Uchambuzi wa Kitabu cha How To Live On 24 Hours A Day: Jinsi ya kuishi masaa 24 katika siku.

Habari rafiki yangu mpendwa ambaye umeendelea kujifunza kupitia Makala za uchambuzi wa vitabu ambazo nimekuwa nashirikisha jamii kupitia mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI. Karibu katika uchambuzi wa kitabu cha leo ambacho ni cha 7 kati ya vitabu 30 ambavyo nimejiwekea lengo kuvisoma katika kipindi cha mwaka huu 2020.

Kama bado hujajiunga na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la tafakari kila siku pamoja na kujumuika na watu wenye mtazamo sawa, tafadhali JIUNGE SASA.

Kitabu ninachokushirikisha kupitia makala hii ni How To Live on 24 Hours A Day” kutoka kwa mwandishi Arnold Bennett. Mwandishi anatumia kitabu hiki kutushirikisha namna ambavyo kila mmoja anaweza kutekeleza majukumu yake ya siku kwa furaha na ufanisi. Mara nyingi katika jamii watu wengi huwa wanafanya kazi kwa nguvu na kwa bidii ya kiwango cha juu katika masaa mawili ya mwanzo kazini. Mfano, kama ni wafanyakazi masaa ambayo yanatumika ipasavyo kwa ajili ya uzalishaji ni masaa mawili ya awali na masaa sita yalibakiwa kwenye muda wa kazi yanatumiwa kwa kiwango cha kawaida cha utendaji kazi.

Hata hivyo, tunatakiwa kutambua kuwa siku ina masaa 24, hivyo baada ya kumaliza majukumu ya mwajiri wako au majukumu ya biashara zako kwa muda wa kawaida wa kazi unatakiwa kujiuliza masaa yanayobakiwa yanatumiwa vipi kwa ajili ya kuzalisha mafanikio zaidi kwenye kila sekta ya Maisha yako. Je unatumia muda mwingi kuangalia TV na kusinzia muda mrefu? Kuna mambo mengi ambayo unapuuzia kufanya katika muda wako wa ziada lakini kama yangefanyika yana nafasi ya kubadilisha Maisha yako. Je kila siku asubuhi unashindwa kuamka asubuhi na mapema kabla ya watu wengine hawajaamka ili upangilie majukumu yako ya siku? Anza kuamka mapema lisaa au masaa mawili kabla ya wengine na utaona utofauti katika Maisha yako.

Karibu ushirikiane nami kujifunza machache kati ya mengi ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:

1. Muda ni zawadi ambayo watu wote wamepewa kwa usawa. Katika siku watu wote tumepewa masaa 24 ambayo kila mmoja ana ratiba yake. Mengi yameandikwa kuhusu jinsi gani watu wanatakiwa kuishi kwa bajeti ya pesa lakini ni machache yameandikwa kuhusu kuishi kwa bajeti ya muda. Wengi tumezoea kusikia kauli kama vile “muda ni fedha”. Ni sahihi kuwa muda ni pesa lakini kauli hii haijitoshelezi kwa kuzingatia kuwa thamani ya muda zaidi ya pesa endapo umetumiwa vyema.

2. Wanasayansi wamefanya kila aina ya chunguzi kuhusiana na ulimwengu na sayari nyinginezo lakini wameshindwa namna ya kupunguza au kuongeza muda. Muda ni rasilimali kwa ajili ya kufanikisha chochote; kupitia muda kila kitu kinaweza kufanyika na pasipo muda hakuna linaloweza kufanyika. Hivyo, muda ni bidhaa ya kipekee ambayo kila mtu anayeishi ana uhakika wa kuimiliki tena bila hofu wala wasiwasi kuwa inawezakuibiwa kama ilivyo kwa bidhaa nyinginezo. Bidhaa hii binadamu wote kila siku tunapewa kiwango sawa kwa maana hakuna anayepata zaidi au pungufu ikilinganishwa na mwenzake.

3. Watu wengi wanaishi katika muda iliopita au muda ujao. Pamoja na kwamba hakuna mwenye uhakika na muda wa baadae lakini bado watu wanashindwa kuishi katika muda uliopo mbele yao. Mfano, ni mara nyingi tunasikia kauli kama vile: “nikipata muda nitatekeleza hilo”, “nikiwa na muda zaidi nitakamilisha….” na kauli nyingine nyingi ambazo zinaonesha kana kwamba watu wana uhakika wa kupata wa ziada nje ya yale masaa 24 kwa siku. Somo kubwa ni kwamba kila saa katika siku tunatakiwa kuishi kwa ukamilisho wa majukumu yenye tija katika Maisha yetu.

