Habari rafiki yangu mpendwa
ambaye umeendelea kujifunza kupitia Makala za uchambuzi wa vitabu ambazo
nimekuwa nashirikisha jamii kupitia mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI. Karibu katika
uchambuzi wa kitabu cha leo ambacho ni cha 5 kati ya vitabu 30 ambavyo nimejiwekea
lengo kuvisoma katika kipindi cha mwaka huu 2020.
Kama bado hujajiunga
na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la
tafakari kila siku pamoja na kujumuika na watu wenye mtazamo sawa, tafadhali JIUNGE
SASA nafasi
ni chache.
Kitabu ninachokushirikisha
kupitia makala hii ni “The Sience of Getting Rich” kutoka
kwa mwandishi Wallace D. Wattles. Kupitia kitabu mwandishi anatushirikisha
mbinu na kanuni ambazo zinaweza kutumiwa na mtu yeyote kwa ajili ya kutengeneza
utajiri anaotamani. Mwandishi anatushirikisha kuwa kwa kutumia mbinu zilizopo
katika kitabu hiki milango ya kipato chako itafunguka na pato lako litaanza
kuongezeka mara mbili, mara tatu na zaidi na zaidi. Pia, kwa kutumia kanuni
hizi utashangaa unaanza kupata marafiki wapya ambao watawezesha kupata taarifa
na fursa ambazo zitafanikisha ukuaji wa biashara zako.
Msingi wa kanuni
zinazoshirikishwa kitabu hiki ni Imani. Kanuni unazoshirikishwa katika kitabu
hiki badala ya kuhoji uhalisia wake unatakiwa kutanguliza Imani kuwa sayansi ya
kanuni hizi imefikiwa baada ya kutumiwa na watu wengi kufanisha utajiri. Hivyo,
unachotakiwa kufanya ni kutumia sayansi hii katika Maisha yako bila kuhofu wala
kuhairisha.
Karibu ushirikiane nami kujifunza
machache kati ya mengi ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:
1.
Utajiri ni yako ya kuzaliwa. Tunaweza kuongea chochote
kuhusiana na Maisha ya umasikini lakini ukweli unabakia kuwa ili mtu aishi
Maisha yenye mafanikio ni lazima awe tajiri. Ukweli ni kwamba mtu anaweza kuwa
na kipaji lakini ili aweze kuendeleza kipaji hicho ni lazima awe na vitu vya
msingi ambavyo vitamwezesha kukuza kipaji chake. Maendeleo ya mtu kiroho,
kimwili na kiakili anahitaji amiliki vitu vya msingi ambavyo upatikanaji wake
unahitaji mhusika awe na pesa. Kwa tafsiri hiyo uhai wa mtu unahusisha mhusika
kupata haki ya kutumia vitu vya msingi ambavyo vitamuwezesha kujiendeleza
kimwili, kiroho na kiakili. Kwa maneno mengine ni kila mtu ana haki ya kuwa
tajiri.
2.
Kuridhika na hali ya umasikini ni dhambi. Mwandishi anatushirikisha kuwa furaha ya kuishi ni
kuendelea kupata zaidi kutoka kwenye mazingira yanayokuzunguka. Na kadri
unavyopata zaidi ndivyo unatengeneza utajiri, mamlaka na nguvu ambazo
zinakuwesha uishi Maisha ya ukamilifu. Maisha yenye kupata kila hitaji muhimu
katika uhai wako. Hakuna maana ya kuridhika na uchache (umasikini) wakati
umeumbwa kwa ajili ya kupata zaidi (utajiri). Kwa asili kila mwanadamu
anatamani kufikia mafanikio makubwa sana katika Maisha. Dhamira au matamanio hayo
amerithishwa toka enzi za kuumbwa kwake. Hata hivyo ili mwanadamu ili afikie
mafanikio ya matamanio yake ni lazima atumie vitu vinavyomzunguka na kiwango
cha upatikaji wa vitu hivyo kinategemeana na uwezo wa kifedha ambao mhusika
anao.
3.
