Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha Noble Purpose: The Joy of Living Meaningful Life (Furaha ya Kuishi Kusudi la Maisha Yako)

Rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri ni matumaini yangu kuwa upo vizuri na unaendelea kupambana kwa ajili ya kuyaboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa fikra za kitajiri kwa ajili ya kupata chakula cha akili yako kutoka kwenye uchambuzi wa kitabu cha wiki hii.  Kama kawaida mtandao wa fikra za kitajiri unaendelea kutimiza ahadi yake ya kukuletea uchambuzi wa kitabu kimoja kila mwisho wa wiki (ijumaa) ili kupitia uchambuzi wa vitabu hivi tuendelee kuyaboresha maisha yetu.

Lengo kubwa la mtandao wa fikra za kitajiri ni kuona wewe unaanza kuishi kusudi la maisha yako ambapo kazi kubwa iliyopo mbele yako ni kubadilisha fikra zako. Mtandao huu umedhamiria kufanya kila liwezekanalo ili kukupatia maarifa yatakayo kusaidia ubadili fikra zako ili ziwe za kitajiri katika kila sehemu ya maisha yako. Kujiunga na mtandao wa fikra za kitajiri BONYEZA HAPA na kujaza fomu ili upate makala moja kwa moja kwenye barua pepe yako.

Katika wiki hii ya sita ninakuletea uchambuzi wa kitabu cha Noble Purpose ambacho kimeandikwa na mwandishi William Damon. Mwandishi kupitia kitabu hiki anahamasisha kila mtu kuishi kusudi la maisha yake ili kuwa na maisha yenye furaha. Kwa ujumla mwandishi anatufundisha kuwa maisha ni zaidi ya kuziridhisha tamaa za mwili na badala yake chimbuko la maisha yenye furaha ya kweli ni kuishi kalama za wito wetu kwa ajili ya kuishi maisha yenye faida kwenye jamii. Muhimu tunafundishwa kuwa ili kufanikiwa katika maisha haya ni lazima tuongozwe na roho mtakatifu au waweza sema nguvu iliyo nje ya upeo wa fahamu zetu kulingana na imani yako.

Karibu tufaidike wote maarifa niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki:-

1. Ili kuishi maisha yenye furaha ni lazima uongozwe na vitu vitatu (a) kitu unachokiishi (something to live on) (b) kitu kinachokufanya uishi (something to live for) na (c) kitu ambacho upo tayari kufa kwa ajili yake (something to die for). Hapa mwandishi anatufundisha kuwa maisha ambayo hayana misingi angalau miwili kati ya hii mitatu ni maisha ambayo ni mfu. Ili uishi maisha yenye madhumuni katika ulimwengu huu ni muhimu kuhakikisha unatumia misingi hiyo mitatu katika yale unayoyafanya.

2. Kadri tunavyofahamu sisi ni nani na ulimwenguni humu tumo kwa makusudi gani inasaidia kukuza safari yetu ya kuishi maisha ya mafanikio. Haijalishi kusudi la maisha yako ni lipi cha msingi ni wewe kutambua kwa nini uliumbwa katika ulimwengu na baada ya hapo wajibu wako ni kuishi kwa kadri ya wito wako. Wapo wenye wito wa kumtumikia Mungu, wapo wenye wito wa kuwa baba/mama wa familia bora, kuwa mwanamuziki, mwanasiasa au mfanyabiashara hivyo kuanzia sasa hakikisha unatambua kusudi la maisha yako na anza kuliishi mara moja.

3. Kadri unavyotambua kusudi la maisha yako ndivyo unapata msukumo wa nguvu kubwa kutoka ndani mwako kwa ajili ya kufanikiwa zaidi. Hapo ndipo utatambua kuwa kuna nguvu na vipawa zaidi ambavyo vilikuwa havijatumiwa kutokana na wewe kutokujitambua wewe ni nani na umeumbwa kutimiza madhumuni yapi katika ulimwengu huu.

4. Hakikisha kila siku unafanya jambo ambalo linachangia kufikia kusudi la maisha yako. Hapa ni muhimu kufahamu kuwa ili kufanikiwa kuishi kusudi la maisha yako ni lazima uwe tayari kuipangilia siku yako ili kila siku ikupe ushindi mdogo na ushindi huu utumike kama msingi wa kufikia kusudi kubwa la maisha yako.

5. Ili tuishi kusudi la maisha yetu ni lazima kwanza tutambue vipaumbele vya maisha yetu kwa kuhakikisha tunatanguliza kutumia kalama na ujuzi wetu kufanya yale ambayo yanaridhisha roho zetu. Hapa tunakiwa kufahamu kuwa katika maisha furaha ya kweli inatokana na kufanya yale ambayo nafsi zetu zinaridhishwa na matokeo ya matendo yetu. Kama una matendo ambayo yanasababisha huzuni ya roho huna budi kuachana nayo mara moja ili utoe nafasi kwa matendo yanayoifurahisha roho yako.

