Habari ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia
ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku ya saba kati ya siku 21 ambazo kama taifa
tunajumuika kwa pamoja kuomboleza kifo cha mpendwa wetu, Rais na Jemedari
Shujaa wa Afrika, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. Tukiwa katika kipindi hiki
cha maombolezo naendelea kukuletea mafundisho kuhusu kifo, huzuni na maombolezo
ili kwa pamoja tutumie kipindi hiki kwa ajili ya kutafakari kuhusu hatma ya maisha
yetu hapa Duniani. Katika neno la tafakari ya jana tuliona kuwa katika
uninadamu wetu ni kawaida kuhuzunika kutokana na vifo vya wapendwa wetu.
Je wajibu wetu katika kipindi cha maombolezo?
Kuna mambo mengi ambayo tunaweza kufanya ikiwa ni njia ya kusaidia wafiwa
kupita salama katika kipindi cha huzuni, maombolezo, na kufiwa. Uwepo wetu karibu na wafiwa kwa njia yoyote ile ni
muhimu sana na kunaleta mabadiliko na tumaini kubwa kwa wafiwa. Kama
taifa tupo kweye msiba, lakini kadri tunavyoona mataifa mengine yalivyoguswa na
msiba huu tunafarijika. Vivyo hivyo, familia ya Hayati Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli kadri inavyoona watu wengi kila kona wanalia inapata tumaini kuwa
mpendwa wao aliyatoa sadaka maisha yake kwa watu wenye shukrani.
Je imani yako inasema nini katika kipindi kama hiki cha maombolezo? Kwa wale Wakatoriki, Imani yetu ina mengi ya kutufundisha hasa kuhusiana na siri ya kifo, nyakati za kuelekea kufa na maombolezo. Kupitia Kanuni ya Imani tunakili kuwa kuna: “Ushirika wa Watakatifu, Maondoleo ya Dhambi, Ufufuko wa Miili na Uzima wa Milele”. Maneno haya katika kanuni ya Imani kwa Wakatoliki yana mengi ya kutufariji katika kipindi kama hiki cha maombolezo. Ni kupitia maneno hayo tunatakiwa kuwaombea dua njema wale waliokufa sambamba na kufahamu kuwa hata sisi ipo siku tutakufa. Pia, tunakumbushwa kuwa kwa pamoja na tunaungana (Watakatifu, Waliokufa na Waliopo Duniani) kupitia ushirika wa Watakatifu na kutukumbusha kuhusu kuwa kuna uzima milele ambao unatungojea.
Kipindi cha maombolezo ni kipindi cha kuonesha upendo wa dhati dhidi aliyekufa na wafiwa. Uwezo wetu wa kuombeana na kupeana salamu za rambirambi zinazoambatana na matoleo ni tendo la kuheshimiana, sio tu kwa kile tunachoweza kufanya kwa wale ambao wametutangulia, bali pia kutambua kuwa tunaungana nao kiroho katika makazi yao mapya kwa kuwa tunaungana katika ushirika mmoja.
Je tunaweza kusema nini juu ya ufufuo wa wafu? Katika mafundisho mengi ya imani tunatafundishwa kuwa
nafsi/roho kamwe haifi bali kinachokufa ni mwili. Je ni kweli kuwa mwili huu
ambao tunao hapa Duniani utafufuliwa siku ya mwisho? Hilo ndilo fumbo la imani ambalo mimi na wewe
tumefumbwa. Kwa imani tunaamini kuna ufufuo na ikiwa ufufuo huo upo maana yake kuna
uzima wa milele baada ya kifo. Kwa imani hili ni fumbo ambalo linatupa faraja katika
kipindi cha maombolezo kwa kunaamini ipo siku tutakuja kukutana na wapendwa
wetu waliotangulia katika Maisha mengine baada ya Maisha haya.
Mwisho, kupitia neno
la tafakari ya leo tumeendelea na mafundisho yanayoendana na kippindi hiki cha
maombolezo. Lengo la mafundisho haya ni kukumbusha kutumia kipindi hiki kwa
ajili ya kutafakari upya maisha yako. Mimi na wewe hatujia siku wala saa lakini
tunachojua ni kwamba ipo siku tuyaacha maisha haya ya hapa Duniani. Katika kila
tunachofanya tuendelee kutambua kuwa yale tunayojihusisha nayo yana mchango
mkubwa katika kuamua aina ya kifo chetu na maombolezo kwa wanaobakia. Kumbuka,
mbegu ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu
hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi
katika Maisha yako.
PS: Ongeza maarifa yako kupitia usomaji wa
vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha
hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs.
3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
BORN TO WIN ~
DREAM BIG
Mawasiliano: 0763
745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com