Habari ya leo rafiki yangu
na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Karibu tena katika uchambuzi wa
kitabu ambapo leo hii ikiwa ni wiki ya sita katika mwaka 2017 naendelea
kutimiza ahadi yangu kwako ya kuhakikisha nakuletea uchambuzi wa kitabu kimoja
kila mwisho wa wiki (Ijumaa).
Pia, rafiki napenda
nikufahamishe kuwa ahadi yangu kwako haina gharama yoyote kwa maana ya kwamba
ni ya bure kabisa na hivyo unachotakiwa kufanya ni kutenga angalau saa moja
kila ijumaa au jumamosi kwa ajili ya kupitia mafundisho haya ili kwa pamoja tufanikiwe
kuyaboresha maisha yetu. Niendelee kukumbusha pia kama unataka kupata makala za
mtandao wa fikra za kitajiri moja kwa moja kwenye anuani yako ya barua pepe BONYEZA HAPA na kuacha taarifa zako na utakuwa
umeunganishwa bure kwenye mtandao wa fikra za kitajiri.
Katika uchambuzi wa wiki
hii nitakushirikisha machache niliyojifunza kwenye kitabu cha Mind
Frick ambacho kimeandikwa na T. Harv Eker. Mwandishi wa huyu ni Milionea,
Mwandishi na Mzungumzaji mashuhuri kwenye masuala ya kuihamasisha jamii kuishi
ndoto za maisha yao kwa mafanikio makubwa sana. Pia, unaweza kusoma kitabu
chake cha Secrets of the Millionaire Mind ambapo katika kitabu hiki pia
anatufundisha umuhimu wa kubadilisha fikra zetu ili ziwe za kitajiri (kupata
vitabu hivi tuma ujumbe kwenye fikrazakitajiri@gmail.com
nitakutumia nakala ya pdf).
Karibu tujifunze wote yale
ambayo ni ya muhimu kuboresha maisha yetu kutoka katika kitabu hiki;
1. Katika
maisha watu wengi hawaishi kusudi la maisha yao bali wanaishi ili mradi tu
maisha yaende. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa katika jamii wengi wameishi
maisha ya msongo wa mawazo kutokana na kufanya yale ambayo si vipaumbele vya
mapenzi yao bali tu wanafanya kwa vile wamekosa mbadala. Lakini habari ni njema
ni kwamba milango ipo wazi kwa ajili wale ambao wana nia ya kweli na wapo
tayari kutafuta kusudi halisi la maisha yao. Hivyo kila mmoja anaweza
kubadilisha maisha yake na kuishi maisha mapya yenye vipaumbele vya mapenzi
yake.
2. Njia
pekee kwa kila mmoja kuishi kusudi la maisha yake ni kuhakikisha kwanza
anajiamini ya kwamba anaweza kufanikisha jambo lolote ambalo amedhamiria. Hapa tunafundishwa
kwamba ni lazima kwanza tujipende na kujiamini kutokana na ukweli kwamba kama
haujipendi/kujiamini kamwe hauwezi kupendwa wala kuaminiwa na wengine. Pale unapojipenda
na kujiamini mwenyewe kuna nguvu kubwa yenye hamasa inayotoka ndani mwako hivyo
kukufanya ubadili mtazamo na vitendo vyako katika mazingira yanayokuzunguka.
3. Kama
unataka kuwa na maisha yenye furaha hakikisha unafanya vitu ambavyo hautajutia
mara baada ya kuvifanya au hata baada ya ukomo wa maisha yako. Mwandishi
anatuhamasisha kuwa furaha ya kweli inatokana na kufanya kwa ubora wa hali ya
juu yale ambayo ni kipaumbele katika maisha yetu. Kwa ufupi ni kwamba inabidi
tuishi maisha yetu kwa viwango vya juu ili pale ukomo wa maisha yetu
utakapowadia tusijutie yale ambayo hatukutekeleza. Hata hivyo kufanikisha
maisha haya ni lazima tutambue kuwa chanzo cha kweli cha furaha ya maisha yetu
kipo ndani mwetu na hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuishi maisha yenye furaha
pasipokujali ya maisha aliyonayo.
4. Hali
ya maisha tunayoyataka yamo ndani ya uwezo wetu na hivyo ni lazima tutambue
kuwa maisha yetu tunayaandaa sisi wenyewe. Kila mmoja ni muhusika mkuu
(steering) wa filamu ya maisha yake hivyo ni wajibu wa kila mmoja kufanya kila
liwezekanalo kuboresha matukio ya maisha yake.
