Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha Alex Ferguson Autobiography (Hisitoria ya Maisha ya Alex Ferguson)

Rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri ni matumaini yangu kuwa upo vizuri na unaendeleza mapambano kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Kama ambavyo nimekuhalika mwaka huu kuwa nami katika usomaji wa vitabu mbalimbali leo hii ikiwa ni wiki ya kumi na moja naendelea kutimiza ahadi yangu.  Mwaliko huu ni kwa ajili ya kila mwenye kiu ya kubadilisha maisha yake kupitia usomaji wa vitabu ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu na maarifa tunayojifunza kwenye vitabu hivi. Kampeni hii ni kwa ajili ya kila mtu pasipokujali anajua kiingereza au haujui cha msingi ni kujua kusoma kwani vitabu vyote vinachambuliwa kwa lugha ya Kiswahili.

Kujiunga na mtandao wa fikra za kitajiri BONYEZA HAPA na ujaze fomu ili uendelee kunufaika na mwaliko huu ambao unakulenga wewe mwenye kiu ya kutimiza ndoto za maisha yako. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala za mtandao wa fikra za kitajiri moja kwa moja kwenye barua pepe yako.

Kitabu cha wiki hii ni “Alex Ferguson My Autobiography” ambacho kwa ufupi ni hisitoria ya maisha ya Kocha Mstaafu wa Timu ya Mpira ya Manchester United. Katika kitabu hiki mwandishi Sir Alex Ferguson anatushirikisha maisha yake ambayo kwa ujumla kuna mengi ya kujifunza kwa mtu yeyote ambaye anahitaji kuishi maisha ya mafanikio.

Itakumbukwa kuwa Sir Alex Ferguson ni kati ya makocha ambao hauwezi kutaja mafanikio ya klabu ya Manchester United pasipo kutaja jina lake kutokana na heshima ya mafanikio aliyojijengea kwa kipindi chote cha miaka 26 (1986/17 – 2012/13) akiwa maneja wa timu hii. Kwa kipindi hiki chote alikutana na vipindi vya kupanda na kushuka lakini hatimaye alifanikiwa kuhitimisha safari yake kwa mafanikio makubwa sana.

Karibu tujifunze wote machache ambayo nimejifunza kwenye kitabu hiki;

1. Ili kupata mafanikio ya muda mrefu ni lazima uwe na uvumilivu. Mwandishi anatushirikisha kuwa maisha ya mafanikio yanaanzia kwenye kilima ambacho mwanzo wa safari utaona kama vile ni ndoto kufanikiwa kupanda kilima hicho. Hii ni kutokana na hali ambayo yeye mwenye alikumbana nayo kipindi anakabidhiwa timu mwaka 1986.

2. Ili ufanikiwe ni lazima uwe na watu wanaokusapoti kwanza kabisa ukianzia na familia yako. Mara nyingi tumekuwa tukisikia msemo wa “kila kwenye mafanikio ya mwanamme fahamu kuwa kuna mwanamke nyuma yake”. Kocha Sir Alex Ferguson amedhihirisha msemo huu kwa kutuambia kuwa mafanikio yake kwa ujumla yalichangiwa na sapoti ya mwenza wake na watoto wake kwa ujumla.

3. Mafanikio ya kesho yanajengwa na msingi imara wa leo. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika maisha yake kuna kipindi alihisi kuwa angefukuzwa kazi kutokana na imani yake ya kujenga timu ya vijana jambo ambalo lilipelekea timu kuyumba katika michezo ya ligu kuu. Lakini kwa vile alikuwa na nia thabiti kwenye kazi yake alifanikiwa kushawishi viongozi wake na hatimaye akajenga timu imara ambayo ilishinda mataji mengi.

4. Ili upate mafanikio ni lazima utafute changamoto mpya kwa kuhama mazingira uliyokulia na kutafuta sehemu mpya. Mwandishi alianzia kazi yake nchini mwake (Scotland) lakini baada ya kuhamia Uingereza alifanikiwa kupata changamoto nyingi ambazo zilimjenga katika kazi yake na hatimaye kufanikiwa kustaafu akiwa kocha mwenye mafanikio zaidi.

5. Ili ufanikiwe ni lazima dhamira yako yote iwekwe kwenye kazi husika unayofanya. Sir Alex Ferguson anatushirikisha kuwa kuna kipindi aliwahi kuhojiwa kuwa kwa nini timu yake ikiwa uwanjani hajawahi onekana akiwa na tabasamu na yeye alijibu kuwa timu yake ikiwa inacheza sio sehemu ya kutabasamu bali ni sehemu ya kutafuta ushindi basi. Muhimu hapa tunafundishwa kuthamini kazi zetu kwa kutuliza akili zetu (mind concentration) pindi tunapowajibika.

