Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha How The Stock Markets Works (Mwongozo wa Jinsi Soko la Hisa Linavyofanya Kazi)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri.

Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 37 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.

Makala hizi za uchambuzi wa vitabu zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu vya maarifa mbalimbali. Ni matarajio yangu kuwa muda ninaotumia kushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada mkubwa kwako katika kubadilisha maisha yako. Hata hivyo, mtandao huu bado unahitaji maoni/ushauri au shuhuda kwa namna ambavyo umekuwa wa msaada kwako au namna ambavyo unahitaji makala hizi ziboreshwe zaidi (tuma maoni/ushauri/ushuhuda wako kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com).

Ili uendelee kunufaika na makala za mtandao huu BONYEZA HAPA na ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.

Kitabu cha wiki hii ni How the Stock Markets Workskutoka kwa Profesa Ramon P. De Gennaro wa Chuo Kikuu cha Tennessee, Knoxville. Hapa tunashirikishwa mwongozo wa kufahamu namna ambavyo Soko la Hisa linafanya kazi kwa ajili ya kila mmoja wetu kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji kwenye hisa za kampuni mbalimbali.

Linapokuja suala la ukwezaji kwenye hisa ni wachache sana hasa kwa vijana ambao wanafahamu uwekezaji huu. Pia, vijana wengi hawavutiwi na uwekezaji wa hisa kwa vile walio wengi wanataka utajiri wa haraka. Uwekezaji wa hisa unabadirika kila wakati na hivyo ni uwekezaji ambao kabla ya kuwekeza unahitaji kufahamu mabadiliko ya namna hiyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba soko la hisa linaendeshwa na hisia za wanunuaji pamoja na wauzaji wa hisa.

Karibu tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:

1. Unapoamua kununua au kuuza hisa fanya hivyo kwa dhana ya kuwa bei ya wakati huo ni halisi kwa maana ya kwamba hisa husika haiuzwi kwa bei ya juu/chini kuliko thamani yake. Hata hivyo, unahitaji kukumbuka kuwa hata kama bei ni halisi bado bei hiyo si ya uhakika kwani inaweza kubadilika ndani ya masaa au siku. Na hii ndio itathibitisha kuwa bei husika ilikuwa/haikuwa halisi. Na hivyo uwekezaji wa hisa ni biashara ambayo muhusika ni lazima awe tayari kubeba hatari (risk) kwani hakuna ambaye anajua bei ya hisa za kampuni fulani zikuwa na thamani gani siku zijazo.

2. Pia katika uwekezaji wa mtaji unahitaji kufahamu uwekezaji kwenye dhamana. Kwa kifupi moja ya tofauti kati ya hisa na dhamana, dhamana zinauzwa kwa makubaliano maalumu katika kipindi cha muda maalumu (muda wa kuiva dhamana). Zipo dhamana za muda mfupi, muda wa kati na dhamana za muda mrefu. Katika uwekezaji wa dhamana, mwekazaji ananufaika na ongezeko la thamani ambalo ulipwa kwa pamoja na mtaji uliowekezwa baada ya muda kuisha wa dhamana alizonunua. Hapa unahitaji kutambua kuwa katika uwekezaji wa dhamana mwekezaji anakuwa na uhakika wa kupata faida pamoja na mtaji wake aliowekeza mara baada ya kuiva kwa dhamana husika.

3. Unapowekeza kwenye hisa unategemea kufaidika kupitia ongezeko la thamani ya hisa za kampuni husika pamoja na gawio kwa wanahisa kulingana na idadi ya hisa zako. Hapa unahitaji kujifunza vitu viwili; moja, kama thamani ya hisa za kampuni husika itashuka basi na wewe utegemee kupata hasara kwenye uwekezaji wako (mtaji) na endapo thamani ya hisa ikiongezeka ndivyo na wewe mtaji wako utaogezeka. Mbili, gawio la kila mwaka linakokotolewa kulingana na faida iliyotengenezwa na kampuni katika kipindi husika. Kama kampuni imepata hasara ndani ya kipindi husika tegemea kupata gawio kidogo. Hizi pia ni tofauti nzuri kati ya uwekezaji wa kwenye hisa na dhamana kwani uwekezaji wa kwenye dhamana hautegemei faida iliyotengenezwa au kupanda na kushuka kwa thamani kama ilivyo kwenye hisa.

