Habari
ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Leo naendelea kukuletea
uchambuzi maalumu wa kitabu cha The Rules of Money ambapo wiki hii tunaendelea
na shehemu ya pili ya kitabu hiki. Kama hukusoma sehemu ya kwanza ya uchambuzi
wa kitabu hiki BONYEZA HAPA.
Karibu
tuendelee kujifunza wote kanuni hizi muhimu kwa ajili ya kuboresha maisha
yetu:-
20. Kanuni ya Ishirini: Fahamu
Upo Wapi Kabla Haujaanza. Safari ya utajiri inaanzia kwenye hali
yako ya sasa na wala husitegemee kuwa kuna muujiza ambao utakuja kukuamsha ili
uianze safari hii. Unachotakiwa kufanya kwa sasa ni (a) orodhesha rasilimali
ulizonazo kwa sasa (b) orodhesha madeni uliyonayo kwa sasa (c) orodhesha wadeni
wako (d) tambua katika orodha yako ni vitu vipi vinaweza kutumika kwa sasa na
jinsi vinaweza kutumika kukuzalishia fedha na (f) andaa mpango wa wa
kuhakikisha unalipa madeni yako yote. Hapa unatakiwa kujifanyia ukaguzi wa
fedha na rasilimali ulizonazo kwa sasa na hatimaye upate mwongozo wa wapi
unaweza kuanzia kwa wakati huu.
21. Kanuni ya Ishirini na
Moja: Tengeneza Mpango Kazi Wako. Mpango kazi ni sehemu ya kukuongoza juu
ya matumizi ya fedha zako kwani pasipo kufanya hivyo pesa zako zitatumika hovyo
nje ya makusudio ya safari yako ya utajiri. Pasipo kuwa na mpango kazi ni
rahisi sana kushawishika kutumia fedha zako badala ya kuziwekeza kwenye vitega
uchumi vya kukuongezea kipato zaidi (rejea kanuni ya 10 & 11 katika sehemu
ya kwanza ya uchambuzi wa kitabu hiki). Pia, kwa kutengeneza mpango kazi wako
ni rahisi kuona ni fursa zipi zinafaa na zipi hazifai katika safari yako ya
utajiri. Hata hivyo unatakiwa kukumbuka kuwa mpango kazi wako ni lazima uwe
tayari kwa mabadiliko au maboresho kwa kadri unavyosonga mbele. Hatimaye tumia
mpango kazi huu kutoa kipaumbele juu ya kipi unatakiwa kukiendeleza au kuachana
nacho kwa kutegemea umuhimu wake katika kuboresha kipato chako. Kumbuka kuwa
utajiri unatokana na dili za kibiashara (kukunua au kuuza) hivyo mpango kazi
wako unatakiwa kuzingatia yote hayo kwa ajili ya kukuza kipato chako.
22. Kanuni ya Ishirini na
Mbili: Hakikisha Fedha zako Zipo chini ya Utawala Wako (Dhibiti fedha zako). Unaweza
kuwa na fedha nyingi lakini kama hauna mfumo mzuri wa kuzitawala fedha hizo
zitaishia kuvuja kwenye mikono hisiyo salama. Sehemu ambazo zinaweza kuvujisha
fedha zako ni (a) matumizi mabaya (b) ulipaji kodi (c) uwekezaji mbovu (d)
mikopo hisiyokuwa na tija ambayo unalipia asilimia kubwa ya riba (e) manunuzi ambayo
hayakupangwa n.k. Hapa mwandishi anatufundisha kuwa unapoianza safari yako ya
utajiri hakikisha kwanza unafahamu mianya ambayo imekuwa ikivujisha fedha zako
na hatimaye dhibiti uvujaji huo kwa kadri uwezavyo. Njia nzuri ya kufanya hivyo
ni kuandika kila aina ya matumizi kwa muda wa wiki au mwezi ili hatimaye ufanye
uchunguzi wa matumizi yapi yanatumia kiasi kikubwa cha fedha na ujiulize kama
matumizi hayo ni ya muhimu.
