Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku nyingine ikiwa
ni mwendelezo wa siku za maombolezo. Jana tumeshuhudia jinsi ambavyo kama taifa
tumeagana kimwili na mpendwa wetu shujaa wa Afrika, Hayati Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli. Ni tukio la huzuni kwa taifa hila limemalizika kwa heshima ya
kipekee. Tunaweza kulia na kuomboleza kwa kila namna lakini ukweli utabakia
kuwa Maisha ya Magufuli yalikuwa ni zawadi kwa Watanzania. Katika siku za uhai
wake kila siku alipigana vita japo hatukuwahi kutangaziwa kuwa nchi ipo vitani.
Tunapoagana na shujaa huyu wa Afrika kimwili tuna kila sababu ya kutambua kuwa “Mashujaa huwa hawafi bali wanalala katika usingizi mzito”. Mwili wao unaweza kuondoka lakini: KAULI zao zitaishi milele; MIFANO yao itaishi milele; HAMASA yao itaishi milele; ROHO itaishi ndani ya vizazi na vizazi; MATENDO yao yataishi milele. Tuna kila sababu ya kuomboleza kupotezana kimwili na shujaa huyu wa Afrika lakini katikati ya maomboelezo hayo tunatakiwa kumshukuru Mungu kwa shujaa kama huyu kuishi katika ardhi ya nchi yetu. Tuna kila sababu ya kuthamini kuwa tumepata fursa ya kujifunza mengi tena kwa mifano hai kutoka kwenye maono na matendo ya shujaa huyu mwenye ngozi nyeusi.
Kimwili umeondoka JPM lakini kiroho nakuona ukiwaambia Watanzania na Afrika kwa ujumla kuwa: “nimewachia kila kitu ambacho kitawawezesha kuishi Maisha ya yenye maendeleo halisi kulingana na rasilimali za nchi. Tanzania na Afrika kwa ujumla ni masikini kwa jina lakini kwa rasilimali, Afrika ni Tajiri kuliko mabara yote. Nimewaachia mifano halisi jinsi gani utajiri wa rasilimali unaweza kubadilishwa kuwa utajiri wa maendeleo ya nchi na watu wake”.
Kimwili umeondoka lakini naiona Roho yako ikisema “nitaendelea kufarijika ikiwa kila mmoja wenu ataendeleza vita dhidi ya UVIVU – natamani muendelee kuchapa kazi; NIDHAMU – kila mmoja aendeleze nidhamu ambayo nimewajengea kuanzia na nidhamu sehemu ya kazini; UADILIFU – kupitia uadilifu yote niliyoyaanzisha naamini yataendelezwa siku zote; KUJITEGEMEA – tupigane vita vyetu bila kutegemea kuwa kuna msaada kutoka nje maana kila msaada unaambatana na masharti yake; KUINUANA NINYI KWA NINYI – jengeni uchumi imara unaotegemea uchumi wa viwanda ambavyo vimejengwa na wawekezaji wa ndani na nje katika ardhi ya nchi yetu; IMANI – hakuna lisilowezekana ikiwa unaishi kwa Imani; RUSHWA – popote nilipo nitaendelea kufutwa machozi ya kuachana nanyi ikiwa kila mmoja ataendeleza mapambano dhidi ya rushwa maana nimewaonesheni mfano na hakikisha mnaendeleza vita hiyo”.
Kimwili umeondoka lakini ukweli unabakia kuwa umeondoka kwa faida maana Maandiko Matakatifu yanasema “Mpanzi alikwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akipanda hizo mbegu, nyingine zilianguka njiani na wapita njia wakazikanyaga na ndege wakazila. Nyingine zilianguka penye mawe na baada ya kuota zikanyauka kwa kukosa maji, nyingine ziliangauka kati ya miti na miiba, ile miti na miiba ilipoota ikazisonga. Nyingine zilianguka katika udongo mzuri zikaota na kuzaa matunda kwa asilimia mia…mwenye masikio na asikie” (Luka 8: 5 – 8). Kimwili imekubidi ufe ili uote na kuzaa matunda na matunda hayo yataendelea kuzaa matunda kizazi na kizazi.
Hakika Shujaa wa Afrika, mbegu yako imeota na kuzaa matunda kwa asilimia mia ndani ya ardhi ya Tanzania. Sasa ni jukumu letu kuhakikisha mbegu zilizozalishwa zinaendelea kuzaa matunda daima. Ni jukumu letu kama Watanzania kuishi kwa vitendo, kupitia mifano yako. Ni jukumu letu kuhakikisha maadui wakubwa wa rasilimali za taifa letu hafumbiwi macho na badala yake keki ya taifa itumike kwa manufaa ya Watanzania.
Mwisho,
hakika mashujaa huwa hawafii bali wanalala kimwili katika usingizi mzito, JPM
umelala katika usinginzi mzito wa kimwili lakini Roho yako inaendelea kuishi
katika mioyo ya Watanzania ambao uliyatoa sadaka Maisha yako kwa faida yao na
vizazi vijavyo. Kumbuka, mbegu ikidondoka
ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha
kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Ongeza maarifa yako kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com