Habari
ya leo rafiki yangu na msomaji wa mtandao wa Fikra za Kitajiri. Ni matumaini
yangu kuwa hujambo na unaendelea vyema katika majukumu yako ya
kuhakikisha unaiandaa kesho iliyo bora. Ni jambo la heri kuona kila siku
unapigana kuhakikisha unaboresha maisha yako kwani ni wazi kuwa mafanikio
hayaji kama ajali bali yanaandaliwa kupitia vitu vidogo vidogo
vinavyokamilishwa kila siku. Hongera sana rafiki.
Karibu tena tujifunze yale ambayo ni muhimu kwa ajili ya
kuboresha maisha yetu tunapoendelea kushika kasi ya mwaka 2017. Rafiki naamini
kuwa tayari umejiwekea malengo kwa yale mambo muhimu ambayo ungependa
kuyakamilisha mwaka huu ili kupitia malengo hayo mwaka huu uwe chachu ya mafanikio
unayoyataka.
Katika makala ya leo nitakushirikisha mambo kumi muhimu
ambayo unatakiwa kusema HAPANA kwa kadri uwezavyo endapo unataka uhuru wa kifedha (financial freedom). Katika safari ya mafanikio ni muhimu sana kusema hapana bila kujali
jamii inasema juu ya yale unayosimamia na hivyo ni lazima uwe tayari kuwa mtu
wa tofauti katika jamii inayokuzunguka. Karibu tujifunze wote;
Moja;
Sema HAPANA kwa matumizi yanayozidi kipato chako. Siri
kubwa ya kuwa na uhuru wa kifedha ni lazima uhakikishe matumizi yako hayazidi
pato lako. Mwaka 2017 hakikisha unaanza kwa kutenga sehemu ya pato lako kwa
ajili ya kujilipa kwanza kabla haujafanya matumizi ya namna yoyote ile kwenye
pato lako la kila siku au mwezi. Maana ya kujilipa kwanza ni tabia ya kutenga
kiasi flani cha pesa kutoka kwenye pato lako kwa ajili ya uwekezaji kwenye miradi
inayoingiza kipato (Assets). Unaweza ukatumia mbinu hii kwa ajili ya kudunduliza
kiasi flani cha pesa kama mtaji wa kuwekeza kwenye mradi wowote ambao
kwa sasa hauna fedha za kutosha kuuanzisha. Jambo muhimu la kuzingatia ni
kuhakikisha kuwa fedha hizo unaziwekeza sehemu ambayo hautashawishika kuitumia.
Mfano, unaweza ukawekeza kwenye hisa za kampuni mbalimbali au ukanunua vipande
vya mifuko ya UTT (http://www.utt-tz.org/).
Mbili;
Sema HAPANA kwa manunuzi ambayo hayapo kwenye mipango. Ili
ufanikiwe kifedha lazima ufahamu kuwa fedha inaenda sehemu inakopendwa zaidi. Hivyo
pasipo kuipenda fedha kupitia fedha hizi ndogo ndogo ulizonazo kamwe hauwezi kuwa
na uhuru wa kifedha. Imekuwa ni kawaida kwa watu wengi kununua vitu ambavyo
havikuwa kwenye mpango wa manunuzi yao bali wananunua tu kwa vile amekutana na
vitu vya namna hiyo au kwa vile tu kashawishiwa na machinga kununua. Mwaka 2017
sema hapana kwa manunuzi kama hayo na hakikisha unaweka mpango wa vitu vya
kununua na fanya manunuzi kwa kutekeleza mpango huo. Pia, hakikisha unaandika
fedha zote unazotumia kwenye manunuzi pasipo kujali ni ndogo kiasi gani.
Tatu;
Sema
HAPANA kwa mtu yeyote anayetaka
kukupotezea muda wako. Kuna msemo kuwa “Muda ni Mali”. Hakika muda ni
mali japo watu wengi hatujajua jinsi gani tunaweza kutumia muda huu kupata hiyo
mali. Mwaka 2017 hakikisha unakuwa na orodha ya vitu ambavyo unatakiwa
kuvitekeleza kwa siku husika na bila kupoteza muda fanyia kazi orodha hiyo
pasipo kuruhusu mtu akupotezee muda. Kwa kufanya hivyo mwishoni mwaka 2017
utaniambia jinsi ambavyo umekuwa ukipoteza mali yako (muda) kwa kuruhusu watu
wachezee muda wako.
Nne;
Sema HAPANA kwa marafiki ambao unaona wanaenda kinyume na mtazamo wako. Rafiki
kuwa na uhuru wa kifedha unahitaji kwanza uwe na misingi imara ambayo
umejiwekea na upo tayari kuisimamia katika maisha yako ya kila siku. Kibaya ni
kwamba misingi hii itakufanya uonekane wa tofauti katika jamii inayokuzunguka
wakiwemo hata rafiki zako wa karibu. Hivyo mwaka 2017 hakikisha unasema hapana
kwa rafiki yeyote utakayeona anakupoteza kwenye misingi uliyojiwekea. Hepuka marafiki
ambao wamekata tamaa na kutumia muda mwingi kwenye kulalamikia mfumo. Kama mwanamafanikio
unatakiwa kutambua kuwa mfumo kamwe hauwezi kukuzuia kufikia kilele cha
mafanikio unayoyataka.