23. Kanuni ya Ishirini na
Tatu: Mifumo ya Bima Inalipa Watu Kiasi Kidogo Kuliko Walichochangia. Hapa
tunafundishwa kuwa mifumo ya bima ni chanzo kikubwa cha upotevu wa pesa nyingi
za watu kuliko nafasi zilizopo kurejeshewa fedha hizo. Mwandishi
anatushirikisha kuwa haina maana ya kuwa na bima kwa vitu ambavyo sio vya
lazima kwa mujibu wa sheria kwani kufanya hivyo utajikuta unatumia pesa nyingi
kwenye malipo ya bima wakati pesa hizo ungezitumia kwenye mambo mengine ya
muhimu.
24. Kanuni ya Ishirini na
Nne: Ukiwa na Mwonekano wa Kitajiri Utakuwa Tajiri. Unaweza
ukarejea kwenye kanuni ya kumi na saba katika sehemu ya kwanza ya uchambuzi wa
kitabu hiki kwa ajili ya uelewa zaidi wa kanuni hii. Katika kanuni hii
tunakumbushwa umuhimu wa kuonekana kama matajiri walivyo. Hii inajumuisha
mwonekano wetu kwa wengine lakini pia mtazamo wetu sisi wenyewe juu ya nafsi
zetu. Hivyo, mwonekano wa kitajiri haumaanishi mavazi au umiliki wa vitu vya
thamani badala yake unazingatia picha ya maisha yako kwa ujumla. Ni namna gani
picha yako inaonekana kwa wengine, Je picha yako imetawaliwa na woga, uvivu,
kukata tamaa na mengine mengi.
25. Kanuni ya Ishirini na
Tano: Fikiria zaidi Kuongezeka/Kukua (Sio Kupitia Michezo ya Kamali). Kuwa
tajiri ni lazima uwe tayari kufanya kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu wa hali
ya juu. Hapa tunafundishwa kuwa utajiri unaongezeka kadri unavyoongeza au
kukuza kile ulichonacho kwa sasa. Kama tabia yako ni kutumia kiasi chote cha
pesa unachopata pasipo kutenga kiasi flani kwa ajili ya akiba kamwe husifikirie
kuwa siku moja utakuwa tajiri. Katika kutafuta utajiri sahau msamihati wa
bahati, kwani hakuna kitu kama hicho, katika ulimwengu wa utajiri watu
wanaitafuta bahati na wala sio bahati kuwafuata wao. Bahati inatafutwa kwa
kutumia mbinu na kanuni za wazi ambazo mtu anaweza akakadria kuwa bahati yake itaongezeka
kwa kiasi gani baada ya miaka kadhaa.
26. Kanuni ya Ishirini na
Sita: Kuwa na Mtazamo Wako juu ya Neno Hatari (Risk). Mwandishi
anatufundishwa kuwa watu wengi wameshidwa chukua hatua za kiuwekezaji kutokana
na kuwa waoga kwa vile wengi wanahisi kuwa wanaweza kupoteza fedha zao. Ili uwe
tajiri ni lazima uwe na maana yako ya neno hatari kwa kuhakikisha unajiwekea
viwango vya hatari (risk) ambavyo upo tayari kuvibeba. Hata hivyo tunasisitizwa
kuwa makini kwenye uwekezaji wa pesa ili kupunguza kiwango cha hatari ya
kupoteza fedha hizo. Hivyo ni muhimu sana husiweke mayai yote kwenye kapu moja.
27. Kanuni ya Ishirini na
Saba: Fikiria Njia Mbadala ya Kuchukua Hatari (Risk). Katika
uwekezaji ni lazima kukumbuka kuwa kadri risk inavyokuwa kubwa ndivyo na tija
kutoka kwenye uwekezaji husika inavyoongezeka na kinyume chake ni sahihi. Hivyo,
mwandishi anatushirikisha kuwa kabla ya kubeba risk husika jiulize mbadala gani
wa uwekezaji ambao unaweza kuzalisha kipato sawa na huo uwekezaji ambao
ulikusudia kuutekeleza. Hapa unatakiwa kuangalia faida na hasara za uwekezaji
ambalo unalenga kuutekeleza ikilinganishwa na mbadala wake. Mfano, inaweza kuwa
kuangalia kipi kinalipa zaidi kati ya uwekezaji wa muda mfupi na muda mrefu.
