Habari
ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Leo naendelea
kukuletea uchambuzi maalum wa kitabu cha The Rules of Money ambapo wiki
hii tutaangalia mwendelezo wa sehemu ya pili na shehemu ya sehemu ya tatu
kitabu hiki. Kama hukusoma sehemu ya kwanza na pili ya uchambuzi wa kitabu hiki
BONYEZA HAPA - SEHEMU YA KWANZA au BONYEZA HAPA - SEHEMU YA PILI.
Karibu
tuendelee kujifunza wote kanuni hizi muhimu kwa ajili ya kuboresha maisha
yetu:-
46. Kanuni ya Arobaini na
Sita: Tenga Asilimia ya Pato Lako kwa Ajili ya Akiba. Katika
safari ya utajiri ni lazima ufahamu kuwa kamwe hauwezi kuwa tajiri kama
unatumia kiasi chote cha fedha unazopata. Ili uwe tajiri ni lazima uwe na
utaratibu wa kuwekeza sehemu ya pato lako kama akiba. Mwandishi anatushirikisha
kuwa ni vyema ukawa na utaratibu wa kutenga pesa nyingi kwa ajili ya akiba yako
ya baadae kwani wengi wamekuwa wanatumia pesa zote wanazopata pasipo
kutenga hata shilingi kwa ajili ya akiba. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa
ni vyema ukawekeza akiba yako sehemu ambayo ina ongezeko la riba kwa kila mwaka
ili fedha zako ziongozeke.
47. Kanuni ya Arobaini na
Saba: Husikodi bali Nunua. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni vyema
ukanunua au kujenga nyumba yako hata kama ni kwa mkopo kuliko kukodi. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba pesa unayolipa kwenye pango kamwe haitarudi kwako
tofauti na ambavyo ungekuwa unalipia mkopo na riba yake ambao uliutumia kujenga
au kununua nyumba. Epuka gharama ya pango la aina yoyote ile kwa kuweka mipango
ya kununua rasilimali ambayo unakusudia kukodishwa. Pia, fahamu kanuni ya
kwamba nunua kwa bei rahisi na uza kwa bei ya juu ili kuepuka hasara katika
biashara zako.
48. Kanuni ya Arobaini na
Nane: Fahamu Nini Maana ya Uwekezaji. Kwa ujumla uwekezaji unakuwa na malengo
mawili ambayo ni ambayo ni kuzalisha kipato na kuongezeka thamani. Mfano kama
unawekeza kwenye majengo lengo lako linapaswa kuwa kuongeza kipato kupitia
kwenye malipo ya wapangaji na ongezeko la thamani ya nyumba zako. Vivyo hivyo
kwenye uwekezaji wa hisa ni lazima unufaike kupitia gawio na ongezeko la
thamani la hisa zako ikilinganishwa na thamani ya hisa uliyonunulia. Hata hivyo
unatakiwa kufahamu kuwa uwekezaji wa aina yoyote ile ni sawa na kucheza kamari
hivyo unatakiwa kuwa na taarifa sahihi kabla ya kuwekeza.
49. Kanuni ya Arobaini na
Tisa: Kusanya Mtaji na Uwekeze kwa Umakini. Mwandishi
anatushirikisha kuwa watu wengi wameshindwa kuwa tajiri kwa vile ni wavivu na
wanashindwa kuzalisha pesa kutoka kwenye pesa ndogo wanazopata kila siku. Walio wengi
wameshindwa kuwekeza pesa wanazopata kwa vile wanatumia pesa zote wakiamini kuwa watapata pesa nyingine. Hii ni tabia mbaya ambayo kamwe hauwezi kuwa
tajiri kwani utajiri unapatikana kwa kutumia pesa uliyonayo kuzalisha pesa
zaidi na zaidi. Husikubali kuendeshwa na starehe na badala yake tenga kiasi cha
fedha kwa ajili ya uwekezaji kabla ya kufanya matumizi mengine.
