Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha The Art of Power (Sanaa ya Madaraka)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa upo vizuri na mapambano yanazidi kushika kasi katika kipindi hiki ambacho tunamalizia robo ya kwanza ya mwaka 2017. Ikiwa ni wiki ya kumi na mbili tokea nianze kukushirikisha uchambuzi wa kitabu kimoja kila wiki ni matarajio yangu kuwa uchambuzi wa vitabu hivi umekusaidia kwa kiasi flani katika kipindi hiki cha robo ya kwanza ya mwaka. 

Kama mpaka sasa haujafanikiwa kujifunza kitu chochote katika makala hizi za uchambuzi wa vitabu nakushauri ni vyema husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye mambo ambayo umeyazoea. Hii ni kutokana na ukweli kwamba uchambuzi wa vitabu kupitia kwenye mtandao wa fikra za kitajiri unalenga uwasaidie wale wenye kiu ya kubadilisha maisha yao kupitia usomaji wa vitabu ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu na maarifa tunayojifunza kwenye vitabu hivi katika kuboresha maisha yetu.

Kujiunga na mtandao wa fikra za kitajiri BONYEZA HAPA na ujaze fomu ili uendelee kunufaika na mwaliko huu ambao unakulenga wewe mwenye kiu ya kutimiza ndoto za maisha yako. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala za mtandao wa fikra za kitajiri moja kwa moja kwenye barua pepe yako.

Kitabu cha wiki hii ni “The Art of Power” kutoka kwa mwandishi na Mtawa wa Kibuddha Thich Nhat Hanh. Mwandishi wa kitabu hiki amekuwa ni mpenda amani kwa muda mrefu kiasi cha kutumia muda wake mwingi katika kusuruhisha sehemu zenye vita ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wahanga wa vita.

Kwa ujumla mwandishi anatushirikisha kuwa kwa maumbile kila mmoja wetu amezaliwa na nguvu ya madaraka ndani mwake na nguvu hii inaanza kutumika ipasavyo pale muhusika anapotambua yeye ni nani na ameumbwa ili atimize nini katika ulimwengu huu. Pia katika kitabu hiki mwandishi anatushirikisha umuhimu wa kutumia vizuri nguvu ya madaraka yetu kwa kutambua kuwa madaraka uliyonayo ndani mwake kuna nguvu ya kuyaangamiza pale yanapotumiwa vibaya.

Karibu tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki:

1. Madaraka halisi kwa kila mtu chimbuko lake ni kuishi maisha yenye furaha kwa wakati uliopo, maisha yasiyo na hofu, ulevi, ubaguzi, hasira na upumbavu wa kila aina. Hii ndio haki ya kuzaliwa ambayo kila mtu amezaliwa nayo hata kama yeye mwenyewe hajatambua haki hiyo. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi katika jamii wameishi kwenye msingi wa uongo wa kuwa madaraka yanatokana na elimu, utajiri, mafanikio, ukubwa wa vyombo vya jeshi, umaarufu, kipaji na nguvu au nafasi ya kisiasa. Hii ni kinyuma kabisa na maana halisi ya madaraka ambayo mwandishi anatushirikisha hapa kutokana na ukweli kwamba madaraka yanatakiwa yaanzie kwenye mfumo wa fikra wa kila mtu pasipo kujali nafasi au elimu yake.

2. Kutaka kuwa tajiri, maarufu au mafanikio ya namna yoyote ile sio jambo baya endapo tunatafuta vitu hivi kama msingi wa kutusaidia kuendelea kuishi maisha yenye furaha ya kweli katika nafsi zetu na wale tunaowapenda au jamii inayotuzunguka kwa ujumla. Kama vitu hivi vinapelekea madaraka ambayo yana athari kwa watu wengine na nafsi zetu basi vyote hivi havifai katika maisha yetu.