Mwanadamu anaishi kwa ajili ya kujiendeleza katika vitu muhimu vitatu ambavyo
ni: roho, mwili na akili. Sehemu hizi tatu katika Maisha yeu ni muhimu na
hakuna sehemu ambayo ni bora kuliko nyingine hivyo hakuna sehemu ambayo itaishi
kwa ukamilifu pale ambapo sehemu nyingine zinaachwa. Siyo sahihi kuendeleza
roho na kusahau mwili na akili au kuendeleza akili huku ukisahau mwili na roho.
Hapa ndipo tunaona umuhimu wa utajiri kutokana na ukweli kwamba mtu hawezi
kujiendeleza kimwili bila mahiaji muhimu ya chakula; mavazi; kinga dhidi ya
mvua, jua kali au Wanyama wakali; na vitu muhimu vinavyomuwezesha kufanya kazi.
Vivyo hivyo, mtu hawezi kujiendeleza kiakili kama hana uwezo wa kupata vitabu
na muda wa kuvisoma; bila kuwa na uwezo wa kutembea nje ya mazingira aliyozoea
na kujifunza kwa kuona; au uwezo wa kujifunza kutoka kwa marafiki wenye maarifa
mbalimbali. Pia, ili kujiendeleza kiroho mhusika anatakiwa kuishi Maisha ya
upendo na ni ukweli mtupu kuwa hakuna upendo katika Maisha ya dhiki kwa kuwa
upendo msingi wake mkuu ni Maisha ya kutoa kwa wengine. Kwenye dhiki inayotokana
na upungufu wa vitu kila mtu anatanguliza nafsi yake.
4.
Kuna sayansi ya kuwa
tajiri ambayo inafanya kazi kwa mtu yeyote ambaye anaitumia na kuiheshimu.
Umiliki wa pesa na rasilimali za kila aina vyote kwa pamoja vinakuja kutokana na
kufanya vitu kwa kufuata misingi na kanuni. Wale wanaofuata misingi na kanuni
hizo iwe kwa kufahamu au kwa bahati wanafanikiwa kuwa matajiri wakati wale
wasiyofuata misingi na kanuni hizo bila kujali jitihada kiasi gani walizonazo
katika kazi wanaendelea kuwa masikini. Hivyo kuwa tajiri siyo swali la
mazingira, sura, umri au rangi maana kama ingekuwa hivyo watu wote katika eneo
moja au wenye rangi inayofanana wote wangekuwa na utajiri. Ili uwe ajiri ni
lazima ufanye kazi njia flani (doing things in a certain way) na ili ufanye
vitu katika hali flani ni lazima ufikirie katika njia flani (thinking in a
certain way). Hii ni kutokana na ukweli kwamba jinsi tulivyo ni matokeo ya yale
tunayoyafikiria kwa muda mrefu.
5.
Hakuna mtu ambaye anakosa fursa za kumwezesha kuwa tajiri.
Unaweza kushindwa kufanikiwa katika sekta moja lakini kuna sekta kadhaa ambazo
zipo wazi kwa ajili yako kufanikiwa kimaisha. Hivyo, hakuna sababu ya
kulalamikia hali uliyonayo na badala yake unatakiwa kuanza kufanya vitu kwa
kufuata misingi na kanuni za kuwa tajiri. Hakuna mtu ambaye anakuwa masikini
kutokana na upungufu wa fursa bali kinachomfanya awe masikini ni kushindwa
kuishi misingi na kanuni za kutengeza utajiri. Vitu vinavyoonekana (visible) na
visivyooneka (invisible) havijawahi kupungua kwa mtu yeyote anayetaka
kufanikiwa kimaisha. Tafsiri yake ni kwama hakuna mtu ambaye ni masikini kwa
kuwa asili (nature) imeishiwa vitu muhimu vya kumwezesha kuwa tajiri. Umasikini
wa mtu unatokana na jinsi anavyoishi Maisha yake. Asili ina kila kitu muhimu
cha kumwezesha mtu yeyote kuwa tajiri.
6.
