Hii Hapa Kauli Mbiu Ambayo Nakusihi iwe Mwongozo wako kipindi chote cha mwaka 2017


Tunapoelekea kuumaliza mwaka 2016 na kuuanza mwaka 2017 ni matumaini yangu kuwa rafiki unaendelea vizuri. Ni jambo la heri na la kujivunia kuona mpaka sasa tu wazima wa afya kwani wapo wengi ambao walitamani kufikia siku kama ya leo lakini hawakufanikiwa. Hivyo mimi na wewe ni akina nani hasa mpaka tumefanikiwa kufikia muda kama huu? Shukrani za pekee ni kwake muumba kwani ndiye anaejua makusudi ya uwepo wetu hapa duniani.

Karibu tena katika makala yangu ya leo ambapo leo hii nitakushirikisha kauli mbiu muhimu ambayo inatakiwa kuwa dira ya mafanikio yako katika kipindi chote cha mwaka 2017. Kabla ya kufahamu kauli mbiu hii, ningependa nikukumbushe kuwa nimekuwa nikijitahidi kuhakikisha kila makala ninayoandika inakuwa na hamasa ya kukutaka wewe rafiki yangu uwe na mtazamo wa kuona kuwa kila aina ya mafanikio unayoyataka yanaanzia ndani mwako na wala si kwingineko. Kwa maana hii leo hii jinsi ulivyo ni matokeo ya mambo ambayo umekuwa ukiyachagua katika maisha yako ya kila siku.

Miaka itakuja na kupita kama ambavyo majuzi tulisherekea mwaka 2016 ndivyo ilivyo hata kesho tutasherekea mwaka 2017 hali kadhalika 2018. Jambo moja la kujiuliza kila tunaposherekea mwaka mpya ni je tupo kwenye njia sahihi ya kuzielekea ndoto zetu? Bila kufanya hivyo tutaendelea kusherekea sherehe za mwaka mpya enzi na enzi mpaka pale ambapo maisha yetu yatafikia ukomo kwenye sayari hii huku tukizikwa na ndoto zetu.

Rafiki yangu leo hii unaposherekea mwaka mpya 2017 naomba nikupe kauli mbiu ambayo itakuwa mwongozo wako katika kipindi chote cha mwaka 2017. Kauli mbiu hii si nyingine bali ni KUWAZA CHANYA (POSITIVE THINKING) katika kila hali/tukio.

Nini Maana ya Kauli Mbiu Hii?
Kuwaza Chanya maana yake ni kwamba unaifundisha akili (ubongo) yako muda wote ifikilie katika hali ya uchanya pasipo kutoa nafasi kwa mawazo hasi. Kwa maana hii ni kwamba kila tukio unalokutana nalo unatakiwa ufahamu kuwa tukio hilo lina sura mbili (Chanya au Hasi) na hivyo wajibu wako mkubwa ni kutafuta hali ya uchanya kwenye tukio husika.


Ukiwa unawaza katika hali chanya kamwe wewe haupaswi kuwa mtu wa kunungunika, kulalamika, kukasirika, kuwa na hofu, kuwa mmbea, kuwa na visingizio, kukata tamaa, kuhahirisha mambo n.k. bali unatakiwa matukio yote unayokutana nayo unayachambua ili upate upande chanya wa hayo matukio. Mfano, umepanga kukutana na mtu sehemu flani na umejitahidi ukafika muda ule ule mliokubaliana lakini kwa bahati mbaya yeye amechelewa kufika kwa muda wa nusu saa. Kwenye tukio kama hili unachoweza kufanya ni kuangalia kwa muda huo unaomsubiria ni kitu gani unaweza kufanya ili akiendelea kuchelewa husipoteze muda wako bure, unaweza ukasoma kitabu/makala kama unacho kwenye simu (softcopy), unaweza ukasikiliza nyimbo ambazo huwa ukisikiliza zinakupa hamasa au faraja au ukasikiliza sauti za vitabu vilivyosomwa (audio books).

