Habari ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni matumaini yangu kuwa umeamka salama na upo tayari kuendelea na majukumu yako katika siku ya leo. Leo ni siku 14 kati ya siku 21 za maombolezo ya kifo cha mpendwa wetu, shujaa wa Afrika, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Kama bado hujajiunga na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la tafakari kila siku, tafadhali JIUNGE SASA.
Katika neno la
tafakari ya leo nitakushirikisha sehemu ya mwisho ya majuto kwa watu
wanaokaribia kukata roho. Masomo haya kama nilivyodokeza katika sehemu
zilizotangulia ni maalum kwa ajili ya kukuimarisha katika kukabiliana na kifo
sambamba na kuishi maisha ambayo yatakuwezesha kufa kifo bora. Kifo ni kifo,
lakini kila mmoja anatamani baada ya kifo apate kuacha alama kutokana na
matendo yake katika kipindi cha muda mfupi wa uhai wake. Karibu tuendelee
kujifunza:-
"NINATAMANI
NISINGECHUKULIA POA UHAI WANGU.” Ni kawaida katika maisha yetu ya kila
siku kutokuona thamani ya uhai wetu katika maisha ya kila siku. Kila siku
tunaishi kana kwamba tuna tiketi mkononi kwa ajili ya maisha ya kesho. Pia,
wengi wetu tunachukulia poa kila kinachotuzunguka katika mazingira tunayoishi
pasipo kuona umuhimu au thamani ya vyote vinavyounda mazingira yetu. Mfano,
nyuki wanachavusha mimea kwa ajili ya uendelevu wa vyakula tunavyokula – ni
wangapi wanaoona thamani ya wadudu wa aina hiyo? Mimea inatupatia chakula,
dawa, kivuli, hewa safi ya Oksijeni kwa ajili mwili kupata nguvu, inalinda
vyanzo vya maji na kuvuta mvua kwa ajili ya kuendelea kupata mazao na miili
yetu kupata maji ya kunywa – lakini ni wangapi wanaoona thamani ya mimea hiyo
katika maisha yao ya kila siku? Kumbe, pamoja na kwamba kila siku tunabanwa na
majukumu tuna kila sababu ya kusema asante kwa mengi ambayo yamewezesha
tuendelee kuishi katika uso wa dunia hii. Hata kama huna mengi maishani,
unaweza angalau kusema shukrani yako kwa kuwa na misingi ambayo ulimwengu
hukupa.
SOMA: MAJUTO KWA WANAOKARIBIA KUKATA ROHO – SEHEMU YA TATU.
"NINATAMANI
NINGEPATA MUDA KIDOGO WA KUREKEBISHA MAKOSA NILIYOFANYA."
Katika nyakati za kukaribia kukata roho watu wengi wanatamani kama ingewezekana
kifo kihairishwe na wapewe angalau muda kidogo kwa ajili ya kurekebisha sehemu
ambazo wamekosea. Nyakati ya kusubiria kukata roho, mhusika anapata nafasi ya
kuangazia maisha yake katika kipindi cha uhai wake. Hapa ndipo anagundua yapo
mengi ambayo alikimbizana nayo hila angepata muda wa kuishi tena hasingeweza
kukimbizana nayo. Pia, katika tathimini ya maisha yake anaona kuna mengi ambayo
anaacha kabla ya kukamilika japo ikiwa angepata muda wa kuishi zaidi angetamani
kukamilisha vipaumbele hivyo. Katika muda kama huo mhusika anaangazia watu
ambao angetamani kuwa nao karibu zaidi na wale ambao angetamani kuwa mbali nao
kwa ajili ya ukamilifu wa maisha ambayo kwa wakati anaona yangekuwa maisha
yenye tija.
"NINATAMANI NINGEISHI KULINGANA NA WAKATI ULIOPO." Mara nyingi watu tunashindwa kuishi kulingana na wakati uliopo hali inayopelekea kutoyafurahia maisha. Yapo matukio yaliyowahi kutokea katika maisha yetu na yanaendelea kutuumiza katika maisha ya sasa. Pia, yapo matukio au nyakati ambazo zilikuwa za neema katika historia ya maisha yetu na tunatamani matukio hayo yawe sehemu ya maisha ya sasa lakini haiwezekani tena. Mbaya zaidi ni pale ambapo tunashindwa kufurahia maisha ya sasa kwa kutegemea kuwa huko mbeleni kuna maisha mazuri zaidi ya haya. Mfano, tunafikiria kuwa tutaishi maisha yenye furaha ikiwa tutafanikiwa kupata vitu flani katika maisha yetu. Hali hii kwa ujumla wake inapelekea tunashindwa kufurahia maisha wa wakati uliopo na mwisho wake hakuna siku ambayo tunayafurahia maisha. Wengi wameishi maisha hayo lakini katika kufikia ukomo wa maisha yao wakagundua kuwa walikuwa wanapoteza muda kwa maana yale waliyokimbizana nayo kipindi chote cha maisha yao hayakuweza kukidhi hitaji halisi la maisha waliyokusudia.
“NINATAMANI NINGEWEZA KUTAMBUA NA KUONESHA UBUNIFU WANGU.” Ubunifu ni zawadi ambayo kila mmoja amerithishwa toka alipoumbwa. Hata hivyo, ni wachache sana ambao wanafanikiwa kutumia hazina hii iliyopo ndani mwao kwa maana wengi wanaishi kwa mazoea katika jamii waliyopo. Unapofanikiwa kuwa mbunifu wa vitu mbalimbali hakika roho yako inafurahi kila mara unapoangalia kazi ambazo ni matunda ya ubunifu wako. Ikiwa umefanikiwa kutumia hazina ya ubunifu uliyopewa toka enzi za kuumbwa kwako, baada ya maisha haya utaacha ukumbusho halisi wa maisha yako kutokana shughuli au matendo uliyofanya. Yote hayo yatathiminiwa na familia yako, wafuasi wako au jamii kwa ujumla.
“NATAMANI
NINGEPONYA UHUSIANO ULIOVUNJIKA.” Kuwa sehemu ya upatinisho na kuishi
maisha ya msamaha ni jambo la heri na hekima katika jamii. Walakini, wengi
wanaishi maisha ya kuchonganisha na kubeba vinyongo katika roho zao. Hakuna haja
ya kuendelea kushikilia ugomvi au makosa uliyotendewa katika maisha ya sasa
maana kuendelea kufanya hivyo unajiumiza mwenyewe. Ikiwa umemkosea mtu kuwa
mwepesi wa kusema “naomba unisamehe” na ikiwa kuna mtu amekukosea kuwa tayari kusamehe
hata husipoombwa samahani. Kuwa sehemu
ya mazungumzo yanayotafuta suruhisho badala ya kungangania kutafuta mkosaji ni
nani.
Mwisho,
neno la tafakari ya leo ni sehemu ya mwisho wa mafundisho kuhusiana na majuto
kutoka watu wanaokaribia kukata roho. Ni matumaini yangu kuwa sehemu hizi zote
zimekufundisha maarifa muhimu katika maisha yako ya kila siku. Kumbuka, mbegu
ikidondoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii
niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika
Maisha yako.
PS: Ongeza maarifa yako kupitia usomaji wa
vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha
hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs.
3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
ππΎππΎππΎππΎππΎ
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu
Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com