4. Gawio linaweza kulipwa kwa mfumo wa hisa au kwa mfumo wa pesa taslimu kulingana na utaratibu wa kampuni husika. Hii ina maana kwamba kama kampuni inalipa gawio kwa mfumo wa hisa wawekezaji wanategemea idadi ya hisa zao kuongezeka kila mwaka kwa kutegemea faida iliyotengenezwa na kampuni husika katika kipindi hicho. Na pale kampuni inapotoa gawio kwa mfumo wa fedha taslimu maana yake ni kwamba idadi ya hisa za wawekezaji inaendelea kuwa ile ile kama hawajanunua hisa zaidi ndani ya kipindi husika na gawio lao hulipwa moja kwa moja kwenye akaunti zao au kwa cheki kila mwaka kulingana na faida iliyotengenezwa.

5. Kwa ujumla tunakiwa kujifunza kuwa hisa na dhamana ni mfumo unaowezesha wamiliki wa kampuni husika kugawana mali zinazomilikiwa na kampuni husika au mali zinazozalishwa na kampuni husika ndani ya kipidi husika. Ugawanaji wa mali hizi unategemea na kiasi ulichowekeza kwenye kampuni husika na hivyo kwa maana nyingie uvuna kulingana na ulichopanda.

6. Je soko la hisa ni nini? Kama ambavyo tunafahamu kuwa soko sehemu inayounganisha watu zaidi ya mmoja kwa ajili ya kufanya biashara aidha ana kwa ana au kwa kuunganishwa na mtandao wa internet, pia soko la hisa lina maana hii kwa kuwa ni mtandao wa kifedha unaowaunganisha watu kwa ajili ya kuuza au kununua umiliki wa hisa au dhamana. Soko hili linafanya kazi sawa na masoko mengine kwa maana misingi muhimu ya masoko kama vile ushindani kwenye soko. Hii ina maana kwamba kama unauza hisa zako unahitaji wateja makini wa kununu hisa zako na kama unanunua unahitaji wauzaji wa makini wa kuuza hisa/dhamana.

7. Msingi mwingine wa soko la hisa ni idadi ya kampuni zinazouza hisa zake kwenye soko husika. Kama ilivyo kwenye masoko mengine, bei nzuri ya bidhaa Y inategemea na idadi ya watu wanaouza au kuzalisha bidhaa Y kwenye soko husika. Kadri wauzaji wa bidhaa Y wanavyokuwa wachache ndivyo bei ya bidhaa hii itapangwa kulingana na mapenzi ya muuzaji na watumiaji watatokosa uchaguzi zaidi ya kununua bidhaa Y hata kama bei ipo juu. Ndivyo ilivyo kwenye soko la hisa ili kuondoa tabia ya kampuni moja kuhodhi (kumiliki) soko ni lazima makampuni mapya kwenye soko yawe yanaongezeka mara kwa mara na hivyo kuleta ushindani kwenye soko la hisa.

8. Katika masoko ya hisa taarifa ni muhimu kwa wawekezaji wapya. Kabla ya kuamua kununua hisa unahitaji kufanya tafiti za ni kampuni zipi hisa zake zimekuwa zikifanya vyema kwenye soko kwa muda mrefu. Hii ni tofauti ni kwenye masoko ya bidhaa nyingine kama gari. Mfano, kama unahitaji kununua gari ambalo lilishatumika hauwezi kufahamu matatizo ya gari husika mpaka pale utakapokuwa umenunue. Na hii inafanya wanunuaji kushusha bei ya bidhaa husika wakidhani kuwa pengine bidhaa hiyo inaweza kuwa na mapungufu. Kwenye soko la hisa hii ni tofauti kwani kuna kampuni nyingi na kila moja ina maelfu ya hisa inazouza zenye thamani sawa. Wajibu wako ni kuchagua kampuni ipi ambayo itakuwezesha kupata faida nzuri kulingana na kiasi ulichowekeza.

