Salamu za Mwaka 2017 kwa Wafanyakazi wa Umma na Sekta Binafsi. Fahamu siri 10 Ambazo Zitayabadilisha Maisha Yako kwa Ujumla

Habari ya leo rafiki yangu na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Naamini upo vizuri na unaendelea kupambana kwa ajili ya kuyaboresha maisha yako. Ni jambo la heri kuona una nguvu hata za kukuwezesha kusoma ujumbe huu ambao ni muhimu kwa ajili ya chakula cha ubongo wako.

Kama ambavyo mtandao wa fikra za kitajiri umeendelea kukuhamasisha kuchukua hatua kwa ajili ya kuyaboresha maisha yako, leo hii kupitia mtandao huu ningependa kutumia dakika chache kuongea na wafanyakazi wa sekta ya umma na sekta binafsi kwa ujumla. Makala ya leo inawalenga wale wote walioajiriwa kwenye sekta ya umma na sekta binafsi pamoja na wale wanaotarajia kuingia kwenye ajira. Karibu nikushirikishe siri kumi ambazo zitayabadirisha maisha yako kwa ujumla endapo utazifanyia kazi kuanzia mwaka 2017.

1# Siku ulipoanza kazi ndo mwanzo wa maandalizi ya kustaafu. Kwa mujibu wa sheria waajiriwa kwenye sekta zilizo rasmi wanakatwa sehemu ya mshahara kama malipo ya mifuko ya jamii ambayo kwa baadae yanalipwa kama kiinua mgongo na mafao ya uzeeni. Makusudi ya makato haya ni kumwezesha mwajiriwa apate unafuu wa maisha pindi anapostaafu.

Wafanyakazi wengi wana shauku ya kuhitimisha safari yao ya utumishi ili mwhishowe wapate stahiki zao ambazo wamekuwa wakichangia kila mwisho wa mwezi. Asilimia kubwa ya wafanyakazi wamekuwa wakisubiria fedha hii wakidhani kuwa ni fedha nyingi ambazo zitawawezesha kuishi maisha ya furaha katika kipindi cha uzee wao. Lakini kumbe ni kinyume na matarajio yao, kwa uzoefu wastaafu wengi utumia fedha hizi kinyume na matarajio na mwisho wake zinaisha kwa muda mfupi. Hii ni kutokana na wengi wao kuona ni fedha nyingi ambazo zinaweza kutatua kila aina ya matatizo waliyonayo. Na wengine mara baada ya kupata fedha hizi ndo wanafikiria kuanzisha miradi ya biashara ambayo hawakuwahi kufanya na hatimaye biashara hizi zinakufa kwenye miezi ya mwanzoni kutokana na wamiliki kukosa uzoefu kwenye biashara husika.

Ili uepuke changamoto za namna hiyo hakuna namna nyingine zaidi ya wewe kufanya maandalizi binafsi ukiwa bado kijana. Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha kila pesa inayoingia mkononi mwako unatenga asilimia yake kwa ajili uwekezaji. Hakikisha unatenga asilimia ya mshahara wako na fedha za kuwa safarini kikazi au kufanya kazi ya ziada (extra duty) kwa kujiwekea mazingira mazuri ya kustaafu. Ukifanya zoezi hili kwa nidhamu na uadilifu kwa kipindi cha miaka uliyobakiza kazini nakuhakikishia kuwa fedha utakayojiwekea itakuwa zaidi ya mara tatu ya hiyo unayotarajia kupewa kutoka mfuko wa hifadhi ya jamii ambao wewe ni mwanachama. Hata hivyo unaweza kuwekeza fedha hizo kama sehemu ya kukusanya mtaji ili uwekeze kwenye vitega uchumi kama ardhi, majumba ya biashara, kilimo, ufugaji na biashara nyinginezo ambazo ni rahisi kuziendesha huku ukiendelea kufanya kazi.

