Rafiki msomaji wa mtandao
wa fikra za kitajiri naamini upo vizuri na unaendelea kupambambana kwa ajili ya
kuhakikisha kuwa kesho inakuwa bora. Karibu tena kwenye mtandao wetu wa fikra
za kitajiri ili uendelee kupata chakula cha ubongo. Kama kawaida ikiwa ni wiki
ya saba katika mwaka 2017, mtandao huu unaendelea kutimiza ahadi yake ya
kukuletea uchambuzi wa kitabu kimoja kila mwisho wa wiki (ijumaa) ili kupitia
uchambuzi wa vitabu hivi pamoja tuboreshe maisha maisha yetu.
Lengo kubwa la mtandao wa
fikra za kitajiri ni kuona wewe unaanza kuishi kusudi la maisha yako ambapo
kazi kubwa iliyopo mbele yako ni kubadilisha fikra zako. Hivyo, mtandao huu
umedhamiria kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha wewe msomaji wetu unapata
maarifa yatakayokusaidia ubadili fikra zako ili ziwe za kitajiri kwenye kila
sekta ya maisha yako. Kujiunga na mtandao wa fikra za kitajiri BONYEZA HAPA na ujaze
fomu ili uendelee kupata makala zinazochapishwa kwenye mtandao huu moja kwa
moja kwenye barua pepe yako.
Wiki hii ninakuletea
uchambuzi wa kitabu cha Illusions ambacho kimeandikwa na Richard
Bach. Richard Barch ni mwandishi na rubani binafsi. Kitabu hiki ni tamthilia
ambayo imeandikwa katika kipindi ambacho mwandishi alikuwa kwenye ombwe ambalo dhamira
yake ilikuwa kutoandika kitu kingine tena kwa vile alijiridhisha kuwa kupitia
vitabu vyake vya nyuma tayari alikuwa amekamilisha kazi yake hapa duniani.
Akiwa katika ombwe hilo ndipo akaanza kupata mawazo ya kwamba itakuwaje endapo
angetokea mtu wa kumfundisha namna ambavyo maneno yake yanafanya kazi na jinsi
gani anaweza kuyadhibiti maneno yake.
Akiwa anaendelea na kazi
yake ya kurusha ndege kwa malipo ya $3 kwa kila abilia wake kwa muda wa dakika
10 ndipo alikutana na rubani Donald William Shimoda ambaye naye alikuwa
anafanya kazi kama hiyo. Donald William Shimoda alikuwa ni mtu ambaye alikuwa
mzuri sana kwenye ufahamu wa dunia hii na nafsi yake pia (supernatural spirit).
Kutokana na hali hii, wawili
hawa wakajikuta katika hali ya mwalimu na mwanafunzi na hivyo mwandishi wa
kitabu hiki akawa anamuona Donald William Shimoda kana kwamba huyu ndiye “masiha
mkaidi” kwa vile rafiki yake kamwe hakukubali kuitwa masiha kwani aliamini kila
mtu naweza kufanya miujiza ya kila aina endapo ataamini kuwa ana uwezo huo.
Karibu tujifunze wote kwa
hiki kidogo nitakachokushirikisha kati ya mengi niliyojifunza kwenye kijitabu
hiki.
1.
Mwandishi anatushirikisha kuwa Masiha aliwafundisha
wafuasi wake kuwa ndani ya kila mmoja wetu ipo nguvu ya ridhaa yetu kwenye
masuala ya afya na magonjwa, utajiri na umasikini, uhuru na utumwa, na furaha
na huzuni. Hata hivyo tunafundishwa kuwa tunatofautiana katika vitu hivyo kwa
kutegemea namna gani tunavyotumia nguvu hii kwani sis indo tunadhibiti hali
hizo na si mwingine.
