Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kushika kasi
ya mwaka 2017 kwa kuweka jitihada zaidi ili mwaka huu uwe ni mwaka wa tofauti
kwako.
Binafsi mwaka huu nimeamua uwe wa tofauti kwa kuhakikisha nasoma vitabu na
kufanyia kazi yale ninayojifunza kwa ajili kuboresha maisha yangu. Kampeni hii
nimelenga imuguse kila mmoja mwenye kiu ya kubadilisha maisha yake kwa
kuhakikisha kila mwisho wa wiki ninakushirikisha yale ninayojifunza kutoka
kwenye uchambuzi wa vitabu hivi. Pia, kampeni hii ni kwa ajili ya kila mtu
pasipokujali anajua kiingereza au haujui cha msingi ni kujua kusoma kwani vitabu
vyote vinachambuliwa kwa lugha ya Kiswahili.
Kujiunga na mtandao wa fikra za
kitajiri BONYEZA HAPA na
ujaze fomu ili uendelee kunufaika na kampeni hii ambayo imekulenga wewe mwenye
kiu ya kutimiza ndoto za maisha yako. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata
makala zinazochapishwa na mtandao huu moja kwa moja kwenye barua pepe yako.
Kitabu
cha wiki hii ni “Hiring and Keeping the Best People na tafsiri yake ni Kuajiri na
Kulinda Wafanyakazi Bora” ambacho ni kati ya vitabu vya biashara
ambavyo vinaandikwa na Kitengo cha Biashara cha Chuo Kikuu cha Havard. Kwa ujumla
kitabu hiki kinaelezea mbinu muhimu zinazoweza kutumiwa na kila Mkurugenzi wa
taasisi, mashirika au wamiliki wa Kampuni za Biashara pindi wanapoajiri na kuendelea
kuwabakiza wafanyakazi bora. Hii ni kutokana na ukweli kuwa mafanikio ya
biashara nyingi au taasisi nyingi kwa sasa yanategemea rasilimali watu kuliko
kitu chochote kile. Hivyo ni wazi kuwa ili ufanikiwe ni lazima uwe na timu ya
wafanyakazi bora na wala sio fedha, majengo, vifaa au teknolojia kwani vitu
vyote hivi ni nyenzo za utendaji kazi ambazo ufanisi wake unategemea timu ya watu
ulionao.
Karibu
tusafiri wote ili tunufaike na yale muhimu niliyojifunza kwenye hiki:-
1. Kama
mkurugenzi au mwajiri kabla ya kutangaza ajira unatakiwa kufahamu mahitaji na
majukumu ya kazi ambayo unataka ijazwe. Hapa unatakiwa kufahamu ni ujuzi,
elimu, uzoefu na maarifa yapi mhusika anatakiwa kuwa nayo kwa ajili ya kuendana
na utamaduni wa taasisi au kampuni yako. Pia ni muhimu kufahamu ni mtu mwenye
historia ipi atakuwa anafaa kujaza nafasi husika. Baada ya kujiridhisha katika
haya unashauriwa kuandaa maelezo mafupi juu ya nafasi inayotangazwa na sifa za
mtu anayetakiwa kujaza nafasi hiyo.
2. Kama
mwajiri wa taasisi au kampuni yako unatakiwa kufanya usaili kwa watu
waliojitokeza kuomba kazi uliyoitangaza. Mwandishi anatushauri kuwa usaili ni
hatua muhimu kwa mwajiri na yule anayeomba kazi. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba katika usaili ndipo mwajiri anaweza kupata taarifa zaidi juu ya msailiwa
na msailiwa kupata taarifa kutoka kwa mwajiri mtarajiwa kwa kutumia njia ya
mahojiano. Mahojiano haya yanaweza kufanyika kwa njia ya simu au kwa njia ya
ana kwa ana.
3. Usaili
unatakiwa uendeshwe kwa njia za wazi ambazo hazina upendeleo au uonevu kwa
wasailiwa. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika ya vitu ambavyo unapaswa
kuepuka kwenye usaili ni; kuonesha kumkubali msailiwa akiwa bado kwenye usaili,
kuonesha kutomkubali msailiwa kabla hajamaliza kusailiwa, kujaji uwezo wa mtu
kupitia uongeaji wake, kuamini kuwa wahitimu kutoka chuo flani ndio bora kuliko
wengine n.k. Haya ni kati ya vitu muhimu ambavyo mwandishi anatushirikisha kuwa
unapoendesha usaili huna budi kuepukana navyo ili kuepuka makosa ya kuajiri
watu ambao hawana ubora kama ilivyotarajiwa.
4. Baada
ya kukamilisha usaili ni vyema kubakia na majina ya watu watatu ambao
wameonekana kuwa bora na hatimaye majina hayo yachambuliwe na kupata jina moja.