50. Kanuni ya Hamsini: Fahamu
Kuwa Uwekezaji Kwenye Majumba Katika Kipindi cha Muda Mrefu Kamwe Hauwezi
Kuuzidi Uwekezaji wa Hisa. Baada ya kukusanya mtaji wengi
wanajiuliza ni sehemu ipi sahihi wawekeze fedha zao. Mwandishi anashauri kuwa
kama lengo lako ni kuwekeza kwa muda mrefu ni vyema ukachagua kuwekeza kwenye
hisa ikilinganishwa na majengo. Muhimu unatakiwa kufahamu
kuwa uwekezaji wa hisa unatengemea kupata faida kupitia gawio ambalo pia linategemea
faida iliyotengenezwa na kampuni husika. Njia nyingine ya kunufaika na hisa ni
kupitia ongezeko la thamani ya hisa zako na ndio maana unapochagua uwekezaji wa
namna hii ni lazima uwe na malengo ya kuwekeza kwa muda mrefu ikilinganishwa na
uwekezaji wa aina nyingine.
51. Kanuni ya Hamsini na
Moja: Kuwa Mtaalamu wa Sanaa/sayansi ya Kuuza. Kama
ambavyo tumeona kuwa ili kuwa tajiri ni lazima ujifunze sanaa ya kufanya dili
za biashara (rejea kanuni namba 33) ndivyo ilivyo sanaa ya kuuza. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba sanaa ya dili za kibiashara inategemea sanaa ya
kuuza. Unanunua kwa ajili ya kuuza tena kwa faida kwani huu ndio msingi wa kukuza
utajiri wako. Hauwezi kutengeneza pesa kama hauwezi kuuza na hii ni siri ambayo
matajiri wengi wanafahamu na kuitumia ikilinganishwa na masikini au watu wa
kawaida. Pia unatakiwa kufahamu kuwa ili uwe na mauzo ya juu ni lazima ufahamu
ni vitu vipi vinanunuliwa kwa wingi na watu wengi.
52. Kanuni ya Hamsini na Mbili: Jione Wewe Mwenyewe Kama Wengine Unaowakubali. Kama unahitaji kuongeza mauzo yako ni lazima uwe tayari kufanya yale yanayofanywa na wauzaji wakubwa. Hivyo ni vyema ukajifunza jinsi kutoka kwa wauzaji mahiri kwa ajili ya kuongeza mauzo yako. Hii inajumuisha tabia yako, mwonekano wako, uchangamfu wako, ahadi zako, fikra zako, mawasiliano yako na bidii zako kwani haya yote ndo yanaamua mauzo yako.
53. Kanuni ya Hamsini na
Tatu: Husiamini Kuwa Utashinda Kila Wakati. Safari hii ya
kuwa tajiri inabidi uende nayo kwa umakini hasa kwenye suala la bahati na
sibu, kamwe husiamini kuwa unaweza kushinda na kuwa tajiri kwa haraka na badala
yake unatakiwa kuongeza bidii katika yale unayofanya kwa ajili ya kuongeza mapato yako.
Pia, mwandishi anatushirikisha kuwa katika safari hii kuna kupanda na kushuka
hivyo ni vyema kujifunza katika kila hali tunayokutana nayo.
54. Kanuni ya Hamsini na
Nne: Husinunue Hisa Mwenyewe Kama Haujui Kinachoendelea Kwenye Soko la Hisa.
Mwandishi anatushirikisha kuwa kabla ya kuwekeza kwenye soko la hisa ni vyema
kwanza ukawa na uelewa jinsi soko la hisa linavyofanya kazi. Unaweza kujifunza
kuhusu soko la hisa kwa kusoma taarifa za fedha zinazohusu soko la hisa, kwa
kuongea na watu wenye uelewa na soko la hisa, kwa kuangalia vipindi maalumu vya
TV au kwa kuomba ushauri kutoka watu mbalimbali wanaohusika na soko la hisa. Fuatilia
mwenendo wa hisa za kampuni tofauti tofauti kwenye soko la hisa kabla haujaamua
kununua hisa za kampuni flani.