2# Nyongeza ya mshahara si suruhisho la matatizo yako. Imekuwa kawaida kwa wafanyakazi hasa watumishi wa umma kusubiria mwisho wa mwezi wa saba kwa hamu kutokana na mazoea kuwa serikali imekuwa ikiongeza mshahara kila mwaka. Lakini jambo muhimu ambalo naomba ulifahamu ni kuwa kamwe mshahara hauwezi kutatua matatizo yako ya kiuchumi hata ungekuwa mkubwa kiasi gani. Chukulia mfano ni kawaida sana kukuta watumishi wa kada nyingine kutamani mshahara wa daktari, mhandisi, mwanasheria au kada nyingine ambazo kwenye jamii inaaminika zina mishahara mikubwa. Lakini cha ajabu ni kwamba hata waliopo kwenye hizo kada kilio chao ni kile kile mshahara kutokutosheleza.

Fundisho kubwa hapa ni kwamba kadri mshahara wako unavyoongezeka ndivyo na matumizi yako yanavyoongezeka na mwisho wake kila kitu kinarudi kwenye mringanyo wake (state of equilibrium). Hata hivyo, unapaswa kufahamu kuwa mshahara umekokotolewa katika njia ambayo itakufanya uendelee kuwa tegemezi kwa mwajiri wako kwani bila kufanya hivyo watu wengi wangeacha kazi.

Nakusihi sana rafiki yangu badala ya kusubiria mshahara uongezeke ndo uanze kuchukua hatua za kuyaboresha maisha yako anza sasa kwa mshahara huo mdogo ulionao. Hakikisha unajenga nidhamu ya kutumia hicho kidogo ulichonacho ili hatimaye kikupatie mafanikio makubwa sana. Kufanikiwa katika zoezi hili ni lazima ujenge utamaduni wa kutenga sehemu ya mshahara wako kwa ajili ya akiba kama nilivyoeleza kwenye siri ya kwanza.

3# Ajira siyo sehemu salama. Zamani wafanyakazi walikuwa na usalama na uhakika wa vibarua vyao kutokana na idadi ya wataalamu walikuwepo kipindi hiko pamoja na mfumo wa Serikali. Leo hii mambo yamebadilika na Serikali imebadilika kiasi kwamba unaweza kuaga asubuhi unaenda kazini na kufika ukakutana na barua ya kuachishwa kazi. Katika mazingira kama haya unatakiwa ujiandae kwa ajili ya lolote linaloweza kutokea.

4# Epuka ugonjwa wa nikipanda cheo. Fanya kazi ukiwa na nadharia ya kwamba cheo ulichonacho kwa sasa ndo utadumu nacho mpaka unastaafu. Chukulia kama vile mshahara wako wa sasa pamoja na marupurupu yako hayataongezeka hadi kustaafu kwako na hatimaye fikiria jinsi gani utafanikiwa kutatua changamoto za kifedha kwa muda wote utakaokuwa kazini.

Rafiki ninachotaka ujifunze hapa ni kwamba wafanyakazi wengi wamekuwa na tumaini la kwamba siku watakapopanda cheo ndo wataweka mambo yao sawa au ndo watapata fedha nyingi lakini ukweli ni kwamba hata hao mabosi bado wanateseka katika kukamilisha mahitaji yao ya kifedha. Ndio maana makazini ni kawaida sana kuona bosi anapindisha hata elfu hamsini iliyokuwa iende kwa mtu wake wa chini ili mradi tu aichukue yeye.

5# Husiruhusu mtu achezee muda wako nje ya muda wa mwajiri. Rafiki yangu naomba utambue kuwa ukitoa masaa 8 ya mwajiri hasa kwa wafanyakazi wa Serikali katika siku unabaki na masaa 16 ambayo kati ya hayo angalau una masaa yasiyopungua 5 kila siku kwa ajili ya kufanya shughuli zako ukiachilia mbali siku za jumamosi na jumapili ambazo una masaa yote kufanya shughuli zako. Tatizo ni kwamba wafanyakazi wengi tumejenga mazoea kuwa baada ya muda wa kazi ndo muda wa kupumzika. Mbaya zaidi wengi wanatumia muda huu kwa ajili ya kwenda kwenye sehemu za starehe na kwenye makundi yasiyokuwa na tija.