Kanuni ya kwanza ya utajiri: Fikra ni nguvu pekee ambayo inawezesha
kuumba vitu vinayoonekana kutoka kwenye visivyoonekana. Kila kitu unachookiona
katika ulimwengu kimeanzia kwenye fikra. Kuanzia sekta ya miundombinu,
usafirishaji, kilimo, ujenzi na mengine yote yaliyo umbwa kwenye uso wa dunia
hii yameanzia kwenye fikra. Hivyo, tunaishi katika ulimwengu wa fikra na kama
unahitaji kufanikisha chochote katika Maisha yako ni lazima kitu hicho kianzie
kwenye fikra. Hata hivyo, ili kitu hicho kiumbike ni lazima mhusika aendelee
kuishi katika fikra hizo kwa kipindi cha muda wote hadi pale ambapo atakuwa
amekamilisha uumbaji wa kitu husika. Kutokana na kanuni hii tunatakiwa kutambua
kuwa chochote kile ambacho tunahitaji kifanyike katika mikono yetu ni lazima
mfumo wa fikra ufanye kazi yake kwanza.
7.
Pale mtu anapokuwa na wazo juu ya umbo analotaka kuumba cha kwanza kabisa
anatakiwa kufikiria ni malighafi zipi kutoka kwenye asili ambazo atatumi
kukamilisha uumbaji wa umbo lake. Hata hivyo tunatakiwa kukumbuka kuwa chanzo
cha uumbaji ni Muumba mwenyewe ambaye katika Maandiko Matakatifu anasema “natumfanye
mtu kwa mfano wetu, sura yetu..”. Kupitia uumbaji huo mwanadamu alipewa mamlaka
ya kuumba vitu vinavyoonekana kutoka katika asili inayomzunguka na
anayekamilisha uumbaji huo wa vitu si yeye bali ni nguvu ya Mungu ndani mwake.
Hata hivyo, wanadamu hawatumii mamlaka ya uumbaji waliyopewa kwa kuwa ni
wachache wenye kuunganisha nguvu ya fikra na inayofanya kazi ndani mwao kwa
ajili ya uumbaji wa vitu vipya. Watu wengi wamejikita kwenye kuboresha vitu
ambavyo vimeshaumbwa tangu zamani.
8. Kutoka katika kanuni hii tunakumbushwa kuwa:
Moja,
kuna nguvu ya fikra
yenye uwezo wa hali ya juu na kutoka katika nguvu hiyo inaendelea kuruhusu
uumbaji ambao unawezesha kuujaza ulimwengu huu. Nguvu hiyo inawezesha kuumbwa kwa maumbo
mbalimbali yenye uhalisia kutoka kwenye picha inayoumbika katika fikra.
Hivyo, kila mtu anaweza kuumba vitu kutoka kwenye fikra pale ambapo
anaruhusu muunganiko wa kweli wa fikra zake na fikra iliyo kuu ambayo ni Mungu
mwenyewe.
Mbili,
hatua ya kwanza ya
kuwa tajiri ni kuwa
na uwezo wa kudhibiti fikra zako, uwezo ambao utakuwezesha kufikiria UKWELI ambao ni
upande chanya kwenye kila hali bila kujali hali inayokuzunguka. Mfano, kuhusu
umasikini unatakiwa kuifanya akili yako muda wote ione kuwa haiwezekani uwe
masikini kwa kuwa asili ina kila kitu cha kukuwezesha uwe tajiri. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kazi hii ya kudhibiti fikra ni ngumu kuliko kazi yoyote
ile hapa Duniani. Mfano, hebu tafakari kufikiria kuwa umeumbwa kwa ajili ya
kuwa na afya bora katika kipindi ambacho unazungukwa na magonjwa. Hata hivyo,
mtu anayefanikiwa kudhibiti fikra zake anakuwa mtawala wa akili yake na ana
nafasi kubwa ya kufanikisha mambo mengi katika Maisha yake.
Tatu,
nguvu ya kudhibiti
fikra inapatikana kwa kuamini kuwa “kuna
nguvu iliyo moja na kipekee ya fikra ambayo ndiyo chanzo cha uumbaji wa kila
kitu duniani hapa”.
Pale unapoamini katika nguvu hiyo tunapata mamlaka ambayo inatuwezesha kuumba
kila kitu ambacho kimejengeka kwenye mfumo wa fikra zetu. Pale tunapogundua
ukweli huu tunaondoa shaka na hofu zote kwa maana tunatambua kuwa “tunaweza
kuunda kitu chochote kile tunachotaka kuunda, tunaweza kupata kile tunachotaka
kuwa nacho, na tunaweza kufikia mafanikio tunayoyataka”.