4. Tunaishi katika ulimwengu ambao kila mara tunakuwa na matamanio ya kufanikisha baadhi ya vitu kwenye Maisha yetu. Ni kawaida mwanadamu yeyote kutamani katika Maisha kwa kuwa matamanio hayo ndiyo yanafanya Maisha yawe na thamani. Hali hii ya kutamani zaidi katika Maisha inatokana na ukweli kwamba kila siku tunawajibika kisheria kuhakikisha tunajilinda wenyewe pamoja na familia zetu katika hali ya afya bora na salama, kukidhi mahitaji yote ya kifedha, kulipa madeni tuliyonayo, kuwekeza na kuhakikisha kila mara tunaongeza thamani ya rasilimali tunazomiliki. Hili ni jukumu kubwa ambalo ni wachache wanaofanikiwa katika kipindi cha Maisha yao. Wachache hao ni wale ambao wanatambua umuhimu wa kuishi kulingana na muda walionao wa masaa 24 katika kila siku ya Maisha yao. Hata hivyo, ni lazima tukubaliane kuwa hata hao wachache waliofanikiwa kimaisha, Maisha yao kila siku wanakabiliwa na shauku ya kuongezeka zaidi. Hivyo, wote kwa ujumla masaa 24 katika siku yanakabiliwa na hitaji la kutimiza majukumu yetu kwa ajili ya kupata ridhiki zaidi ya Maisha.

5. Siri muhimu ya kufurahia maisha ni kuwa na mpangilio wa majukumu kulingna na muda wa masaa 24 katika siku. Ndani ya masaa hayo 24 unatakiwa kuridhika na yale yanayotekelezeka kwa kutumia uwezo wako wa juu na kuacha yale ambayo yapo nje ya uwezo wako kulingana na nyakati husika. Tumeona kuwa kila siku tunaishi kwa ajili ya kutimiza shauku ya nafsi ya kutaka kuongezeka zaidi katika Maisha, hata hivyo, ni lazima tufahamu kuwa wanaoridhisha nafsi zao ni wale ambao kila mara wapo tayari kuchukua hatua za kuboresha Maisha yao kwenye muda wao wa kila siku. Kama hauchukui hatua zinazolenga kutimiza shauku ya nafsi yako mar azote utajikuta unaishi Maisha yenye msongo wa mawazo na hisia ovu.

6. Uzuri uliopo katika rasilimali ya muda ni kwamba hauwezi kuadhibiwa kwa kunyanganywa au kupunguziwa rasilimali hiyo kutokana na matendo yaliyopelekea upoteze muda katika historia ya Maisha yako. Rasilimali hii inakusubiria katika utimilifu wake kwa siku zote za baadae katika Maisha yako. Mwaka kesho, mwezi ujao, wiki ijayo, kesho na lisaa lijalo vyote vipo katika ukamilifu wake kwa ajili yako kana kwamba haujawahi kupoteza muda. Tafsiri yake ni kwamba kama huko nyuma uliwahi kufanya makosa ambayo yamepelekea kujutia muda uliopotea sasa una nafasi ya dhahabu ya kujifunza kutokana na makosa hayo.

7. Tumeona kuwa nafsi imeumbwa katika hali ya kutoridhika kamwe, hali ya kuhitaji kuongezeka zaidi na hali ya kutaka kujimilikisha kila linalowezekana katika ulimwengu huu. Hivyo ndivyo kwa asili Maisha yetu yalivyo. Hata hivyo, mwandishi anatushirikisha kuwa kuna umuhimu wa kuwa na vipaumbele katika Maisha. Wapo watu wengi ambao wameharibu Maisha yao kutokana na tabia ya kujaribu kila kitu badala ya kukamilisha jambo moja kwa wakati. Hivyo, katika kuhakikisha tunaishi katika ukomo wa muda wa masaa 24 katika siku hatuna budi kukwepa visababishi au viashiria vya kutokufanikiwa kwenye jambo lolote ambalo tumeamua kufanya.

