha yetu.
16. Ili uishi maishi ya furaha ni lazima ujenge tabia ya kuridhika na hali au vitu ulivyonavyo kwa sasa. Baada ya kujenga tabia ya kuridhika unatakiwa uwe na mfumo mpya wa maisha ambao utakuongoza kupata matokeo makubwa sana huku ukiendelea kufurahia jinsi ulivyo na yale unayoyafanya.
17. Njia rahisi ya kufanya maamuzi katika maisha yetu ni kila tufanyapo maamuzi kukumbuka kuwa maamuzi yetu kamwe hayaathiri maisha yetu bali kinachoathiri maisha ni jinsi gani tunavyokabiliana na matokeo ya uamuzi wetu. Mfano, unaweza kukosea kuchagua kazi lakini athari ni kuendelea kufanya kazi husiyoipenda kwa zaidi ya miaka mingi. Kwani katika kipindi hiki utaendelea kuishi maisha ya kulalamika na hatimaye kukosa furaha ya maisha kwa kipindi chote hicho. Hivyo tunapofanya maamuzi ni lazima tujiulize jinsi tukavyokabiliana na athari za matokeo ya maamuzi yetu. Njia bora ya kufanya hivyo ni kuhakikisha tunafanya maamuzi yanayoridhisha na kujitoshereza kukidhi mahitaji ya tukio husika pasipo kujali maamuzi hayo yamepelekea uchaguzi ulio bora au la kwa wakati huo.
18. Hisia ulizonazo kwenye maisha yako ya kila siku ni mwitikio wa moja kwa moja wa fikra/mawazo yako na sio kwa sababu ya mazingira yanayokuzunguka. Kama unataka kudhibiti hisia zako ni lazima ujifunze kudhibiti fikra zako. Na kadri unavyogundua kuwa hisia zako ni matokeo ya fikra zako ndivyo unatakiwa kujifunza kudhibiti fikra ambazo zimekuwa zikipelekea ufanye vitu unavyojutia mara baada ya kuvifanya. Kutokana na mtazamo huu hakuna kitu kama “siku flani kuwa mbaya au mwaka wenye namba flani kuwa mbaya”. Kwa mfano, Jamii imezoea kuwa miaka inayoishia na namba ambazo sio shufwa kuwa ni miaka yenye mikosi. Pia, tumezoea kusikia kuhusu siku ya Jumatatu na Ijumaa kuonekena kama siku zenye uzalishaji mdogo. Huo ni uongo ambao tokea sasa unatakiwa kuukimbia kwani hizo ni hisia ambazo zimetokana na fikra zetu. Siku njema unaiandaa mwenyewe kwani sio siku inayoandaa hali ya akili yako (mood) bali hali ya akili yako ndiyo inayoiandaa siku. Ondoa fikra hasi kwenye akili yako na hatimaye utakuwa na siku njema daima.
19. Kila kitu unachoamua kufanya au kutokufanya ni uchaguzi wa maamuzi yako. Swali muhimu la kiujiliza katika maamuzi yetu ni kwa nini tunafaya yale tunayoyafanya? Au kwa nini kuna mambo mengine huwa hatufanyi? Mara nyingi tunafanya vitu kwa matarajio ya baadae. Mfano, tunafanya kazi ili tupate kula na tunakula ili tuendelee kuishi. Jambo la msingi katika maisha ya mafanikio ni kujenga misingi ya kutuongoza kwa yale tunayopaswa kuyafanya na yale ambayo hatupaswi kuyafanya. Na kutekeleza misingi hii katika maisha yetu ya kila siku ni lazima tuongozwe na nidhamu binafsi. Hivyo, maisha ya mafanikio yamejikita katika kufanya yale tunayoyapenda na kuepuka yale ambayo hatuyapendi au tunayafanya kwa manunguniko.
20. Tunatengeneza watu kwa maana ya kuwapa motisha kadri tunavyowasikiliza. Na tunavyowasikiliza wenzetu ndivyo tunavyojifunza kutoka kwao. Kadri tunavyo wasikiliza ndivyo tunavyo waweka karibu na mfumo wa fikra zetu na hivyo tunatengeneza picha zao katika mfumo wetu wa akili. Hivyo jifunze kuwasikiliza watu wa karibu na wewe, mwenza wako, watoto, wazazi, wafanyakazi wenzako, waajiriwa wako na marafiki ili kwa kufanya hivyo utajifunza mengi kutoka kwao na hatimaye nao watabadilika. Hata hivyo, unapowasikiliza watu huna budi kuchambua yale ambayo yanaendana na falsafa za maisha yako.
