Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 37 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako
kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu
zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha
kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu vya maarifa mbalimbali. Ni matarajio
yangu kuwa muda ninaotumia kushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada
mkubwa kwako katika kubadilisha maisha yako. Hata hivyo, mtandao huu bado
unahitaji maoni/ushauri au shuhuda kwa namna ambavyo umekuwa wa msaada kwako au
namna ambavyo unahitaji makala hizi ziboreshwe zaidi (tuma
maoni/ushauri/ushuhuda wako kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com).
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “How the Stock
Markets Works” kutoka
kwa Profesa Ramon P. De Gennaro wa Chuo Kikuu cha Tennessee, Knoxville. Hapa
tunashirikishwa mwongozo wa kufahamu namna ambavyo Soko la Hisa linafanya kazi
kwa ajili ya kila mmoja wetu kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji kwenye hisa za
kampuni mbalimbali.
Linapokuja
suala la ukwezaji kwenye hisa ni wachache sana hasa kwa vijana ambao wanafahamu
uwekezaji huu. Pia, vijana wengi hawavutiwi na uwekezaji wa hisa kwa vile walio
wengi wanataka utajiri wa haraka. Uwekezaji wa hisa unabadirika kila wakati na
hivyo ni uwekezaji ambao kabla ya kuwekeza unahitaji kufahamu mabadiliko ya
namna hiyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba soko la hisa linaendeshwa na hisia
za wanunuaji pamoja na wauzaji wa hisa.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:
1. Unapoamua kununua au kuuza hisa
fanya hivyo kwa dhana ya kuwa bei ya wakati huo ni halisi kwa maana ya kwamba
hisa husika haiuzwi kwa bei ya juu/chini kuliko thamani yake. Hata hivyo, unahitaji
kukumbuka kuwa hata kama bei ni halisi bado bei hiyo si ya uhakika kwani
inaweza kubadilika ndani ya masaa au siku. Na hii ndio itathibitisha kuwa bei
husika ilikuwa/haikuwa halisi. Na hivyo uwekezaji wa hisa ni biashara ambayo
muhusika ni lazima awe tayari kubeba hatari (risk) kwani hakuna ambaye anajua
bei ya hisa za kampuni fulani zikuwa na thamani gani siku zijazo.
2. Pia katika uwekezaji wa mtaji unahitaji kufahamu
uwekezaji kwenye dhamana. Kwa kifupi moja ya tofauti kati ya hisa na dhamana,
dhamana zinauzwa kwa makubaliano maalumu katika kipindi cha muda maalumu (muda
wa kuiva dhamana). Zipo dhamana za muda mfupi, muda wa kati na dhamana za muda
mrefu. Katika uwekezaji wa dhamana, mwekazaji ananufaika na ongezeko la thamani
ambalo ulipwa kwa pamoja na mtaji uliowekezwa baada ya muda kuisha wa dhamana
alizonunua. Hapa unahitaji kutambua kuwa katika uwekezaji wa dhamana mwekezaji
anakuwa na uhakika wa kupata faida pamoja na mtaji wake aliowekeza mara baada ya
kuiva kwa dhamana husika.
3. Unapowekeza
kwenye hisa unategemea kufaidika kupitia ongezeko la thamani ya hisa za kampuni
husika pamoja na gawio kwa wanahisa kulingana na idadi ya hisa zako. Hapa
unahitaji kujifunza vitu viwili; moja, kama thamani ya hisa za kampuni husika
itashuka basi na wewe utegemee kupata hasara kwenye uwekezaji wako (mtaji) na
endapo thamani ya hisa ikiongezeka ndivyo na wewe mtaji wako utaogezeka. Mbili,
gawio la kila mwaka linakokotolewa kulingana na faida iliyotengenezwa na
kampuni katika kipindi husika. Kama kampuni imepata hasara ndani ya kipindi
husika tegemea kupata gawio kidogo. Hizi pia ni tofauti nzuri kati ya uwekezaji
wa kwenye hisa na dhamana kwani uwekezaji wa kwenye dhamana hautegemei faida
iliyotengenezwa au kupanda na kushuka kwa thamani kama ilivyo kwenye hisa.