9. Kanuni
ya pili: Kila kiumbe kilicho
hai ni lazima mara zote kitafute kuongezeka kimaisha kwa kuwa Maisha yenyewe ni
kwa ajili ya kuongezeka au kukua zaidi. Mbegu inayodondoshwa
ardhini ikiwa hai inaota na kuongezeka na hatimaye inazaa matunda zaidi ambayo
yanawezesha upatikanaji wa mbegu zaidi na zaidi. Hali kadhalika binadamu katika
kipindi cha Maisha yake anatakiwa ajikite kwenye kuongezeka kithamani. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba nguvu ya fikra iliyopo ndani mwake inahitaji
kuongezeka zaidi. Kila maarifa unayojifunza yanakufanya utamani kujifunza
maarifa mapya zaidi, kila kipaji unachoendeleza kinakufanya upanuke zaidi
katika sekta nyingine za Maisha. Kwa ujumla tumeumbwa kwa ajili ya
kufahamu/kujua zaidi, kufanya zaidi na kuongezeka zaidi. Hilo ndilo hitaji kuu
katika Maisha.
10. Kutamani kuwa tajiri ni moja ya hitaji muhimu
katika Maisha kwa kuwa tumeona hitaji muhimu katika Maisha ni kutaka kuongezeka
zaidi. Hivyo ili tupate zaidi katika Maisha hatuna budi ya kuwa tajiri kwa kuwa
huo ndiyo ukamilisho wa Maisha sawa na ilivyo kwa mmea wa aina yoyote ni lazima
ujikite kutafuta chakula kwa ajili ya kuongezeka zaidi. Hii ni sheria ya asili
ambayo inafaya kazi kwenye kila kiumbe chenye uhai. Dhamira ya Mungu nikuona
wewe unakuwa tajiri ili ajidhihirishe kwa wengine kupitia nafasi yako na
ataishi ndani mwako kwa kuwa unaendelea kutumia nguvu iliyo kubwa ambayo
umepewa toka enzi za kuumbwa kwako. Asili pia inatamani uwe tajiri na ndiyo
maana haijawahi kupungukiwa ipo tayari kukuzawadia kila hitaji ulilonalo.
Wajibu wako ni kubadilisha fikra na kuona kuwa kila unachohitaji kipo tayari
kupatikana kutoka kwenye ulimwengu huu kwa kuwa asili ni rafiki kwa mipango yako.
11. Tengeneza sababu zinazokusukuma kutaka utajiri.
Kubwa kabisa unatakiwa kutambua kuwa unahitaji kuwa Tajiri ili upate kula,
kunywa huku ukifurahia Maisha wakati wote. Unataka kuwa Tajiri ili uweze kuzungukwa
na vitu vizuri, kutembea na kutazama mazuri katika nchi za mbali, kulisha na
kukuza akili yako; na ili upende na kufanya mambo mema kwa wengine. Na
unahitaji kuwa tajiri ili upate kuwa sehemu ya wanaosaidia walimwengu kuujua
ukweli na kuuishi. Katika yote husitafute utajiri kwa ajili ya kuwaumiza au
kushindana na wenzako kwa kuwa asili imejaa kila aina kitu kuutosheleza
ulimwengu. Husitafute utajiri kwa kuwa kunyang’anya au kudhurumu mali za wengine.
Wewe ni Muumbaji kwa nini upoteze muda kwa kuwa na hila au wivu kwenye mali
wanazomiliki wenzako? Utajiri ambao unajivunia ni ule ambao unatengenezwa bila
kuumiza wala kuangamiza watu wengine. Hivyo, kupitia sheria hii tunakumbushwa
kuwa asili inajitosheleza kumpa kila mmoja utajiri anaotaka hivyo hakuna haja
ya kushindana.
12.
