Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa upo vizuri na mapambano
yanazidi kushika kasi katika kipindi hiki ambacho tumeianza robo ya pili ya
mwaka 2017. Naamini mpaka sasa umejifanyia tathimini kwa yale ambayo ulilenga
kuyafanya katika mwaka huu na kuona maendeleo yako katika kipindi cha robo ya
kwanza. Basi wiki hii ikiwa ni wiki ya kumi na tatu tokea nianze kukushirikisha
uchambuzi wa kitabu kimoja kila wiki ni matarajio yangu kuwa uchambuzi wa
vitabu hivi umekusaidia kubadilisha maisha yako kwa kiasi flani.
Kama mpaka sasa haujafanikiwa kujifunza
kitu chochote katika makala hizi za uchambuzi wa vitabu nakushauri ni vyema
husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye mambo ambayo umeyazoea.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba uchambuzi wa vitabu kupitia mtandao wa
fikra za kitajiri unalenga uwasaidie wale wenye kiu ya kubadilisha maisha yao
kwa kusoma vitabu na makala mbalimbali.
Kujiunga na mtandao wa fikra za
kitajiri BONYEZA HAPA na
ujaze fomu ili uendelee kunufaika na mwaliko huu ambao unakulenga wewe mwenye
kiu ya kutimiza ndoto za maisha yako. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata
makala za mtandao wa fikra za kitajiri moja kwa moja kwenye barua pepe yako.
Kitabu
cha wiki hii ni “Zero to One” kutoka kwa mwandishi Peter Thiel. Mwandishi wa
kitabu hiki ni mjasiliamali na mwekezaji kwenye teknolojia ya
mtandao. Peter Thiel ametumia kitabu hiki kutushirikisha jinsi ya kuanzisha na
kukuza biashara yako hasa kwa kutanguliza ubunifu kuliko kutanguliza kigezo cha
mtaji. Naamini wengi wetu tumeshindwa kuanzisha biashara kwa kutanguliza upungufu
wa mtaji na hivyo kushindwa kusonga mbele zaidi.
Kupitia
kitabu hiki utajifunza namna bora ya kuepuka changamoto kwa kuhakikisha unakuwa
na hulka ya ubunifu badala ya kukopi kutoka kwa yale ambayo tayari watu
wamefanya. Mwandishi anatushirikisha kuwa unapogundua kitu kipya moja kwa moja
unatoka kwenye hatua ya sifuri kwenda kwenye hatua ya moja na unapoiga au kuboresha kitu unatoka hatua ya moja kwenda namba nyingine.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki:
1. Hakuna
mtu mwenye kujua kesho itakuwaje lakini wote tunakubaliana na ukweli kwamba ulimwengu
wa kesho utakuwa wa tofauti na ulimwengu wa leo na msingi wa utofauti huu
unatokana na ulimwengu wa leo. Mwandishi anatushirikisha kuwa kwa kukopi vitu
vilivyopo kwa sasa ni rahisi kutabiri ulimwengu wa kesho utakuwaje kwa kuwa
tayari vitu vipo na tunavifahamu lakini kwa kuvumbua vitu vipya ni vigumu
kutabiri ulimwengu wa kesho kutokana na ukweli kwamba vitu hivyo hatujui
vitakuwa na sura ipi. Na kama unataka kuwa wa tofauti ni lazima ujipinde
kuhakikisha unaleta vitu vipya na hatimaye ufanikiwe kutoka kwenye sifuri
kwenda moja.
2. Kuendelea
kuongeza utajiri kwa kutumia njia za utandawazi na teknolojia zilizopo kwa sasa ni lazima
utafikia sehemu ambapo uharibifu utakuwa mkubwa sana, mfano, mdogo ni athari za
mabadiliko ya tabia nchi. Ni lazima tuwe tayari kuvumbua teknolojia mpya ambazo
zitakuwa na athari ndogo kwa viumbe na mazingira kwa ujumla.
3. Ili
kugundua vitu vipya ni lazima kujenga utamaduni wa kufikiria nje ya boksi. Katika
jamii watu wengi wanaishi kwa mazoea ya maisha ya watangulizi wao. Mwandishi anatushirkisha
kuwa katika ulimwengu wa uvumbuzi ni lazima kujenga utamaduni wa kufikiria kwa mapana
zaidi ili kupata mbadala wa teknolojia zilizopo kwa sasa.
4. Tumia
historia ya matukio yaliyopita kwa ajili ya kutabiri matukio ya ulimwengu wa
kesho. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili kufanikiwa kwenye ulimwengu wa
kugundua teknolojia mpya ni lazima uepuke kurudia makosa ya nyuma. Hii itakusaidia
kujitofautisha na watu wanaokimbilia teknolojia mpya na hivyo kukujengea msingi
imara wa maisha yako katika ulimwengu wa kesho.