21. Unaweza kuomba kitu chochote kutoka kwa mtu yeyote pasipokujali utapewa jibu la ndio au hapana. Mfano, kama unatangaza biashara au bidhaa za namna yoyote ile husikatishwe tamaa na jibu la HAPANA kutokana na ukweli kwamba kati ya watu ambao utawafikia kuna ambao watakuwa tayari kukusikiliza. Kama tulivyoona kuwa furaha inatoka ndani mwetu vivyo hivyo hata yale tunayotaka lazima yaanzie ndani ya nafsi yetu na tukifanya hivyo ulimwengu upo tayari kutupa vyote tutakavyoomba kulingana na imani na jitihada zetu. Tunapoomba tunatakiwa kuzingatia kanuni nane:-
- Omba ukiwa na imani ya kwamba utapata na si vinginevyo;
- Omba kwa mtu ambaye unahisi anaweza kukupa kile unachohitaji;
- Kuwa wazi na moja kwa moja eleza unachoitaji;
- Omba kwa ucheshi na ubunifu;
- Omba kutoka rohoni mwako;
- Kuwa tayari kutoa chochote kwa ajili ya kupata kile unachohitaji;
- Husichoke kuomba bali omba mara kwa mara; na
- Kuwa tayari kupokea HAPANA au NDIYO kwa furaha.
22. Uhuru
wa kifedha hautokani na kiasi cha fedha ulichonacho kwa sasa bali unatokana na uwezo
wako wa kupata zaidi ya kiasi hicho wakati wowote pale unapotaka. Hii ni kutokana
na ukweli kwamba fedha ni sawa tu na bidhaa nyingine kama vile mbao, chuma,
mchanga, nyama n.k. Tofauti ya fedha na bidha nyingine ni kwamba unaweza
kutumia fedha kupata bidhaa hizo au ukatumia bidhaa hizo kupata fedha. Kupata kiasi
chochote cha fedha unachohitaji kwa wakati wowote inategemea uwezo na ufahamu
wako juu ya fedha na bidhaa zinazokuzunguka.
23. Hali ya maisha yako hisipimwe kwa kiasi cha fedha ulichonacho mfukoni au kwenye akaunti yako. Ili uwe na uhuru wa kifedha ni lazima kuweka misingi ya kuitawala fedha ili kwa kufanya hivyo maisha yako yaendeshwe na misingi hiyo na wala sio kiasi fedha ulichonacho.
24. Jifunze sanaa ya kuwatumikia wengine ili uwe na uhuru wa kifedha hapo baadae. Kwa maana nyingine kila unachofanya fanya kwa mapenzi yako juu ya hicho unachofanya nasi kwa ajili ya kupata fedha bali fedha zikufuate baadae. Ili kufanikisha siri hii unatakiwa kujiuliza thamani ya yale unayoyafanya kama yanagusa jamii inayokuzunguka. Kama unayoyafanya yana thamani ndogo kwenye jamii inayokuzunguka itakuwa sio rahisi kwako kuwa na uhuru wa kifedha.
25. Kuwa na tumaini la maisha yako. Tumaini jema la maisha lina nafasi kubwa ya kuwezesha ndoto zako, kuonyesha mianya ya fursa zilizopo na kukuwezesha uishi zaidi ya mipaka ya tamaduni za jamii inayokuzunguka. Hii ni kutokana na ukweli kwamba tumaini jema linakupa nafasi ya kupanga yale unayoyataka yatokee katika maisha yako ya baadae huku ukiendelea kutekeleza ndoto za maisha yako.
Haya ndiyo niliyojifunza katika kitabu hiki. Ni matumaini yangu kuwa ukiyafanyia kazi yatabadilisha maisha yako kwa ujumla. Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi. Nakutakia mapambano mema.
Ili kupata makala za namna
hii acha taarifa zako kwa kujaza fomu hapo chini.
Karibuni kwenye fikra
tajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.
Born to Win~Dream Big
A.M.
Bilondwa
0786881155
fikrazatajiri@gmail.com
0786881155
fikrazatajiri@gmail.com