NENO LA LEO (MACHI 14, 2021): JE HISTORIA, MILA, IMANI NA TAMADUNI VIMEATHIRI VIPI MAISHA YAKO?
Ni jumapili ambayo imejaa baraka zake Muumba,
kiasi ambacho tumewezeshwa kuwa hai kwa ajili ya kuendelea kumtumkia yeye. Kipekee
naamini unaendelea kuitumia siku hii kumtukuza Mungu kupitia yale unayofanya. Ikiwa
unayofanya kila siku yana muunganiko wa vitendo na vitendo hivyo vina mchango
katika kuliishi kusudi la maisha yako hakika una kila sababu ya kumshukuru
Mungu kwa siku ya leo.
Mwanadamu
ni kiumbe ambaye maisha yake mara nyingi yanatawaliwa na matukio ya yaliyopita.
Yapo matukio yaliyopita ambayo yanaweza kuwa na mchango chanya na mengine yana
mchango hasi katika maisha ya wakati uliopo na wakati ujao. Katika maisha yetu
ya kila siku wengi tumeendelea kuteswa na matukio ya historia bila ufahamu wetu
na wakati mwingine tunaishi katika fikra, mitazamo, mila na tamaduni zilizopitwa
na wakati. Karibu tujifunze kwa pamoja kuhusu matukio ya historia na athari
yake kwa maisha ya sasa:-
Katika jamii au familia watu huwa wana mila na tamaduni wanazoamini na mila hizo huwa zinapitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mila hizi zinajumuisha zile ambazo zinamuongoza mtoto kwenye namna ya kuwapenda wengine, kujithamini, kujiheshimu na kuwaheshimu wengine, namna ya kufanikiwa pamoja na kuwasaidia watu wanaomzunguka. Pia, zipo mila nyingine ambazo zinapelekea mtoto ashindwe kujiamini, awe mtu wa visasi, mchoyo, mwizi na mtundu.
Ikiwa unahitaji kuishi kulingana na kusudi la maisha yako huna budi kutambua mila ambazo zimekuwa zinakuzuia kusonga mbele. Mfano, yawezekana zipo nyakati unajiona unatengwa, zipo nyakati unajiona haupendwi, zipo nyakati unaona hakuna unalofanikisha, zipo nyakati unahisi wewe ni mtu wa kushindwa, zipo nyakati unahisi wewe ni kiwango flani cha maisha na hauwezi kuvuka ngazi hizo; au zipo nyakati unahisi wewe umeumbwa kuwa masikini. Vyote hivi vina uhusiano na historia ya maisha yako (malezi na makuzi).
Fanya tathimini inayolenga kujifunza kujifunza kuhusu Imani au mila zilizopo ndani ya ukoo wenu. Mfano, katika jamii zetu ni kawaida koo za kimasikini kuwa na mtazamo na kauli hasi dhidi ya koo tajiri. Wengi katika koo hizi utakuta wanakuambaia matajiri ni watu wabaya au wachoyo au free masoni. Kwa kauli kama hizo ni vigumu sana wanafamilia katika koo hizo kufanikiwa kifedha.
Unahitaji kusikiliza kutoka kwa ndugu zako pamoja na kuisikiliza sauti yako ya ndani ili utambue kauli ambazo zimekuwa zikikukwamisha kupiga hatua. Epuka kauli kama vile; “ni bora kuwa masikini kuliko kuwa tajiri maana matajiri hawana amani; sisi familia yetu huwa ni watu wa kukosa, wanaume/wanawake siyo wakuaminiwa; au mapenzi ni maumivu na mahusiano yanaumiza hivyo ni bora ya kuwa peke yangu”. Kumbuka maneno huwa yanaumba.
Jichunguze ni imani/mila zipi umeifadhi katika akili yako ya ndani (subconscious mind) ambazo zimekuwa zikikuzuia kusonga mbele. Mfano, inaaminika kwa watu wengi kuwa kuwa maisha ya furaha na heshima yanapatikana pale mtu anapokuwa na fedha nyingi; anamiliki magari na majumba; msomi wa juu sana na mengine mengi. Imani kama hizi zinaendelea kuwazuia wengi kuishi maisha ya furaha na heshima kwa vile wanajiona hawastahili maisha hayo kulingana na kiwango cha vitu wanavyomiliki.
Je
unahifadhi kumbukumbu na matukio ya sifa zipi? Mila/imani potofu zilizohifadhiwa
kwenye mfumo wako wa kumbukumbu zina athari katika maisha ya sasa na maisha ya
baadae. Binadamu ana mfumo wa kuhifadhi kumbukumbu kama ilivyo kompyuta hivyo
unachotakiwa kufanya baada ya kugundua imani/mila ambazo zimekukwamisha kwa
muda ni kuhakikisha unaondoa mila hizo kwenye mfumo wa kumbukumbu na nafasi
yake ukiijaza na imani/mila ambazo zitakuwezesha kusonga mbele.
Mwisho, kupitia Makala hii nimekushirikisha athari ya mila/tamaduni ambazo zimekuwa na athari hasi katika maisha yako. Kamwe husikubali maisha ya laana inayotokana na historia ya watangulizi wako. Kila kizazi kinaumbwa kuishi maisha ya kipekee ikilinganishwa na kizazi kilichotangulia. Tengeneza historia ya maisha yako kwa kwenda kinyume na imana, mila na kauli potofu ulizorithi kutoka kwa watangulizi wako. Kumbuka, mbegu ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
ππΎππΎππΎππΎππΎ
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com