3. Madaraka ya kweli ni lazima yazingatie mambo yanayotokea ndani na nje ya mhusika. Kwa maana hii mwandishi anatushirikisha kuwa madaraka ambayo kila mtu amerithishwa kupitia uumbaji ni lazima yazingatie mahitaji ya nafsi kupitia mfumo wa fikra lakini pia mahitaji ya watu wanaokuzunguka. Madaraka ya namna hii yanajengwa katika msingi wa kufurahia kazi unayofanya ambayo pia ni lazima iwe inawasaidia watu wanaokuzunguka kutambua na kutumia vyema madaraka yao. Hii ni kwa mtu yeyote yule kuanzia kwa mfanyabiashara, mkulima, msanii, mwanasiasa au mfanyakazi. Kila mmoja katika makundi haya ni vyema kutanguliza lengo kubwa la kuwasaidia watu kupitia kazi yake na hatimaye mafanikio mengine yafuate.

4. Madaraka ya kweli ni yale yanayoongozwa na furaha kwa nafsi yako na watu wako wa karibu katika kila hatua unayopiga. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu kuishi maisha ya furaha kila iitwapo leo kana kwamba kesho hatutakuwepo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wengi wetu tumekuwa tukisubirisha furaha ya maisha yetu kwa kutegemea kuwa tutafurahi siku tukimiliki vitu flani lakini hata pale tunapofanikiwa kuvipata tunajikuta bado hatuna furaha rohoni mwetu. Ili kuondokana na hali kama hii mwandishi anatushauri kuishi leo kwa vile hakuna mwenye uhakika wa kwamba kesho atakuwepo.

5. Msingi wa madaraka tuliyonayo au tunayoyataka ni lazima uwe ni mapenzi ya dhati kwa familia zetu, wenza na watoto wetu, jamii inayotuzunguka. Ili kufanikiwa katika msingi huu ni lazima tusikubali kuruhusu maisha yetu yatawaliwe na yale tunayoyafanya kiasi cha kusahau kuwa karibu na wapendwa wetu. Daima tunakiwa kufahamu kuwa kuna furaha nje ya hayo tunayokimbizana nayo kila siku na furaha hiyo haipo sehemu nyingine zaidi ya kuwa na muda wa kufurahi na familia zetu.

6. Hata kama wewe ni tajiri mkubwa au maarufu kiasi gani ni lazima utambue kuwa hakuna furaha kama hauna mapenzi yanayoongozwa na hamasa ya ndani mwako bila kufahamu hili ni dhahiri kuwa yote unayofanya ni sawa na bure. Mwandishi anatushirikisha kuwa utajiri au mafanikio ya namna yoyote ile ni lazima yatokane na misingi ya kiroho ambayo ni upendo kwa nafsi zetu na wengine, huruma na kuepuka kiburi.

7. Madaraka ya kweli ni lazima yajengwe kwenye msingi wa imani kwani tunafahamu kuwa hata maandiko matakatifu yanasema kuwa kwa imani ndogo mtu anaweza kuhamisha milima. Katika hili ni lazima tutambue imani ni kuwa na uhakika pamoja na uhaminifu katika mambo yanayotarajiwa. Hivyo imani ni kufuata njia ambayo inakupeleka kwenye uhuru, wokovu au ukombozi na yenye uhakika wa kukutoa kwenye kila aina ya mateso. Hii ndiyo imani ya kweli ambayo kwa undani wake utagundua kuwa ndiyo msingi wa madaraka ambayo mwandishi anatufundisha kupitia kitabu hiki.

8. Madaraka ya kweli yanatokana na mwendelezo wa bidii zako pasipo kurudi nyuma au kutafuta njia ya mkato. Njia rahisi ya kufanikiwa katika siri hii ni kujenga tabia ya utulivu wa akili katika kila jambo unalofanya na kuhakikisha unatenga muda wa kuongea na nafsi yako kila siku. Pia, mwandishi anatushirikisha kuwa mafanikio ya zoezi hili ni muhimu yapate baraka za wanafamilia. Hata hivyo mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu kujenga tabia ya kupenda kufanya tajuhudi/tafakari (meditation) kama njia ya kutuwezesha kuwa na utulivu wa akili.

