Habari ya leo rafiki na
msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
vizuri na mapambano kwa ajili ya kuyaboresha maisha yako. Leo hii tukiwa kwenye
wiki ya tano ya mwaka 2017 naendelea kutimiza ahadi yangu ya mwaka 2017 ya kukuletea
uchambuzi wa kitabu kimoja kila mwisho wa wiki (ijumaa) ili kupitia vitabu hivi
pamoja tuweze kuboresha maisha yetu.
Kitabu cha leo kimeandikwa
na waandishi mahiri saba (7) ambao kwa pamoja wanatushirikisha yale ambayo
wamekuwa wakifanya katika safari zao za maisha ya utajiri (uhuru wa kifedha).
Kitabu hiki kimehaririwa na Donald J. Trump ambaye ndiye Rais wa sasa wa
Marekani ambaye pia ni mwanzilishi wa Chuo Kikuu cha Trump (Online Trump
University). Kitabu hiki kinatushirikisha misingi ya mafundisho ambayo utolewa
katika Chuo Kikuu cha Trump kupitia uzoefu wa yeye mwenyewe Trump pamoja na
washirika wake.
Katika kitabu hiki, kwa
ujumla waandishi wanatushirikisha kuwa maisha ya utajiri yanajengwa kwenye
misingi ya kujifunza na kutumia mbinu za maarifa mapya kwa ajili ya kukuza utajiri
wako na hivyo ni wajibu wa muhusika kujielimisha kila iitwapo leo. Hata hivyo,
waandishi hawa wanatushirikisha hatua saba ambazo kila mtu anaweza kuzitumia
kama anataka kuwa tajiri. Karibu tusafiri pamoja kwa ajili ya kujipatia maarifa
mapya kupitia machache niliyojifunza kupitia waandishi wa kitabu hiki;
Hatua
ya Kwanza: Kuwa na Fikra za Kitajiri (Na Donald
J. Trump na Marshall Sylver)
1. Kuwa
na fikra zenye mapana (think big). Mwandishi Donald J. Trump anatushirikisha
umuhimu wa kuhakikisha tunakuwa na fikra pana kutokana na ukweli kwamba ukiwa na
fikra finyu matokeo yake unaishia kufanya vitu ambavyo ni vya kawaida. Kama
unataka kuwa tajiri ni lazima uwe na fikra pana ambazo zitakusuma kufanya vitu
vikubwa vitakavyopelekea ushindi wa hali ya juu katika maisha yako. Hata hivyo,
unaweza kuanza na hatua fupi fupi huku kichwani mwako ukiwa na fikra pana za
hatua ndefu ambazo ndo injini ya maisha ya utajiri. Ili uwe na fikra pana unatakiwa
kujiuliza vitu vitatu ambavyo ni (i) Jiulize kwa nini una mipango finyu? (ii)
Fikria zaidi jinsi ya kuboresha maisha yako ya baadae na sio kutumia nguvu
nyingi kwenye yaliyopita (historia yako) na (iii) fikria zaidi kwenye suluhisho
na sio changamoto tu.
Soma: Mambo 25 Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha Keys to Leadership (Misingi ya Uongozi)
Soma: Mambo 25 Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha Keys to Leadership (Misingi ya Uongozi)
2. Kuwa
na fikra pevu juu ya fedha zako. Watu wengi wamekuwa na fikra hasi juu ya
matumizi ya fedha zao kwa kudhani kuwa fedha zinatakiwa zilindwe ili ziishe na
hivyo wanashindwa kutumia fedha walizonazo kuzalisha fedha nyingine. Kama
unataka kuwa tajiri lazima uwe tayari kuifanya fedha yako ikuzalishie fedha za
ziada kutokana na ukweli kwamba fedha inatakiwa ikutumikie wewe na sio wewe
kuwa mtumwa wa fedha.
