Mpendwa rafiki yangu kwenye ukurasa huu wa facebook
naamini kuwa upo vizuri na unaendelea kupambana ili kuhakikisha kuwa kesho
yako inakuwa bora kwani naamini unatambua kuwa hakuna kesho bora
ambayo haikundaliwa.
Kama ndo hivyo ni jambo la kujivunia kwa hatua hiyo katika
safari uliyoianzisha. Safari hii ni ndefu na tofauti na safari nyingine
yenyewe haina mwisho badala yake imejaa milima na mabonde. Ni katika safari hii
unatambua kuwa kadri unavyomaliza hatua moja ndivyo unavyojifunza kuwa kuna
hatua zaidi mbele. Nelson Mandela alilielezea hili vizuri; nanukuu tafsiri ya
Kiswahili “Baada ya kupanda kilima na kufika kileleni ndipo nilipojifunza kuwa
kuna vilima vingi ambavyo napaswa kuvipanda”.
Hivyo mpendwa rafiki
yangu hakikisha kuwa kila iitwapo leo unafanya jambo ambalo ni ushindi wa
kukufikisha kwenye kilele cha mafanikio huku ukitambua kuwa ushindi mmoja
unaanzisha safari nyingine.
Kama ambavyo tumeona kuwa maisha ni safari ambayo haina
mwisho endapo upo duniani humu ndivyo ilivyo kwenye elimu. Leo hii ningependa
rafiki yangu nikuletee makala inayohusu jinsi gani dunia inavyobadirika kwa
kasi na namna ambavyo unatakiwa kujilinda dhidi ya mabadiriko haya, kwa maana
nyingine unatakiwa kuijenga safina yako. Karibu tujifunze wote na baada ya
mafundisho haya ujiulize je umeijenga safina yako??
Kabla ya kuanza somo la leo ningependa tujikumbushe
kidogo kwenye kwenye historia ya binadamu na ugunduzi wa teknolojia. Tuliopita
shule tunakumbuka kuwa binadamu amepitia kwenye mifumo ya ugunduzi wa
teknolojia tokea kipindi cha zama za mawe, kikafuatiwa na kipindi za zama za
chuma, kilichofuatiwa na mapinduzi ya viwanda na baadae ndipo zama za taarifa
(information era).
Katika mapinduzi haya ujifunze yafuatayo; Moja,
Mabadiriko ya teknolojia yanalenga kuongeza tija ya utendaji kazi pamoja
kuongeza/kuboresha uzalishaji mali. Kwa maana ya kwamba binadamu amekuwa na
ugunduzi wa teknolojia ambayo moja kwa moja unalenga katika kurahisisha
utendaji kazi. Mfano, katika zama za mawe mwanadamu alitegemea zaidi matumizi
ya vifaa vya mawe ambavyo utendaji na uzalishaji wake ulikuwa duni
ilikilinganishwa zama za mapinduzi ya viwanda.
Pili, kila umbuzi wa teknolojia unalenga kuimaliza
kabisa teknolojia iliyokuwepo mwanzo au kuiboresha kwa ajili ya ufanisi zaidi.
Mfano, ugunduzi wa teknolojia ya habari/mawasiliano umepelekea kuboresha utendaji
kazi wa sekta ya viwanda. Sote ni mashahidi kuwa kwa sasa dunia imekuwa ni
familia moja ambayo kila linatokea sehemu yoyote linaweza kumfikia mtu yeyote
cha msingi awe ameunganishwa na ulimwengu mpya kwa maana ya mtandao wa
intaneti. Kwa maana hiyo ni rahisi mtu kutangaza bidhaa zake na kuuza popote
apendako kwa urahisi zaidi ata kama yeye hajawahi kufika huko.
Tatu, kila ugunduzi wa teknolojia upo kwa ajili ya
mafanikio yako. Tumeona ni jinsi gani mwanadamu aliweza kuboresha hali ya
maisha yake kipindi cha zama za chuma ikilinganishwa na zama za mawe. Pia,
baada ya mapinduzi ya viwanda ukisoma historia utaona kuwa ndipo mfumo wa
upebapari ulipoibuka kwa kasi. Kwa hisitoria utagundua kuwa katika kipindi
hicho ndipo mataifa mengi yalikuwa na mitaji ya kutosha na ndipo wakaanza
kutafuta sehemu za uwekezajaji nje ya mipaka yao.
Ninachotaka ujifunze hapa ni kuwa katika kipindi cha
ubepari au kipindi cha mapinduzi ya viwanda ndipo matajiri wengi wa historia
waliweza kufanikiwa kiuchumi, mifano michache ni kama Andrew Carnegie ambaye
alikuwa tajiri kupitia kiwanda cha kutengeneza vyuma (steel industry) na
bilionea mwingine ni John D.