Nakushauri sana rafiki yangu uhakikishe unatumia muda huu kwa ajili ya kufanya shughuli binafsi za kujiongezea kipato. Na hautakiwi kuchagua kazi kwa kuogopa kuwa Afisa utaonekana vipi kwa kufanya kazi ya namna hiyo kwani wewe ndo mwenye hatma ya maisha yako na wewe ndo unajua nini unafanya na kwa nini unafanya hivyo. Jifunze sana kufanya vitu ambavyo hauvunji sheria lakini jamii inayokuzunguka inakushangaa kwa nini wewe na elimu yako unafanya vitu hivyo.

6# Epuka ugonjwa wa kuairisha mambo (Procrastination syndrome). Mpendwa mwajiriwa ugonjwa wa kuairisha mambo umekuwa ni kizuizi kikubwa kwa wafanyakazi wengi kufikia ndoto zao. Hii ni kutokana na wafanyakazi wengi kuishi maisha ya “ubize” ambao kiuhalisia ni ubize wa kinadharia uliojengeka kwenye mfumo wa fikra za wafanyakazi wengi kuliko majukumu ya kazi zao. Kwa mfumo huu wafanyakazi wengi wamekuwa ni wapangaji wazuri wa mipango binafsi lakini utekelezaji wake wengi wao wameshindwa kufanya hivyo.

Rafiki yangu kama unataka kuishi kusudi la maisha yako huna budi kuchukua hatua mara moja kwa yale ambayo unalenga kuyatekeleza katika maisha yako. Hakikisha unakuwa na ndoto hai ambazo unazitafsri katika maisha yako ya kila siku. Epuka sana kauli za nitafanya na badala yake anza pasipo kujali hatua zako ni fupi kiasi gani kwani hata Mji wa Roma ulijengwa kwa zaidi ya miaka 50. Na hii ni kutokana na ukweli kwamba mafanikio yanakuja kwa kupata ushindi mdogo kwa muda mrefu.

7# Mshahara wako ndio kipato pekee cha uhakika kazini kwako. Imekuwa ni kawaida kwa wafanyakazi walio wengi kufikiria zaidi fedha nje ya mshahara wao hasa zile za marupurupu ya kazini au pengine kupitia “dili”. Kutokana na ukweli kwamba fedha za namna hii upatikanaji wake unakuwa hauna kanuni maalumu na hivyo sio rahisi kuweka mipango ya muda mfupi au mrefu wa jinsi gani unaweza kuzitumia fedha hizi. Mbaya zaidi fedha za namna hii zinaweza kusababisha upoteze kazi yako hasa zile zinazopatikana kwa njia ya udanganyifu.

Kwa upande wa fedha za posho kazini na zenyewe upatikanaji wake sio rahisi kwa kuwa kila mmoja katika kituo chako cha kazi anazitolea macho. Jambo hili limesababisha wafanyakazi wengi kuwa na msongo wa mawazo kutokana na ukosefu wa fedha nje ya mshahara kwani ni wazi kuwa mshahara hautoshi na hivyo wengi wao wanakuwa na manunguniko kwa mabosi wao au wenye mamlaka.

Rafiki yangu ili kuepuka maisha ya namna hiyo nakusihi sana utambue kuwa kipato chako cha uhakika ni mshahara wako unaopokea kama malipo ya kazi yako kila mwisho wa mwezi. Kutokana na uhakika wa mshahara huu unaweza kujiwekea kanuni maalum za namna gani utatumia kipato chako kwa ajili ya kufikia maisha ya mafanikio unayoyataka.

8# Kila mtu anatolea macho fedha yako. Mpendwa rafiki mfanyakazi naomba kuanzia leo hii utambue kuwa ni wewe pekee ambaye kila mtu ana uhakika na fedha yako. Ukiingia mtaani na jamii zinazotuzunguka zinafahamu fika kuwa wafanyakazi wana fedha za kutosha. Popote utakapoenda ukishafahamika kuwa wewe ni mfanyakazi wapo tayari kukuuzia kitu chochote au huduma yoyote hata kama siyo mahitaji yako. Vilevile ni wewe pekee ambaye unakopesheka kwenye taasisi za fedha na hata mitaani na hasa kwa upande wa mikopo yenye riba. Watu/taasisi zipo zinakusubiria ili uende ukakope na pengine unabembelezwa kutokana na uhakika walio nao juu ya fedha zako.