5. Mafanikio
kwenye biashara au kitu chochote kile ambacho mtu ameamua kufanya ni lazima
yaanzie ndani. Biashara yoyote ambayo imejengwa kwa dhamira kutoka ndani ni
lazima iwe biashara yenye mafanikio kwa mmiliki. Muhimu nikutambua kuwa undani
wako (fikra) ndo unaumba mwonekano wako kwa nje hivyo furaha, amani na nguvu ni
lazima vianzie ndani mwako.
6. Furaha
na mafanikio vyote vinaanzia akilini mwako hivyo wewe huyo huyo unaweza kuwa
katika hali ya uchanya au hasi. Ili ufanikiwe zaidi katika maisha yako ni
lazima uifundishe akili yako kuona uchanya katika matukio ya maisha yako.
7. Nafsi
yako inaishi (exist) katika nafsi mbili ambazo ni nafsi yako halisi (wewe wa
ukweli) na nafsi yako ya uongo (wewe wa uongo). Nafsi yako halisi ni jinsi vile
ulivyoumbwa na nafsi yako ya uongo ni ile ambayo umejifunza kuwa katika maisha
yako ya kila siku. Hapa tunafundishwa kuwa tulikuja ulimwenguni humu tukiwa
wazi na kupitia jamii inayotuzunguka tumejikuta tupo jinsi tulivyo kwa sasa.
Hivyo utagundua kuwa fikra na mitazamo juu ya maisha yetu kwa sasa ni chimbuko
la yale tuliyojifunza katika ulimwengu huu. Kumbe basi kwa ukweli huu kila
mmoja ana nafasi ya kubadilisha fikra na mitazamo juu yake yeye mwenyewe na
maisha yake kwa ujumla.
8. Asilimia
kubwa ya mwonekano na tabia zako ni matokeo ya makuzi na malezi yako kutoka kwa
wazazi/walezi, walimu, viongozi wa dini, ndungu, marafiki au jamii
inayokuzunguka kwa ujumla wake. Pamoja na ukweli huu kila mmoja anaweza
kubadilisha mwonekano au tabia zake kwa kujifunza kutenda yale ya muhimu katika
maisha yake.
9. Wewe
ni tunda la yale unayoyawaza kwa muda mrefu. Una uwezo wa kuchagua yale ambayo
yana kipaumbele katika maisha yako ili yatawale sehemu kubwa ya mfumo wa fikra
zako.
10. Wengi tumeshikiliwa na fikra au
mitazamo yetu kila tunapojaribu kusonga mbele pasipokufahamu. Kwa vile hatujui
kuwa sisi ndo tunaumba matokeo ya maisha yetu tumeendelea kulalamikia mfumo wa
nje ya nafsi yetu kama vile serikali, wazazi au mazingira kwa ujumla. Maisha ya
namna hii yametufanya tuwe na hofu, wivu, chuki na mambo mengine mabaya katika
maisha yetu ya kila siku. Lakini habari njema ni kwamba siku ambayo utatambua
kuwa wewe ndo umekuwa ukijikwamisha kupitia mitazamo na fikra zako ndo siku
utaanza kubadilika mara moja.
11. Kila mmoja ana kuishi kusudi la maisha
yake kwa kubadilisha mazoea ya fikra/mtazamo wake. Kwa kufanya hivyo hisia na
vitendo vya mhusika vinabadilika kuelekea kwenye maisha mapya ya kusudi la
maisha yake. Maisha haya yatakuwa ni maisha yenye amani, furaha, upendo,
busara, hekima na kila aina ya mafanikio.
12. Ili kuwa na maisha yenye utulivu wa
fikra na amani katika mazingira yanayotuzunguka ni lazima tukubali kuwa kuna
nguvu ya ziada ambayo inafanya kazi juu ya maisha. Nguvu hii ya asili
imefichika kwenye upeo wetu wa fikra na hivyo kwa asili kila mtu ana imani yake
juu nguvu hii; wapo wanaosema kuwa kuna Mungu, wengine wanasema ni miungu na
wengine wanasema kuna nguvu ya ajabu ya kisayansi. Sisi ni sehemu ya nguvu na
yenyewe ni sehemu yetu na kila sehemu tulipo nguvu hii pia ipo kwa ajili ya
kutuongoza. Hivyo la muhimu ni wewe kufahamu na kutii misingi ya imani yako ili
ikuongoze kuishi maisha ya amani na upendo.