3. Kama
unataka kuwa milionea unapaswa kufanya kazi ambazo zina ujira mzuri na
unazipenda kutoka rohoni mwako. Hapa tunafundishwa kuwa matajiri wanatumia
vyema muda wao kwa kuhakikisha kuwa kila sekunde katika muda wao ina thamani katika
kuongeza vipato vyao. Kamwe hauwezi kuwa tajiri kama unafanya kazi ambazo
hazileti tija halisi ya thamani ya muda wako kutokana na ukweli kwamba fedha ni
hesabu ambazo msingi wake mkuu ni matumizi ya muda wako. Mamilionea muda wote
wanajiuliza ni kipi chenye thamani kubwa wanaweza kufanya kwa ubora wa hali ya
juu katika kila dakika ya maisha yao.
Muhimu chukua kalamu na karatasi na
fanya mahesabu ya jumla ya masaa unayofanya kazi kwa wiki na hatimaye kwa
mwaka. Baada ya kufanya hivyo kila lisaa lipe thamani ya fedha mabayo inapaswa
kuwa wastani wa masaa yote unayofanya kazi kwa wiki halafu zidisha wastani huo
kwa siku za kazi kwenye wiki na hatimaye zidisha idadi ya wiki ambazo unahisi
ni za kazi kwa mwaka mzima. Tathmini matokeo ya kiasi cha fedha utakachopata
kama kinakupeleka kwenye maisha ya utajiri ama sivyo na chukua hatua za
kuboresha zaidi ili kufikia maisha ya utajiri. Katika yote haya unatakiwa
kukumbuka kuwa muda ni zawadi pekee ambayo watu wote tumepewa sawa bila kujali
wewe ni masikini au tajiri, tumia zawadi hii kufikia mafanikio makubwa sana
katika maisha yako.
4. Ili
uwe tajiri ni lazima uongeze thamani ya muda wako kwa kufanya vitu ambavyo kila
mtu yupo tayari kulipia. Hii ni kutokana na ukweli kuwa watu wapo tayari
kulipia vitu vya thamani au ubunifu ulionao kwa ajili ya faida yao. Ndio maana
hakuna mwajiri ambaye yupo tayari kumlipa mtu ambaye hazalishi chochote badala
yake wanalipia thamani ya huduma yako. Katika yote haya mafanikio yako
yanategemea fikra zako na namna ambavyo unadhibiti hisia zako.
5. Nunua
kitu unachopenda na kitumie kukuingizia kipato zaidi. Tunafundishwa kuwa
mamilionea wana tabia ya kununua vitu vile wanavyopenda kutoka rohoni mwao na
kuvitumia kwa ajili ya kujiongezea kipato zaidi. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba sio fedha, ardhi, intaneti, watu au madini vitakavyokufanya uwe tajiri
bali kitakachokufanya uwe tajiri ni nini unafahamu kuhusu vitu hivi na hatimaye
kupitia tabia zako ndo unaweza kuvitumia kufikia utajiri wa ndoto za maisha
yako.
6. Utajiri wenye furaha maishani ni ule ambao
umejengwa kwenye misingi ya imani ya kiroho. Hii ni kutokana na ukweli kwamba
kadri utakavyopata utajiri ndivyo utakuwa na fedha nyingi na za ziada ambazo
unaweza kuzitumia kwa lolote lile; kama hujajiweka sawa kiimani utajiri wako
unaweza kutumika kukumaliza kimwili na kiroho. Wote tunafahamu kuwa pasipo
misingi imara ya imani fedha zako zitakuwa za kwanza kukuweka mbali na watu
wako wa karibu, kukufanya ujiingize kwenye ulevi, anasa za mwili na mambo
mengine ya hovyo.
Hatua
ya Pili: Kuwa Makini na Mipango Yako; Njia yako ya mafanikio ya kifedha (Na John
R. Burley,)
7. Andika dira yako ya mafanikio ya kifedha. Moja
ya siri kubwa ambayo imeendelea kufanya matajiri waendelee kufanikiwa zaidi ni
uwezo wao mkubwa wa kuwa na picha kubwa ya mafanikio yao ya kifedha na hatimaye
kuitafsiri picha hiyo katika sentensi ambazo zinakuwa ni dira ya maisha yao
yote. Wengi wameshindwa kutumia siri hii kwa ajili ya kujipatia utajiri
kutokana na kukosa maarifa kama ambavyo maandiko matakatifu yanatuambia kuwa
“watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.