9. Soko la hisa linafanya kazi chini ya aina mbili ambazo ni soko la awali/msingi na soko la upili (secondary stock market). Katika soko la awali wamiliki wa kampuni wanakuwa na lengo la kuongeza mtaji wao na hivyo wanaweka hisa mpya katika soko kwa ajili ya kupata wamiliki wapya. Katika soko la upili ni kwamba wamiliki wanaomiliki hisa zao wanaamua kuuza hisa au sehemu ya hisa zao kwa ajili ya kupata fedha. Suala ya kujifunza hapa ni kwamba katika soko la awali fedha za mauzo ya hisa zinakwenda moja kwa moja kwa mmiliki wa kampuni wakati katika soko la upili umiliki unahama kutoka kwa mtu mmoja kwenye mwingine kulingana na idadi ya hisa alizouza. Anachofanya mmiliki wa kampuni ni kuhamisha idadi ya hisa zilizouzwa kutoka kwa mmiliki wa awali kwenda kwa mmiliki mpya.

10. Wekeza kwenye hisa ukiwa na malengo ya muda mrefu. Mwandishi anatushirikisha kuwa uwekezaji wa hisa sio aina ya uwekezaji ambao utawekeza leo na kesho ukaamka tajiri. Kama unahitaji utajiri wa haraka basi tambua kuwa aina hii ya uwekezaji haitokufaa kwani inahitaji muda kwa ajili ya kuvuna kwa faida kile ambacho umewekeza.
11. Thamani ya hisa ipatikana/kutambuliwa kwa kuangalia vitu vitatu; moja, kiasi cha fedha ambacho unategemea kutengeneza kutoka kwenye hisa husika (kadri kiasi cha fedha kinavyokuwa juu ndivyo na thamani ya hisa inakuwa juu). Mbili, ni kwa muda gani unatakiwa kusubiri kwa ajili ya kupata fedha tarajiwa katika hisa zako (kadri unavyotakiwa kusubiri kwa muda mrefu kupata fedha tarajiwa ndivyo na thamani ya hisa inakuwa chini na kinyume chake ni sahihi). Tatu, kiwango cha riba katika muda unaotakiwa kusubiri kwa ajili ya kupata fedha tarajiwa kutoka kwenye uwekezaji wako (kadri kiwango cha riba kinavyokuwa juu ndivyo na thamani ya hisa inavyokuwa chini na kinyume chake ni sahihi).

12. Katika soko la hisa ni vigumu sana kusema kuwa umefanya dili la maana au baya kibiashara. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ni vigumu kutabiri thamani ya hisa za kampuni husika kwa siku zijazo. Hisa zinazouzwa kwa thamani leo hii kesho unaweza kushangaa zinashuka thamani kwenye soko la hisa. Hapa ndipo utangundua kuwa unapowekeza kwenye hisa ni lazima uwe tayari kubeba hatari za kiuwekezaji (investment risks).

13. Ni busara kuwekeza kwenye hisa za kampuni zinazotofautiana kibiashara kuliko kuwekeza fedha zako zote kwenye kampuni moja (diversification). Mwandishi anatushirikisha kuwa kuwekeza kwenye kampuni moja kunaweza kupelekea kupoteza sehemu ya uwekezaji wako pale ambapo kampuni husika zitafanya vibaya kwenye soko. Muhimu, unahitaji kufanya uchaguzi wa kampuni za kuwekeza ili kama kampuni moja hisa zake zitashuka thamani basi unaweza kufaidika kupitia kwenye kampuni nyingine ambayo hisa zake zina thamani kwenye soko kwa kipindi hicho.