4. Gawio
linaweza kulipwa kwa mfumo wa hisa au kwa mfumo wa pesa taslimu kulingana na
utaratibu wa kampuni husika. Hii ina maana kwamba kama kampuni inalipa gawio
kwa mfumo wa hisa wawekezaji wanategemea idadi ya hisa zao kuongezeka kila
mwaka kwa kutegemea faida iliyotengenezwa na kampuni husika katika kipindi
hicho. Na pale kampuni inapotoa gawio kwa mfumo wa fedha taslimu maana yake ni
kwamba idadi ya hisa za wawekezaji inaendelea kuwa ile ile kama hawajanunua
hisa zaidi ndani ya kipindi husika na gawio lao hulipwa moja kwa moja kwenye
akaunti zao au kwa cheki kila mwaka kulingana na faida iliyotengenezwa.
5. Kwa
ujumla tunakiwa kujifunza kuwa hisa na dhamana ni mfumo unaowezesha wamiliki wa
kampuni husika kugawana mali zinazomilikiwa na kampuni husika au mali
zinazozalishwa na kampuni husika ndani ya kipidi husika. Ugawanaji wa mali hizi
unategemea na kiasi ulichowekeza kwenye kampuni husika na hivyo kwa maana
nyingie uvuna kulingana na ulichopanda.
6. Je
soko la hisa ni nini? Kama ambavyo tunafahamu kuwa soko sehemu inayounganisha
watu zaidi ya mmoja kwa ajili ya kufanya biashara aidha ana kwa ana au kwa
kuunganishwa na mtandao wa internet, pia soko la hisa lina maana hii kwa kuwa ni
mtandao wa kifedha unaowaunganisha watu kwa ajili ya kuuza au kununua umiliki
wa hisa au dhamana. Soko hili linafanya kazi sawa na masoko mengine kwa maana
misingi muhimu ya masoko kama vile ushindani kwenye soko. Hii ina maana kwamba
kama unauza hisa zako unahitaji wateja makini wa kununu hisa zako na kama
unanunua unahitaji wauzaji wa makini wa kuuza hisa/dhamana.
7. Msingi
mwingine wa soko la hisa ni idadi ya kampuni zinazouza hisa zake kwenye soko
husika. Kama ilivyo kwenye masoko mengine, bei nzuri ya bidhaa Y inategemea na
idadi ya watu wanaouza au kuzalisha bidhaa Y kwenye soko husika. Kadri wauzaji
wa bidhaa Y wanavyokuwa wachache ndivyo bei ya bidhaa hii itapangwa kulingana
na mapenzi ya muuzaji na watumiaji watatokosa uchaguzi zaidi ya kununua bidhaa
Y hata kama bei ipo juu. Ndivyo ilivyo kwenye soko la hisa ili kuondoa tabia ya
kampuni moja kuhodhi (kumiliki) soko ni lazima makampuni mapya kwenye soko yawe
yanaongezeka mara kwa mara na hivyo kuleta ushindani kwenye soko la hisa.
8. Katika
masoko ya hisa taarifa ni muhimu kwa wawekezaji wapya. Kabla ya kuamua kununua
hisa unahitaji kufanya tafiti za ni kampuni zipi hisa zake zimekuwa zikifanya
vyema kwenye soko kwa muda mrefu. Hii ni tofauti ni kwenye masoko ya bidhaa
nyingine kama gari. Mfano, kama unahitaji kununua gari ambalo lilishatumika
hauwezi kufahamu matatizo ya gari husika mpaka pale utakapokuwa umenunue. Na
hii inafanya wanunuaji kushusha bei ya bidhaa husika wakidhani kuwa pengine
bidhaa hiyo inaweza kuwa na mapungufu. Kwenye soko la hisa hii ni tofauti kwani
kuna kampuni nyingi na kila moja ina maelfu ya hisa inazouza zenye thamani
sawa. Wajibu wako ni kuchagua kampuni ipi ambayo itakuwezesha kupata faida
nzuri kulingana na kiasi ulichowekeza.
9. Soko
la hisa linafanya kazi chini ya aina mbili ambazo ni soko la awali/msingi na soko la upili (secondary stock market).
Katika soko la awali wamiliki wa kampuni wanakuwa na lengo la kuongeza mtaji
wao na hivyo wanaweka hisa mpya katika soko kwa ajili ya kupata wamiliki wapya.
Katika soko la upili ni kwamba wamiliki wanaomiliki hisa zao wanaamua kuuza
hisa au sehemu ya hisa zao kwa ajili ya kupata fedha. Suala ya kujifunza hapa
ni kwamba katika soko la awali fedha za mauzo ya hisa zinakwenda moja kwa moja
kwa mmiliki wa kampuni wakati katika soko la upili umiliki unahama kutoka kwa
mtu mmoja kwenye mwingine kulingana na idadi ya hisa alizouza. Anachofanya
mmiliki wa kampuni ni kuhamisha idadi ya hisa zilizouzwa kutoka kwa mmiliki wa
awali kwenda kwa mmiliki mpya.