Mwandishi anatushirikisha kuwa lengo linatakiwa kuwa ni yupi katika ya hao
watatu atafanikisha malengo ya kampuni au taasisi kwa ufanisi zaidi na si
vinginevyo. Malengo ya kampuni au taasisi kwanza yanatakiwa kupewa kipaumbele.
5. Waombaji
wa kazi wenye ubora wengi wanaangalia jina la kampuni au taasisi kabla ya
kuomba kazi. Hivyo waajiri wanatakiwa kuhakikisha taasisi au kampuni zao
zinakuwa na jina zuri kupitia kwenye idara ya masoko na idara ya utumishi kwa kutegemea
aina ya bidhaa au huduma inayotolewa na taasisi au kampuni husika.
6. Ajiri
watu ambao wanapenda kufanya kazi husika kwa mapenzi ya dhati na sio tu kwa
sababu wanataka kazi hizo kwa ajili ya pesa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba
waajiriwa wanaofanya kazi kwa ajili ya pesa ufanisi wa utendaji kazi wao ni wa
chini kwa vile waajiriwa wa aina hii wanahitaji husimamizi wa karibu. Watu
wanaofanya kazi kwa vile wanapenda kazi hizo ni rasilimali muhimu kwa vile watu
hawa muda wote wanakuwa wabunifu kwa manufaa ya taasisi au kampuni.
7. Mchakato
wa kuajiri unaweza kuendeshwa kwa njia ya kutumia kampuni za mawakala wa
kuajiri lakini ni vyema kufahamu kuwa makampuni haya yanaweka pesa mbele jambo
ambalo linaweza kufanya taasisi au kampuni husika kupata waajiriwa wenye ubora
wa chini.
8. Katika
kutafuta waajiriwa wapya ni vyema kujikita kwenye utamaduni wa kampuni au
taasisi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba utamaduni wa taasisi au kampuni ndio
unaoitambulisha kampuni au taasisi husika kwenye jamii. Utamaduni wa taasisi au
kampuni unafafanua njia zinazotumiwa kutoa huduma, unafafanua maadili ya
kampuni au taasisi na jinsi gani watu wanahusiana ndani na nje ya taasisi au kampuni
husika.
9. Waajiri
ni lazima watambue kuwa ili kampuni iendelee kufanya vyema hawana budi kuwalinda
wafanyakazi walio bora. Hii ni kwa ajili ya kuendelea kulinda uhusiano wa
kampuni au taasisi na wateja wake pamoja na kuepuka gharama za kuajiri/mafunzo ya
mara kwa mara kwa waajiriwa wapya. Mwandishi anatushirikisha kuwa kuwalinda
wafanyakazi bora waajiri wanahitaji kuwa karibu na wafanyakazi wao kwa ajili ya
kufahamu mahitaji ya wafanyakazi hao ikiwa ni pamoja na kutatua kero walizonazo.
10. Waajiri wanapaswa kufahamu kuwa sababu
zinazopelekea wafanyakazi bora kuacha kazi ni pamoja na kutafuta malisho bora,
mabadiliko ya viongozi wasimamizi (mfano wakuu wa idara/vitengo), migogoro na
wasimamizi wao, ushawishi kutoka kwa marafiki wao wa karibu ambao wameacha kazi
kwenye taasisi au kampuni husika na wakati majukumu yao ya kazi
yanapobadilishwa pasipo kuboresha maslahi yao. Hivyo kama mwajiri unatakiwa
kuzingatia sababu
11. Waajiri wanatakiwa kufahamu kuwa siku
hizi kulinda wafanyakazi bora kumekumbwa na changamoto nyingi hasa kutokana na
kukua kwa teknolojia ya habari, kuongezeka kwa idadi ya watu, mategemeo ya
jamii au waajiriwa na mabadiliko ya kiuchumi na kiutamaduni. Haya yote yamekuwa
ni kichocheo cha watu kuacha kazi kwa ajili ya kutafuta sehemu nyigine au
kuachishwa kazi kutokana na utendaji kazi wao kutoendana na malengo ya kampuni
au taasisi.
12. Njia mojawapo ya kuwalinda waajiriwa
wako hasa vijana ni kuhakikisha unakuwa na bajeti ya mafunzo kulingana na
majukumu ya kazi zao. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri teknolojia inavyobadilika
ndivyo na taasisi au kampuni inatakiwa kutenga bajeti kwa ajili ya kuendeleza
watumishi wake ili waendane na mabadiliko ya teknolojia.
13. Kama mwajiri unatakiwa kufahamu kuwa sababu
zinazofanya wafanyakazi wengi waendelee kukaa kwenye taasisi au kampuni ni
pamoja na usalama wa kazi, utamaduni wa kampuni au taasisi, malipo mazuri, usawa
katika kazi, heshima na utu, muda wa kufanya kazi na udugu kazini. Hivyo kama
mwajiri unatakiwa kuhakikisha unafanyia kazi sababu hizi kwa ajili ya kuwalinda
wafanyakazi walio bora katika kampuni yako. Ni muhimu kuzingatia kuwa
wafanyakazi bora hawalindwi na maslahi tu bali ukaribu wa viongozi wao kazi ni
nyenzo muhimu katika mazingira ya utendaji kazi wao.