Dira yako ya mafanikio ya kifedha inapaswa iwe ni matokeo ya (i) picha kubwa ya maisha yako jinsi unavyotaka yawe – yale yote ambayo unataka kuyakafanikisha katika maisha yako kwa ujumla; na (ii) vipaumbele vya maisha yako kwa kuzingatia vile ambavyo vina thamani kubwa katika maisha yako.
8. Tengeneza
mpango wako wa uhuru wa kifedha. Hapa unatakiwa kuhakikisha unatengeneza tabia
za matumizi ya fedha unayoipata kwa ajili ya kuongeza kipato chako. Pia,
unatakiwa kuorodhesha hali ya kipato chako ulichonacho kwa sasa na kipato
ambacho unahisi ukikipata kitakuwezesha kuwa na uhuru wa kifedha ili kupitia
kipato hicho ufanikiwe kuishi ndoto za maisha yako. Mwandishi anatufundisha
kuwa hapa unatakiwa uandae orodha ya matumizi na kipato chako cha mwezi baada
ya kufanya hivyo uandae orodha ya madeni yako yote na hatimaye uandae mkakati
wa kulipa madeni yako yote.
9. Tengeneza
timu ya ushindi wako wa kifedha. Hapa tunashirikishwa kuwa kama ndo unaanza
kwenye uwekezaji unatakiwa uwe makini na mawakala (brokers) pamoja na washauri
wako wa kifedha kutokana na tabia ya makundi hayo kuchaji fedha nyingi ambazo
ungezitumia kwenye shughuli nyingine za kujiongezea kipato. Na pale unapotakiwa
kuwa na timu ya washauri wa kifedha hakikisha unakuwa na timu bora ambayo ina
uaminifu wa hali ya juu na ina uzeofu katika masuala ya fedha. Timu yako inaweza kuwajumuisha watu wenye taaluma ya mauzo, wahasibu au wanasheria.
Hatua
ya tatu: Anza Sasa (Na John R. Burley)
10. Kama
unataka kuwa tajiri unatakiwa uanze kujilipa kwanza kwa kila kipato unachopata.
Hakikisha unatenga kiasi cha asilimia flani kwenye kila pato lako kwa ajili ya
akiba yako ambayo kimsingi kwa baadae unaweza kutumia pesa hiyo kuwekeza kwenye
shughuli za kukuza kipato chako. Matajiri wengi wamekuwa wanatumia siri hii
kukuza utajiri wao. Tatizo kubwa ambalo watu wengi wameshindwa kutumia siri hii
ni kutokana na fikra za watu kuona kuwa fedha wanayopata ni ndogo kiasi kwamba
hawawezi kutoa fedha za kuwekeza na hivyo wanaishia kutumia kiasi chote
wanachopata pasipo kuweka akiba.
11. Tengeneza
mfumo wako wa fedha wa moja kwa moja na tumia mfumo huu kuhakikisha matumizi
yako ya fedha yanaendeshwa na mfumo huu. Kupitia mfumo huu hakikisha unaepuka
madeni yasiyo na tija kwa kuhakikisha unalipa kwa keshi unapofanya manunuzi ili
kuepuka ongezeko la bei kutokana na kununua kwa mkopo. Pia, unatakiwa
kutengeneza mpango wa kumaliza madeni yako yote ili uanze maisha mapya yasiyo
na madeni kwa ajili ya kukuwezesha kupangalia vizuri kipato chako pasipo kufikiria
mzigo wa madeni.
Soma: Mwaka 2017 Jifunze Kusema Hapana kwa Mambo haya ili Kuwa na Uhuru wa Kifedha
Soma: Mwaka 2017 Jifunze Kusema Hapana kwa Mambo haya ili Kuwa na Uhuru wa Kifedha
12. Tengeneza
bajeti ambayo itakupa uhuru wa kufanya yote ya muhimu kwako. Hapa unatakiwa uwe
na mfumo wa moja kwa moja unaokuongoza kwenye matumizi yako ya fedha. Hakikisha
kupitia mfumo huu unakuwa na uhuru wa kutekeleza vipaumbele vyako ili pesa
ikufanyie kazi na siyo wewe kuwa mtumwa wa pesa yako. Pia, unatakiwa kupunguza
matumizi ya pesa yasiyo ya lazima kwa kuhakikisha unafanya manunuzi ya vitu
muhimu tu na andika kila aina ya matumizi kwenye kijitabu chako kidogo.