Kanuni ya tatu: Utajiri unakuja
kwako kupitia KUTOA thamani kubwa kuliko UNAYOPOKEA. Tafsiri ya kanuni hii ni
kwamba kabla ya kulenga kupokea kutoka kwa wengine unatakiwa kulenga kuwa mtu
wa thamani. Husimshawishi mtu kumuuzia mtu kitu ambacho unajua hakina thamani
yoyote katika Maisha yake. Hivyo, chochote unachouza hakikisha kinaongeza
thamani ya matumizi kwenye Maisha ya kila siku ya muhusika. Kwa kufanya hivyo
utakuwa umewezesha kurahisisha Maisha kwa wale ambao unafanya nao dili za
kibiashara. Kama kuna watu ambao umewaajiri hakikisha unaweka mpango ambao
utawezesha kupiga hatua badala ya kuendelea kukutegemea.
13. Tumeona kuwa utajiri unatengezwa kupitia nguvu ya
fikra ambayo inawezesha uumbaji wa vitu vipya kutoka kwenye chanzo halisi
kisicho na umbo (from a formless substance).
Baada ya kujenga picha ya kitu unachohitaji katika akili yako sasa unatakiwa
kuwa na imani isiyoyumbishwa juu ya uhakika wa kitu hicho kukamilika katika
Maisha yako. Imani hiyo ndiyo itawezesha nguvu iliyo kubwa (supreme power au
Mungu) ambayo inafanya kazi kupitia watu wanaokuzunguka kukupatia unachojitaji.
Hata hivyo, ili uumbaji ukamilike ni lazima uwe tayari kutafsiri picha ya kitu
kilichopo kwenye akili yako kwa vitendo ambapo ni lazima uusishe viungo vya
mwili wako kama vile mikono. Hivyo, ndivyo utajiri unavyokuja kwako kupitia
nguvu ya fikra ambayo ndiyo chanzo halisi cha uumbaji. Nguvu hiyo ya fikra
inafanya kazi kwa watu wote wanaoitumia na wote wanaunganishwa kwa pamoja bila
kujali umbali walipo, hivyo pale unapowaza kitu ambacho hauna kuna mwingine
mwenye nacho ambaye anahitaji mtu wa kubadilishana nae labda kwa pesa na kitu
alichonacho.
14. Hivyo, kwa ujumla tunatakiwa kutambua kuwa: utajiri
unakuja kwetu kupitia kujenga picha halisi ya kitu tunachohitaji na kuhakikisha
picha hiyo kila mara kwa Imani isiyo na shaka tunaifikisha kwa nguvu kuu ya
uumbaji ambayo ni Muumba mwenyewe ambaye tangu enzi za kuumbwa kwa ulimwengu ameendelea
kuumba vitu vipya kupitia kwa wanadamu.
Mungu hapendi watu wake waishi Maisha ya dhiki kutokana na umasikini bali yupo
tayari kuwezesha upatikani wa utajiri kwa kila mmoja ambaye anafanya kazi
katika hali ya utofauti (doing things in a certain way). Mungu anafurahi kuona
watu wake wakipendeza kupitia mavazi bora, kupata chakula au kinywaji kizuri,
wanaishi kwenye nzuri na za kifahari, wanatembelea magari mazuri na mengine
mengi ambayo kwa ujumla wake ndiyo hitaji na dhamira ya kila mwanadamu hapa
Duniani. Kwa kumiliki na kutumia vitu hivyo Mungu anafurahi na kupata fahari
kwa kujivunia uumbaji wake kwa kilichopo Duniani kimetokana na kazi ya mikono
yake.
15. Kanuni
ya nne: Utajiri unakuja kwa
kuwa mtu wa shukrani. Mpaka sasa unaamini kuwa: Moja, kuna nguvu moja iliyo kuu
kuliko zote (Muumba) ambayo ndiyo chanzo halisi cha uumbaji wa vitu vyote.
Pili, unaamini kuwa nguvu hiyo inao uwezo wa kukupatia kila kitu ambacho
unatamani katika Maisha yako. Tatu, kupitia shukrani ya dhati ndipo tunadumu
katika muunganiko mkubwa na nguvu iliyo kuu kuliko nguvu zote. Watu wengi
wanashindwa kudumu katika muunganiko na nguvu iliyo kuu kwa kuwa baada ya
kufanikiwa kupiga hatua moja wanakata mahusiano ya kifikra na nguvu iliyo kuu. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kama tunahitaji kuwa tajiri ni lazima tukae karibu na
chanzo halisi cha utajiri ambacho si kingine bali ni Mungu mwenyewe. Na njia
rahisi ya karibu na Mungu wetu ni kuwa na roho ya shukrani. Na kadri
unavyoshukuru ndivyo unajiongezea nafasi ya kupewa vingine zaidi ya
ulivyonavyo.