14. Kiasi cha fedha ambacho unaweza kutengeneza kupitia uwekezaji wa hisa kinategeme vitu vitatu, moja, kiasi cha fedha ulichowekeza; mbili, kiwango cha riba ambacho ndicho kitaamua gawio lako; na muda ambao utaendelea kudumu na hisa zako. Kwa ufupi hii ndio siri ya uwekezaji wa aina yoyote ile ambayo matajiri wengi wanaitumia kwa ajili ya kutengeneza pesa zaidi. Siri hii ni sawa na msemo wa wachina kuwa “muda mzuri kwako wa kufanya maamuzi ya kupanda miti ilikuwa pindi ukiwa na miaka 15 na muda bora zaidi wa kufanya maamuzi hayo ni sasa”. Msemo huu unatuambia kuwa katika uwekezaji hakuna kauli ya nilishachelewa kufanya maamuzi – muda wowote katika umri wowote ni nyakati sahihi za kufanya maamuzi ya uwekezaji.

15. Taarifa sahihi juu ya kampuni ipi uwekeze fedha zako ni muhimu kuliko kitu chochote kabla ya kutumbukiza fedha zako. Taarifa hizo ndio mwongozo wa kukuwezesha kununua hisa za kampuni husika katika bei ambayo ni nzuri kwavyko. Hata hivyo, unahitaji kufahamu kuwa taarifa za mienendo ya kampuni sio kinga dhidi ya mabadiliko kwenye thamani ya kinga kwa siku za baadae bali kwa kiasi flani taarifa hizi zinatoa picha ya ufanisi wa kampuni kwenye soko.

16. Bei ya hisa za kampuni katika soko la hisa zinaendeshwa na hisia za wateja kwa kadri wanavyouza au kununua hisa. Mwandishi anatushikisha kuwa kadri hisa za kampuni husika zinavyokimbiliwa na kila mtu ndivyo na bei yake inavyopanda. Hata hivyo, itafikia pointi ambayo wanaokimbilia kununua hisa husika watapungua na hivyo bei itarudi kwenye mlinganyo wake. Hii inamaanisha kuwa kupanda au kushuka kwa thamani ya hisa kunaendeshwa na maamuzi ya wateja wa hisa kupitia kununua au kuuza hisa wanazomiliki.

17. Kama ilivyo kwenye fani nyingine ambazo umekuwa ukitafuta washauri wabobevu kwenye fani husika pia kwenye uwekezaji wa hisa unaweza kutafuta mshauri wako binafsi. Mshauri huyu anaweza kuwa ni dalali wa hisa ambaye ana uzoefu wa kutosha kwenye uwekezaji wa hisa na hivyo mtu huyu ni lazima awe na taarifa sahihi juu ya mienendo ya makampuni mbalimbali kwenye soko la hisa.

18. Tengeneza sera yako ya uwekezaji. Sera hii inatakiwa kuwa mwongozo wako kwenye uwekezaji wa hisa ikiwa ni pamoja na kuonyesha maono na malengo yako kwenye uwekezaji wa hisa. Sera hii pia inatakiwa kuonyesha ni kiasi gani cha hatari ya uwekezaji ambacho upo tayari kubeba kupitia uwekezaji wa hisa.

19. Unaweza kuwekeza kwenye hisa ambazo zinauzwa kwa bei chini kuliko thamani yake halisi kwenye soko la hisa. Mwandishi anatushirikisha kuwa zipo tafiti ambazo zimedhihirisha kuwa baadhi ya kampuni hisa zake zinakuwa zinauzwa kwa bei ya chini kuliko thamani ya kampuni husika. Hisa hizi zina nafasi kubwa ya kufanya vyema kwenye soko kwa siku za baadae na hivyo kumfanya mhusika kupata faida kutokana na uwekezaji wake.