28. Kanuni ya Ishirini na
Nane: Husifanye Bisahara na Watu Ambao Hauna Imani Nao. Kanuni
ya Biashara ni “Fanya Biashara na Watu Unaowaamini”. Hii kanuni amabyo hata
wewe unatakiwa kuitumia kwa ajili ya kuepuka migongano ya kibiashara hisiyokuwa
na maana. Endapo ukihisi kuwa kuna mazingira ya kutapeliwa katika biashara
ambayo ulilenga kujitosa huna budi kukimbia biashara hiyo haraka iwezekanavyo
na kuangalia ustaarabu mwingine. Kanuni hii pia unaweza kuitumia kwa bosi wako
kama umeajiriwa au ukaitumia kwa waajiriwa wako. Yeyote ambaye hauna imani nae
huna sababu ya kuenrdelea kushirikiana nae kwa jambo lolote lile.
29. Kanuni ya Ishirini na
Tisa: Kamwe Husiseme Tayari Nimechelewa Siwezi kuwa Tajiri. Rejea
kanuni ya kwanza ya uchambuzi wa kitabu hiki katika sehemu ya kwanza ambayo
inatuambia kuwa kila mtu anaweza kuwa tajiri. Hii ni kutokana na ukweli kwamba
kama kweli umedhamiria kuwa tajiri ni lazima ufanikiwe. Hautakiwi kusema siwezi
kuwa tajiri kutokana na historia yangu badala yake historia yako hiyohiyo
inatakiwa iwe kichocheo cha wewe kusonga mbele zaidi. Jambo la msingi ni wewe
kubadilisha mtazamo wako juu ya utajiri na hivyo kuanza kujibidisha kufanya
yale ambayo matajiri wanafanya.
30. Kanuni ya Thelathini:
Anza Kuweka Akiba Mapema (Kama Umechelewa Wafundishe Wanao Kufanya Hivyo). Mchezo
wa kutengeneza pesa kwa njia ya kuweka akiba unatakiwa kuwa sehemu ya asili
yako kutokana na ukweli kwamba utajiri unahitaji muda kukua. Mfano kama
unawekeza kwenye hisa, hatifungamani au vipande unahitaji muda kwa ajili ya
uwekezaji wako kuongezeka thamani. Kama unaona umechelewa kwenye uwekezaji wa
namna hii unaweza kuwafundisha hata wanao au ndugu na maarafiki kwa ajili ya
kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba wakiwa na umri mdogo.
31. Kanuni ya Thelathini na Moja: Fahamu Kuwa Mahitaji Yako ya Fedha Yanabadilika Kutokana na hatua za Maisha Yako. Wote ni mashahidi kuwa kadri umri unavyozidi kusogea ndivyo ilivyo kwa mahitaji yako ya fedha. Mfano, unapofikia hatua ya kuoa matumizi yako ni lazima yaongezeke vivyo hivyo kadri wanao wanavyozidi kukua ndivyo na mahitaji yao ya fedha yanavyoongezeka. Kwa ujumla kanuni hii inatukumbusha kuhakikisha tunafanya tathmini ya mahitaji yetu ya fedha katika kila hatua ya maisha yako hivyo kuongeza jitihada za kujiwekea maandalizi sasa kwa ajili ya wakati ujao.
32. Kanuni ya Thelathini
na Mbili: Unapaswa Kufanya Kazi kwa Bidii ili Uwe Tajiri.
Mwandishi anatushirikisha kuwa matajiri wengi tunaowaona wote wana sifa moja ya
kufanya kazi kwa bidii. Waliamka asubuhi na mapema na walichelewa kulala, hawakuwa
na muda wa kuangalia TV, walijitoa kukabiliana na ugumu na hawana muda wa kupoteza
bali muda wote wanakuwa makini na kazi zao. Hivyo na wewe kama kweli unataka
kuwa tajiri ni lazima uwe tayari kufanya kama wao. Ni lazima uwe tayari kufanya
kazi kwa bidii kwa ajili ya kuwa na fedha za kutosha ili baadae fedha zako
zianze kukutumikia wewe. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika hatua hii ndipo
tunaweza kutofautisha watu wenye nia ya kweli ya kuwa tajiri na wale ambao
wanajaribu, kutofautisha kati ya mwanaume na mvulana au kati ya msichana na
mwanamke. Hata hivyo, siyo kila kazi utakayofanya kwa bidii itakufanya uwe
tajiri ni lazima ujifunze ni kazi zipi uzifanye kwa bidii kwa ajili ya kupata
utajiri wako.