5. Tengeneza
biashara au Kampuni ambayo inatoa huduma/bidhaa zenye utofauti na biashara
zilizopo sokoni. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni rahisii kutabiri mafanikio
ya bidhaa au huduma zako kwenye soko kama zipo tofauti na bidhaa/huduma
zinazotolewa na watu wengine na hivyo kupata mauzo makubwa. Kinyume chake ni
kwamba kama unafanya vitu ambavyo kila mtu anafanya itabidi usubirie upepo wa
soko ndo uamue mwenendo wa mauzo yako. Pia, kwa kujitofautisha na wengine
itakuwa rahisi kupenya kwenye soko kwa vile hauna wapinzani.
6. Lenga
kuwa bepari (capitalist) kwa kuvumbua bidhaa/huduma zenye wigo mpana wa
machaguo kwa wateja wako. Wape wateja kitu wanapenda kila siku wakilinganisha
na bidhaa/huduma nyingine zilizopo sokoni. Mwandishi anatushirikisha kuwa
mabepari si wema tu kwenye jamii bali wana mchango mkubwa wa kuibadilisha dunia
kuwa mahala pema pa kuishi kwa viumbe vilivyopo na vijavyo. Mwandishi anatolea
mifano ya kampuni ya Google na Apple kama baadhi ya makampuni ambayo yana
misingi ya kibepari japo michango ya kampuni hizi kwenye ulimwengu wa sasa inajipambanua
vizuri kwa kila mtu.
7. Ubepari
wenye ubunifu ni zawadi kwa jamii lakini pia ni tunu kwa mgunduzi. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba unapogundua teknolojia mpya ni lazima ilete
huduma/bidhaa mpya kwenye jamii. Bidhaa/huduma hii ni lazima iwe bora
ikilinganishwa na zilizopo hivyo jamii itafaidika kwa matumizi ya teknolojia
hii huku mgunduzi akiendelea kupata faida.
8. Ushindani
kwenye soko ni chanzo cha kukandamiza fikra za ubunifu mpya wa teknolojia. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba jamii ipo tayari kufanya vitu ambavyo ni rahisi na
tayari vipo machoni kwa walio wengi kuliko kuwekeza jitihada nyingi kwenye ubunifu
mpya. Unaweza kuthibitisha hili kwa kuangalia biashara nyingi zinazoanzishwa
katika mtaa mmoja; ni wazi utaona kuwa kuna mwanzilishi na walioiga biashara
yake. Matokeo yake ni kwamba mtaa mzima una biashara za aina moja na mwisho
wake ni kufilisika kwa walio wengi hasa wanaoiga wengine.
9. Mfumo
wa elimu na tamaduni zilizopo zinawaandaa wahitimu kulelekea kwenye ushindani
kuliko ubunifu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba jamii imefundishwa kuheshimu
wale wanaofanya vizuri hasa darasani na kubeza wanaojikongoja. Matokeo yake ni
kwamba wahitimu nao wamemezwa kwenye mfumo huu kiasi kwamba badala ya kusoma
kutafuta maarifa wanasoma kutafuta kazi za kitaaluma. Kazi hizi zinapelekea mtu
kuishi maisha ya taaluma yake miaka yote badala ya kuwa na ubunifu katika
mazingira yanayomzunguka.
10. Kuporomoka kwa makampuni yaliyo mengi
ni matokeo ya upinzani wa kibiashara. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri
kampuni moja inavyopambana na kampuni nyingine kwenye huduma wanazotoa matokeo
yake ni kupolomoka kwa mauzo ya bidhaa/huduma za kampuni zote mbili. Kupolomoka kwa
kampuni hizi ni matokeo ya kuzalisha/kutoa bidhaa/huduma zenye ubora
unaokaribiana na na hivyo hatima yake ni kutoa nafasi kwa kampuni mpya kuibuka.
11. Thamani ya biashara si tu kiwango cha
pesa inayotengenezwa kwa sasa bali ni uimara wa biashara husika katika
ulimwengu wa kesho. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa unapoanzisha biashara
unatakiwa ufikirie zaidi jinsi ambavyo biashara hiyo itakuwa endelevu katika
siku za usoni kwa kuzingatia changamoto za wapinzania wakaojitokeza. Hapa unatakiwa
kukumbuka kuwa ili biashara iweze kuzalisha faida kwa muda mrefu ni lazima iwe
inaweza kukua na kuimili changamoto kwenye soko.
12. Tengeneza biashara yenye utamaduni
ambao unaifanya iwe na ubora zaidi ya mara kumi ya ule uliopo sokoni. Mwandishi
anatushauri kuwa njia pekee ya kufanya vizuri kwa muda mrefu ni kuhakikisha
biashara yako inatoa bidhaa/huduma zenye ubora wa hali ya juu ukilinganisha na
biashara nyingine zilizopo kwa wakati huo.