Hatua ya Nne: Kuwa Bosi – Ujasiliamali Njia ya
Utajiri (Na Michael E.
Gordon, PhD)
13. Kama
unataka utajiri ni lazima uwe tayari kujiajiri mwenyewe (kuwa mjasiliamali). Hii
ni kutokana na ukweli kwamba kama umejiajiri unakuwa na uhuru wa kutosha kwenye
fikra, muda na vitendo. Hivyo ni rahisi kuendesha shughuli zako na kuzitekeleza
kwa ubunifu wa hali ya juu. Hapa tunatakiwa kutambua kuwa kila mmoja wetu ni
mjasiliamali pale anapoamua kuwa mbinufu na kuanzisha miradi kwa ajili ya
kujiongezea faida. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ujasiliamali hauna uhusiano
wowote na tabia za kurithi ambazo usambazwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine
kupitia kwenye vinasaba (genes) bali kila mtu anaweza kujifunza kuwa
mjasiliamali.
14. Husiwe
tayari kukatishwa tamaa. Katika safari ya ujasiliamali utakutana na changamoto
nyingi ambazo pengine zitapelekea kupoteza hata fedha zako kutokana na miradi
yako kushindwa kufikia viwango ulivyokusudia lakini katika yote haya haupaswi
kukata tamaa kwani kushindwa ni somo kubwa kwa mjasiliamali. Hivyo hakikisha
una roho ya kuvumilia mpaka pale ambapo utafanikisha ndoto za maisha yako. Pia
tunatakiwa kukumbuka kuwa baada kufanikisha hatua moja kuna hamasa kubwa kutoka
ndani mwetu ambayo inatutaka kuendelea kupambana zaidi kwa ajili ya mafanikio
makubwa sana.
15. Anzisha
biashara yako na hakikisha ina vitu vya tofauti ukilinganisha na wapinzani wako.
Kama unataka kuwa tajiri ni lazima uwe tayari kuanzisha biashara, wengi
tumekuwa waoga wa kuanzisha biashara zetu hasa kutokana na uoga wa kutanguliza
mahitaji ya biashara ambayo pengine kwa wakati huo tunajikuta hatuna. Katika
kitabu hiki tunahamasishwa kuwa na wazo la biashara kwanza na baadae ndipo
tugeukie kwenye mahitaji ya wazo la biashara husika.
Hatua
ya Tano: Miliki Rasilimali – Biashara ya Ardhi na Majengo Njia Yako ya Utajiri
(Gary W. Eldred, PhD)
16. Uwekezaji
kwenye ardhi na majengo ya biashara ni njia mojawapo ambayo matajiri wengi
wameitumia kukuza utajiri wao. Hii ni kutokana na upekee wa uwekezaji huu
ukilinganisha na aina nyingine za uwekezaji. Uwekezaji huu una faida nyingi
baadhi zikiwa ni kuongezeka thamani kwa kasi, kuzalisha pato kwa muda mrefu
kutoka kwa wapangaji, gharama ndogo za marekebisho, gharama ndogo za uendeshaji
na nyingine nyingi. Uwekezaji wa majengo na ardhi unaongezeka kwa kasi kutokana
na kuongezeka kwa idadi ya watu ambao wanahitaji chakula, kazi na maradhi.
17. Kabla
ya kuwekeza kwenye biashara ya ardhi na majengo hakikisha una taarifa sahihi
juu ya uwekezaji huu katika maeneo unayotaka kuwekeza. Mwandishi anatufundisha
kuwa sio ardhi au majengo yatakayokufanya uwe tajiri bali elimu juu uwekezaji
wa namna hii ndo msingi namba moja ya kukuza utajiri wako. Hivyo kama unataka
kununua ardhi au majengo hakikisha una taarifa na maarifa ya kutosha juu
umiliki na uendeshaji wa uwekezaji wa namna hii.