8. Watu wengi wanashindwa kufanikiwa kimaisha kwa kuwa wanaishi katika yaliyopita. Kundi la kwanza linahusisha wale wanaoishi kwa kujivunia mafanikio yaliyopita bila kutambua kuwa hayo yamebaki kuwa historia. Mfano, katika jamii kuna watu wengi ambao wanajivunia mafanikio yao ya darasani enzi za uanafunzi wao. Pia, wapo ambao wanajivunia mafanikio ya kifedha au kikazi waliyowahi kupata katika kipindi cha Maisha yao. Kundi la pili linahusisha wale ambao wanaishi katika huzuni kubwa kutokana na matendo waliyofanya katika Maisha yao au kutokana na familia au malezi waliyopewa enzi za ukuaji wao. Hapa ndipo kuna idadi ya watu wengi ambao wanaishia kusema nilichezea ujana wangu kwa kuwa hakuna la maana nililofanya pasipo kuchukua hatua zinazolenga kurekebisha makosa hayo katika Maisha ya sasa.  Ili ufanikiwe kuishi kwa muda wa masaa 24 katika siku, Mwandishi anatushirikisha kuwa hauna budi kuishi kulingana na wakati uliopo kwa kutekeleza majukumu ya kila siku pasipo kudharau ukubwa au udogo wa kazi.

9. Binadamu wa kawaida ambaye anahitaji kuishi maisha kwa ukamilifu anatakiwa ndani ya fikra zake awe na mpangilio wa kila siku ambayo amebahatika kuishi. Katika majukumu ya kawaida anatakiwa aianze siku kuanzia saa 12 kamili asubuhi na kumaliza siku yake saa 4 usiku. Katika siku anakuwa na jumla ya masaa 16 yaliyokamilika ukiondoa lisaa limoja kwa ajili ya maandalizi baada ya kuamka. Katika masaa hayo anatakiwa kutekeleza majukumu ambayo yanamwezesha kujiendeleza kiroho, kimwili, kiakili na kusaidia jamii inayomzunguka. Muda huo wa masaa 16 siyo kwa ajili ya kukimbizana na presha za Maisha bali ni kufanya kile ambacho roho yako inapenda na inajivunia kujihusisha nacho. Hautakiwi kuwa mtumwa wa pesa bali kupitia upendo kwenye majukumu yako ndipo utalipwa kulingana na thamani unayoitoa kwa wengine.

10. Watu wengi wanapoteza muda mwingi kufuatilia taarifa zisizo na tija katika Maisha yao. Tunaishi katika ulimwengu uliojaa taarifa za uongo au zinazoandikwa kwa makusudi maalumu na taarifa hizi zinadumu kwa muda mfupi sana. Mfano, taarifa nyingi ambazo tunafuatilia kwenye magazeti au vyombo vingine vya habari muda wa uhalisia wa taarifa hizo ni mdogo mno na nyingi zinatolewa kwa lengo la kukuza mauzo au kuongeza idadi ya wafuatiliaji wa chombo husika cha habari. Mwandishi anatushirikisha kuwa baada ya kufahamu ukweli huu kuhusu taarifa zinazoandikwa kila siku hakuna haja ya kuendelea kupoteza muda kwa kusoma magazeti au kuangalia TV.

11. Jenga mazingira yatakayopelekea uwe na majukumu ya thamani baada ya masaa ya kawaida ya mwajiri wako au biashara zako. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi katika jamii wameifundisha akili kuhisi uchovu kila baada ya kumaliza masaa ya kazi katika ratiba iliyozoeleka. Mfano, katika masaa 16 ambayo tumeona kuwa mtu wa kawaida anatakiwa awe nayo katika kila siku; asilimia kubwa ya watu huwa wanahesabu masaa yenye tija ni yale ambayo wanatakiwa kwa lazima kuwepo kwenye sehemu zao za kazi. Matokeo yake ni kwamba, baada ya kutoka kazini mtu anazunguka tu mtaani au anakuwepo nyumbani bila kujishughulisha na kazi yoyote yenye tija katika Maisha yake. Ili upate tofauti katika Maisha ni lazima uwe tayari kufanya kazi za ziada baada ya muda wako wa kazi za lazima.