55. Kanuni ya Hamsini na
Tano: Fahamu Undani wa Jinsi Soko la Hisa Linavyofanya Kazi. Kama
ilivyo kwenye masoko mengine kuwa kuna kununua na kuuza, kununua kwa bei ya
chini na kuuza kwa bei ya juu, ndivyo ilivyo kwenye soko la hisa. Utanunua hisa
za kampuni uliyochagua na kuuza hisa zako pindi thamani ya hisa ikiongezeka.
Zaidi ya hapo unatakiwa ujifunze ni kipindi kipi unatakiwa kununua hisa na
kipindi kipi unatakiwa kuuza hisa zako.
56. Kanuni ya Hamsini na
Sita: Nunua Hisa (au Kitu chochote kile) Ambazo ni Rahisi Kuelewa. Mwandishi
katika kanuni hii anatufundisha kuwa kununua hisa au kitu chochote kile kwa
ajili ya kuuza kwa faida ni aina nyingine ya kamari hivyo ni muhimu sana kuwa
na uelewa wa kutosha kabla ya kujitosa kununua. ili ufanikiwe kwenye kanuni hii ni
muhimu kuepuka kununua kwa hisia na badala yake unatakiwa kununua kitu ambacho
umefanyia utafiti na kujiridhisha kuwa asilimia ya kutengeneza faida ni kubwa
kuliko hasara.
57. Kanuni ya Hamsini na
Saba: Tumia Kichwa Chako. Sababu kubwa ya kuendelea kusoma kanuni
hizi ni kwa vile una msukumo wa kuwa tajiri. Katika safari ya utajiri ni lazima
utambue kuwa kila maamuzi utakayofanya ni lazima yawe na nguvu ya kukusogeza
hatua moja hadi nyingine katika utajiri wako. Kwa maana hii hauna nafasi ya kujutia
matokeo ya maamuzi yako kutokana na uzembe wa kutumia kichwa chako katika
kufanya maamuzi kwenye kila hatua unazopiga. Daima maamuzi yako yatokane na
mchanganuo wa faida na hasara ambazo zinaweza kujitokeza.
58. Kanuni ya Hamsini na
Nane: Katika
Kila Hali Watumie Wabobevu wa Masuala ya Uwekezaji (Lakini Husikubali
Wakuendeshe). Mwandishi anatushirikisha kuwa pale ambapo tumekwama ni bora
kupata ushauri kutoka kwa watu wenye uzoefu kwenye masuala ya uwekezaji lakini
ni muhimu tuendeshwe na busara zetu kwa yale tunayoshauriwa. Kama unahitaji
ushauri kutoka kwa mawakala wa hisa muda wote ni lazima wakupe ushauri wa
kukuvutia ili ufanye nao biashara hivyo ni vyema kutafuta taarifa zaidi na
kujiridhisha juu ya kile unachoshauriwa.
59. Kanuni ya Hamsini na
Tisa: Kama Unahitaji Ushauri wa Kifedha Ulipie Kwanza. Wapo
watu wengi ambao wanakusubiria kwa ajili ya kukupa ushauri, taarifa au miongozo
ya kifedha. Mfano kwa hapa Tanzania kama unahitaji taarifa za mienendo
ya hisa za kampuni tofauti unaweza kulipia kupitia tovuti ya DSE na utapewa
taarifa unazohitaji. Pia zipo kampuni na watu ambao wanatoa ushauri wa kifedha
na masuala yote ya uwekezaji hivyo ni wewe kujiweka sawa kutegemeana na ushauri
unaohitaji. Muhimu, unatakiwa kuwa makini na sehemu ambazo unatafuta ushauri ili
husije kuangukia kwenye mikono ya matapeli.