20. Taarifa za kifedha za kampuni zinazouza hisa kwenye soko la hisa zinaweza kutoa mwanga juu ya mienendo ya kampuni japo hazijitoshelezi kukupa uhakika wa mwenendo wa kampuni husika kwenye soko kwa siku za zijazo.  Hii ni kutokana na ukweli kwamba taarifa hizi kiuchumi inafahamika kuwa zinaandaliwa kwa kumfumo wa dhana ya makisio ambayo mara nyingine yanaweza kubadilika kwenye uhalisia wa utekelezaji.

21. Moja ya mbinu unazoweza kutumia kwa ajili ya kuamua hisa za kampuni ipi ununue ni kuangalia kiasi cha fedha kinachotolewa kwa kila hisa moja (earnings per share). Kiwango hiki cha fedha ndicho kinachopelekea kampuni husika kutoa gawio kila kila mwaka kulingana na idadi ya hisa kila mmoja anazomiliki. Mfano, kwa kila mwanahisa wa CRDB kila hisa moja kuna TSHS 10 inatolewa kama gawio hivyo kama unamiliki hisa 1000 gawio lako kwa mwaka itakuwa ni TSHS 10,000 kabla ya makato ya kodi. Kwa upande wa NMB kwa kila hisa moja kuna gawio la TSHS 104 inatolewa kwa kila mwanahisa kulingana na idadi ya hisa anazomiliki.

22. Kuwa makini na hisa ambazo zinawekwa sokoni kwa mara ya kwanza. Hizi ni hisa ambazo kampuni inaziweka sokoni mara baada ya kubadilisha mfumo wa umiliki kutoka kwenye kampuni mfumo wa binafsi (private company) na kuingia kwenye mfumo wa umma (public company). Mwandishi anatushirikisha kuwa mara nyingi hisa hizi huwa zinatolewa kwa bei ya juu na hivyo zinapoorodheshwa kwenye soko la hisa katika miaka ya awali hisa hizi zinashuka kiwango na hivyo kama umewekeza fedha nyingi kwa lengo la kutengeneza faida zitakutoa nje ya malengo. Mfano mzuri ni hisa za kampuni ya mkononi ya Vodacom ambazo bei ya kutolewa ilikuwa TSH 850 lakini baada ya kuorodheshwa kwenye soko la hisa kwa sasa zinauzwa mpaka TSHS 700.

Haya ni machache ambayo nimeweza kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.

PATA UCHAMBUZI WA KITABU CHA THE RULES OF MONEY ( KANUNI ZA PESA)
 

Mwandishi Richard Templar katika kitabu hiki ametushirikisha kanuni 107 ambazo kila mtu anaweza kuzitumia kutengeneza pesa na hatimaye kuwa tajiri. Uchambuzi wa kina wa kanuni zote (107) umeandaliwa kwa mfumo wa pdf na unapatikana kwa gharama ya Tshs. elfu tano tu (5,000/=). Kanuni zote zimechambuliwa na kuandaliwa kijitabu kidogo chenye kurasa 39 ambazo unaweza kusoma kwenye simu ya mkononi (smart phone) au kwenye kompyuta (pc).

Kupata uchambuzi wa kanuni zote tuma pesa yako kwa njia ya M-pesa au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-

M – Pesa tumia namba: 0763 745 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Airtel Money tumia namba: 0786 881 151 451 (Majina ni Augustine Mathias)

Baada kutuma pesa hiyo nitumie ujumbe kwenye namba ya airtel (0786 881 151 451) ukiwa na barua pepe yako ili nikutumie uchambuzi wa kanuni hizi moja kwa moja kwenye mtandao wako.

UTAJIRI NI HAKI YAKO YA KUZALIWA "BEING RICH IS YOUR BIRTH RIGHT"

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com


onclick='window.open(