6. Maisha ya kusudi la maisha yako yapo hapo ulipo na wala husitegemee kuwa ni yapo sehemu nyingine. Maisha haya yanahusisha matendo yetu ya kila siku japo ni wachache wanajua hilo. Kama wewe ni mwalimu fikiria kufundisha wanafunzi wako kuliko mwalimu yeyote yule ambaye amewahi kuwepo, kama ni daktari lenga kuwahudumia wagonjwa kwa roho moja, kama ni mfanyabiashara fikiria kutoa huduma bora kwa wateja wako kwa kadri uwezavyo na kama wewe ni kiongozi au mwajiri fikiria kuwatendea watu wako unaowaongoza kwa kadri unavyoweza kuwaridhisha. Haya ndiyo maisha bora ambayo kila mtu ameumbwa kuyaishi.

7. Maana halisi ya kusudi la maisha yako ni lile lengo kubwa la maisha yako ambalo ni imara na linajumuisha kila sekta ya maisha yako na unapaswa kulikamilisha katika maisha yako si tu kwa ajili ya faida yako bali kwa ajili ya jamii nzima. Somo la kujifunza hapa ni kuwa kusudi la maisha ni (a) lengo kubwa ambalo ni msingi wa maisha yako yote (b) imara na halitakiwi kubadilika mara kwa mara (c) ni ufunguo wa sisi kuujua ukweli wa tuliumbwa kukamilisha nini hapa duniani (d) linajikita kwenye kukamilisha kitu katika maisha yetu si tu kwa faida yetu tu bali kwa ajili ya wengine. Kutokana na ukweli huu utagundua kuwa unapoishi kusudi la maisha yako utajikuta katika ulimwengu wa matendo mema ambayo hayana athari mbaya kwa maisha ya wengine wanaokuzunguka.

8. Wito wako upo kwenye kazi yako ya kila siku. Watu wengi wameshindwa kuishi wito wa maisha yao kwa vile wamekuwa wanatofautisha kazi wanazofanya na wito wao. Hapa tunafundishwa kuwa wito wetu upo kwenye kazi zetu za kila siku na hivyo ili kuishi wito huu ni lazima kwanza uipende kazi yako na hatimaye kupitia kazi hiyo watu wengi wanufaike na matunda yako. Kwa ukweli huu pale unapoiona kazi yako kama wito wako au kusudi halisi la maisha yako moja kwa moja kazi itabadilisha mtazamo wako wote juu ya kazi yako na hivyo kufanikiwa kupata mafanikio makubwa kwako wewe na wale unaowahudumia.

9. Unapoikubali kazi yako kama wito wako inakuwa mwanzo wa safari ya kuishi kusudi la maisha yako. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kazi unayofanya inachukua sehemu kubwa ya muda wako na hivyo husipokuwa na furaha katika muda huu ni vigumu kupata furaha kwa muda uliobakia. Kanuni hii inatakiwa kufanya kazi kwa wafanyakazi wote pasipokujali cheo, muda walionao kazini au kazi wanazofanya. Kama unafanya kazi ya kufagia barabara fagia kana kwamba hakuna mtu mwingine ambaye atafagia vizuri kuliko wewe vivyo hivyo kwa kazi nyinginezo unazofanya fanya kama vile wewe ndo mtaalamu namba moja kwa ubora katika kazi hiyo.

10. Unapoiona kazi yako kama wito huna budi kusukumwa na wito huo kufanya kazi badala ya kusukumwa na malipo ya fedha ya kazi husika. Hapa tunafundishwa kuwa katika kila kazi tunayofanya hatupaswi kutanguliza fedha mbele badala tunatakiwa kutoa huduma yenye thamani kubwa kwa wale tunaowahudumia na hatimaye fedha zitafuatia baadae. Pia tunasisitizwa kuweka lengo la kutoa huduma bora kwa wateja badala ya kuweka lengo la kuongeza faida tu. Nilichojifunza hapa ni kwamba unapojikita kwenye kuongeza faida tu ni rahisi kutumia mbinu ambazo sio halali kama vile kushindwa kujali afya za wateja unaowahudumia na hivyo kwenda kinyume na kusudi la maisha yetu.