Je nini unatakiwa kufanya ili uwaze chanya muda wote?
Ili uwaze chanya kwenye kila aina ya tukio fanya mambo yafuatayo;

Fikiri kama mtoto. Watoto huwa wana mfumo wa mawazo ambao mtu mzima ukifanikiwa kuuhishi mfumo huu kamwe hauwezi kuwa na mawazo hasi. Mfano, watoto muda wote wana furaha, hawana hofu na matukio ya baadae au yaliyopita (wanaishi maisha ya sasa), hawakati tamaa pale wanapokutana na jambo jipya na hawafikirii kuhusu sheria zinasemaje. Kwa hali kama hii watoto wanawaza mambo mema kwenye kila hali wanayokutana nayo kwani hawajui mabaya yaliyopo kwenye ulimwengu huu.
Kama mtu mzima unaweza kuwaza kama mtoto pale ambapo unafanya jambo jipya. Husifikirie kushindwa kwenye kila jambo unalofanya bali fahamu ya kuwa una mfumo wa mawazo ambao unaweza kutekeleza kila jambo endapo umetumiwa ipasavyo. Pia, tumia njia hivyo kujiepusha hofu ambayo imekuwa ikuzuia kutekeleza malengo yako.
Tumia lugha ya mwili (Body language). Mwaka 2017 hakikisha kuwa mwonekano wako wa nje unaonyesha kile unachokiwaza ndani mwako. Mara nyingi kwenye jamii inayotuzunguka tumezoea kusikia kauli kama kijana yule anaonekana kuwa na tabia nzuri, yule mzee huwa ana busara sana… Unaweza ukajua mawazo ya mtu hata kabla hajaongea ila kwa kuangalia mwonekano wake wa nje. Hivyo ndivyo na wewe unatakiwa uwe kama kweli unawaza chanya ili jamii inayokuzunguka ione vitu vya tofauti kutoka kwako. Tambua kuwa tupo jinsi tulivyo kutokana na yale tunayoyawaza muda mwingi.

Kuwa na muda wa kuongea na nafsi yako. Unapoishi kwenye kauli mbiu ya uchanya, mwaka 2017 hakikisha unakuwa na muda wa kuongea na nafsi yako. Kuongea na nafsi yako ni pale ambapo unakuwa na maneno ya kujiongelea mwenyewe na mara nyingi inafaa uwe sehemu yenye utulivu kwa ajili ya kuepuka mwingiliano na kalele nyingine ambazo zinaweza kukuhamisha.
Unapoongea na nafsi yako hakikisha unajisemea maneno chanya ambayo yanakuhamasisha kuchukuwa hatua za ushindi. Epuka sentensi kama “Kila ninalogusa linaniendea kinyume, Siwezi kukamilisha kazi hii kwa muda, Siwezi kufanya biashara, Siwezi kufaulu somo hili, n.k”. Maneno chanya ambayo unaweza kujisemea ni;
  • Kila ninalogusa lazima nifanikiwe;
  • Sijawahi kushindwa, hivyo lazima niishinde changamoto hii;
  • Naweza kufanya jambo lolote ninalodhamiria;
  • Najiamini katika huduma ninazotoa hivyo lazima nipate wateja;
  • Mimi ni bingwa katika tasnia hii;
  • Mimi ni hodari; n.k

Kuwa mtu wa kutathmini mawazo yako. Zoezi la kuwaza chanya ni gumu kama ulikuwa hujazoea kufanya hivyo. Kwa vyovyote vile lazima utajikuta unaanza kutawaliwa na mawazo hasi. Ili kukabiliana na mawazo hasi lazima uwe na muda wa kujiuliza mara kwa mara juu ya lile unalowaza kama lina mchango kwenye mafanikio yako na pale unapotambua kuwa upo katikati ya mawazo hasi achana nayo mara moja.