18. Hakikisha
unajali sana majengo yako ili kuwavutia wapangaji ambao watakuwa
ni wateja wazuri kwenye malipo. Na hapa unatakiwa kuhakikisha unakuwa na mfumo
wa utakaowezesha nyumba zako ziwe na wapangaji ambao hawasumbui kwenye malipo
pamoja na uharibifu wa nyumba zako. Husimvumilie mteja ambae anaenda kinyume na
masharti ya nyumba yako ili kuepusha usumbufu na madhara kwa wateja walio wema.
Zaidi ya yote wateja wote wanatakiwa kulipia kodi zao kwa muda ili kutoa nafasi
kwako kutekeleza majukumu mengine.
19. Panua
wigo wako wa uwekezaji kwenye majengo na ardhi kwa kuangalia maeneo mapya. Hapa
unatakiwa kuangalia maeneo mapya yenye fursa kama vile kwenye miji mipya,
maeneo ya viwanda vipya au masoko. Na muda wote unatakiwa kutafuta fursa mpya
za uwekezaji wa namna hii ili kabla wengi hawajashutuka wakute tayari
umeshajiwekeza.
Soma: Ardhi ni Mali. Fahamu Kwa Nini Unapaswa Kuwekeza Kwenye Ardhi - Sehemu ya Kwanza
Soma: Ardhi ni Mali. Fahamu Kwa Nini Unapaswa Kuwekeza Kwenye Ardhi - Sehemu ya Kwanza
Hatua
ya Sita: Wekeza Kwenye Soko la Hisa, Hatifungamani au Vipande – Njia Yako ya
Kustaafu Ukiwa Tajiri (Philip A. Springer)
20. Weka
akiba kwa kununua hisa au hatifungamani au vipande kwa kadri uwezavyo. Utajiri
ni mchakato na wala sio suala la kuamka asubuhi na kujikuta tajiri. Hivyo ni
lazima uwe na mpango wa kuweka akiba na njia nzuri za kufanya hivyo ni kununua
hisa/hatifungamani/vipande ili baada ya muda thamani ya kile ulichowekeza iongezeke.
Hata hivyo uwekezaji wa aina hii umekuwa ukipanda na kushuka hivyo unachotakiwa
kufanya ni kuwa na tazamio la uwekezaji wa muda mrefu na sio kukatishwa tamaa
na kupanda/kushuka kwa hisa/vipande kwani hilo ni suala la kawaida. Katika
mpango wako wa kuweka akiba ni lazima ujikite kwenye kutenga asilimia flani ya
pato lako kwa kila mwezi na hatimaye kwa mwaka mzima. Hivyo unatakiwa kufanya
hivyo ukiongozwa na nidhamu ya hali ya juu pasipo kujali hali ya kifedha
uliyonayo.
21. Unapowekeza
kwenye hisa hakikisha unachagua hisa za Makampuni ambayo ni imara kifedha kupitia
historia ya biashara ya kampuni husika. Hapa tunafundishwa kuwa tunatakiwa
kuchagua kampuni ambazo hazina madeni mengi na zina uwezo wa kujiendesha
kibiashara kwa faida katika siku za mbeleni. Kwa ujumla chagua kampuni ambazo
zinatengeneza faida kwa ajili ya kukuwezesha kutengeneza faida kubwa.
Soma: Salamu za Mwaka 2017 kwa Wafanyakazi wa Umma na Sekta Binafsi. Fahamu siri 10 Ambazo Zitayabadilisha Maisha Yako kwa Ujumla
Soma: Salamu za Mwaka 2017 kwa Wafanyakazi wa Umma na Sekta Binafsi. Fahamu siri 10 Ambazo Zitayabadilisha Maisha Yako kwa Ujumla
Hatua
ya Saba: Linda Utajiri Wako. (Na J.J.