11. Unaweza kupata kusudi la maisha yako sehemu yoyote ile. Kusudi la maisha yako linaweza kuwa kwenye jamii yako ya karibu, marafiki, ndugu, familia, imani (kanisani au msikitini), jamii na hata kwa watu walio mbali na upeo wako. Mfano katika ngazi ya familia kusudi la maisha yako linaweza kuwasaidia wafamilia wote kufikia ndoto zao au kuwasaidia wale wasiojiweza. Vivyo hivyo kusudi la maisha yako linaweza kuwa baba/mama bora wa familia. Hivyo hauna sababu ya kuumiza kichwa sana ukifikiria ni wapi utapata kusudi la maisha yako badala yake anzia hapo ulipo. Kwa upande wa imani unapata nafasi ya kutambua kwa undani upendo wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu.

12. Unaweza kuishi kusudi la maisha yako kupitia matendo mema kwenye jamii. Matendo haya yanajumuisha upendo kwa watu wote mfano, upendo kwa wazee, watoto, walemavu, yatima na wajane. Unaweza kuanzisha mfuko au taasisi ya kusaidia watu wenye mahitaji na kupitia taasisi hiyo ukafanikiwa kuwafiki watu wengi. Mfano, angalia maisha ya Mother Theresa, unaweza ukafuatilia historia ya maisha yake kwenye mtandao kama haujui historia yake.

13. Kusudi la maisha yako linaweza kuwa kwenye utamaduni wako. Baadhi ya tamaduni zinawaongoza wanajamii kuishi maisha yenye thamani kwa watu wengine. hivyo kupitia utamaduni wako unaweza kupata kusudi la maisha yako. Mfano, baadhi ya tamaduni zetu zinatenga wajibu wa watu kulingana na umri au jinsi zao, hivyo kupitia tamaduni hizi unaweza kupata kusudi la maisha yako.

14. Kusudi halisi la maisha yako ni lazima lijikite kwenye matendo ya halali kwenye jamii inayokuzunguka. Ni lazima yale tunayoyafanya kupitia wito wetu yawe ni matendo yanayokubalika kisheria pasipo kufanya hivyo tunakuwa bado hatujafahamu ukweli juu ya maisha yetu.

15. Ni lazima tuwe tayari kuomba msamaha au kujisahihisha pale inapotokea matendo yetu yameenda kinyume na matarajio yetu hadi kusababisha madhara kwa wengine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba sisi ni binadamu na hivyo ni rahisi kufanya makosa. Hata hivyo kama bado huna nafasi ya kufanya marekebisho ya makosa yako kabla hayajasababisha madhara makubwa fanya hivyo mara moja pale unapopata angalizo. Hivyo ni muhimu maamuzi na matendo yetu ambayo yanailenga jamii yakafanywa kwa tahadhari na unyenyekevu wa hali ya juu.

16. Kila mtu anaweza kuishi kusudi la maisha lakini njia pekee ya kujua kama kusudi hilo ni halisi ni kuona kama linaendana na misingi ya kijamii. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuna watu wanaishi maisha yenye kiburi na kila aina ya ubinafsi labda kutokana na madaraka yao lakini bado wakajiona kuwa wanaishi kusudi la maisha yao. Jambo la kujifunza hapa ni kwamba matendo yetu ni lazima yakubalike kwenye jamii zetu kwa kuzingatia sheria na tamaduni zetu.

17. Maisha yaliyojengwa kwenye misingi ya kusudi la maisha ni maisha ambayo yametumiwa vizuri ulimwenguni hapa na kinyume chake ni kwamba maisha ambayo hayajajengwa kwenye kusudi lake ni maisha yaliyopotezwa. Hii haijalishi maisha hayo ni marefu au mafupi, masikini au tajiri, afya njema au maradhi, yenye madaraka au yasiyokuwa na madaraka. Hivyo ni muhimu kila mmoja wetu kutafuta kusudi halisi la maisha yake na kuanza kuliishi mara moja.

18. Tafiti za kisaikolojia zinaonyesha kuwa watu wenye furaha ya maisha ni wale ambao hawatumii nguvu nyingi kupata furaha hiyo. Kwa maana nyingine ni kwamba watu wenye furaha ya maisha ni wale ambao wamejitosa kufanya vitu ambavyo vinawapa furaha ya nafsi zao. Hivyo, kama unataka kuishi maisha yenye furaha huna budi kufahamu ni yapi yanairidhisha nafsi yako na kuanza kuyatekeleza mara moja. Mambo hayo si mengine bali ni yale yanayounda msingi wa kusudi la maisha yako.

19. Kusudi la maisha yako linaweza kuwa wokovu kwa maisha ya wengine. Hapa mtu yupo tayari kupoteza maisha yake ajili ya kuokoa maisha ya wengine au nchi yake. Mfano, katika nyakati za vita kuna baadhi ya watu ambao wapo tayari kufa kwa ajili ya kuilinda nchi yao. Hata hivyo, humu duniani kuna kila aina ya vita ambayo kila mmoja wetu anapigana kuishinda. Hivyo unaweza kuangalia ni vita ipi inawatesa watu wengi na wewe ukajitosa kuwasaidia ili wapambane dhidi ya vita hiyo.