14. Kama mwajiri ni muhimu kufahamu kuwa
wafanyakazi wengi upenda kukaa kwenye kazi pale wanapoona kazi wanazofanya zina
kusudi katika maisha yao. Mwandishi anatushirikisha kuwa kuna maisha baada ya kustaafu
hivyo wafanyakazi walio bora wanapenda kufikia kusudi la maisha yao kupitia
kazi wanazofanya.
15. Waajiri wanatakiwa kutofautisha thamani
ya wafanyakazi wao kulingana na majukumu, uzoefu, ujuzi na maarifa ya kila
mmoja. Hii ni mbinu muhimu ambayo kila mwajiri anatakiwa kuitumia kwa ajili ya
kulinda kila mfanyakazi ambaye utendaji kazi wake ni bora pasipokujali elimu
yake au muda wake kazini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri unavyopoteza
mfanyakazi bora athari zake kwa taasisi au kampuni ni nyingi ikiwa ni pamoja na
gharama za kupata mwajiriwa mwingine na kushuka kwa uzalishaji au utoaji
huduma.
16. Unaweza kuwalinda wafanyakazi bora kwa
kuboresha maslahi yao. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni vigumu kudumu na
wafanyakazi bora kama wana maslahi/stahiki duni ikilinganishwa na taasisi au
kampuni nyingine zenye kutoa huduma sawa na za kwako. Hivyo njia moja wapo ya
kuwalinda wafanyakazi bora ni kuhakikisha wanakuwa na ‘package’ nzuri
ukilinganisha na taasisi au kampuni pinzani. Pia, stahiki zao zinatakiwa
kuboreshwa mara kwa mara kwa ajili ya kuendana na mabadiliko ya kiuchumi.
17. Njia nyingine ya kulinda wafanyakazi
bora ni kupitia muundo wa kazi zao mara kwa mara. Hapa mwandishi
anatushirikisha kuwa unapokuwa na utaratibu wa kupitia muundo wa kazi kwa kila mfanyakazi
wako ni rahisi kugundua ni majukumu yapi ambayo yanalalamikiwa na baadhi ya
wafanyakazi. Njia hii itakusaidia kupunguza majukumu yanayolalamikiwa na
wafanyakazi wa kada moja na kuyahamishia kwa kada nyingine au ngazi nyingine ya
utendaji kazi.
18. Pia waajiri wanaweza kulinda
wafanyakazi bora kwa kuwaona wafanyakazi wao kama wateja wazuri wa taasisi au
kampuni zao. Kama ambavyo mara nyingi tumekuwa tukisikia msemo wa “mteja ni
mfalme”, mwandishi anatushirikisha kuwa waajiri wanaweza kulinda wafanyakazi
walio bora kwa kuwapa kipaumbele katika kutimiza mahitaji yao.
19. Mwajiri anatakiwa kutambua kuwa ni
wajibu wake kuhakikisha anaendeleza wafanyakazi wake ambao utendaji kazi wao
upo chini au wastani. Wafanyakazi wa aina hii wanaweza kuwa wanapungukiwa ujuzi
kwenye baadhi ya majukumu yao na hivyo njia pekee ya kuwaweka kwenye mstari
wafanyakazi hawa ni kuwapa mafunzo sahihi yanayohusu majukumu yao.
20. Pia kama mwajiri unatakiwa kufahamu
kuwa utamaduni wa kampuni yako ni njia mojawapo ya kuwavuta au kuwafukuza
wafanyakazi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba utamaduni wa taasisi au kampuni
unatoa mwelekeo wa aina ya wafanyakazi wanatakiwa kwenye taasisi au kampuni
husika. Hivyo, ni rahisi kuwapoteza wafanyakazi bora ambao wanaona utamaduni wa
taasisi au kampuni kuwa kinyume cha matarajio yao. Kama mwajiri unatakiwa
kuhakikisha unajenga utamaduni ambao utakuwezesha kudumu na wafanyakazi kwa
muda mrefu.
Haya ni machache kati ya mengi ambayo
nimejifunza kwenye kitabu hiki ni matarajio yangu kuwa endapo utayafanyia kazi
yataboresha maisha yako ya kila siku. Kila mtu ni mwajiri kwa kadri ya uwezo
wake hivyo ni vyema ukatumia mbinu hizi kuboresha maisha yako na wafanyakazi
wako ili ufanikiwe kujenga ngome imara itakayofanikisha ndoto zako.
Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com. Niendelee
kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie
wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa
kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share
link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: 0786881155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com