Childers)
22. Linda
utajiri wako kwa kupunguza fedha unazotumia kulipia kodi. Hapa mwandishi
anatushirikisha jinsi ambavyo unaweza kupunguza malipo ya kodi pasipo kuvunja
sheria ya nchi. Njia ya kufanya hivyo ni kwa kubadilisha mfumo wa mifereji ya
kipato chako. Anzisha mifereji ambayo itakuingizia fedha pasipo makato yoyote
ya kodi au kwa kuwa na makato kidogo. Mfano rahisi, linganisha malipo ya kodi
ya mtu ambaye ameajiriwa na yule ambaye amejiari kupitia shughuli kama za
kilimo biashara au ufugaji. Mfugaji au mkulima anapata kipato chake pasipo makato yoyote
tofauti na mwajiriwa ambaye analipa kodi kabla hata ya kupata malipo yake. Matajiri
wanatumia mbinu hii kuhakikisha wanalipa kodi kidogo kwenye kodi au pengine kutokulipa kabisa na hivyo kuongeza
utajiri wao pasipo kuvunja sheria.
23. Andaa
mpango wa mirathi ya utajiri wako. Watu wengi tunaweza kushangaa pointi hii
lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu ambaye anataka nguvu zake zipotee bure mara
baada ya ukomo wa maisha ya hapa duniani. Hivyo mwandishi hapa anatuhamasisha
umuhimu wa kuhakikisha tunaandaa mirathi ya mali zetu ili pindi tukifariki tuziache
katika mikono salama. Pasipo kufanya hivyo ukifa utakuwa umeenda na kila
kilicho chako jambo ambalo ni kinyume na misingi ya wanamafanikio kwani
wanamafanikio maono yao ni kuishi milele kupitia alama zao.
24. Kuwa
na kinga ya utajiri wako. Utajiri wako unaweza kuyeyuka ndani ya sekunde kama
hauna kinga ya kisheria. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ukishakuwa tajiri wapo wengi ambao watakuwa wanatafuta namna ambavyo watatumia fedha zako
kwa njia haramu au halali. Mfano, wapo watu hasa wanasheria ambao watakuwa
wanakufuatilia kila unalolifanya ili pale ambapo utaenda kinyume waweze
kunufaika na fedha zako. Wapo wengine ambao watakuwa tayari hata kukushitaki
kwa makosa ya hovyo ili mradi hata kama utashinda kuna wanasheria wenzao ambao
watakuwa wamefaidi. Hivyo unatakiwa kujiandaa na kuhakikisha kila unachofanya
unakuwa na kinga ya kisheria. Hapa pia unatakiwa kujikinga dhidi ya wapinzani
wako kwani wanaweza kufanya lolote ili mradi tu wakuangushe.
25. Hakikisha
rasilimali zako nyingi zina bima. Bima ni njia mojawapo ambayo wengi hawataki
kulipia lakini hapa mwandishi anatushirikisha kuwa njia moja wapo ya kuwekea
kinga biashara yako ni kuhakikisha inakuwa na bima kama tahadhari kwa majanga
yanayoweza kutokea.
Mwisho, mpendwa rafiki na
msaomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri, nakushauri sana kama kweli unataka
kuwa tajiri hakikisha unasoma kitabu hiki. Haya niliyokushirikisha ni machache
kiasi kwamba kwa kila hatua ningeweza kukushirikisha mambo zaidi ya 25 lakini
kutokana na muda nimeshindwa kufanya hivyo. Kwa haya machache naamini
utayafanyia kazi kwa ajili ya kufikia ndoto zako za kuwa tajiri. Niendelee
kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie
wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa
kuishi. Nakutakia mapambano mema.
Tumia
kanuni hii kama sara kujiongezea utajiri “If I educate myself, if I discipline my spending
and borrowing, if I learn the art and science of investing wisely, then through
property I can build as much wealth as I want (or need).” Tafsiri yake ni “Kama nitajielimisha, kama nitakuwa na nidhamu
kwenye matumizi ya fedha na nidhamu ya mikopo, kama nitajifunza sanaa na
sayansi ya uwekezaji kwa umakini, mwisho kupitia kwenye rasilimali nitaweza
kuwa tajiri kwa kadri nipendavyo”
Karibuni kwenye fikra za kitajiri
ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.
Born
to Win~Dream Big
http://fikrazakitajiri.blogspot.com