6. Mafanikio ya aina yoyote ile yanajengwa kwenye msukumo wa dhati wa kuhitaji mafanikio kwa kila hali. Mwadishi anatushirikisha kuwa yeye binafsi baada kuondoka Scotland na kuhamia Uingereza alikuwa na nia moja nayo si nyingine bali ni kufanikiwa katika kazi yake mpya.

7. Jamii inayokuzunguka inatazama mabaya yako na kusahau mema uliyotenda. Hii ni sawa na msemo uliyotumiwa na Bwana Yesu kuwa “watu wanataka mikate” kwa maana ya kwamba watu wapo kwa ajili ya mazuri unayofanya na hasa kwa faida yao na pale unapoteleza kidogo hakuna hata mmoja atakumbuka wema wako wa jana. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika kipindi chake chote ilikuwa ni kawaida mashabiki kumtukana kutokana na timu kupoteza mchezo mmoja tu huku wakisahau makombe yote waliyowahi kushinda akiwa timu meneja.

8. Muda wote kuwa tayari kwa changamoto na fursa mpya pasipo kujali umri wako ili kuepuka kukaa bila kazi. Kocha Alex Ferguson anatushirikisha kuwa yeye binafsi baada kustaafu akiwa na umri wa zaidi ya miaka 70 aliamua kutafuta fursa mpya ili apate changamoto na uzoefu mpya na hatimaye kuepuka kukaa bila kazi.

9. Kubali kuteseka kwa ajili ya mafanikio ya baadae. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika miaka 39 aliyofanya kazi ya ukocha mara nyingi alipata hamasa ya kusonga mbele pasipo kujali ugumu wa matokeo kwani aliamini katika msemo wa mazuri yanakuja kutokana na mateso ya sasa. Kwa maana nyingine mafanikio yako ya kesho yanaandaliwa na bidii na jitihada zako za sasa.


10. Chimbuko/asili yako haina nafasi ya kuamua hatma ya mafanikio yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa wapo wengi ambao walimbeza kutokana na chimbuko lake hasa ikizingatiwa kuwa alizaliwa katika wilaya ambayo shughuli kubwa ya kiuchumi ilikuwa kutengeneza boti. Wengi walidhani kuwa hakuwa na lolote katika tasnia ya mpira ingawa kadri muda ulivyosogea walinyamazishwa na mafanikio yake. Na hapa mwandishi anatushirikisha kuwa ukifuatilia maisha ya watu wengi wenye mafanikio utagundua kuwa wengi wao wamekulia katika mazingira magumu kuanzia kwenye familia zao hadi jamii zilizowazunguka.

11. Katika kila hatua unazopiga tengeneza marafiki wanaoendana na mitazamo yako. Mwandishi anatushirikisha jinsi ambavyo marafiki wake katika ngazi tofauti walivyokuwa na mchango mkubwa kwake hasa katika ngazi ya familia na hatimaye ufanisi wa kazi yake. Pia, kupitia marafiki hawa mara nyingi waliweza kumpa mrejesho na ushauri juu ya mwenendo wa timu yake ikiwa ni pamoja na taarifa za wachezaji wazuri.

12. Mara zote tofautisha mambo binafsi/familia na majukumu ya kazi yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu sana kila unapokuwa kazini hakikisha unatimiza majukumu yako pasipo kuruhusu mwingiliano wa mambo binafsi au familia. Hii itakusaidia kutimiza majukumu yako kwa ufanisi na hivyo kupata mafanikio makubwa katika kila unalogusa.

13. Epuka mazoea yaliyopitiliza na wafanyakazi wako. Mwandishi anatushirikisha kuwa yeye binafsi katika kipindi chake chote ambacho amefanya kazi ya ukocha amekutana na wachezaji wa kila aina na wenye kila tabia. Kwa ujumla ufanisi wake ulitokana na misimamo yake ya kusimamia haki na wajibu wa kila mchezaji pasipo kuruhusu mazoea yasiyo ya lazima na wachezaji wake.

Soma:Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha “Hiring and Keeping the Best People” (Kuajiri na Kulinda Wafanyakazi Bora)

14. Ili uwe na ufanisi ni lazima uwe na msimamo na uwe tayari kusimama kwenye kile unachokiamini pasipo kuogopa au kuyumbishwa na mtu yeyote. Kila mtu ana wajibu na mamlaka katika nafasi yake hivyo kwa kila namna ni lazima utumie mamlaka uliyonayo kusimamia maamuzi yako.