9. Mfumo wa ubongo wetu umejengwa katika namna ambayo unahifadhi mbegu za mema na mabaya. Kadri utakavyomwagilia mbegu za mema kupitia fikra zako ndivyo utapata matokeo mema na kinyume chake ni kwamba utapata matokeo mabaya kwa kutoa nafasi ya mawazo hasi katika fikra zako. Hivyo kuanzia sasa fahamu kuwa hasira, chuki, wivu, hofu, roho ya visasi, kutokujiamini na mengine mengi ambayo yamekusumbua kwa muda ni matokeo ya mbegu hasi ambazo umekuwa ukizimwagilia katika mfumo wako wa fikra. Hili kuepuka fikra hasi mwandishi anatushirikisha kuwa hatuna budi ya kuendelea na fikra hizo hadi zikajidhihirishe kwenye vitendo na badala yake tunatakiwa kubadilisha fikra hasi kwa fikra chanya.

10. Jifunze kutumia nguvu ya utulivu wa akili katika kila hali inayokuzunguka. Mwandishi anatufundishwa kuwa utulivu wa akili ni dhana pekee ya kumwezesha mtu kufikia mafanikio makubwa katika ulimwengu wa roho na mwili. Dhana hii imejengwa kwenye siri ya kuhakikisha akili yako kila wakati inatambua ni kipi kinatakiwa kufanyika kwa wakati huo na kipi hakipaswi kupewa nafasi. Mfano, kama unatembea badala kuwaza makosa yako ya nyuma au uoga wa maisha ya baadae unatakiwa akili yako yote iwe kwenye kila hatua ya mguu wako na hivyo utajikuta unapata furaha kwenye tendo la kutembea vivyo hivyo kwenye shughuli nyinginezo. Kwa kuishi msingi wa nguvu hii utafanikiwa kuepuka kufanya makosa na madhara mengi ya kiafya na hivyo kufanikiwa kuishi maisha yenye furaha muda wote.


11. Jifunze kufanya vitu kwa ukamilifu. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa hakuna mwenye uhakika kuwa kesho atakuwepo kwani yawezekana leo upo vizuri lakini kesho ukaaga dunia kwa ajili au tukio lolote lile. Hivyo ni muhimu kuishi maisha ya ukamilifu kwa kila jambo unalofanya. Kama umetenga muda wa kuwa na mwenzi wako kuwa naye kana kwamba hautakuwa na muda mwingine wa kukaa naye. Kwa ujumla tunafundishwa kuepuka kusubirisha jambo lolote kwa kutegemea kuwa litafanywa baadae.

12. Fahamu kuwa madaraka na vitu vyote tulivyo navyo katika dunia hii ni vya muda tu na hivyo umiliki wake sio wa kudumu. Hii inajumuisha maisha yetu. Wapendwa wetu na umiliki wa mali tulizonazo katika dunia hii. Mwandishi anatushirikisha kuwa unapotambuwa kuwa kila ulichonacho una umiliki wa muda itakuwa rahisi kwako kuhakikisha unapata furaha ya kutosha wakati huu kikiwa bado kwenye miliki yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa kwenye msiba sio wote wanalia kwa sababu ya kupoteza mpendwa wao bali wengi wao wanalia kwa kujutia kuwa kwa muda ambao wameishi na marehemu hawakupata muda wa kumtumia vizuri na hivyo ameondoka kabla hawajafaidi uwepo wake.

13. Tumia madaraka uliyonayo vizuri ili uepuke kuumiza watu wa chini yako. Kama wewe ni mwalimu, baba/mama, kiongonzi au mwajiri hakikisha unatumia madaraka yako vizuri pindi unapowakanya watu wa chini yako ili kuepuka kuumiza nafsi yako au wale waliopo chini yako. Hapa mwandishi anatushauri kuwa muda wote tunatakiwa kutumia madaraka yetu vizuri ili tuwasaidie watu wa chini wafikie malengo yao pasipo kuwa na msongo wa mawazo au maumivu ya roho. Kiongozi bora ni yule anayetanguliza upendo, busara, huruma na hasiye na majivuno kwa watu wake kwa kuhakikisha anaishi hisia za machungu wanayopata watu wake.