10. Wekeza kwenye hisa ukiwa na malengo ya
muda mrefu. Mwandishi anatushirikisha kuwa uwekezaji wa hisa sio aina ya
uwekezaji ambao utawekeza leo na kesho ukaamka tajiri. Kama unahitaji utajiri
wa haraka basi tambua kuwa aina hii ya uwekezaji haitokufaa kwani inahitaji
muda kwa ajili ya kuvuna kwa faida kile ambacho umewekeza.
11. Thamani ya hisa ipatikana/kutambuliwa
kwa kuangalia vitu vitatu; moja, kiasi cha fedha ambacho unategemea kutengeneza
kutoka kwenye hisa husika (kadri kiasi cha fedha kinavyokuwa juu ndivyo na
thamani ya hisa inakuwa juu). Mbili, ni kwa muda gani unatakiwa kusubiri kwa
ajili ya kupata fedha tarajiwa katika hisa zako (kadri unavyotakiwa kusubiri
kwa muda mrefu kupata fedha tarajiwa ndivyo na thamani ya hisa inakuwa chini na
kinyume chake ni sahihi). Tatu, kiwango cha riba katika muda unaotakiwa kusubiri
kwa ajili ya kupata fedha tarajiwa kutoka kwenye uwekezaji wako (kadri kiwango
cha riba kinavyokuwa juu ndivyo na thamani ya hisa inavyokuwa chini na kinyume
chake ni sahihi).
12. Katika soko la hisa ni vigumu sana
kusema kuwa umefanya dili la maana au baya kibiashara. Hii ni kutokana na
ukweli kwamba ni vigumu kutabiri thamani ya hisa za kampuni husika kwa siku
zijazo. Hisa zinazouzwa kwa thamani leo hii kesho unaweza kushangaa zinashuka
thamani kwenye soko la hisa. Hapa ndipo utangundua kuwa unapowekeza kwenye hisa
ni lazima uwe tayari kubeba hatari za kiuwekezaji (investment risks).
13. Ni busara kuwekeza kwenye hisa za
kampuni zinazotofautiana kibiashara kuliko kuwekeza fedha zako zote kwenye
kampuni moja (diversification). Mwandishi anatushirikisha kuwa kuwekeza kwenye
kampuni moja kunaweza kupelekea kupoteza sehemu ya uwekezaji wako pale ambapo
kampuni husika zitafanya vibaya kwenye soko. Muhimu, unahitaji kufanya uchaguzi
wa kampuni za kuwekeza ili kama kampuni moja hisa zake zitashuka thamani basi
unaweza kufaidika kupitia kwenye kampuni nyingine ambayo hisa zake zina thamani
kwenye soko kwa kipindi hicho.
14. Kiasi cha fedha ambacho unaweza
kutengeneza kupitia uwekezaji wa hisa kinategeme vitu vitatu, moja, kiasi cha
fedha ulichowekeza; mbili, kiwango cha riba ambacho ndicho kitaamua gawio lako;
na muda ambao utaendelea kudumu na hisa zako. Kwa ufupi hii ndio siri ya
uwekezaji wa aina yoyote ile ambayo matajiri wengi wanaitumia kwa ajili ya
kutengeneza pesa zaidi. Siri hii ni sawa na msemo wa wachina kuwa “muda mzuri kwako wa kufanya maamuzi ya
kupanda miti ilikuwa pindi ukiwa na miaka 15 na muda bora zaidi wa kufanya
maamuzi hayo ni sasa”. Msemo huu unatuambia kuwa katika uwekezaji hakuna
kauli ya nilishachelewa kufanya maamuzi – muda wowote katika umri wowote ni
nyakati sahihi za kufanya maamuzi ya uwekezaji.
15. Taarifa sahihi juu ya kampuni ipi
uwekeze fedha zako ni muhimu kuliko kitu chochote kabla ya kutumbukiza fedha
zako. Taarifa hizo ndio mwongozo wa kukuwezesha kununua hisa za kampuni husika
katika bei ambayo ni nzuri kwavyko. Hata hivyo, unahitaji kufahamu kuwa taarifa
za mienendo ya kampuni sio kinga dhidi ya mabadiliko kwenye thamani ya kinga
kwa siku za baadae bali kwa kiasi flani taarifa hizi zinatoa picha ya ufanisi
wa kampuni kwenye soko.