15. Daima husikubali kuridhishwa na mafanikio uliyonayo. Kila hatua ya mafanikio inabidi ifungue hatua moja ya ziada juu ya pale ulipo. Mwandishi anatushirikisha kuwa yeye binafsi baada ya kushinda Kombe la Ulaya (European Cup) akiwa na umri wa miaka 60 alihisi ulikuwa muda muhafaka wa kustaafu. Hii ni kutokana na mafanikio aliyoyapata japo baada ya kupata ushauri kutoka kwa familia yake alifanikiwa kufanya kazi miaka 11 mingine na kupata mafanikio ya kunyakua makombe mengi.

16. Safari ya ushindi inaambatana na safari ya kushindwa; muda wote jifunze kutoka kwenye makosa unayofanya. Mwandishi anatushirikisha jinsi ambavyo mara nyingi alifanya makosa hasa kwenye mauzo ya wachezaji muhimu akidhani kuwa ni biashara. Baada ya msimu kumalizika na kuanza msimu mpya alijikuta kwenye wakati mgumu wa kuziba pengo la mtu aliyeuzwa. Hili kukabiliana na changamoto hii ilibidi kabla ya kuuza mchezaji awe ameandaa mbadala wake.

17. Kama meneja/kiongozi unatakiwa ufahamu tabia za unaowaongoza kwa undani ikiwa ni pamoja na kuwafahamu mapungufu ya kila mmoja. Mwandishi anatushirikisha kuwa yeye binafsi mafanikio yake yalitokana na wachezaji wake katika vipindi tofauti na hivyo kama meneja ilimbidi kufahamu tabia na mapungufu ya kila mchezaji wake. Mwandishi anamtolea mfano David Beckham kama mchezaji ambaye kamwe hakuwahi kukubali makosa yake hata kama amesababisha timu ipoteze mchezo. Pamoja na mapungufu hayo, Kama meneja wa timu ilimbidi atafute namna bora ya kuendelea kumtumia David kutokana na kipaji alichokuwa nacho.

18. Kama meneja au kiongozi daima husivumilie tabia za mwajiriwa ambaye anajiona yeye ni bora kuliko mwajiri wake. Hapa mwandishi anatushirikisha jinsi ambavyo ilimbidi alazimishe uongozi kumuuza David kutokana na tabia zake zisizovumilika ambazo zilikuwa zinaigharimu timu. Hii ilitokana na tabia yake ambapo ilifikia hatua ya kuona yeye ni bora kuliko Alex Ferguson.

19. Kama kiongozi au meneja unatakiwa kulinda wafanyakazi wako wenye mchango mkubwa kwenye kampuni au taasisi yako. Hapa mwandishi anatushirikisha jinsi ambavyo ilimbidi awalinde Ryan Giggs na Paul Scholes kwa kipindi cha miongo miwili kutokana na tabia pamoja na mchango wao kwa Club ya Mancester United.

20. Jifunze kuepuka kupoteza fursa uliyonayo mkononi. Mwandishi anatolea mfano jinsi ambavyo Sporting Lisbon ilimuuza Christiano Ronaldo kwa Manchester United kwa makubaliano kuwa pindi Manchester ikitaka kumuuza lazima Sporting ipewe kipaumbele. Lakini cha kushangaza Ronaldo aliyenunuliwa kwa £12 milioni baada ya kipindi cha miaka 6 aliuzwa kwa £80 kiasi ambacho Sporting walishindwa na ndipo Ronaldo akatimukia Real Madrid. Hili ni fundisho kwetu kwa fursa tulizonazo, mfano viwanja au ardhi au rasilimali yoyote ile, kabla ya kuuza hakikisha unafanya tathimini ili kesho husije kujutia maamuzi yako.

21. Jifunze kutoka kwa wapinzani wako ili uboreshe kazi zako. Mwandishi anatushirikisha kuwa daima hakuwaona mameneja wa timu pinzani (Arsene Wenger, Jose Mourinho na wengineo)  kama maadui na badala yake aliwatumia kujifunza ni wapi aboreshe zaidi kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.

Haya ni machache kati ya mengi ambayo Sir Alex Ferguson anatushirikisha kupitia historia ya maisha yake. Kitabu hiki kina mengi ambayo tunaweza kuyatumia katika maisha yetu ya kila siku hivyo nashauri kila mwenye utamaduni wa kusoma vitabu akisome. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786881155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com


onclick='window.open(