33. Kanuni ya Thelathini
na Tatu: Jifunze Sanaa ya Kufanya Dili za Kibiashara. Kama
ambavyo Rais wa Marekani Donald J. Trump anavyosema kupitia kitabu chake cha How To Get Rich nanukuu “Napenda kufanya dili hasa dili kubwa na
ndivyo ninavyosonga mbele” na
mwandishi wa kitabu hiki nae anatushirikisha umuhimu wa kufanya dili za
kibiashara tena dili kubwa kwa ajili ya kuwa tajiri. Kama unataka kuwa tajiri
ni lazima ujifunze namna ya kupata zaidi kutoka kwa wengine kupitia mauzo na
manunuzi kwa kutegemea rasilimali ulizonazo. Hapa tunafundishwa kuwa kamwe
husiseme sina pakuanzia na badala yake jifanyie tathimini vitu ulivyonavyo kwa
sasa na hatimaye anza kutumia kimoja baada ya kingine kwa ajili ya kujiongezea
kipato zaidi.
34. Kanuni ya Thelathini
na Nne: Jifunze Sanaa ya Makubaliano. Kama ambavyo tunafahamu kuwa biashara
yoyote ni lazima pawepo makubalino katika ya pande mbili. Mwandishi wa kitabu
hiki katika kanuni hii anatukumbusha umuhimu wa kujifunza sanaa ya makubaliano
kwa ajili ya kuboresha dili zako za biashara. Katika sanaa hii ni lazima uwe
tayari kumridhisha mshirika wako wa biashara ili aone kuwa anafaidika sawa na
wewe kwenye biashara ambayo mnataka kufanya. Kama kuna vitu unauza jifunze
mbinu za kuwafanya wateja wako wagundue faida ya bidhaa au huduma zako mapema
iwezekanavyo ili baada ya mauziano siku nyingine wawe tayari kufanya biashara
na wewe. Hivyo katika kila dili la biashara unalofanya lenga kwenye hali ya
ushindi wa pande zote mbili (win win situation).
35. Kanuni ya Thelathini
na Tano: Uchumi Mdogo Hauwezi Kukupa Utajiri Badala Yake Utakufanya Uwe na
Huzuni. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa kama unataka
kuishi maisha ya utajiri hauna budi kupanua uchumi wako ili ukuruhusu kufanya
mahitaji muhimu ya maisha yako. Hii ni kutokana na ukweli kwamba uchumi mdogo utakubana
kukamilisha mahitaji yako na hivyo kujikuta unaishi maisha ya msongo wa mawazo.
Na hapa ndipo tunakumbushwa kanuni ya ishirini na mbili kuwa inabidi tudhibiti
uvujaji wa pesa zetu ili tutumie pesa tulizonazo kwa ajili ya kukuza uchumi
wetu. Hata hivyo tunahamasishwa kuishi maisha ya kitajiri katika matumizi yetu
ya kila siku kwani maisha ni sasa na hivyo hatupaswi kuhairisha furaha ya maisha
yetu kwa ajili ya kesho.
36. Kanuni ya Thelathini
na Sita: Utajiri wa Kweli Unatokana na Dili za Kibiashara na Siyo Kulipia Hada.
Ni vigumu kuwa tajiri kwa kuuza muda wako (kwa kuajiriwa
japo kwa asilimia ndogo unaweza) kwa mtu mwingine badala yake unatakiwa kutumia
muda wako vizuri kwa ajili ya kuzalisha utajiri wako. Hapa tunazungumzia
utajiri ambao utakufanya uwe na maisha yenye uhuru wa kifedha ambao unaweza
kuurithisha kwa vizazi vyako na sio fedha za kubadilisha mboga ambazo waajiriwa
wengi wanaangukia hapa. Kama unataka kuwa tajiri ni lazima uwe tayari kufanya
dili za biashara za kuuza na kununua na si vinginevyo. Mwandishi anatushirikisha
kuwa haupaswi kuacha kazi yako kwa sasa lakini anachosisitiza ni kuweka mipango
ya kujiajiri kwa ajili ya kutengeneza utajiri wa kukutosheleza wewe na vizazi
vyako.
