Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku 12 kati
ya 21 za maombolezo ya kifo cha mpendwa wetu shujaa wa Afrika, Hayati Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli. Katika kipindi hiki cha maombolezo naendelea kukushirikisha
mafundisho mbalimbali kuhusiana na kifo. Kupitia mafundisho haya tunajifunza jinsi
gani tunatakiwa kukabiliana na kifo pale tunapofiwa na wapendwa wetu sambamba na
namna ya kujiandalia kifo chema. Karibu katika sehemu ya pili ya mafundisho
kuhusiana na majuto kwa watu wanaokaribia kukata roho.
“NINATAMANI MAISHA YANGU YASINGETAWALIWA NA HISIA ZA MATUKIO YANGU YALIYOPITA.” Haya ni majuto namba tatu kulingana na orodha ya Bronnie Ware. Wagonjwa wengi walijutia muda wa Maisha yao kutawaliwa na hisia za matukio yaliyopita. Katika kundi hili wengi walitamani wangetumia muda mwingi kuishi maisha yao kulingana na nyakati zilizopo ili kuruhusu amani na furaha itawale maisha yao. Yawezekana ni miongoni mwa watu ambao wanaishi kwa kuandamwa na hisia za matukio yaliyopita katika historia ya maisha yako. Unatakiwa kuwa mkweli kuhusu hilo na ikiwezekana ongea kwa sauti katika sehemu ambayo upo peke yako kwa kuorodha matukio ambayo yamendelea kukuandama katika maisha yako ya kila siku. Tafakari kwa nini matukio hayo yameendelea kuwa sehemu ya maisha yako (sababu zinazopelekea matukio hayo yatawale hisia zako). Weka mkakati wa kuachana na matukio kama hayo hata kama itahusisha kupoteza marafiki.
"NINATAMANI NINGEISHI MAISHA YA KUWA KARIBU NA WAPENDWA WANGU MUDA WOTE." Watu katika kundi hili walijutia kutokuwa na muda wa kutosha kwa ajili ya familia, ndugu na marafiki. Waliona maisha waliyochagua yalipelekea kupoteza mawasiliano ya marafiki muhimu kwao. Katika muda ambao wanapambana kwenye dakika za mwisho za uhai wao, wanatamani wangeweka bidii zaidi katika mawasiliano na wapendwa wao. Tunaweza kuwachukulia marafiki zetu kwa urahisi katika maisha ya sasa, lakini kumbuka, hatuwezi kuwa karibu nao kila wakati. Pia, hatuna uhakika kama wataendelea kuishi mpaka mwisho wa uhai wetu maana hakuna anayejua mwisho wake ni lini. Katika muda ambao upo mbali na wapendwa wako jaribu kutumia kila mbinu za mawasiliano kwa ajili ya kuonesha hisia zako kwao. Marafiki wana mchango mkubwa katika maisha maana kupitia wao tunashikamana na kufanikiwa kuzishinda changamoto za maisha. Maisha yanaweza maisha yanaweza kukutenga na marafiki zako kwa njia tofauti, lakini hakikisha unakuwa karibu nao.
"NINATAMANI
NINGEISHI MAISHA YA FURAHA." Ni kawaida watu wengi kufikiria kuwa
nguvu za nje zinadhibiti hisia zao, lakini ukweli ni kwamba ufunguo wa udhibiti
wa kila aina ya hisia upo ndani mwetu. Hatuwezi kuchagua kila tukio linalotokea
kwenye maisha yetu ya kila siku lakini tunao uwezo wa kuamua jinsi gani ya
kuitikia au kulichukulia tukio husika. Maisha yanaenda haraka sana, kwa nini
utumie muda mwingi kubeba kinyongo na malalamiko ya kila mara dhidi ya matukio
madogo madogo? Kuwa na furaha hakugharimu chochote, hukufanya uwe na afya
njema, hufanya maisha kuwa ya kuridhisha zaidi, huvutia uhusiano mzuri zaidi,
na kadhalika. Kwa hivyo, kutokuwa na furaha, basi, hugharimu ZAIDI mwishowe, na
inaweza hata kusababisha magonjwa makubwa. Afya yetu ya kiakili, kihisia, na ya
mwili hutegemea jinsi tunavyohitikia matukio ya kila siku kwenye maisha yetu. Kumbe,
ikiwa unataka kuanza kuishi maisha bora na yenye furaha sasa huna budi kubdilisha
mtazamo na mwitikio wa matukio unayokutana nayo kila mara.
Mwisho,
neno la tafakari ya leo ni mwendelezo wa mafundisho kuhusiana na majuto kutoka
watu wanaokaribia kukata roho. Majuto hayo yanagusa maisha yetu moja kwa moja
hivyo tunapata nafasi ya kuboresha maisha yetu ili kuepuka majuto ya aina hii
katika kipindi cha mwisho wa uhai wetu. Kumbuka,
mbegu ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii
niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika
Maisha yako.
PS: Ongeza maarifa yako kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
ππΎππΎππΎππΎππΎ
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com