16. Bei ya hisa za kampuni katika soko la
hisa zinaendeshwa na hisia za wateja kwa kadri wanavyouza au kununua hisa. Mwandishi
anatushikisha kuwa kadri hisa za kampuni husika zinavyokimbiliwa na kila mtu
ndivyo na bei yake inavyopanda. Hata hivyo, itafikia pointi ambayo
wanaokimbilia kununua hisa husika watapungua na hivyo bei itarudi kwenye
mlinganyo wake. Hii inamaanisha kuwa kupanda au kushuka kwa thamani ya hisa
kunaendeshwa na maamuzi ya wateja wa hisa kupitia kununua au kuuza hisa
wanazomiliki.
17. Kama ilivyo kwenye fani nyingine ambazo
umekuwa ukitafuta washauri wabobevu kwenye fani husika pia kwenye uwekezaji wa
hisa unaweza kutafuta mshauri wako binafsi. Mshauri huyu anaweza kuwa ni dalali
wa hisa ambaye ana uzoefu wa kutosha kwenye uwekezaji wa hisa na hivyo mtu huyu
ni lazima awe na taarifa sahihi juu ya mienendo ya makampuni mbalimbali kwenye
soko la hisa.
18. Tengeneza sera yako ya uwekezaji. Sera hii
inatakiwa kuwa mwongozo wako kwenye uwekezaji wa hisa ikiwa ni pamoja na
kuonyesha maono na malengo yako kwenye uwekezaji wa hisa. Sera hii pia
inatakiwa kuonyesha ni kiasi gani cha hatari ya uwekezaji ambacho upo tayari
kubeba kupitia uwekezaji wa hisa.
19. Unaweza kuwekeza kwenye hisa ambazo
zinauzwa kwa bei chini kuliko thamani yake halisi kwenye soko la hisa. Mwandishi
anatushirikisha kuwa zipo tafiti ambazo zimedhihirisha kuwa baadhi ya kampuni
hisa zake zinakuwa zinauzwa kwa bei ya chini kuliko thamani ya kampuni husika. Hisa
hizi zina nafasi kubwa ya kufanya vyema kwenye soko kwa siku za baadae na hivyo
kumfanya mhusika kupata faida kutokana na uwekezaji wake.
20. Taarifa za kifedha za kampuni zinazouza
hisa kwenye soko la hisa zinaweza kutoa mwanga juu ya mienendo ya kampuni japo
hazijitoshelezi kukupa uhakika wa mwenendo wa kampuni husika kwenye soko kwa
siku za zijazo. Hii ni kutokana na
ukweli kwamba taarifa hizi kiuchumi inafahamika kuwa zinaandaliwa kwa kumfumo
wa dhana ya makisio ambayo mara nyingine yanaweza kubadilika kwenye uhalisia wa
utekelezaji.
21. Moja ya mbinu unazoweza kutumia kwa
ajili ya kuamua hisa za kampuni ipi ununue ni kuangalia kiasi cha fedha
kinachotolewa kwa kila hisa moja (earnings per share). Kiwango hiki cha fedha
ndicho kinachopelekea kampuni husika kutoa gawio kila kila mwaka kulingana na
idadi ya hisa kila mmoja anazomiliki. Mfano, kwa kila mwanahisa wa CRDB kila
hisa moja kuna TSHS 10 inatolewa kama gawio hivyo kama unamiliki hisa 1000
gawio lako kwa mwaka itakuwa ni TSHS 10,000 kabla ya makato ya kodi. Kwa upande
wa NMB kwa kila hisa moja kuna gawio la TSHS 104 inatolewa kwa kila mwanahisa
kulingana na idadi ya hisa anazomiliki.
22. Kuwa makini na hisa ambazo zinawekwa
sokoni kwa mara ya kwanza. Hizi ni hisa ambazo kampuni inaziweka sokoni mara
baada ya kubadilisha mfumo wa umiliki kutoka kwenye kampuni mfumo wa binafsi
(private company) na kuingia kwenye mfumo wa umma (public company). Mwandishi anatushirikisha
kuwa mara nyingi hisa hizi huwa zinatolewa kwa bei ya juu na hivyo
zinapoorodheshwa kwenye soko la hisa katika miaka ya awali hisa hizi zinashuka
kiwango na hivyo kama umewekeza fedha nyingi kwa lengo la kutengeneza faida
zitakutoa nje ya malengo. Mfano mzuri ni hisa za kampuni ya mkononi ya Vodacom ambazo
bei ya kutolewa ilikuwa TSH 850 lakini baada ya kuorodheshwa kwenye soko la hisa
kwa sasa zinauzwa mpaka TSHS 700.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha
haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala
ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
|
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com