37. Kanuni ya Thelathini
na Saba: Fahamu Kuwa Kuwafanyia Kazi Wengine si Lazima Kukufanye Uwe Tajiri;
Japo Kunaweza Kukupa Utajiri. Hapa tunashirikishwa kuwa ni muhimu
kufahamu kuwa tajiri kupitia kazi tulizoajiriwa kwa sasa lakini muhimu kufahamu
kuwa ni vigumu sana kutengeneza utajiri kwa kutegemea ajira hizo asilimia mia
moja. Kupitia kanuni hii tunahamasishwa kufanya kazi kwa bidii katika shughuli
zetu za kila siku kwa ajili ya kukuza utajiri wetu. Na hivyo ni muhimu kufungua
macho kwa fursa zinazotunguka ambazo tunaweza kuzitumia kukuza utajiri wetu.
38. Kanuni ya Thelathini
na Nane: Husipoteze Muda Wako Kwa Kuhairisha – Fanya Maamuzi ya Kipesa Haraka
Iwezekanvyo. Mwandishi anatupa mfano kuwa kama
unaendesha boti na ukakumbwa na dhoruba ya mawimbi hauwezi kusubiria mpaka ufikie
sehemu ya pwani uliyoizoea badala yake utatafuta sehemu yoyote ile ya pwani ili
kuepukana na hatari ya wimbi. Vivyo hivyo ndivyo ilivyo kwenye utengenezaji wa
fedha. Kamwe hakuna siku ambayo patakuwepo mazingira mazuri ya kutengeneza
fedha kutokana na ukweli kwamba kila siku utengezaji wa fedha umeghubikwa na
mazingira hatarishi hivyo ni muhimu kuwa na taarifa sahihi, sehemu sahihi na
muda sahihi kwa fursa unazotaka kuwekeza. Husiogope kushindwa kwani hata kama
utashindwa kuna somo utakuwa umejifunza.
39. Kanuni ya Thelathini
na Tisa: Fanya Kazi Kama Vile Haufanyii Kazi Kwa Ajili ya Kupata Fedha. Katika
jamii watu wengi wanafanya kazi kwa ajili ya kupata pesa badala ya kufanya kazi
kwa vile wanapenda kazi wanazofanya. Katika kitabu hiki mwandishi anatufundisha
kuwa tunatakiwa kufanya kazi kwa ajili ya kupata fedha badala yake tufanye kazi
kutokana na mapenzi yetu katika kazi hizo na fedha zitatufuata. Hii ni kutokana
na ukweli kwamba unapofanya kazi kwa ajili ya pesa unakuwa unauza muda wako na hivyo
ni rahisi kuwa mtumwa wa kazi yako jambo ambalo litapelekea ukose furaha ya
maisha. Njia pekee ya kuwa na furaha na utajiri wako ni kufanya kazi
kutokana na msukumo wa ndani yako juu ya
kazi hizo na kama yale unayofanya hayakupi furaha rohoni ni vyema kufanya
maamuzi ya kuachana na kazi hizo mara moja.
40. Kanuni ya Arobaini: Matumizi
Yako Yasizidi Pato Lako. Hii ni kanuni kuu ambayo matajiri
wanaitumia kukuza utajiri wao na kanuni hii ipo wazi kwa ajili kutumia na mtu
yeyote yule. Kanuni hii inatuhamasisha kuacha maisha ya kuigiza na badala yake matumizi
yetu ya kila siku yaongozwe na pato letu. Hakuna sababu ya kulazimisha kula
nyama kila siku wakati pato lako linahitaji upate nyama mara moja kwa wiki au hakuna
sababu ya kulazimisha kutembelea gari wakati pato lako linahitaji utembelee
baiskeli. Mwandishi anatufundisha kuwa matumizi yako yanatakiwa yapatikane baada
ya kutoa fedha kwa ajili ya uwekezaji (kujilipa kwanza) pamoja na fedha kwa
ajili ya dharura. Hii ni njia pekee ambayo itapelekea ufanikiwe kukwepa kuishi
kwenye madeni na hatimaye kuwa na maisha ya furaha.