14. Cheo hakitoi madaraka ya kweli bali madaraka ya kweli yanapatikana kutokana na juhudi za muhusika kujifunza mbinu za uongozi wa kweli. Madaraka ya kweli yanaanzia kwanza kwa muhusika kujifunza na kutumia mbinu za utulivu wa akili. Utulivu wa akili ni chanzo cha furaha, amani, upendo na busara na vyote hivi ndo nyenzo muhimu za madaraka ya kweli. Hii ni kutokana na ukweli kwamba unapokuwa na vitu hivi ni rahisi wafuasi wako kukusilikiliza kile unachoongea na hivyo nguvu ya madaraka yako itakufuata pasipo kutumia nguvu nyingi. Hapa tunajifunza kuwa viongozi wengi wamekuwa wakitumia nguvu nyingi ili waonekane kuwa wana madaraka makubwa.

15. Viongozi wengi wametumia nguvu nyingi na hivyo kuwanyanyasa watu wengi kupitia maamuzi yao. Hii inasababishwa na kushindwa kutambua kuwa madaraka waliyonayo yana nguvu ya roho mtakatifu ndani mwake hivyo kama kiongozi ni lazima uwe tayari kuongozwa na vipaji vya roho mtakatifu kuliko kuongozwa na maono binafsi. Maono haya mara nyingi yamejaa majivuno, kiburi na visasi. Kwa kutambua kuwa wewe hapo ulipo tayari ni kiongozi kwa madaraka uliyonayo kuanzia sasa mfanye roho mtakatifu akuongoze katika matendo yako yote. Mwandishi anamalizia kwa kusema kuwa viongozi watapata upinzani kutoka kwa wafuasi wao endapo watatumia madaraka yao vibaya na pale wanapotumia madaraka yao vizuri kwa kuongozwa na nguvu ya roho watafanikiwa kufanya vitu vikubwa pasipo kupata changamoto nyingi.

16. Pesa na vyeo vya siasa vyote vinaweza kukupa nguvu ya madaraka lakini vyote hivi hakuna hata kimoja ambacho kitakuhakikishia furaha ya kweli endapo hujajua jinsi za kuvitumia. Kwa pesa unaweza kununua kila kitu, unaweza kununua mtu yeyote yule au kwenda mahali popote japo bado kuna muda utajikuta kwenye sononeko la roho kutokana na matendo yako ambayo yanawaumiza watu wengi.

17. Pesa na umaarufu kama vyenyewe havina ushetani ndani yake bali ushetani unakuja pale ambapo unashindwa kuvitumia kama inavyotakiwa. Unaweza kutumia pesa na umaarufu wako kwa ajili ya kuwanyanyasa watu wengine unaweza kutumia vyote hivyo kwa ajili ya kuwainua watu wengi zaidi. Kwa ujumla ni kwamba ufanisi katika vyote ni lazima uongozwe na roho mtakatifu. Wote ni mashahidi kuwa pamoja na kwamba Marekani ni taifa kubwa duniani lakini Marekani haipo hata kati ya mataifa kumi yenye watu wenye furaha zaidi. Hivyo ni muhimu kujifunza kuwa furaha ya kweli inatokana ndani mwetu pasipo kujali magumu au mema tuliyonayo.

18. Furaha ya kweli haitokani na ukubwa wa akaunti zetu za benki bali furaha ya kweli inatokana jinsi tunavyochukulia mazingira yetu ya kila siku. Kwa ujumla furaha ya kweli inatokana na kuwa na uhuru, huruma, upendo, busara na kuridhika na kile tulichonacho kwa sasa. Hapa tunakiwa kufahamu kuwa furaha hainunuliwi kwa wingi wa mali kwani wapo matajiri wakubwa lakini bado wanaishi maisha yenye huzuni rohoni mwao.