2. Kutokana
na mafundisho ya masiha wote tumeumbwa katika hali sawa lakini kadri mtu
anavyojifahamu yeye pamoja na ugumu wa mazingira yanayomzunguka ndivyo anajenga
ukuta mgumu zidi ya mazingira yasiyo rafiki kwake. Kwa kufanya hivi mtu huyu
atakuwa amejitofautisha na umati wa watu wanaomzunguka na kuwa mtu wa hali
tofauti. Katika hatua hii watu ambao wamekubali kuondoshwa au kutawaliwa na
ugumu wa mazingiara wanaanza kumshangaa mtu huyu kwa kusema yule mbona
alikuwaga mwenzetu na kauli nyingine nyingi. Hivyo wengi wataanza kuita ewe “mkombozi/masiha”
njoo utuokoe na sisi.
3. Katika
hali ya watu kushangaa wale waliofanikiwa kupita kwenye ugumu wa mazingira
ndivyo na hawa waliofanikiwa nao wanawashaa watu ambao wameshindwa kukabiliana na
ugumu huo. Pale wanapoitwa “masiha/mkombozi” ndipo na wao wanawajibu mbona mimi
sio masiha wala mkombozi zaidi yenu. Mimi ni sawa na nyie na wala sijatokea
sehemu nyingine zaidi hapo mlipo ninyi.
4. Mwandishi
anatushirikisha kuwa wengi wetu tunafanya kazi tunazofanya kwa sababu tunabanwa
na mahitaji ya chakula, maradhi na mavazi. Hapa mwandishi anatushirikisha jinsi
yeye mwenyewe pamoja na hatari za kurusha ndege angani alikuwa hapendi kazi
hiyo japo alilazimika kufanya hivyo kwa ajili ya uhakika wa chakula chake.
5. Watu
wengi wanasubiria muujiza uwatokee kumbe muujiza tayari wanao katika maisha yao
ya kila siku. Siku wanapogundua namna bora ya kutumia muujiza huo ndivyo
wanapata mafanikio zaidi ambayo hawakuwahi kutegemea kuwa wangefikia hatua
hiyo.
6. Unaweza
kuachana na kitu au tabia yoyote ile kwa kuacha kuwaza juu ya kitu hicho au
tabia husika.
7. Mwendo
mzima wa wakati wetu hapa duniani ni kutoka kwenye ulimwengu wa kimwili kwenda
kwenye ulimwengu wa kiroho. Hili ni jukumu la kila mmoja wetu na hivyo
inategemea juhudi za kila mmoja wetu katika kuelekea kwenye ulimwengu wa
kiroho.
8. Tumeumbwa
kwa upendo wa Mwenyezi Mungu kwa namna ambayo kama unataka uhuru na furaha
hivyo vyote havipo sehemu nyingine tofauti na ndani mwako. Hivyo badala ya
kutafuta miujiza ya vitu hivyo nje yetu ni sawa na kupoteza muda na badala yake
tunafundishwa kutafuta ndani yetu sisi wenyewe.
9. Kujifunza
ni maarifa mapya nje ya yake unayoyajua. Na kujifunza ni lazima kuambatane na
vitendo kwani ni kupitia tunajua kuwa unafahamu vitu flani. Na ili ujuzi wako
uwafadishe wengine ni bora kuwafundisha ili kuwakumbusha kuwa wanajua na
wanaweza kama wewe.
10. Wajibu wako mkuu katika maisha ni kuwa
mkweli juu yako mwenyewe kwani kuwa mkweli kwa mtu mwingine au kitu kingine sit
u haiwezekani bali inakupa alama “masiha/mwokozi” bandia.
11. Njia rahisi ya kugundua kama wewe ni
mkweli wa nafsi yako ni kujiuliza maswali haya rahisi lakini pia magumu kufikia
hatma yake: Uzaliwa wapi? Nyumba yako ipo wapi? Unafanya nini? na unaenda wapi?
Fikiria kuhusu majibu na maana ya maswali haya na kuwangalia nafasi yako kwa
sasa katika kuishi ukweli wa nafsi yako na anza kubadilika mara moja.