Rockefeller ambaye alifanikiwa kupitia biashara ya mafuta. Lakini pia,
angalia kipindi hiki cha mapinduzi ya habari/teknolojia ya mawasiliano ambacho
mtu anaweza kulala masikini na akaamka tajiri. Katika kipindi hiki jarida la
Marekani la Forbes linakuambia kuwa ni kipindi ambacho kimetengeneza mabilionea
wengi kuliko kipindi chochote kile, mifano michache ni kama Bill Gates kupitia ugunduzi wake wa Microsoft na Mark Zuckerberg mmiliki wa facebook na
wengineo wengi.. swali la kujiuliza ni
je umeijenga safina yako katika kipindi hiki cha mapinduzi ya mawasiliano???
Nne, kila uvumbuzi wa teknolojia unasababisha mifumo ya
maisha ya mwanadamu kubadirika. Hapa ndipo patamu, kama hujagundua kuwa dunia
inabadirika na inakutaka kwa lazima ubadirike utateseka sana kwa vile utaendelea
kuishi katika mfumo ambao umepitwa na wakati. Mfano mzuri enzi za babu zetu na
baba zetu ilikuwa ni kawaida kutuambia kuwa nenda shule mwanangu na ujifunze
kwa bidii ili uje upate ajira nzuri kwa ajili ya kutusaidia wazazi wako…..
lakini leo hii kizazi chetu ni mashahidi kuwa wapo wasomi wengi wanaoendelea
kuhangaika mitaani kwa ajili ya ajira pasipo mafanikio. Dunia imebadirika
lazima tubadirike na kufikilia zaidi kuwasomesha watoto wetu kwa ajili ya wao
kuzalisha ajira nasi kutegemea ajira. Kama mzazi hakikisha unaanza kuzalisha
ajira leo hii kwa kadri uwezavyo ili kesho na kesho kutwa mwanao ukamwajiri
kipindi anaanza maisha yake.
Dunia imebadirika… zamani ilikuwa ni kawaida mwanafunzi
kusomeshwa bure na Serikali kuanzia shule ya msingi mpaka chuo kikuu, baada ya
hapo kikafuatia kizazi cha bodi ya mikopo ya wanafunzi (ambacho ndio kizazi
chetu) ambacho tumekopeshwa kabla ya hata kujua tutarudisha vipi hiyo mikopo na
leo hii tunaitwa wadaiwa sugu. Pamoja na hayo tutakumbuka kuwa kipindi chetu
mikopo hata kama ilikuwa kwa madaraja lakini wanafunzi wengi walipata mikopo.
Dunia inabadirika leo hii kupata mikopo ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu. Sipo
kuelezea ugumu wa kupata mikopo kwa sasa la hasha kwani mimi kamwe si mtu wa
kulalamikia mfumo bali ninachotaka ujifunze hapa ni kuwa dunia inabadirika kwa
kasi sana hivyo ni vyema ukaanza kujenga safina yako kwa ajili ya masomo na
ajira ya watoto wako pamoja na ndugu zako kwa kizazi chako na vizazi vyao. Je umeijenga safina?
Mwisho, kadiri dunia inavyobadirika ndivyo inavyowainua
watu na kuwaangamiza wengine. Mfano, kuna biashara ambazo enzi zilizopita
zilikuwa zinavuma sana na ilikuwa rahisi wamiliki kutengeneza faida kupitia
biashara hizo lakini leo hii biashara hizo hazifai kitu tena, mifano michache
ni kama biashara ya internet café baada ya ugunduzi wa smartphone hazifai kitu
tena kwa sababu kila mtu anatembea na intaneti mikononi mwake, mfano mwingine
ni biashara ya modem kwa sasa hazifai kitu tena kwani kila mwenye smartphone
anaweza kuunganisha intaneti na compyuta yake na mfano mwingine ni ugunduzi wa
kutuma pesa kwa njia ya simu kulivyoharibu soko la western union na mengine
mengi. Jenga safina yako ukiwa makini kungalia ni biashara hipi inafaa katika
kipindi hiki cha mapinduzi ya teknolojia ya habari/mawasiliano.
Mpendwa rafiki yangu nimekushirikisha mambo matano ya
kukuonesha kuwa tupo katika dunia ambayo inabadilika kwa kasi. Naomba utumie makala
hii kujikumbusha na kujitazama upya kama unacheza ngoma ambayo inachezwa na
walimwengu wa sasa hasa katika kufikia ndoto zako. Tengeneza safina yako juu ya
msingi imara ili kesho na kesho kutwa hisiyumbishwe na mawinbi ya dunia.
Kama umejifunza kitu kwenye makala hii naomba uisambaze
kwa kadri uwezavyo ili somo hili liwafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuifanya dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi. Karibuni kwenye ulimwengu wa
elimu hisiyokuwa na mwisho.
Born to Win~Dream Big
A.M. Bilondwa
0786881155
fikrazakitajiri@gmail.com