20. Ulimwengu unakusubiria utumie kalama/vipawa ulivyopewa kwa ajili kuboresha dunia hii kuwa mahali pazuri kwa viumbe wote. Hivyo, kadri unavyozidi kuchelewa kutumia vipawa hivyo ndivyo unavyozidi kupoteza jambo ambalo ni kinyume na malengo ya uwepo wako hapa duniani. Pia, tunatakiwa kukumbuka kuwa suala la kuishi kusudi la maisha yako sit u faida kwa ulimwengu bali ni fadia na kwako pia kwa vile unaboresha afya yako ya kiroho, kiakili na kimwili.

Mambo Muhimu ya Kuzingatia katika Kutafuta Ukweli wa Kusudi/Dhamira ya Maisha Yako.

Mwandishi anatushirikisha kanuni tisa kwa ajili ya kufikia kusudi la maisha yetu. Karibu tujifunze wote kanuni hizi:-

21. Kamwe hatupaswi kusema ni mapema mno au tumechelewa kuishi kusudi la maisha yetu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kusudi la maisha yako unaweza kuliishi katika sehemu yoyote na muda wowote wa maisha yako.

22. Pamoja na kwamba kusudi la maisha yako lipo sehemu yeyote ile, ukweli ni kwamba ni rahisi kulipata kusudi la maisha katika sehemu ambazo una uzoefu nazo. Sehemu hizi zinaweza kuwa familia yako, marafiki, kanisani, kipaji chako, ajira au biashara yako na mazingira yanayokuzunguka kwa ujumla.

23. Tafuta watu ambao ni “role model” wako. Hawa ni watu ambao kupitia maisha yao unapata hamasa ya kufikia maisha ya ndoto zako. Ni watu ambao wameishi maisha ya mafanikio kwenye jamii zao hivyo na wewe kupitia wao unaweza kujifunza mengi. Hapa unaweza kuanza kuwa karibu na wale ambao unatamani maisha yao kwa ajili ya kujifunza kutoka kwao.

24. Kama inawezekana pata sapoti kutoka kutoka kwa watu wenye mtazamo kama wako. Lakini kuwa tayari kusimama kwenye kusudi la maisha yako hata kama hakuna mwenye mawazo au maisha ya namna hiyo. Hii ni kutoka na ukweli kwamba kusudi la maisha yako linaweza kuwa sio maarufu kwa wakati huu na hivyo ukajikuta hauna sapoti kutoka kwa watu wengine.

25. Kuwa tayari kusimama imara kwa vikwazo na changamoto za hapa na pale. Katika safari yako utapata mafanikio pamoja na kushindwa kufikia baadhi ya malengo lakini katika yote haya haupaswi kuicha njia yako.

26. Endelea kuwa mnyenyekevu na mwenye hekima katika matendo yako. Haupaswi kudanganywa au kuridhika na mafanikio unayoyapata kutoka kwenye kusudi la maisha yako na badala yake unatakiwa kuendelea kuishi maisha yenye faida kwa watu wote.

27. Kuwa na uhakika kuwa kusudi la maisha yako linaendelea kuwa halisi lakini pia na njia unazotumia kulifikia kusudi hilo hazina athari kwa wengine. katika kila hatua jiulize maswali haya: Je nini nahitaji kupata katika maisha haya? Kwa nini nahitaji kupata kitu/vitu hivi? na Je njia ninazotumia kupata vitu hivyo ni halali? Ni rahisi sana kupata kusudi la maisha yako lakini vigumu kuliishi kwa kuzingatia njia na sababu zinazokusukuma kuishi kusudi hilo.

28. Sherekea kusudi la maisha yako na ona fahari ya kuliishi kwa watu wanaokuzunguka. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kusudi la maisha yako ni zawadi tena zawadi ambayo unapaswa kuitumia kwa faida ya wengi.

29. Hakikisha zawadi ya kusudi la maisha yako inarithiwa na vizazi na vizazi. Wafanye watoto wako na jamii nzima ijufunze kutoka kwako na hata pale ambapo ukomo wa maisha yako utaisha utakuwa umeacha alama kwa wengine.

Mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri, haya ni machache kati ya mengi ambayo nimejifunza kwenye Noble Purpose, naamini kama utayafanyia kazi yataboresha maisha yako. Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.

Ili kupata makala za namna hii kwenye barua pepe yako BONYEZA HAPA na acha taarifa zako. 

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win~Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      0786881155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com

onclick='window.open(