Katika mazingira kama haya rafiki yangu unatakiwa kuwa makini sana vinginevyo fedha zako zitaishia kwenye kulipa madeni miaka nenda rudi. Jambo la msingi hapa unatakiwa kujitazama upya katika madeni unayodaiwa na kuweka mkakati wa kuyalipa mara moja na baada ya hapo husijiingize kwenye mkopo ambao hauna tija kwenye kutimiza malengo yako. Kabla ya kuchukua mkopo fanya tathmini ya kufahamu kama unaweza kutumia mkopo huo kuanzisha mradi na kupitia mradi huo utaweza kulipa deni la mkopo na faida juu yake.

9# Huduma yako ndo thamani yako. Imekuwa ni kawaida sana kwa wafanyakazi walio wengi kwenda kazini ili mradi kuwaridhisha wakubwa wao wa kazi. Katika hali kama hiyo unakuta mtu hana vipaumbele vya nini anatakiwa kufanya kwa siku husika bali sana sana akifika ofisini anaanza kuangalia yaliyojiri kwenye mitandao ya kijamii, kupiga stori na hatimaye kusubilia muda wa kuondoka. Kwa mazingira ya namna hii hata pale mteja akija kwa ajili ya kupata huduma anapewa majibu ya juu juu kutokana na ukweli kwamba muhusika hana muda wa kufuatilia yanayohusu taaluma yake.

Rafiki yangu nakuomba sana hakikisha unatambua majukumu yapi unatakiwa kuyamilisha kila siku unapokuwa kazini. Njia nzuri ya kufanya hivyo ni kuhakikisha kila asubuhi ukifika mezani kwako unaandaa orodha ya vitu vya kukamilisha kwenye siku husika na baada ya hapo unaanza kuvitekeleza mara moja.

10# Kuwa na muda wa kujielimisha. Kama nilivyotangulia kusema kuwa wafanyakazi wengi wamejenga nadharia ya ubize kwenye maisha yao. Hivyo ni kawaida mtu ukimuambia suala la kusoma vitabu, makala au majarida mbalimbali moja kwa moja atakuambia kuwa hana muda wa kufanya hivyo. Cha kushangaza mtu huyo ana muda wa kusoma posts zote za mitandao ya kijamii, kusoma magazeti ya siasa, mitandao ya udaku ili kujua Diamond kafanya nini kwa mwanae na mengine mengi. Mbaya zaidi wafanyakazi wengi wamejifungia kwenye fani zao na hawapo tayari kupata maarifa mengine. Hii ni sawa na kujiweka kifungoni bila ya wewe kufahamu.

Wanamafanikio wanatufundisha kuwa elimu wala sio stashahada au shahada bali elimu ya kweli ni ule uwezo wa mtu kujua vitu vichache kwenye kila fani na kuvitumia kutatua changamoto za kila siku kwenye maisha ya mwanadamu. Hivyo, unapaswa utambue kuwa kama lilivyo tumbo lako kwa kuhitaji chakula kila siku na ubongo wako ndivyo ulivyo kwa kuhitaji maarifa mapya kila siku. Epuka sana kauli za hayo nayafahamu, hakuna jipya na badala yake pigana sana kuulisha ubongo wako kwa kutenga muda wa kujisomea kila siku.

Hizi ndizo siri kumi ambazo nimekushirikisha ewe mfanyakazi ili ziwe mwongozo wa maisha yako. Ni matumaini yangu kuwa endapo utazifanyia kazi zitabadilisha maisha yako kwa ujumla. Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi. Nakutakia mapambano mema.

Ili kupata makala za namna hii acha taarifa zako kwa kujaza fomu hapo chini.

Karibuni kwenye fikra za tajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.
Born to Win~Dream Big
A.M. Bilondwa
0786881155
fikrazatajiri@gmail.com


Jiunge na Mtandao wa Fikra za Kitajiri ili kutumiwa makala moja kwa moja kwenye email

* indicates required

onclick='window.open(