Chagua marafiki na makundi ya kujumuika nayo. Kuna msemo maarufu usemao kuwa ndege wenye manyoa yanayofanana huruka pamoja. Kama ulikuwa na marafiki ambao mmekuwa mnatumia muda mwingi kufanya mambo yasiyo na tija katika mafanikio yako kwa sasa unatakiwa kuchagua marafiki wapya ambao watapelekea ufanikiwe kuiishi kauli mbiu ya uchanya. Epuka marafiki ambao muda mwingi wanautumia kulalamika, kusengenya, kubeza yaw engine, kukatishana tamaa n.k

Pia, Katika ulimwengu wa sasa ambao umetawaliwa na mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano husipokuwa makini kwenye makundi (magroup) ambayo umeunganishwa nayo itakuwa vigumu sana kwako kuwaza chanya kwani mara nyingi makundi haya yametawaliwa na mzaha mwingi ambao kwako hauna tija. Mwaka 2017 hakikisha makundi ambayo hayana tija unajiondoa mara moja na kujiunga na makundi mapya ambayo yatakupa mawazo, ushauri pamoja na changamoto katika kutekeleza malengo yako.

Tenga muda wa kusoma vitabu au makala za hamasa. Kama unataka kufanikiwa ni lazima uwe mtu wa kusoma vitabu au makala zinazoendana na yale unayoyahitaji katika maisha yako. Dunia kwa sasa imekuwa ni kijiji kwani unaweza kusoma kitabu chochote kile kwa kutumia simu yako. Tatizo letu tumekuwa wavivu sana katika kujisomea vitabu/makala za namna hii lakini cha kushangaza utakuta mtu muda wote yupo bize na kusoma posti za watu au magazeti ya udaku kwenye mtandao hila ukimuambia tumia saa moja kila siku kujisomea kitabu/makala atakuambia kuwa makala/kitabu kina kurasa nyingi sana.
Mpendwa rafiki yangu naomba mwaka 2017 utambue kuwa hakuna mafanikio yoyote ambayo yatakuja kwa njia ya mkato lazima uwe tayari kuwekeza nguvu, muda pamoja na rasilimali ili hatimaye ufanikiwe. Anza kuwekeza sasa kwa ulisha ubongo wako na maarifa mbalimbali kutoka kwa waliofanikiwa.

Kuwa Mtu wa Vitendo.  Mwaka 2017 unapoongozwa na kauli mbiu ya uchanya hakikisha yale unayoyawaza unayaweka katika mfumo wa vitendo mara moja pasipo kuhairisha au kusubiria. Wanafalsafa wanatuambia kuwa kila kitu kinaumbwa kutokana na mfumo wa mawazo na kupitia mfumo huu kila mtu ana uwezo wa kuumba chochote anachokiwaza. Tatizo kubwa ambalo limekuwa linatutofautisha kwenye uumbaji wa vitu ni pale ambapo wengi wetu tumeruhusu visingizio kukutawala na hivyo kuishia kutofanya lolote. Wengi mtakuwa mashahidi kuwa unaweza kuwa na wazo zuri hila kutokana na mazoea ya kuwaza pasipo kutenda inafikia kipindi mpaka unalisahau wazo lako halafu ghafla ukiwa unatembea mtaani unashangaa kuna mtu ameanzisha biashara au anatoa huduma sawa na lile wazo lako. Hapa kinachokutofautisha wewe na yeye ni kwamba mwenzio alikuwa na wazo na akalitafsiri kwenye vitendo. Mwaka 2017 hakikisha unakuwa mtu wa vitendo badala ya kuishia kuwaza tu.

Mwisho naomba nikutakie sherehe njema za mwaka mpya. Rafiki yangu unaposherekea mwaka mpya hakikisha unauanza mwaka mpya kwa kuwaza chanya kwani nakuhakikishia kuwa miezi 12 ni muda mfupi sana ukiwa unaishi kwenye malengo yako. Ulimwengu wa sasa ni ulimwengu wa teknolojia ya mawasiliano hivyo kama rafiki naomba uendelee kusambaza jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadirisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi. HERI YA MWAKA MPYA 2017.
Karibuni kwenye fikra tajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win~Dream Big
A.M. Bilondwa
0786881155
bilondwam@yahoo.com



onclick='window.open(