41. Kanuni ya Arobaini na
Moja: Husijiingize Kwenye Mkopo Kama sio Lazima Kufanya Hivyo. Hii
ni kutokana na ukweli kwamba hakuna hela ya bure hivyo husikubali kuchukua
mkopo hata kama umeambiwa kuwa utafaidika na mkopo huo. Kila fedha ambayo utapewa
kama mkopo ni lazima ukumbuke kuwa kuna kurejesha na faida juu yake. Kabla ya
kuchukua mkopo unatakiwa kufanya tathimini kabla ya kuchukua mkopo ili mkopo
huo utumike kuzalisha faida na si vinginevyo. Kama tayari una mikopo andaa
mkakati wa kulipa madeni hayo kabla haujafanya kitu kingine.
42. Kanuni ya Arobaini na
Mbili: Achana na Madeni Mapya. Baada ya kujiwekea mkakati wa kumaliza
madeni yako sasa unatakiwa kukabiliana na madeni mapya. Mfano siku hizi ni
kawaida mtu kukopa kwenye simu hata kama hakuwa na shida ya lazima ya kununua
vocha. Mfano mwingine ni watu wengi kupenda kukununua vitu kwa bei ya juu kwa
vile wamekopeshwa. Mwandishi anatushauri kuachana na manunuzi ya namna hii na
badala yake tujikite kwenye manunuzi ya muhimu tu. Kwani ni ulazimike kununua
nguo, shuka au vyombo kwa mkopo?
43. Kanuni ya Arobaini na
Tatu: Jitofautishe na Wengine Kwa Yale Unayofanya. Kama
unafanya vitu vya pekee au una ujuzi wa tofauti ni lazima watu watakuwa tayari
kulipia huduma/ujuzi wako kwa gharama yoyote ile. Hapa mwandishi
anatushirikisha umuhimu kuachana na sentensi kama vile “siwezi, sina uhakika,
sina chochote, sina kipaji n.k” na badala yake inabidi tuwe watu wa kutafuta
maarifa pale ambapo tunaona hatuna maarifa ya kutosha kwenye sehemu tuliyopo au
tunapotaka kuelekea.
44. Kanuni ya Arobaini na
Nne: Kulipa Madeni Yako Iwe ni Kipaumbele Namba Moja.
Kama ambavyo tumeona kuwa ni muhimu kujilipa kwenye kila pato unalopata vivyo
hivyo unapaswa kutenga fedha kwenye pato lako kwa ajili ya kulipa madeni yako. Madeni
yanasababisha ukose raha na hivyo kila ukionana na wadeni wako unakosa amani,
mwandishi anatuambia kuwa hii inatufanya tuwe watumwa kwa wale wanaotudai jambo
ambalo tunakiwa kupingana nalo kwa nguvu zetu zote. Hivyo kadri unavyokuza
utajiri wako inabidi uendelee kuwa na kiu ya kuhakikisha hauna madeni.
45. Kanuni ya Arobaini na
Tano: Husiwe Bize Sana na Kazi Kwa Ajili ya Kutengeneza Pesa Ili Uishi.
Mwandishi anatushirikisha kuwa kuna maisha pia nje ya kazi zetu na hivyo ni
lazima tuzingatie kuwa na maisha ya starehe ili kufurahia na wapendwa wetu. Na njia
pekee ya kufanya hivi kujiwekea ratiba ya kujishughulisha na mambo mengine nje
ya kazi zetu. Sio lazima kila tunalofanya liwe kwa ajili ya kupata pesa kwani
kuna mengi ambayo tunaweza kufanya kwa ajili ya kufurahisha roho zetu.
Tukutane wiki ijayo kwa ajili ya awamu ya tatu ya mfululizo wa
uchambuzi wa kitabu hiki.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win~Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: 0786881155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com