60. Kanuni ya Sitini: Husipoteze
Muda Kwa Yale Ambayo Tayari Umefanya. Baada kukamilisha kazi yako hata kama
haujaridhika nayo husipoteze muda kuirudiarudia ukidhani kuwa ndo itakuwa bora
zaidi kwani pengine unaweza kuifanya iwe mbaya zaidi. Baada ya kufanya kazi
yako unatakiwa kusubiria wakati wa mavuno na sio kurudiarudia kazi husika. Mara
nyingi ni kawaida watu kuwa na wasiwasi au hofu baada ya kufanya maamuzi ya kifedha,
mwandishi anatushirikisha kuwa ukishafanya maamuzi ni vyema kuachana nayo ili
asili (nature) ichukue nafasi yake na wewe uendelee na mambo mengine.
61. Kanuni ya Sitini na
Moja: Fikiria Uwekezaji wa Muda Mrefu. Mwandishi anatushirikisha
kuwa kama unataka utajiri wa muda mfupi ni bora ukaachana na kanuni hizi na
ukaenda kucheza kamari na kwenye mikeka ya mhindi. Utajiri wa kweli unatakiwa uandaliwe
kwa muda mrefu kwani kila unalofanya kwa sasa unapaswa kufikiria mchango wake kwenye
pato lako kwa siku za baadae. Hivyo ni vyema ukawa na uwekezaji wa muda mfupi,
muda wa kati na uwekezaji wa muda mrefu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri
unavyopata utajiri kwa muda mrefu ndivyo unajenga uzoefu wa kulinda utajiri
wako.
62. Kanuni ya Sitini na
Mbili: Kuwa na Muda Katika Siku kwa Ajili ya Kutathimini Mipango Yako. Mwandishi
anatushirikisha kuwa ni muhimu kutenga muda kila siku kwa ajili ya kufikiria juu ya hatua zetu.
Hapa anatushauri kuwa ni vyema muda huu ukawa ni asubuhi na mapema au usiku
wakati kuna hali tulivu ili uweze kuzama kwenye tafakari ya kina ya mipango yako. Hii
inatoa nafasi kwako kutafakari ni wapi umefanikiwa na wapi bado haujafikia
malengo ili hatimaye uweke mikakati ya kuboresha zaidi.
63. Kanuni ya Sitini na
Tatu: Kuwa Makini Kwenye Kila Sehemu ya Uwekezaji Wako. Hii
inajumuisha kuhakikisha kila kinachoingia na kutoka kimeorodheshwa ikiwa ni
pamoja na kuwa na rekodi za lini unatakiwa kulipia kodi, pango, lini unatakiwa
kulipwa, kuangalia riba ya uwekezaji wako, mawasiliano na watu muhimu, emails,
lini unatakiwa kutangaza biashara zako n.k. Mwandishi anashauri kuwa kama
inakuwa ngumu kwako kufanya kazi hii ya uhakiki unaweza kumuajiri mtu maalum
kwa ajili ya kufanya kazi hii.
64. Kanuni ya Sitini na
Nne: Anzisha Mifereji Mipya ya Kipato. Hii ni kanuni muhimu kwa ajili ya
kukuza utajiri wako kwani kadri unavyokuwa na mifereji mingi ni rahisi kuongeza
kipato chako. Mwandishi anatushirikisha kuwa kamwe husitegemee mfereji mmoja
kwani hauwezi kukupa utajiri badala yake utakufanya uwe na maisha ya huzuni. Hakikisha
unawekeza kwenye vitega uchumi kwa kadri uwezavyo ili ufanikiwe kupata pesa
kutoka sehemu tofauti.
65. Kanuni ya Sitini na
Tano: Jifunze Kuwa na Utamaduni wa Kujiuliza Maswali Kabla ya Kuchukua Hatua. Mwandishi
anatushirikisha kuwa ni muhimu kujiuliza maswali nafsini mwako kabla ya kuchukua
hatua. Mfano unaweza kujiuliza maswali kama (a) Itakuwaje kama shamba/kiwanja
hiki kina migogoro? (b) Itakuwaje hisa za kampuni hii zikashuka thamani au
kampuni ikafisilika (c) Itakuwaje wateja wangu wakihamia kwa wapinzani wangu? n.k.