Tano;
Sema HAPANA kwa tabia ambazo zimekuwa zikisababisha matumizi yasiyo ya lazima. Kuwa
na nidhamu ya hali ya juu ni jambo la muhimu katika kuwa na uhuru wa kifedha. Mfano,
kama umekuwa ukitumia vilevi na kujikuta unatumia hadi kiasi cha fedha ambacho
haukupanga kutumia ni dalili za wazi kuwa kamwe hautakaa kuwa na uhuru wa
kifedha. Nimetangulia kusema kuwa fedha zinaenda sehemu zinakopendwa zaidi na
hivyo fedha haziendi kwa mtu ambaye ana matumizi ya starehe za kupindukia au
anasa. Mwaka huu sema hapana kwa starehe na anasa za namna hii.
Sita;
Sema HAPANA kwa mikopo hisiyokuwa na tija. Ili uwe na uhuru wa
kifedha huna budi kudhibiti tabia ya kukopa pesa kwa ajili ya kutekeleza mambo
yasiyo ya msingi. Mara nyingi imekuwa ni kawaida kwa watu kukopa kwa ajili ya matumizi
yasiyo ya lazima, mfano, mtu anakopa kwa ajili ya send off, harusi, kununua
garia, kujenga jina mtaani n.k. Matokeo ya mikopo ya namna hii ni kumdumaza
muhusika kutokana na makato/marejsho ya kila mwisho wa mwezi. Mwaka 2017
hakikisha unakopa ukiwa na malengo ya kuutumia mkopo husika kwa ajili ya
kuzalisha faida zaidi na hivyo kukuza kipato chako na kupitia kipato hiki sasa
ndo unaweza ukakamilisha manunuzi kama gari n.k. Mhamasishaji na mjasiliamali
maarufu Robert Kiyosaki kuhusu hili anatuambia
kuwa starehe ya kweli ni ile inayotokana na sehemu ya faida yako kutoka kwenye miradi
inayokuingizia kipato.
Saba;
Sema HAPANA kwa vitu vinavyohatarisha afya yako. Mara
nyingi tumekuwa wepesi wa kuweka mikakati kwa ajili ya mafanikio yetu hasa
kiuchumi na kusahau kuweka mikakati ya kuboresha ya afya zetu. Wote tunafahamu
kuwa afya ikizorota kamwe hauwezi kufanikisha kazi ambazo ulipanga kuzitekeleza
na badala yake utatumia fedha nyingi kwa ajili ya kutafuta tiba. Mwaka 2017
sema hapana vitu vyote ambavyo vinahatarisha afya yako ikiwa ni pamoja na
kujiwekea miiko juu ya vyakula/vinjwaji ambavyo haupaswi kula kutokana na
athari zake kwenye mwili wako.
Nane;
Sema HAPANA kwa hofu ambayo imekuwa ikukuzuia kuthubutu. Asilimia
kubwa ya binadamu tumeumbwa na hofu juu ya mambo ambayo hatujazoea katika
maisha yetu ya kila siku. Hofu hii imekuwa ikituzuia pale ambapo tunaka kufanya
jambo ambalo ni jipya kwetu na mwisho tunapoteza fursa nyingi za muhimu. Kama unataka
kuwa na uhuru wa kifedha nakushauri kuanzia sasa ni lazima uwe tayari kuishinda
hofu hii na hivyo uaenze mara moja kuthubutu kwa kufanya yale ambayo unaona ni sahihi
katika safari yako ya uhuru wa kifedha. Ni lazima uwe tayari kuchukua hatua
pasipo kujali hatua zako ni fupi kiasi gani la muhimu ni wewe kuanza mara moja.
Tisa,
Sema HAPANA kwa tabia ya kutojifunza vitu vipya. Kama
unataka kuwa na uhuru wa kifedha rafiki yangu hakuna namna utawefanikiwa pasipo
kutenga muda kwa ajili ya kujifunza vitu vipya kila siku. Jifunze, jifunze,
jifunze … kwa kadri uwezevyo kutokana ukweli kwamba kupitia maarifa haya ndo
utafanikiwa kujifunza namna ambavyo watu wengi wamekuwa na uhuru wa kifedha
japo hapo awali walikuwa choka mbaya. Pia, kupitia vitabu, makala na majarida
utajifunza mambo muhimu yatakayokupa ushindi mdogo mdogo katika maisha yako ya
kila siku.
Mwisho
sema HAPANA kwa utajiri wa haraka. Mpendwa rafiki yangu uhuru
wa kifedha unaandaliwa na ni mchakato na wala si swala la kufikiria kuwa
linakuja mara moja. Mchakato huu unaongozwa na kanuni maalumu ambazo kila mtu
anaweza kufanya na kufikia pato analotaka cha msingi ni kufahamu kuwa ili ufanikiwe
katika safari hii ni lazima uwe tayari kujitoa hasa na kujiwekea kanuni binafsi
ili ziwe mwongozo wako katika safari hii. Kwa bahati mbaya sana vijana wengi
siku hizi wamejikita kwenye kutafuta utajiri wa haraka na hivyo kusahau kuwa
utajiri unaandaliwa. Huwa nashangaa sana ninapoona vijana wakijazana kwenye
ofisi za bahati na sibu wakitegemea kuwa unaweza kulala masikini na kesho yake
ukaamka tajiri. Ndugu yangu zinduka utajiri hauji kwa namna hiyo bali unatakiwa
kuutafuta kwa kutumia kanuni ambazo ni halali na zinapimika siku hadi siku.
Kwa leo nimekushirikisha haya kwa ajili ya kuboresha
maisha yako mwaka 2017 endapo utayafanyia kazi. Niendelee kukuomba usambaze
jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye
tufanikiwe kuibadirisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi. Nakutakia mapambano mema.
Born to Win~Dream Big