12. Tenga siku moja katika juma kwa ajili ya kuhuisha/kupumzisha mwili. Mwandishi anatushirikisha kuwa unaweza kufanya kazi kwa muda wa siku zote saba katika juma hila kwa asili mwili wa binadamu unahitaji kupata mapumziko. Watu wengi ambao hawana utaratibu wa kupumzika siku moja katika juma mara nyingi huwa wanakabiliwa na kushuka kwa morali ya kazi hali inayosababishwa na mwili kukosa muda wa kupumzika au kubadilisha mazingira. Hali hii huwa inashusha ufanisi wa utendaji wa kazi bila ya ufahamu wa mhusika. Kumbe, unatakiwa kuandaa programu ya kazi kwa muda wa siku sita na kuiacha siku moja bila majukumu yoyote. Siku hii ni kwa ajili ya kuurejesha mwili katika morali ya kazi kwa juma linalofuata.

13. Katika jamii tunazoishi mara nyingi Ofisi nyingi za Serikali zinafunguliwa saa 1:30 asubuhi na kufungwa saa 9:30 alasiri. Hapa kama wewe ni mfanyakazi wa Serikali kati ya masaa 16 ambayo tumeona hapo juu, ukitoa muda wa kuwa kazini (masaa 8) unakuwa umebakiwa na muda wa masaa 8 mengine ambapo kati ya hayo ukitoa muda wa kwenda na kutoka kazi angalau una uhakika wa masaa yasiyopungua 5 kila siku. Ndani ya juma moja (siku 6) utakuwa na masaa yasiyopungua 30 ambayo hakika ukiyatumia vyema utapata mabadiliko makubwa katika Maisha uliyozoa. Vivyo hivyo, kwa upande wa mfanyabiashara, unatakiwa kujifanyia tathimini inayolenga kujua muda unaopoteza nje ya muda wako wa lazima katika biashara yako.

14. Kuishi kwa masaa 24 katika siku ni lazima mhusika awe tayari kubadilisha tabia zilizoeleka katika mfumo wake wa Maisha. Mwandishi anatushirikisha kuwa utakuwa unajidanganya endapo utasema nitaanza kutumia muda wangu vizuri kila siku pasipo kubadirisha tabia. Zipo tabia ambazo kwa sasa zinapelekea upoteze muda na hatua ya kwanza katika kuishi kulingana na masaa 24 katika siku ni kurekebisha tabia ulizozoea katika mfumo wako wa Maisha. Hapa ndipo kuna changamoto maana siyo kazi mtu kusema sitaki kupoteza muda bali kazi kubwa ni kubadilisha tabia. Hali hii inatokana na ukweli kwamba, mabadiliko yoyote ya tabia ni lazima yaambatane na vikwazo pamoja na maumivu kwa mhusika. Mabadiliko hayo yanaambatana na mabadiliko ya mfumo mzima wa Maisha. Hapa ni lazima uwe tayari kutoa sadaka zinazoambatana na kupoteza marafiki au kushindwa kufuatilia vipindi ambavyo awali ilikuwa kila muda wa jioni upo tayari kwenye TV yako.

15. Yote yanawezekana pale tu mhusika akifanikiwa kudhibiti fikra zake. Hakuna mtu anaweza kudhibiti fikra za mwenzake bali ni mhusika pekee ndo mwenye mamlaka ya kudhibiti mfumo wake wa fikra (kiwanda cha kuzalisha na kuchakata mawazo). Hakuna jambo jema au baya linalotokea katika Maisha ya mhusika pasipo kupitia kwenye mfumo wa ubongo ambako ndiko fikra zinatengenezwa na kufanyiwa kazi. Hivyo, kama unahitaji kuwa mtawala mkuu wa Maisha yako ni lazima udhibiti yanayoingia katika mfumo wako wa fikra. Uwezo huu wa kudhibiti fikra ndiyo utakuwezesha kuwa na utulivu kwenye yale unayofanya kulingana na programu ya siku husika. Hivyo, kama unahitaji kuishi Maisha yenye thamani ni lazima uwe mtawala wa fikra zako. Ni lazima uwezo wa kutuliza akili kwenye jambo moja baada ya jingine kwenye ratiba yako ya siku. Kupitia udhibiti wa fikra utaweza kuepuka maovu mengi ya dunia kwa kuwa chanzo cha maovu hayo pamoja na hisia mbaya kama vile hofu, huzuni na chuki ni kupitia mfumo wa fikra.