16. Roho ya shukrani inakuwezesha kuondokana na Imani
kuwa vitu vinapatikana kwa uchache na hivyo kukufungulia milango ya kupata
zaidi kutoka kwenye asili ambayo haijawahi kupungukiwa. Ni
kutokana na roho ya shukrani unaweza kuendelea kutegemea daima kupata yaliyo
bora badala ya kuwaza kuzawadiwa mabaya katika Maisha. Hivyo, kuna kila sababu
ya kujenga tabia ya kushukuru kwenye kila jema linalokuja katika Maisha yako.
Husitumie muda mwingi kulalamikia mamlaka iliyopo juu yako au kujishusha
kutokana na mapungufu uliyonayo na badala yake tumia muda huo kujivunia mazuri
uliyonayo kwani kupitia mazuri hayo utaweza kupunguza madhaifu yako.
17. Kanuni
ya tano: Utajiri unakuja kwako kwa kutumia uwezo wa
kufikiria katika hali flani (thinking in a certain way). Tumeona kuwa kuna
nguvu ya fikra iliyo kuu kuliko zote na kupitia nguvu hiyo watu wamendelea
kuumba vitu mbalimbali katika uso wa Dunia. Tumeona kuwa ili mhusika aweze
kuumba kitu ni lazima kwanza awe na wazo la kitu husika katika akili yake na
wazo hilo liambatane na umbo au ramani yenye vipimo kamili. Kwa ujumla ni
lazima kitu anachohitaji kiumbike kwanza katika akili yake na picha ya kitu
husika iendelee kuwepo akilini mwake muda wote. Hatua inayofuata ni kuwasilisha
picha/ramani ya kitu husika kwa nguvu ya fikra iliyo kuu (Muumbaji halisi).
Hapa ndipo watu wengi wanashindwa kufanikisha uumbaji wa vitu wanavyotaka
katika Maisha yao kwa kuwa wanashindwa kuwa na mpangilio wa umbo au ramani ya
vitu hivyo katika akili yao. Ili ufanikiwe kupata unachohitaji ni lazima
ufahamu nini hasa unataka na lini unahitaji kitu hicho kiwe kimekamilika. Hatua
ya mwisho ni kuhakikisha unakaa katika matamanio yanayokusukuma kuona picha
uliyonayo akilini anajidhihirisha katika maumbile yake halisi. Pia, hakikisha
picha hiyo inakuwa katika fikra zako kwenye kila unalofanya katika majukumu
yako ya kila siku.
18. Hata hivyo, haitoshi kuwa na picha halisi ya kitu
ambacho unahitaji katika Maisha yako maana ukiishia hatua hiyo inakuwa ni ndoto.
Nyuma ya maono ya fikra zako inatakiwa kuwa IMANI THABITI ambayo inakufanya
ujione tayari unamiliki kitu husika katika Maisha yako ya kila siku. Kama ni
nyumba jione tayari upo ndani ya nyumba husika kulingana na ramani uliyonayo
kichwani. Kama ni gari kwa Imani jione upo ndani ya gari husika ukiendesha na
kama ni shamba jione tayari shamba husika lipo ndani ya miliki yako. Maandiko
Matakatifu yanasema “chochote ambacho mtaomba kwa Imani na kuamini kuwa
mtapata, hakika mtapewa…”. Hivyo, kufanikiwa kupata hitaji lako kutoka
kwenye nguvu ya fikra iliyo kuu ni lazima ujifunze kudumu katika sara.
19. Kanuni
ya sita: Ili utajiri uje
kwako ni lazima uondoe vikwazo vyote vinavyotokana na historia ya Maisha yako.