12. Ishi maisha ya kutokuwa na aibu kwa
yale unayofanya au kusema hata kama yatachapishwa duniani kote pasipokujali
kuwa yana ukweli hama la. Chamsingi yote hayo yatokane na msukumo wa ndani
mwako kwani msukumo huo wa ndani ndo wewe mwenyewe halisi, hiyo ndo nafsi yako
na hiyo ndo nguvu ya ajabu iliyofichika kwenye siri ya kuumbwa kwako. Hivyo kabla
hujakimbia kwenye matarajio yako ya baadae au kwenye historia yako hakikisha
kuna kitu umejifunza ili kiwe mwongozo wako kwenye maisha mapya.
13. Ili kubadilisha historia au tabia zako
ni lazima uanzishe utaratibu wa kukuwezesha usahau na uanze kuishi maisha
mapya. Mfano, kama ulikuwa unasumbuliwa na tabia ya ulevi na sasa umeamua
kuachana nayo ni lazima kwanza uachane na vichocheo vyote vilivyokuwa
vinakusukuma kwenye ulevi; inaweza kuwa kubadilisha kampani ya marafiki zako au
kubadilisha kinywaji ambacho ulikuwa unapendelea. Unatakiwa kufanya zoezi hili
kwa muda kuanzia wiki moja na kuendelea pasipokurudia tabia yako ya awali na
hatimaye utajikuta kwenye ulimwengu wa maisha mapya.
14. Kila tatizo/changamoto tunazokutana nazo
katika maisha yetu kuna zawadi iliyofichika nyuma yake. Hivyo, ni lazima
tujifunze kwa nini tumekutana na changamoto za namna hiyo na kutokana na
changamoto hizo tupate somo la kujifunza katika maisha yetu ya kila siku.
15. Tunaona mambo yanayotokea nje ya ufahamu
wetu kama miujiza au mambo ya ajabu, njia sahihi ya kuepuka hali kama hii ni
kujifunza siri ya miujiza au maajabu hayo na hatimaye tunakuwa kwenye nafasi ya
kutengeneza miujiza mingi kwa kadri tunavyotaka. Ili uweze kutengeneza miujiza
zaidi ni lazima kwanza ujifunze mapana ya dunia hii ikiwa ni pamoja na kufahamu
jinsi inavyofanya kazi. Hapa ndipo utagundua kuwa hakuna muujiza wowote bali ufahamu
wako ndo unakufanya uone miujiza.
16. Watu wengi wanataka watendewe miujiza
lakini hawapo tayari kujifunza kutokana na miujiza hiyo. Hapa tunajifunza kuwa “masiha
mkaidi” aliachana na kazi ya kuwatendea watu mijiuza kwa vile alihuzunishwa na
tabia ya watu kutokujifunza kutokana na miujiza yake na badala walihitaji
miujiza zaidi kutoka kwake.
17. Watu wanaishi maisha yasiyo na furaha
kwa vile wamechagua kutokuwa na furaha maishani mwao. Hii ni kutokana na yale
wanayojishughulisha nayo kila siku kwani hayo ndo yanaamua hatima ya furaha kwa
kila mtu. Mfano, ni kawaida sana watu kutumia muda mwingi kuangalia filamu za
kuogopesha au huzuni na hivyo watu hao ni vigumu kuwa na maisha ya furaha kwani
filamu kama hizo zinawajaza huzuni na hofu rohoni mwao pasipo wao wenyewe
kujitambua.
18. Maisha yetu yamezungukwa na maigizo/uongo
wa kila aina na watu wengi wameishi kwenye maigizo/uongo huu kwa kipindi chote
cha maisha yao. Pamoja na kwamba maigizo/uongo umeumiza watu wengi lakini ni
wachache wanaotambua kuwa wapo kwenye maisha ya maigizo/uongo na hivyo kuachana
na maisha ya namna hiyo. Wengi wameendelea kung’ang’ania maisha ya giza hata
kama wameoneshwa mwanga kila iitwapo leo.