16. Furaha katika Maisha inaanzia kwa mhusika kujitambua yeye mwenyewe pamoja na uhusiano wake na mazingira yanayomzunguka. Ili mhusika ajitambue mwenyewe ni lazima awe na muda wa kufikiri. Unatakiwa kufikiria kuhusu kila sekta ya Maisha yako kwa kuwa kupitia zoezi hilo utapata kujitambua wewe ni nani na upo duniani humu kwa ajili ya kufanikisha nini. Unapojitambua kuwa wewe ni nani na umeumbwa kwa ajili ya kufanikisha nini moja kwa moja unakuwa umevunja mtego wa mazoea ya watu kuwa furaha inapatikana kutokana na umiliki wa vitu vya Duniani humu. Kumbe, furaha ya kweli chimbuko lake halisi ni kuishi kwa ajili ya ukamilisho wa kusudi maalumu na kuhakikisha Maisha yako yanaendeshwa na kanuni ambazo zinakusogea kwenye kulifikia kusudi hilo. Hivyo, kwa ujumla tunatakiwa kufahamu kuwa furaha ya kweli haipatikani nje ya majukumu yetu ya kila siku bali kadri tunavyotekeleza majukumu hayo ndivyo tunapata furaha katika Maisha. Kwa maneno rahisi ni kwamba furaha ya kweli inapatikana kutokana na ushindi mdogo mdogo wa kila siku kwenye malengo tuliyojiwekea katika kila sekta ya Maisha yetu.

17. Tenga muda wa kusoma kitabu au kusikiliza au kujihusisha na mchezo unaoupenda. Lengo la kuishi saa 24 katika siku ni kuepusha masaa yasiyo na kazi kwa kuwa tufahamu kuwa kukaa bila kazi ni dhambi. Yapo maarifa mengi ambayo unatakiwa kujifunza ili kupitia maarifa hayo upate kufahamu mbinu muhimu za kuendelea kuwa wa thamani katika uhai wako. Pia, unaweza kupata furaha kwa kusikiliza nyimbo au mafundisho mbalimbali sawa na ilivyo kujihusisha kwenye sanaa yoyote unayoipenda kutoka rohoni. Kubwa ni kwamba, chochote unachofanya katika muda husika unatakiwa kuwa na furaha nacho kutoka ndani ya roho yako.

18. Kuishi kwa masaa 24 katika siku ni lazima utambue kuwa tunaishi katika ulimwengu wa kisababishi (cause) na athari (effect). Hivyo, chochote ambacho unahitaji kitokee katika Maisha yako huna budi kutenga muda maalumu kwa ya kujiendeleza kila siku kuelekea kwenye ukamilisho wa hitaji hilo. Lengo la kujiendeleza kila siku ni kwa ajili ya kujiendeleza kimwili, kiakili na kiroho kama sehemu ya utayari kuelekea kwenye hitaji lako.

19. Soma kitabu au Makala ambayo inakufanya utumie akili kujifunza kitu kuhusu Maisha yako. Mwandishi anatushauri kuwa katika kazi za uandishi ambazo zina mafundisho mengi ni kazi za mashairi. Mashairi yana kila aina mafundisho ambayo yatamwezesha mtu yeyote kuwa na hekima na busara kama kipindi cha Maisha yake. Kumbuka katika usomaji wako wa vitabu unatakiwa kuchagua sekta moja ambayo unahitaji kuongeza uelewa wako na kila mara tafuta maarifa yanayolenga kukufanya uwe bora zaidi katika sekta hiyo.

20. Pamoja na kuwa na programu ya siku nzima, mwandishi anatushauri kuwa hatupaswi kuwa watumwa wa programu hiyo. Kama ambavyo tumeona kuwa unatakiwa kufurahia majukumu uliyonayo pia, unatakiwa uwe tayari kuruhusu mabadiliko ya lazima yanayotokea nje ya uwezo wako. Zaidi ya yote ili utimize majukumu yako kulingana na programu ya siku ni lazima husiruhusu mtu achezee ratiba yako. Pia, unatakiwa kuhakikisha unaepuka kushiriki semina au mkutano ambao una maudhui ambayo ni kinyume kanuni unazoziishi.   

Kupitia kitabu hiki mwandishi ameweza kutushirikisha namna ya kuishi kulingana na masaa 24 katika siku. Maisha yanakuwa na thamani pale ambapo kila siku unaitumia kwa faida. Jiunge na mtandao wa Fikra za Kitajiri kwa  KUBONYEZA HAPA.


Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.


Born to Win ~ Dream Big 


Mwalimu Augustine Mathias

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com

Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com


onclick='window.open(