19. Kila mtu ameumbwa kuishi maisha yenye furaha hapa duniani na hivyo kila mtu amepewa mamlaka ya kuishi maisha hayo. Pamoja na mamlaka hayo kila mmoja amezungukwa na nguvu zinazomsukuma kutoka kwenye maisha hayo ya furaha. Nguvu hizi zinajumuisha maisha ya kutimiza hanasa za mwili ambazo mara nyingi zinajikita kwenye furaha ya muda mfupi na baada ya hapo ni majonzi na huzuni ya roho.


20. Njia pekee ya kumpenda mwenza wako au watu wanaokuzunguka kwanza kabisa unatakiwa kuuona uzuri na ukweli ndani mwako na baada ya hapo unaweza kuuona uzuri na ukweli katika watu wengine. Mwandishi anatukumbusha kile ambacho maandiko matakatifu yanatueleza kuwa “mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe”. Kwa maana hii hauwezi kuwapenda watu wako wa karibu kama wewe mwenyewe hauoni uzuri ndani mwako. Kama wewe hujipendi hutaweza vipi kuwapenda wenzio? Kama wewe mwenyewe hujitambui, ujielewi au hujikubali utaweza vipi kuwakubali/kuwaelewa watu wengine?

21. Njia rahisi ya kukuza upendo kwa watu wako wa karibu ni kuhakikisha wana uwepo wako wa kiakili na kimwili pale wanapokuhitaji. Ni mara nyingi kukuta wazazi au mtu na mwenza wake wanamezwa na kazi kiasi ambacho kila mmoja anahitaji uwepo wa mwingine pasipo mafanikio. Pia, katika hali kama hii watoto nao wanakosa vitu muhimu kutoka kwa wazazi. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unataka kukuza upendo wako huna budi ya kuhakikisha una muda wa kukaa karibu na uwapendao kwa ajili ya kushirikishana mambo muhimu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba upendo haukuzwi kwa zawadi za vitu bali upendo unaboreshwa kwa kufarijiana.

22. Kiongozi mwenye mafanikio ni yule anayesikiliza na kutatua matakwa ya wafusi wake. Ni lazima kama kiongozi uwepo kwa ajili ya watu wako ili ufahamu changamoto zinazowakabili na hatimaye uwe tayari kuzifanyia kazi kwa maslahi ya wafuasi wako na wewe pia.


23. Kama mfanyabiashara jifunze kufanyia kazi vitu ambavyo sio lazima vichangie kwenye biashara yako. Somo hapa ni kwamba hatupaswi kumezwa na shughuli za kutafuta faida au shilingi kila wakati kwani vitu mambo mengine ambayo tunapaswa kufanya kwa kuongozwa na utu wetu. Hapa tunatakiwa kuishi kwa kuongozwa na sheria ya asili ya uwili kinzani katika kila tunalofanya. Kwa maana hii tunatakiwa kutambua kuwa kama kuna faida pia hasara ipo, kama kuna tajiri pia masikini yupo, kama kuna kupanda pia kuna kushuka n.k. Hivyo muhimu ni kuhakikisha kila tunalofanya tufanye kwa wastani pasipo kuumiza wenzetu kwa kisingizio cha kutafuta shilingi.

Haya ni machache kati ya mengi ambayo mwandishi ametushirikisha kupitia kitabu hiki. Kama ni asilimia basi nilichokushirikisha hapa ni kama asilimia 20 tu katika mafundisho yaliyopo ndani ya kitabu hiki. Mafundisho haya yanagusia maisha ya kiroho, kijamii, kisiasa na kiuchumi hivyo nakushauri upate muda wa kusoma kitabu hiki kwa ajili ya kubadilisha maisha yako. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com



onclick='window.open(