13. Anzisha biashara ambayo inaweza
kutanuka kwa wepesi kupitia teknolojia ya mtandao. Ulimwengu wa sasa mtandao wa
intaneti umekuwa ndio kila kitu kama unataka kuwafikia watu wengi zaidi. Hapa mwandishi
anatushirikisha kuwa ni rahisi kuwa tajiri kutoka kwenye wazo dogo la software
kama unaweza kuingiza software yako kwa wateja na ikawa na uwezo wa kutanuka
zaidi kwa kutegemea mahitaji ya wateja.
14. Anza kidogo, kuza biashara na tanua
biashara yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa ubunifu wa kibepari ni lazima
uzingatie misingi ya kuanza kidogo na hatimaye kuweza kupenya soko kwa hustadi
wa hali ya juu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba pindi unaanza ni rahisi
kutawala soko dogo ikilinganishwa na soko kubwa. Hapa anatushirikisha
mwanzilishi wa facebook alivyoanzisha mtandao huu akiwa na lengo la
kuwakutanisha wanafunzi wenzake. Lakini mpaka sasa facebook ni mtandao wa
kijamii ambao unaoongoza kuwa na watumiaji wengi duniani.
15. Mafanikio hayaji kama ajali bali
yanakuja kwa kufuata misingi na kanuni ambazo zipo wazi kwa kila mtu. Mwandishi anatushirikisha
kuwa ni muhimu kila mmoja kuona suala la mafanikio kuwa ni matokeo ya “vitendo
na athari zake”. Kwa kutumia kanuni hii kila mmoja anapaswa kutambua kuwa mafanikio
yake yatatokana na athari za vitendo vyake katika maisha yake ya kila siku. Kwa
kifupi ni kwamba ili uvune ni lazima uwe umepanda mbegu na si vinginevyo na
baada ya kupanda kiwango cha mavuno yako kitategemea bidii na uvumilivu wako
katika kutunza miche shambani mwako.
16. Kila mwenye nacho ataongezewa na
hasiyekuwa nacho atanyanganywa hata hicho kidogo alichonacho – sehemu ya
mafundisho ya Bwana Yesu Kristu. Hii ni sheria ya asili ambayo hata
mwanafizikia Albert Einsten aliiweka sawa kupitia mahesabu ya aljebra ambayo
kiuchumi tunapata hesabu za kuongezeka kwa riba kwa muda (compound interest). Mwandishi
anatumia sheria hii ya asili kuelezea kuwa pesa inatengeneza pesa na hivyo ni
wajibu wetu kuhakikisha tunatumia pesa kidogo tulizonazo kuzalisha pesa zaidi. Kwa
ufupi ni kwamba pesa inaongezeka thamani na kukutuza wewe kama unaweza kuitumia
kimahesabu zaidi.
17. Fanya maamuzi ya uwekezaji wa fedha
zako kwa ufasaha zaidi ili kuepuka kupoteza fedha zako. Mwandishi anatukumbusha
kuwa maamuzi ya uwekezaji kwenye biashara mpya ni muhimu yafanywe kwa umakini kwa
kuzingatia taarifa sahihi na kwa muda muhafaka. Pia, anatushirikisha umuhimu wa
kutokuweka mayai yote kwenye kapu moja kwani kwa kufanya hivyo ni rahisi
kupoteza fedha zako kwa wakati mmoja.
18. Mambo
ambayo bado ni siri kwa wanadamu katika ulimwengu huu ni mengi mno kiasi ambacho kila mtu
anaweza kugundua siri yake. Mwandishi anatushirikisha kuwa jamii ya sasa imekaa
katika hali ya kuridhika kuwa hakuna jipya la kugundua kwa vile kila kitu
tayari kimegunduliwa. Mwandishi anatuonesha kuwa huu ni uongo kwani bado yapo
mengi ambayo hayajafanyiwa kazi na hivyo ni wajibu wetu kufikiria zaidi kwa
ajili ya kuja na uvumbuzi mpya kwani kuna mengi ya kugundua katika tasnia ya
madawa, uhandisi, sayansi na teknolojia za kila aina.
19. Uendelevu wa biashara unategemea msingi
wake tokea mwanzilishi anapoianzisha kampuni yake. Kama kampuni haina msingi
imara wa kibiashara ni vigumu kufanya vizuri katika soko. Hivyo unapoanzisha
biashara yako hakikisha unakuwa makini kwenye watu ambao utawaajiri au wale unaoingia
nao ubia kwa ajili ya kuanzisha biashara yako.
20. Ajira mpya kwenye biashara yako ni
muhimu kuhakikisha unafanya usahili wa kina kwa ajili ya kuwapata watu makini. Mwandishi
anatushirikisha kuwa ni rahisi kupoteza biashara uliyoijenga kwa muda mrefu
kama haupo makini kwa waajiriwa wapya. Pia, unatakiwa kufanya tathimini ya kina
juu ya ushauri unaopewa na washauri waelekezi kwenye masuala mbalimbali yanaohusu
maendeleo ya kampuni yako.
Haya ni machache ambayo nimeweza kukushirikisha
kati ya mengi niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com