13. Toka kuumbwa kwetu tumekuwa na
muunganiko wa nguvu hii ya asili japo kadri tunavyozidi kukua na kufundishwa
nafsi zetu za uongo (rejea namba 7) ndivyo tunavyotenganishwa na nguvu hii ya
asili au waweza sema roho mtakatifu. Mfano, mtoto kadri anavyokua ndivyo
anabadilika kutoka kwenye roho ya kujiamini na kuanza kuishi maisha ya hofu ambayo
ni kinyume na matakwa ya nguvu hii ya asili.
14. Kadri mtu anavyoanza kuishi kusudi la
maisha yake ndivyo anavyorejesha muunganiko wake na nguvu ya asili (roho
mtakatifu) na hivyo kurejesha nafsi yake halisi (true self rejea namba 7). Na
njia pekee ya kurejesha nafsi yako halisi ni kuutafuta ukweli. Katika
muunganiko huu ni rahisi mtu kuishi maisha yenye furaha na kila aina ya
maifanikio.
15. Kinachowatufautisha watu ni namna
ambavyo wamefanikiwa kuishi kusudi la maisha yao na hivyo kurejesha nafsi yao
halisi yenye muunganiko na nguvu ya asili. Kwa muunganiko huu na nguvu ya asili
watu wenye mafanikio wameweza kuona fursa nyingi na hivyo kuzitumia kupata
mafanikio makubwa sana. Pia, kwa kuunganika na nguvu hii ya asili wanamafanikio
wameweza kuishi maisha yasiyo na msongo wa mawazo ikilinganishwa na watu ambao
hawajui kusudi la maisha yao.
16. Fikra zinaleta hisia, hisia zinaleta
vitendo na kupitia vitendo tunapata matokeo ya fikra zetu. Hivyo kama unataka
kuacha tabia ambayo huipendi katika maisha huna budi kuhakikisha unaanza na
kudhibiti fikra na hisia zako. Unaweza kutumia kanuni hii kuhakikisha
unapambana na hisia zinazopelekea uwe na maisha ya hofu, chuki, wivu au
wasiwasi.
17. Sio lazima kila jambo unalofikria
lifanyiwe kazi. Mfumo wa fikra ni sawa na viungo vingine vya mwili kama vile
mguu, mkono au tumbo. Hatuwezi kusema kuwa wewe ni miguu tu au wewe ni mkono tu
bali tunapotamka kuhusu wewe tunamaanisha wewe kwa ujumla wako. Hivyo jinsi
tunavyoweza kudhibiti viungo vya miili yetu ndivyo tunapaswa kudhibiti mfumo wa
fikra zetu ili kuhakikisha tunawaza yale ambayo ni muhimu katika maisha yetu.
18. Ubora wa maisha yako unategemea na
ubora wa fikra zako. Unakukumbuka msemo mmoja kipindi tunafundishwa kompyuta
enzi hizo? “Gabbage in gabbage out”. Ndivyo
ilivyo hata kwenye mfumo wa fikra zetu kama utaweka mabaya tegemea kupata
mabaya na ukiweka mazuri tegemea kupata mazuri pia. Uamzi upo mikononi mwako
kuchagua ni yapi uendelee kuyawaza kwa muda kwa ajili ya maisha unayoyataka.
19. Msongo wa mawazo ni hatari kwa afya
yako na utajiri wako pia. Yapo magonjwa mengi ambayo yanaambatana na msongo wa
mawazo na hivyo njia ya pekee ya kuepukana na magonjwa haya ni kukabiliana na
fikra zinazopelekea msongo wa mawazo.
20. Unapoamua kuanza kuishi maisha yenye
fikra chanya ni lazima utambue kuwa kuna upande mmoja wa fikra ambao hautakuwa
tayari kukuruhusu kuachana na mazoea yako. Upande huu ni ule wa fikra ambazo
umeizoesha akili yako kwenye tabia za maisha yako ya sasa, hivyo unatakiwa kuwa
tayari kuubadilisha upande huu. Pia, katika mchakato huu wa maisha yako mapya
ni lazima uwe mvumilivu kutokana na ukweli kwamba mabadiliko hayatatokea mara
moja bali ni zoezi la muda ambalo litakuhusisha wewe kwenye kila sekta ya
maisha yako.
Mpendwa rafiki na msomaji
wa mtandao wa fikra za kitajiri, haya ni machache kati ya mengi ambayo
nimejifunza kutoka kwenye kitabu hiki, naamini kama utayafanyia kazi yataboresha
maisha yako. Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale
unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa
mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest
badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Ili kupata makala za namna hii acha
taarifa zako kwa kujaza fomu hapo chini.
Karibuni kwenye fikra za
kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.
Born to Win~Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: 0786881155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com