Changamoto za kifedha, historia ya umasikini katika familia uliyokulia au madhahifu
yako yote yanatakiwa kuwekwa pembeni. Bila kufanya hivyo utakuwa na picha mbili
zinazokinzana (picha ya umasikini na picha vitu unavyotaka) katika mfumo wako
wa fikra. Pia, unatakiwa kuweka pembeni Imani zote ambazo zinaenda kinyume na
ukamilisho wa picha uliyonayo kichwani. Husisome vitabu au Makala ambazo
zinapingana na kanuni hizi za kutengeneza utajiri. Kaa mbali na makundi ya watu
ambao wana mtazamo hasi kuhusiana na utajiri. Mara zote jivunie mema ya nchi
ambayo yana uwezo wa kukupatia utajiri kuliko kujikita kwenye majanga ya nchi
ambayo huwa yanarudisha nyuma jitihada za watu. Akili na mtazamo wako wote uwe
kwenye utajiri badala ya umasikini. Kila unapoongea na watu onesha kuwa kila mtu
anaweza kuwa tajiri na rasilimali za kuwezesha kila mmoja kufikia utajiri
anaotamani zipo za kutosha hivyo hakuna haja ya kushindana.
20. Kanuni
ya saba: Utajiri unakuja
kwako kwa kufanya vitu katika hali flani (acting in certain way).
Kuwa na fikra na pamoja na picha ya vitu unavyotaka katika akili yako hakujitoshelezi
bila ya kuchukua hatua za kivitendo. Fikra zinatakiwa kuunganishwa na vitendo
katika majukumu yako ya kila siku. Kupitia fikra unaweza kuvuta chochote katika
umiliki wako lakini umiliki huo unakamilika kwa kupitia vitendo. Kumbuka
unatakiwa kutoa thamani kubwa kwa wengine ili nao wakupatie kile unachohitaji. Husidhurumu
au kuiba kwa ajili ya kufanikisha kupata kitu kilichopo katika akili yako na
badala yake unatakiwa kutumia mbinu halali za kuvuta vitu kwenye umiliki wako.
Kwa ujumla ni lazima utambue kuwa vitu unavyovitaka vipo kwenye mikono ya watu
wengine na vinapatikana kwa kubadilishana thamani kwa thamani.
21. Kupitia fikra kitu unachohitaji kinakuja kwako hila
unapokea au kumiliki kitu husika kupitia vitendo.
Hivyo, tunapokea kupitia vitendo na kama hauweki bidii katika kazi kwa maana
una tabia za uvivu unajikwamisha kumiliki vitu unavyotamani kupitia mfuko wako
wa fikra. Na unatakiwa kuchukua hatua mara moja bila kuhairisha kwa maana
wakati sahihi ni sasa na mazingira sahihi ni hayo uliyonayo. Hauwezi kufanya
katika yaliyopita au yajayo lakini unachoweza kufanya ni kuanzia pale ulipo. Kile
ulichonacho ni msingi namba moja katika kuelekea kwenye mahitaji yako mapya.
22. Kanuni
ya nane: Utajiri unakuja
kwako kwa kutekeleza majukumu yako kwa ufanisi.
Ulimwengu unaendelezwa na wale ambao wanatekeleza majukumu yao kwa ufasaha na
wale ambao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo ni mzigo kwa serikali, ndugu au wazazi.
Hivyo, kutokutekeleza majukumu yako kwa ufanisi ni kukwamisha kasi ya maendeleo
katika jamii unayoishi. Kila siku ipo kwa ajili yako kufanikiwa au kutofanikiwa
na majumuisho ya siku unazofanikiwa ndiyo yanaamua mafanikio yako. Kama kila
siku unashindwa kufanikiwa kulingana na mipango ya siku husika kamwe
husitegemee kuwa ipo siku utafanikiwa kuwa tajiri. Husidharau kufanya vitu
vidogo vidogo kwa kuwa vitu hivyo kwa pamoja vinatengeneza ushindi mkubwa. Kila
siku hakikisha unafanya yote ambayo yalitakiwa kufanyika katika siku husika kwa
ufanisi mkubwa kwa maana haujui kesho itakuwaje.
23. Kila kitendo unachofanya katika kutekeleza majukumu
yako ni lazima kiwe na uhusiano wa moja kwa moja na picha iliyopo katika fikra
zako. Hivyo kila hatua unayopiga ni ukamilisho wa
vitendo ambavyo kwa pamoja vinapelekea ushindi. Hivyo, muunganiko wa nguvu ya
akili (mental power) na nguvu ya mwili (physical power) ni muhimu kwa kuwa
vyote vinafanya kazi kwa kutegemeana kwa ajili ya kukamilisha hitajili kuu kwa
wakati husika.