19. Maigizo/uongo wa namna yoyote ile
unahitaji nafasi na muda kwa ajili ya kuzoeleka katika maisha ya muhusika. Kadri
mtu anavyozidi kukubali maisha ya maagizo ndivyo anazidi kuona kuwa hayo ndiyo
maisha anayostahili na hivyo kila kukicha anatawaliwa na mawazo ya maisha ya
uongo/maigizo na hatimaye uongo huu unakuwa sehemu ya maisha yake. Kinyume
chake ni kwamba kama unataka kuachana na maisha ya maigizo ni lazima uanze
kuondoa uongo/maigizo kwenye mfumo wa mawazo yako na hatimaye uishi ukweli kila
siku.
20. Vitu vipo jinsi vilivyo kutokana na
matazamo wetu kwenye vitu hivi. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa tunaweza
kufanya vitu vya hali ya juu kutokana na mtazamo wetu juu ya hivi na hivyo yale
tunayofanya yataonekana miujiza kwa wengine ambao hawajui siri hii ambayo msingi
wake mkuu fikra zetu juu vitu hivi.
21. Dunia ni kitabu cha mazoezi na kurasa
zake ni matendo matendo yetu ya kila siku. Katika kila ukurasa wa kitabu hiki
kila mmoja ana uhuru wa kuandika hama habari za furaha, huzuni, chuki, uongo,
machozi na kila aina ya habari ambayo utaamua mwenyewe.
22. Dhambi ya asili ni kujiwekea ufinyu wa
mawazo katika kila hali tunayoikabili. Hapa tunafundishwa kuwa haijalishi ugumu
wa tatizo au changamoto au kazi ziliyopo mbele cha muhimu katika fikra zetu ni
kukubali kuwa tupo tayari kufanikiwa katika kila hali. Na hivyo ili kufanikiwa
katika siri hii yale tunayoyaona magumu tunatakiwa tuyaone katika hali ya
ukamilifu wa matokeo yake. Mfano, kama unahitaji kufanya mtihani mgumu badala
ya kuogopa unatakiwa ujione kwenye nafasi ya ufahulu wa mtihani huo kabla ya
kuingia hata kwenye chumba.
23. Dhamira yako ni kipimo cha uaminifu wa
nafsi yako hivyo unatakiwa kuisikiliza kwa umakini sana. Hii ni kutokana na
ukweli kwamba kila mmoja wetu yupo huru kufanya chochote anachotaka kufanya
kutokana na dhamira yake inavyomtuma. Hivyo maisha yetu yapo jinsi yalivyo
kutokana na maamuzi ya kusikiliza na kufanyia/kutokufanyia kazi mahitaji ya dhamira
zetu.
24. Sisi ni sawa na sukuma na wakati wowote
tunaweza kuvuta vitu au watu ambao tunawahitaji katika maisha yetu. Kumbuka sheria
ya asili ya “fanana uvuta fanana” like attracts each other na hivyo tunaweza
kutumia sheria hii kufanya mambo makubwa katika maisha yetu. Lakini kumbuka
kuwa sumaku haina wasiwasi na kazi yake na hivyo ili na sisi tuvute vitu
tunavyotaka ni lazima kwanza tuondoe wasiwasi wa kupata vitu hivyo.
25. Husiishi kwa ajili ya kuwafurahisha
walimwengu badala yake ishi vile unavyotaka wewe. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba kila mmoja yuko uhuru kufanya yale anayopenda katika maisha yake. Jambo la
muhimu ni kufahamu kuwa hata kama utafanya vitu kuwaridhisha walimwengu bado
una wajibu wa kujibu kwa nafsi yako kama hayo unayofanya yana mchango katika
kuiridhisha nafsi yako.
Haya ni machache kati ya mengi niliyojifunza
kwenye kijitabu hiki. Kwa ujumla kitabu hiki kina dhahabu nyingi ambazo
nimeshindwa kukushirikisha zote hapa hivyo nakushauri sana upate muda wa kukisoma.
Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza
yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali
pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala
yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: 0786881155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
Ukurasa wa facebook: Fikra
za Kitajiri: Fikri na Kutenda Kitajiri: Elimika na Tajirika