Maswali haya ndo yanatakiwa kuwa mwongozo wako katika kuboresha sehemu ambazo
unaona hazijakaa sawa. Pia, maswali haya yanatakiwa kukuongoza kuchangamkia
fursa mpya kwa ajili ya kuanzisha mifereji mipya ya kipato.
66. Kanuni ya Sitini na
Sita: Dhibiti Hisia Zako za Matumizi. Njia ya haraka ya kuharibu utajiri wako
ni kuruhusu hisia za matumizi kwenye kila kitu ambacho hakipo kwenye mipango
yako. Utajiri ni sawa na mbio za marathoni kwani wengi wanaanzisha lakini
wanaofikia mwisho ni wachache. Kinachowatofautisha watu katika mbio hizi ni
namna gani wanaweza kupambana na changamoto ikiwa ni pamoja na matumizi yao ya
kila siku. Uwekezaji wowote ni lazima ufahamu kuwa unahitaji hewa kama ilivyo
kwako ili uishi unahitaji hewa ya oxjeni vivyo hivyo na uwekezaji unahitaji
hewa ambayo ni mwendelezo wa mtaji. Kila shilingi unayotumia kutoka kwenye biashara
yako ni lazima uhakikishe shilingi hiyo si sehemu ya mtaji wako.
67. Kanuni ya Sitini na
Saba: Husijibu Matangazo ya Kwenye Mtandao Yanayohusu Utajiri wa Haraka, Kwani
Hiyo Siyo Sehemu Yako ya Kuwa Tajiri. Pamoja na kwamba kuna njia nyingi za
kutengeneza utajiri wa haraka kwenye mitandao unachotakiwa kufanya ni kuamini
kuwa njia hizo si salama kwako. Hii ni kutokana na ukweli ambao tumeupata
katika kanuni nyingi zilizopita kuwa utajiri wa bahati na sibu si salama kwani ni sumu kwa fedha zako hasa wewe unayeanza safari hii.
68. Kanuni ya Sitini na
Nane: Tambua Kuwa Hakuna Siri. Kutokana na kiu yako kubwa ya kuwa
tajiri njiani utakutana na mengi ambayo yatakushawishi kutoa fedha zako kwa
ajili ya kujua siri za kupata utajiri. Hapa ni lazima usimame imara kwani
hakuna siri ya utajiri zaidi ya hizi ambazo umezipata kupitia kwenye kila
kanuni ya kitabu hiki. Kuwa makini na matapeli vinginevyo watatumia kiu yako ya
utajiri kufilisi fedha zako. Katika kila hatua ongozwa na kauli mbiu kuwa
hakuna siri ya utajiri kwani utajiri upo kwa kila mtu na ni haki ya kuzaliwa
kwa kila mmoja (rejea kanuni namba moja).
69. Kanuni ya Sitini na
Tisa: Husiishie Kusoma Kanuni Hizi Bali Chukua Hatua. Kufahamu
kanuni hizi ni mwanzo lakini haina maana kama haupo tayari kuchukua hatua
kuanzia sasa. Husiishie kusema haya nayafahamu pasipo kuchukua hatua za
kutekeleza yale unayoyafahamu. Tambua kuwa kama kweli una hamasa ya kuwa tajiri
inabidi ubebe siraha zako mara moja na kuanza kupigana vita dhidi ya umasikini.
Kubadili tabia ni jambo ambalo ni gumu kwa kiasi flani lakini huna budi kuanza
taratibu ili hatimaye ufanikiwe kujenga msingi imara ambao ni vigumu
kuharibiwa.
Tukutane wiki ijayo kwa ajili ya awamu ya nne ya mfululizo wa
uchambuzi wa kitabu hiki.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win~Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: 0786881155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
Ukurasa
wa facebook: Fikra za Kitajiri: Fikri na
Kutenda Kitajiri: Elimika na Tajirika