24. Kanuni
ya tisa: Utajiri unakuja
kwako kwa kuchagua sekta au fani sahihi ya kufanyia kazi.
Kila mtu amepewa kalama na vipaji ambavyo anatakiwa kuvitumia kwa ajili ya
kutengeneza utajiri anaohitaji. Kwa ujumla ili uwe tajiri unatakiwa kuchagua
fani ambayo itakufanya utumie ipasavyo kalama na vipaji vyako. Pia, unatakiwa
kutambua kuwa vipaji vinaendelezwa hivyo kama kuna sekta ambayo unaona ni
muhimu kwako hila hauna uzoefu wa kutosha mamlaka ya kujiendeleza katika sekta
hiyo ipo ndani ya uwezo wako. Kwa ujumla katika kuchagua kazi au fani hakikisha
unachagua kazi/fani ambayo unaipenda kutoka rohoni. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba ni rahisi kufanikiwa kikazi kupitia fani unayoipenda kuliko kwenye kazi
ambayo umeingia ili mradi tu kwa kuwa umekosa mbadala. Kazi unayoipenda kutoka
rohoni inaambatana na msukumo wa matamanio ya kufanya kazi na msukumo huo ndiyo
kichocheo cha kujituma katika kazi.
25. Kama upo kwenye kazi au fani ambayo huipendi
unaweza kuitumia kazi hiyo kwa ajili ya kujiendeleza kufikia kwenye fani/kazi ya
matamanio yako. Husiridhike kuendelea kuishi katika
mazingira ya kazi ambayo haikufanyi ufurahie Maisha kutokana na majukumu yako
ya kila siku. Pale inapobidi kuwa tayari kubadilisha mazingira ya kazi kwa
ajili ya kuiridhisha nafsi yako na kuyafurahia Maisha kwa mapana yake. Pale unapokuwa
na shaka katika maamuzi yako hakikisha unaongeza muda kutafakari na kutoa
shukrani ili ufunuliwe zaidi kwenye maamuzi ambayo unakusudia kuchukua. Ondoa
wasiwasi na hofu kwenye maamuzi unayokusudia kufanya kwa kuwa ipo nguvu kuu
ambayo inakuongoza kufanya maamuzi sahihi.
26. Kanuni
ya kumi: Utajiri unakuja
kwako kwa kama una mtazamo wa kuongezeka au kukua zaidi (the impression of
increase) na mtazamo huo unatakiwa kuunesha kwa kila mtu ambaye unabahatika
kukutana nae. Kuongezeka au kukua zaidi ni hitaji la kila
mtu kwa kuwa ni kupitia kukua/kuongezeka mwanadamu anatumia vipaji vyake vyote
kwa faida ya viumbe wote. Hali hii kila mwanadamu amerithi toka enzi za kuumbwa
kwake na ni kutokana na hali hiyo kila mtu anahitaji kupata chakula zaidi, kuwa
na mavazi bora, kupata nyumba nzuri, kutembelea sehemu zenye mvuto na msisimko
au kumiliki kila rasilimali zenye viwango bora. Pale msukumo wa kukua au
kuongezeka zaidi unapoisha ni dalili za kuwa mhusika Maisha yake yanahitimishwa.
Hivyo, kutoridhika na hali ya uliyonayo siyo dhambi bali ni hatua muhimu katika
Maisha kwa ajili ya kuongezeka au kukua zaidi.
Haya ni machache kati ya mengi ambayo
mwandishi ametushirikisha katika kitabu hiki. Kuna sayansi ya kuwa tajiri na
kupitia kitabu hiki tumeshirikishwa mbinu muhimu za kuvuta utajiri katika Maisha
yetu. Sayansi hii inafanya kazi pale ambapo una dhamira ya kweli ya kufanikiwa
kimaisha hila kama dhamira yako inayumbayumba utaona kuwa mbinu
zilizoshirikishwa katika kitabu hiki ni za uongo. Jiunge na mtandao wa Fikra za
Kitajiri kwa KUBONYEZA HAPA.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate
elimu isiyokuwa na mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Mwalimu Augustine Mathias
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com